Jina la Bwana wetu Yesu Kristo
lisifiwe, nakukaribisha mtu wa Mungu tujifunze Maneno ya uzima, na leo
tutajifunza ni kwanini Mungu alitaka kumuua Musa mwanzoni kabisa mwa
huduma yake japokuwa yeye mwenyewe ndio aliyemuita na kumthibitishia
kuwa atakuwa pamoja naye. Tukilifahamu hilo kwa undani itatusaidia na
sisi kuielewa tabia ya Mungu, na hivyo kuchukua hatua stahiki tusije
tukajikuta tunaangamia kwa uzembe fulani.
Tunafahamu
sababu kubwa iliyomfanya Musa akimbie kule Misri ni ile hali ya yeye
kutetea chimbuko lake (yaani la Kiebrania), tunaona alipomuua Yule
Mmisri aliyekuwa anapigana na Mwebrania alikimbilia nyikani kwa
Wamidiani na hakurudi tena Misri mpaka miaka 40 ilipoishia, sasa huo
wakati wote alipokuwa katika Ardhi ile ni wakati ambao Mungu alikuwa
anampitisha Musa katika madarasa ya kimaisha afahamu vizuri chimbuko
lake, Mungu “alimtweza”, hicho kipindi chote, hivyo akafahamu vizuri
asili yake, huku akisaidiwa na mkwewe Yethro, ambaye ndiye alimpa binti
yake aliyeitwa Sipora awe mkewe, Wote hawa walikuwa ni wazao wa Ibrahimu
isipokuwa kwa mama tofauti, Waisraeli walitoka kwa Sara, lakini
Wamidiani (yaani wakina Yethro mkwewe Musa), walitokea kwa mke mdogo
aliyeitwa Ketura ambaye Ibrahimu alimtwaa baada ya Sara kufa.
Hivyo
wote walikuwa ni ndugu, na wote walimwabudu Mungu mmoja, sasa kumbuka
wakati huo Torati ilikuwa bado haijafika, kwani Torati ilikuja kutolewa
na Musa, lakini lilikuwepo agizo moja KUU ambalo Ibrahimu alipewa na
Mungu kwa wazao wake wote, kama dalili ya agano aliloingia yeye na
Ibrahimu, na agizo hilo lilikuwa ni TOHARA
kwamba wazao wake wote watahiriwe, Hivyo mtoto yoyote anayezaliwa bila
kupoteza muda siku ya 8 anapaswa atahiriwe kisha apewe jina..Na kwa
kufanya hivyo atakuwa tayari kashahesabika kuwa ni mazao wa Ibrahimu
mrithi wa Baraka zote Mungu alizomwahidia Ibrahimu na uzao wake.
Hivyo
watoto wote wa Ibrahimu walitahiriwa, haikujalisha ni wa mke yupi ni wa
kijakazi Hajira, au wa Sara au wa Ketura…haikujalisha hiyo, wote
walitahiriwa kufuata maagizo waliyopewa.. Hivyo ilikuwa ni jambo la
ajabu na la kushangaza itokee mzao yoyote mpaka amefikia mtu mzima
hajatahiriwa,kwanza ulikuwa unaonekana ni kafiri, na unatengwa na jamii
yote, Kama tu walikuwa hawashirikiani kwa chochote na mataifa ambayo
hawajatahiriwa unadhani ukiitwa mzao wa Ibrahimu halafu hujatahiriwa
utachukuliwaje?. Sio tu wazao wa Ibrahimu watakukataa bali pia Mungu
mwenyewe atakukataa.
Sasa
Musa alilifahamu hilo, mpaka akazaa watoto, lakini hakuliweka akilini
kuwa kila mzao wa Ibrahimu wa kiume anapaswa atahiriwe, yeye alipuuzia,
alilichukulia kiwepesi wepesi tu, kama jambo lisilokuwa na umuhimu
mkubwa kwenye mambo ya rohoni na hivyo mpaka akazaa mtoto,akakua mkubwa,
siku ya 8 ikipita, mwezi ukapita, miaka ikapata yupo naye tu…
Wakati
huo wote Mungu hakumsemesha chochote, mpaka ikafikia wakati Mungu
alipomwita kule mlimani, na kumpa maelekezo ya kwenda kuwaokoa wana wa
Israeli, Mungu akamthibitishia kuwa atakuwa naye, kwa miujiza na ishara
kubwa..
Na
ndivyo ilivyo leo hii watu wanaona Mungu akitembea nao kwa ishara kubwa
na miujiza wanapumbazika wakidhani kuwa hiyo yote ni kwasababu Mungu
amependezwa nao.
Lakini
angalia kilichomtokea Musa, kumbe huku nyuma Mungu alikuwa amepanga
kumuua, kabla hata hajafika mbali, akiwa njiani usiku, Yule malaika
ambaye alienda kuwaua wazaliwa wa kwanza wa Wamisri alikuwa
ameshaandaliwa kumamliza Musa habari yake iwe imeishia pale pale.
Lakini
mke wake Sipora kuona vile aligundua kuwa ni lile kosa la mume wake
kuwa mzembe kutotimiza maagizo ya Mungu kwa mwanae, hivyo alichofanya
haraka, alidhubutu kwenda kinyume cha taratibu akachukua jiwe kali
akakata govi la mwanae, japo Sipora hakupendezwa na kitendo kile na ndio
maana akamwambia Musa “Hakika wewe u bwana arusi wa damu kwangu mimi.”
