SIFA NJEMA YA KIRUKA NJIA

SIFA NJEMA YA KIRUKA NJIA

Kuna ndege anaitwa kiruka njia, ambaye anatajwa kama mmoja wa ndege najisi, kwenye Kumbukumbu 14:15, lakini ndege huyu anasifa moja ambayo, huwa ina  funzo kubwa sana la kiroho.

Tofauti na ndege wengine, ambao huruka aidha mchana, au usiku, kujitafutia chakula, kwamfano mwewe, mbayuwayu, korongo, tai, ni ndege wa mchana, lakini pia bundi, popo, ni ndege wa usiku, wote hawa hufanya kazi aidha majira ya kutwa nzima ya mchana, au usiku kucha.

Lakini kiruka njia, huruka zaidi, majira ya alfajiri sana, na jioni sana. Majira haya huyapendelea kwasababu, ni wakati wa mageuko ya siku, ambayo ndege wote wawindaji hujitandaa Kwenda mapumziko, au kuamka. Kwamfano muda wa jioni kama vile saa 12, ndege wakali wawindaji kama vile tai, mwewe, kipanga, n.k. wanaacha uwindaji, na kutafuta makao yao kupumzika, lakini pia wakati huo huo ndege wakali wa usiku kama vile bundi, hujiandaa kutoka waende kwenye mawindo yao saa mbili, Kwahiyo huo muda hapo Katikati mazingira kwake huwa si ya upinzani mkubwa.

Kwasababu yeye ni ndege dhaifu, na anaweza kuwindwa na ndege wakubwa, majira hayo kwake ni salama zaidi. Vivyo hivyo ule muda wa alfajiri sana, miale ya jua inapoanza kuonekana kwa mbali sana, hutoka na Kwenda kuwinda, muda huo ndege wa usiku ndio wanakwenda kulala, huku ndege wa mchana wanajiandaa kutoka, mpaka inapofika saa 12 asubuhi, tayari ameshamaliza uwindaji wake.

Licha ya kuwa wakati huo, ndege wengi hawapo hewani, lakini wakati huo, wa alfajiri sana na jioni sana, ndio makundi ya wadudu wengi wa ardhini hutoka kuruka juu, ikiwemo mbu, kumbikumbi, mchwa, nondo, mende n.k. kwasababu yeye hula wadudu, anaweza kukamata wadudu hata elfu moja ndani ya saa moja tu. Hivyo kwa muda mfupi sana akawa ameshashiba, zaidi ya mihangaiko mingi ya kutwa nzima, kugombani vyakula, na masumbufu mengi.

Ndege huyu mchana hupumzika zake, kwenye miti, na usiku pia, lakini hutumia alfajiri yake na jioni yake vizuri. Ndio maana ni vigumu kujulikana, kwasababu shughuli zake anazifanya wakati anga ni tulivu.

Hutufundisha nini?

Bwana alituambia tuwatafakari ndege (Mathayo 6:26)

Ni lazima tuthamini mida hii miwili, kuitumia kuwa uweponi mwa Bwana, Bwana Yesu alipendelea sana, kuamka alfajiri kuomba,

Marko 1:35 Hata alfajiri na mapema sana akaondoka, akatoka akaenda zake mahali pasipokuwa na watu, akaomba huko.

 Ipo faida kubwa sana kuamka  mapema kuomba kwasababu, muda huo anga ni tulivu, wakati watu wamelala, wewe unapokea thawabu za siku kutoka kwa Bwana. Kuna usemi unaosema biashara ni asubuhi, kwasababu wameona  Riziki nyingi huwaga majira hayo, vivyo hivyo rohoni, ukijifunza kuomba majira hayo, na jioni pia kabla hujaimaliza siku, Basi utaona tofauti kubwa sana, na wepesi mwingi wa masumbufu ya siku.

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

Hawa ndege katika Walawi 11:13-19 ndio ndege gani kwasasa?

MTEGO HUTEGWA BURE, MBELE YA MACHO YA NDEGE YE YOTE.

Je tamaa ni dhambi kulingana na Yakobo 1:15?

About the author

Nuru ya Upendo administrator

Leave a Reply