Jina la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe…Karibu tujifunze Neno la Mungu,.
Mojawapo
ya jambo linalochanganya watu wengi wa Mungu..Na hata mimi lilikuwa
linanichanganya mwanzoni sana wakati nampa Bwana maisha yangu…Ni jinsi
ya “kuwatambua watumishi wa uongo”. Nilikuwa nachanganyikiwa kuona mtu
anafanya miujiza kwa jina la Yesu, anatoa pepo, anamwombea mtu anapona,
anaona maono, anatoa unabii n.k lakini bado mtu huyo huyo ni mkorofi, ni
mtu mzinzi, mtukanaji, ni mtu wa majivuno n.k…Nilikuwa nipo njia panda
sana inawezekanikaje mtu akawa hivyo na Mungu bado yupo naye.
Nilipojaribu kuwashirikisha baadhi ya watu kwanini jambo hilo linatokea,
wengi wakaniambia wanatumia nguvu za giza. Wanakwenda kwa waganga
kupokea nguvu za kichawi kisha wanakuja madhabahuni kufanya
wanayoyafanya.
Lakini
baada ya kujifunza zaidi, nilikuja kufahamu kuwa wengi wao hawatumii
nguvu za giza hata kidogo. Leo tutajinza kwa kutumia Biblia ni kwanini
hawatumii nguvu za giza.
Ni
kweli wapo ambao wanatumia nguvu za giza kufanya miujiza, lakini hao
hatutawazungumzia kwasasa kwasababu si wengi sana kama wale ambao
hawatumii nguvu za giza.
Tukisoma
biblia tunamwona Nabii mmoja ambaye alikwenda kinyume na maagizo ya
Mungu, kwani aliambiwa baada ya kutoa unabii kwa mfalme Yeroboamu
aondoke na asirudie njia aliyoipitia, na pia asizungumze na mtu njiani.
Lakini ukisoma habari ile utaona alidanganywa na nabii mwenzake
akayaacha maagizo ya Mungu na hivyo ikawa mauti kwake. Hebu tenga muda
usome hichi kisa kwa utulivu kisha tutaendelea.
1 Wafalme 13: 6 “Mfalme akajibu, akamwambia yule mtu wa Mungu, Umsihi sasa Bwana, Mungu wako, ukaniombee, ili nirudishiwe mkono wangu tena. Yule mtu wa Mungu akamwomba Bwana mkono wa mfalme ukarudishwa tena, ukawa kama ulivyokuwa kwanza.
7 Mfalme akamwambia mtu wa Mungu, Karibu nyumbani kwangu ujiburudishe, nami nitakupa thawabu.
8 Mtu wa Mungu akamwambia mfalme, Ujaponipa nusu ya nyumba yako, sitaingia pamoja nawe, wala sitakula chakula, wala sitakunywa maji mahali hapa;
9 maana ndivyo nilivyoagizwa kwa neno la Bwana, kusema, Usile chakula cho chote wala usinywe maji, wala usirudi kwa njia ile uliyoijia.
10 Basi akaenda zake kwa njia nyingine, wala hakurudi kwa njia ile aliyoijia Betheli.
11 BASI NABII MMOJA MZEE alikuwa akikaa katika Betheli; na wanawe wakamwendea wakamwambia kila neno alilolitenda yule mtu wa Mungu siku ile katika Betheli; na maneno aliyomwambia mfalme, hayo nayo walimwambia baba yao.
12 Baba yao akawaambia, Amekwenda zake kwa njia ipi? Kwa maana wanawe walikuwa wameiona njia ile aliyoiendea yule mtu wa Mungu aliyetoka katika Yuda.
13 Akawaambia wanawe, Nitandikieni punda. Wakamtandikia punda, naye akampanda.
14 Akamfuata mtu wa Mungu, akamkuta ameketi chini ya mwaloni, akamwambia, Je! Wewe ndiwe yule mtu wa Mungu aliyetoka katika Yuda? Akamwambia, Mimi ndiye.
15 Akamwambia, Karibu kwangu nyumbani, ule chakula.
16 Naye akamwambia, Siwezi kurudi pamoja nawe, wala kuingia pamoja nawe; wala sili chakula wala sinywi maji pamoja nawe hapa;
17 kwani nimeambiwa kwa neno la Bwana, Usile chakula wala usinywe maji huko, wala usirudi kwa njia ile uliyoijia.
18 Akamwambia, Mimi nami ni nabii kama wewe, na malaika akaniambia kwa neno la Bwana, kusema, Mrudishe pamoja nawe nyumbani kwako, ale chakula, akanywe maji. Lakini alisema uongo.
19 Basi mtu yule akarudi pamoja naye, akala chakula, akanywa maji nyumbani mwake.
20 Hata ikawa, walipokuwa wameketi mezani, neno la Bwana likamjia nabii yule aliyemrudisha;
21 akamlilia yule mtu wa Mungu aliyetoka katika Yuda, akinena, Bwana asema hivi, Kwa sababu umeiasi kauli ya Bwana, wala hukuishika amri ile aliyokuamuru Bwana, Mungu wako,
22 bali umerudi, ukala chakula ukanywa maji, hapo alipokuambia, Usile chakula, wala usinywe maji; maiti yako haitaliingia kaburi la baba zako.
