UKWELI UNAOPOTOSHA.

UKWELI UNAOPOTOSHA.

Jina la Bwana wetu Yesu litukuzwe!..Maandiko yanatuambia Yesu ndiye njia, kweli na Uzima mtu hafiki kwa Baba isipokuwa kwa njia yake yeye. Ikiwa na maana kuwa hakuna namna yoyote ya kuiona mbingu nje ya Yesu Kristo, yaani unapoizungumzia mbingu unamzunguzia Bwana Yesu. Yeye ndio lile lango na ufunguo wa kuingia mbinguni(Yohana 10:9-16).

Kwa Neema za Bwana leo tutajifunza juu ya UKWELI UNAOPOTOSHA. Si kila ukweli unaozungumzwa lengo lake ni kumwelekeza mtu katika njia ya kweli…Ukweli mwingine lengo lake ni kupotosha!…Kwahiyo upo ukweli unaompeleka mtu kwenye njia sahihi na upo ukweli unapompeleka mtu kwenye njia ya upotofu.

Hebu tafakari hili tukio lifuatalo…

Matendo 16:16 “Ikawa tulipokuwa tukienda mahali pale pa kusali, kijakazi mmoja aliyekuwa na pepo wa uaguzi akatukuta, aliyewapatia bwana zake faida nyingi kwa kuagua.

17 Akamfuata Paulo na sisi akipiga kelele, akisema, Watu hawa ni watumishi wa Mungu aliye juu, wenye kuwahubiria njia ya wokovu.

18 Akafanya hayo siku nyingi. Lakini Paulo akasikitika, akageuka akamwambia yule pepo, Nakuamuru kwa jina la Yesu Kristo, mtoke huyu. Akamtoka saa ile ile”.

Katika tukio hili unaona Mtume Paulo na mwenzake walikutana na mwanamke mmoja kijakazi aliyekuwa na pepo la uaguzi, kwasasa tunaweza kusema alikuwa ni mganga wa kienyeji..Na Yule mwanamke alipowaona tu wakina Paulo, akawatambua hivyo akapaza sauti na kusema ‘hawa ni watumishi wa Mungu aliye juu wenye kuwahubiria watu njia ya wokovu’…Sasa hapo alikuwa hawaambii wakina Paulo, bali alikuwa anawaambia watu waliokuwa karibu kando kando ya hilo eneo.

Lakini kama tunavyosoma Paulo alihuzunika, akalikemea lile pepo likamtoka?…Unaweza ukajiuliza kwanini Paulo ahuzunike?…angepaswa afurahi kwasababu Yule mtu kazungumza ukweli kuwa wao ni wakina nani, isitoshe kakiri hadharani mbele ya watu wote kuwa wao ni watumishi wa Mungu. Lakini Paulo hakufanya hivyo kwasababu aliijua nia na lengo shetani.

Sasa endapo Mtume Paulo na mwenzake wangekubali zile sifa…ni wazi kuwa moja kwa moja Yule mwanamke angezidi kuaminiwa na watu zaidi ya wakina Paulo wenyewe…Watu wangemheshimu Yule mwanamke kwa kuwa na uwezo mkubwa wa kujua siri za ndani,..na hivyo watu endapo wangepatwa na matatizo wasingewatafuta wakina Paulo watumishi wa Mungu..wangemtafuta Yule mwanamke mwenye uwezo wa kutambua mambo ya ndani sana, Na matokeo yake mwanamke Yule angezidi kupata jina kuliko wakina Paulo..Hilo ndilo lilikuwa lengo la shetani.