Hayo tunayasoma katika kitabu cha Kutoka:
Kutoka 4:24 “Ilikuwa walipokuwa njiani mahali pa kulala, Bwana akakutana naye akataka kumwua.
25 Ndipo Sipora akashika jiwe gumu na kuikata govi ya zunga la mwanawe, na kuibwaga miguuni pake akasema. Hakika wewe u bwana arusi wa damu kwangu mimi.
26 Basi akamwacha. Ndipo huyo mkewe akanena, U bwana arusi wa damu wewe, kwa ajili ya kutahiri.”
Unaona,
Musa alipata neema tu kwa Mungu pamoja maono yake makubwa ya kwenda
kuwaokoa wana wa Israeli lakini asingefika mbali. Mambo kama hayo hayo
yalimtokea Balaamu, aliambiwa asiwalaani Israeli lakini yeye
akakang’ang’ania kwenda kule kwa Balaki ambako Mungu amemwambia
asiende….lakini yeye akakazana kung’ang’ania kwenda mwishowe Mungu
akamruhusu aende na kumpa maagizo ya kufanya huko aendako…. lakini kumbe
njiani Mungu a alikuwa amepanga kumuua, Ni Punda tu ndio aliyemsaidia
vinginevyo safari yake ingeishia pale (Hesabu 22).
Ndugu,
Ni vizuri tukaitambua tabia ya Mungu ili na sisi yasitukute kama hayo,
Leo hii Sipora wala Punda hawapo. Kumbuka wakati ule Tohara ya mwili
ilikuwa ni muhimu mpaka Mungu alitaka kumuua Musa kwa uzembe wa Tohara
ambayo si ya kwake, itakuwaje wewe ambaye sasahivi unaipuuzia tohara ya
Roho yako ambayo hiyo inanguvu mara nyingi sana kuliko ile ya mwilini.
Biblia inasema:
Warumi 2:28 “Maana yeye si Myahudi aliye Myahudi kwa nje tu, wala tohara siyo ile ya nje tu katika mwili;
29 bali yeye ni Myahudi aliye Myahudi kwa ndani, na tohara ni ya moyo, katika roho, si katika andiko; ambaye sifa yake haitoki kwa wanadamu bali kwa Mungu”.
Utasema,
mbona Mungu huwa ananionyeshaga maono?, mbona huwa kila siku
ananishuhudia kwenye ndoto mimi ni mteule wake, Mbona huwa ananitumia
kutenda miujiza na maajabu, mbona huwa anajibu maombi yangu, mbona huwa
ananipigania katika biashara zangu na shughuli zangu na mambo yangu
yote, ..Lakini nataka nikuambie kama hujatolewa govi katika moyo wako, KIFO KITOKACHO KWA BWANA KIPO MBELE KINAKUNGOJA.
Sasa swali TOHARA hii YA ROHO ZETU INAFANYIKAJE?
Wakolosai 2:11 “Katika yeye [YESU KRISTO] mmetahiriwa kwa tohara isiyofanyika kwa mikono, kwa kuuvua mwili wa nyama, kwa tohara ya Kristo.
12 Mkazikwa pamoja naye katika UBATIZO; na katika huo mkafufuliwa pamoja naye, kwa kuziamini nguvu za Mungu aliyemfufua katika wafu.”
Unaona hapo, tohara iliyosahihi baada ya kuamini kwa mkristo, kwa kuyaacha maisha yake ya kale, ni KUBATIZWA,
kama ishara ya kwamba umekufa pamoja naye na kufufuka pamoja naye. Watu
wengi wanapuuzia haya maagizo marahisi wanayaweka kando halafu wanataka
kwenda kumtumikia Mungu..
Wanapumbazika
pale wanapoona ishara zikifuatana nao, lakini kumbe Mungu kaweka kifo
mbele yao, ndugu weka kwanza msingi wako imara ndipo nyumba itasimama,
utawahubiria nini watu wamfuate Kristo wakati wewe mwenyewe huamini
katika tohara ya Roho yako na katika ubatizo ambao Bwana wako alikuwa ni
mkamilifu aliuendea wewe ni nani usifanye?…
Ikiwa
wewe ulishamwamini Kristo, au ndio unampokea leo hii, usikawie kwenda
kubatizwa ipasavyo ili kutimiliza haki yote. Na kumbuka pia ubatizo
sahihi ni ule wa kuzamwishwa katika maji mengi na uwe ni katika JINA LA
YESU KRISTO ambalo ndilo jina la Baba na mwana na Roho
Mtakatifu..sawasawa na mitume walivyobatiza (katika Matendo 2:38, 8:16, 10:48, 19:5).
Hivyo Ikiwa unajiiona wewe ni nabii mkuu zaidi ya Musa, au mtu wa rohoni, basi uyatumbue ya kuwa hayo ni maagizo ya Mungu.jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
JE! UMEBATIZWA UBATIZO SAHIHI?
JE! UNAWEZA KUBATIZWA NA USIPOKEE ROHO MTAKATIFU?. NA JE! UNAWEZA KUPOKEA ROHO MTAKATIFU KWA KUWEKEWA MIKONO?
JE, KAMA HAUNA UBATIZO SAHIHI HAUWEZI KUWA NA ROHO MTAKATIFU?
JE! NI HALALI KUTOA CHETI KWA WAKRISTO WANAOOA?
Rudi Nyumbani
Print this post