23 Basi ikawa, alipokwisha kula chakula na kunywa maji, yule nabii aliyemrudisha akamtandikia punda.
24 Na alipokuwa amekwenda zake, simba alimkuta njiani, akamwua. Maiti yake ikatupwa njiani, na yule punda akasimama karibu naye; na yule simba naye akasimama karibu na maiti”.
Sasa
kama umeelewa habari hiyo utaona kuwa huyo Nabii Mzee alimdanganya huyo
nabii mwingine…lakini baadaye Mungu akampa maono huyo nabii mzee
amwambie huyo nabii mwingine aliyedanganywa kuwa atakufa kwa kulikaidi
Neno la Mungu.
Sasa
hapo unaweza ukajiuliza kwanini Mungu aendelee kumpa maono Yule nabii
mzee aliyemwambia uwongo mwenzake na kumsababishia mauti..Hiyo
inadhihirisha kuwa MTU ANAWEZA KUONA MAONO na Bado akawa mtenda
dhambi..mtu anaweza kuwa mwongo au mwasherati na bado Mungu akaendelea
kumpa maono. Unaona?..inaogopesha sana!. Huyu nabii Mzee hapa hakutumia
nguvu za giza kumtabiria kuwa atakufa. Hapana bali alitabiri kwa uweza
wa Mungu. Alifanya dhambi kuzungumza uwongo, lakini Mungu hakumpokonya
karama aliyokuwanayo ya kinabii. Na kama hakutubia dhambi hiyo mpaka
kufa basi siku ya hukumu atakwenda kwenye ziwa la moto.
Ndio maana Bwana Yesu alisema..
Mathayo 7: 22 “Wengi wataniambia siku ile, Bwana, Bwana, hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi?
23 Ndipo nitawaambia dhahiri, Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu”.
Hapo
anasema “hatukufanya unabii kwa jina lako?”… ikiwa na maana kuwa sio
kwa nguvu za mapepo bali kwa jina lake…Mfano wa huyo nabii
aliyemdanganya mwenzake na baadaye akamtolea unabii kwa jina la
Bwana…Lakini Bwana Yesu anasema watu wengi wa namna hiyo siku ile
atawafukuza na kuwaambia siwajui kamwe…ondokeni kwangu ninyi mtendao
maovu.
Hivyo
ndugu hapo tunajifunza kuwa, usiangalia karama uliyonayo au mtu
mwingine anayejiita mtumishi aliyonayo…bali jiangalie matendo yako ndipo
ujihukumu kuwa upo sawa na Mungu au la! Usijiangalie karama yako ya
kuimba ukadhani hichi ndicho kinachompendeza Mungu, au karama yako ya
kiualimu, au karama yako ya kunena kwa lugha, au karama yako ya kinabii,
unaona maono mengi mpaka ya kitaifa ukadhani wewe ni spesheli sana kwa
Mungu…badala yake jiangalie ndani yako je! Unayatenda mapenzi ya Mungu
je! Kuna utakatifu ndani yako??.
Unaweza
ukawa kila anayekuja kwako ukimwombea anapona au tatizo lake
linaondoka…au kila anayekuja kwako Bwana anakufunulia tatizo lake kwenye
maono…lakini bado ukawa mbali na Mungu…Unaweza ukawa umetokewa na
malaika au Bwana Yesu mwenyewe lakini siku ile akakwambia sikujui…Mungu
anaweza akawa anaongea na wewe kila siku na kukupa maagizo ya kufanya
hichi na kufanya kile kama alivyompa huyu Nabii Mzee, lakini siku ile
bado akakukataa..Balaamu alikuwa ni nabii anayezungumza na Mungu na
kupokea maagizo kutoka kwa Mungu lakini bado alikuwa ni mchawi.
Biblia inasema wazi katika Waebrania 12:14 kwamba PASIPO UTAKATIFU HAKUNA MTU ATAKAYEMWONA MUNGU.
Hivyo
ni wakati wa kutafuta kuyatenda mapenzi ya Mungu ambao ndio utakatifu,
Na si kuangalia upako wala karama kama uthibitisho wa kuwa Mungu yupo
pamoja na sisi.Ikiwa karama itafuata baada ya utakatifu hiyo ni vizuri
sana. Vile vile si wakati wa kumhukumu mtumishi wa ukweli au wa uwongo
kwa karama anazozidhihirisha..bali tutawatambua kwa matunda yao biblia
inatuambia hivyo (Mathayo 7:16)…na Matunda yanayozungumziwa hapo ni matendo yao…
Bwana akubariki.jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mada Zinazoendana:
NITAIFAHAMU VIPI KARAMA YANGU?
KARAMA YA ILIYO KUU NI IPI?
KARAMA YA MUNGU NI IPI?
JE KUNENA KWA LUGHA MPYA KUKOJE? NA HIZI LUGHA NI ZIPI, NA JE! NI LAZIMA KILA MKRISTO ALIYEPOKEA ROHO MTAKATIFU ANENE KWA LUGHA MPYA?.
Rudi Nyumbani
Print this post