Unajua kuna njama Fulani huwa wanazozitumia wafanya biashara waliofanikiwa ili wawavutie wateja kwao…wanachofanya ni kuwaambia wateja wao ukweli, utakuta mtu atafika labda katika duka lake, na endapo mteja akikosa hiyo bidhaa aliyokuwa anaitafuta…utaona Yule mwuzaji anamwelekeza sehemu nyingine iliyo sahihi ya kuipata hiyo bidhaa…na Yule mteja akienda hiyo sehemu aliyoelekezwa na kupata alichokuwa anakitafuta…hataliamini lile duka alilokwenda kununulia bidhaa bali atamwamini zaidi Yule aliyemwelekeza kwenye hilo duka…kwahiyo mwisho wa siku Yule mteja atakuwa kila akihitaji kitu anamrudia Yule mtu wa kwanza, kwasababu anajua ni muwazi na mwaminifu. Na wafanyabiashara werevu huwa wanajua kabisa ukitaka upoteze soko lako poteza uaminifu na uwazi kwa wateja wako…

Na ndio haya mapepo yalichokuwa yanataka kufanya hapa…yalikuwa yanataka kutengeneza jina (GOODWILL) kwa wateja wake.

Ndio maana Paulo alilikemea lile pepo mara moja na lilipotoka ndipo uwezo wa Mungu ukadhihirika, watu wote wakajua kuwa kumbe nguvu zilizokuwepo ndani ya Yule mwanamke ni ndogo kuliko zilizokuwepo ndani ya Paulo na wenzake…na hivyo lengo la shetani likaharibika palepale. Kwahiyo si kila ukweli unaozungumzwa unakuwa na lengo zuri.

Ndio maana utaona sehemu nyingi sana Bwana Yesu aliyazuia mapepo yasimdhihirishe…utaona sehemu nyingi alizokuwa akipita yalikuwa yanapiga kelele “wewe ndio mwana wa Mungu” n.k na Bwana alikuwa anayakemea, yanyamaze.

Na pia utaona Edeni jambo lililotokea ni hilo hilo, nyoka alimwambia Hawa ukila matunda utakuwa kama Mungu ukijua mema na mabaya…ni kweli hakumwambia uongo, alimwambia ukweli kabisa! lakini ukweli wenye kupotosha maana alipokula lile tunda alikuwa kweli kama Mungu kwa kujua mema na mabaya hata Mungu mwenyewe alishuhudia hilo, lakini ni ukweli ulioambatana na kifo…madhara yake utaona ndio yale utaona alishushwa na kuwa mdogo zaidi hata ya mume wake…ndio maana akaambiwa atatawaliwa na mumewe. Halikuwa lengo Mungu mwanadamu amtawale mwanadamu mwenzake. Hayo ndio madhara ya ukweli unaopotosha.

Na pia lengo lingine la shetani lilikuwa ni kutaka kupandikiza roho ya kiburi ndani ya wakina Paulo, mioyo yao inyanyuke ili wajione kuwa wanaupako..Na shetani anajua Mungu hapendi kiburi au mtu anayejikweza na hivyo wangeshushwa.

Lakini hebu leo hii, mapepo yazungumze na mtumishi yeyote na kuanza kumsifia uone kama mtu huyo hatanyanyuka moyo, utaona ndio atatumia hiyo fursa hata kuyauliza maswali, kumbe hajui huku nyuma nia ya shetani ni nini..Ndugu usisikilize ukweli wa shetani, ni ukweli unaopotosha….usisikilize mahubiri ya shetani, ni mahubiri kweli ya Neno la Mungu lakini ndani yake yanalengo la kupotosha…

Wakati shetani anamjaribu Bwana Yesu kule jangwani alikuwa anamwambiaje??…alikuwa anazungumza ukweli kabisa wa kimaandiko kwamba “jitupe kwa maana imeandikwa atakuagizia malaika zake wakulinde usijikwae”…Huo ni ukweli kabisa shetani anaouzungumza…lakini ni ukweli wenye lengo lingine tofauti na lile lililokusudiwa kwenye huo mstari.

Hivyo biblia inatuonya tuwe waerevu…tuzichunguze roho, sio tuchunguze miili, hapana bali roho na sifa zinazoletwa mbele yetu…

Bwana akubariki sana. jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

KANUNI RAHISI YA KUFANIKIWA.

NGUVU YA HEKIMA NA AKILI

RACA

WATU WASIOJIZUIA.Rudi Nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
3 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Anonymous
Anonymous
1 year ago

mungu akubariki

Damy
Damy
2 years ago

Amen