UFUNUO:Mlango wa 8

UFUNUO:Mlango wa 8

Jina la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe.Karibu katika mwendelezo wa kitabu cha Ufunuo, leo kwa Neema za Bwana tutajifunza sura hii ya 8.

Ufunuo 8:1 ‘Hata alipoifungua muhuri ya saba, kukawa kimya mbinguni kama muda wa nusu saa’.

Katika mstari huu wa kwanza, Tunaona Yohana anaanza kwa kuonyeshwa ono la kufunguliwa kwa  Muhuri wa saba. Kwenye mlango wa sita wa kitabu hichi tulishaona ni nini maana ya mihuri, na ilipofunguliwa ni nini kilitokea,kwahiyo kama hujapitia Mlango wa 6, ni vizuri ikaipitia ili tuweze kwenda pamoja katika sura hizi zinazofuata…Lakini kwa ufupi tuliona Muhuri huu wa saba umebeba siri ya Ujio wa Yesu Kristo mara ya pili…Na utatimizwa kipindi kifupi sana kabla ya unyakuo, ambapo ndani ya muhuri huo wa saba tuliona ndio umebeba siri ya zile ngurumo saba zilizozungumziwa katika Ufunuo 10:3 ambazo Yohana aliambiwa asiziandike. Kwa kupitia siri hizo kanisa la Kristo (linalojulikana kama bibi-arusi safi) litapata Imani ya kwenda kwenye unyakuo.

Tukiendelea ni mistari inayofuata biblia inasema…

Ufunuo 8:2 ‘Nami nikawaona wale malaika saba wasimamao mbele za Mungu, nao wakapewa baragumu saba.

3 Na malaika mwingine akaja akasimama mbele ya madhabahu, mwenye chetezo cha dhahabu,akapewa uvumba mwingi, ili autie pamoja na maombi ya watakatifu wote juu ya madhabahu yadhahabu, iliyo mbele ya kiti cha enzi.

4 Na moshi wa ule uvumba ukapanda mbele za Mungu pamoja na maombi ya watakatifu, kutoka mkononi mwa malaika’’.

Hapa tunaona Yohana akioneshwa maono mengine..Aliona Malaika saba wanaosimama mbele za Mungu..wakipewa baragumu saba…Sasa hawa malaika Yohana aliowaona sio malaika wa sifa au makerubi hapana! Bali ni malaika wa hukumu. Na utaona wanapewa baragumu saba…kila mmoja baragumu moja..Maana ya Baragumu ni ‘Mbiu’ kwa lugha ya sasa hivi..Kwahiyo kila mmoja alipewa mbiu yake…Sasa kazi za hizi mbiu ni kutoa sauti ya tukio Fulani la ghafla kuanza au kutokea…Zamani vita ilikuwa Ikisikika baragumu (au mbiu) vitani ni ishara ya kuwa vita vimeanza..au mapambano yameanza, au kuna kitu cha hatari kinakuja…Kwahiyo na hawa malaika wanaonekana hapa wakiwa na baragumu kufunua kuwa watakapopuliza tu basi kuna kitu cha hatari kinafuata.

Lakini katika mstari wa tatu, tunaona Yohana anakatishwa yale maono ya wale malaika saba, anapelekwa kwenye maono mengine anaonyweshwa madhabahu na malaika mwingine tofauti na wale saba, anakuja na chetezo pamoja na uvumba ili autie pamoja na maombi ya watakatifu wote juu ya madhabahu iliyokuwa mbele ya kiti cha enzi.

Sasa uvumba unaashiria maombi ya watakatifu, watakatifu tunapoomba maombi yetu yanaenda kama harufu ya uvumba mzuri mbele za Mungu, Daudi alisema katika Zaburi 141:1-2 ‘’Ee Bwana, nimekuita, unijie hima, Uisikie sauti yangu nikuitapo. Sala yangu ipae mbele zako KAMA UVUMBA, Kuinuliwa mikono yangu kama dhabihu ya jioni.’’..ukisoma pia Ufu.5:8 utaona jambo hilo, kuwa uvumba siku zote unawakilisha maombi ya watakatifu.

Kwahiyo Malaika huyu kazi yake ilikuwa ni kuchukua maombi ya watakatifu wote..kuanzia agano la kale hadi mwisho wa dunia na kuyapeleka mbele za Mungu, na yote yalikuwa yanajibiwa kwa wakati..Lakini sasa hapa mwisho utaona kazi yake ya kupeleka maombi ya watakatifu mbele za Mungu inaisha, na inaishia kwa kukichukua kile ‘chetezo’ na kukiweka makaa ya moto yatokayo madhabahuni na kuyatupa juu ya nchi (yaani duniani). Ikiashiria kuwa hakuna tena huduma ya kupeleka maombi ya watakatifu mbele za Mungu, kwani watakatifu wote wameshaondolewa duniani(katika Unyakuo)…kilichosalia ni hukumu tu.

Yule malaika mara baada ya kumaliza kuvukiza uvumba ule mwingi alichokua moto uliokuwa kwenye madhabahu na kuuweka kwenye chetezo chake na kuumwaga juu ya nchi…chetezo ni kifaa kidogo kilichokuwa kinatumika kuwekea ubani (uvumba)..ambacho ndani yake kinawekwa mkaa

wa moto na ubani na kilikuwa na mkono wa Kamba au mnyororo hivi ambacho kuhani mkuu alikuwa ana uwezo wa kutembea nacho ndani ya hekalu wakati wa kufanya upatanisho, na kinakuwa kinatoa moshi wa ule ubani unaochomeka mule ndani(Kutoka 30:5-9) …Hivyo kuhani alipochoma ubani moshi unatoka kwenye kile chetezo na kukijaza chumba chote moshi wa manukato.

 Ufunuo 8:5 ‘Na huyo malaika akakitwaa kile chetezo, akakijaza moto wa madhabahu, akautupa juu ya nchi, KUKAWA RADI NA SAUTI NA UMEME NA TETEMEKO LA NCHI.6 Na walemalaika saba wenye baragumu saba wakajifanya tayari ili wazipige.’’

Hivyo huyu malaika alipotupa ule moto katika roho duniani kukawa na radi na sauti ya umeme na tetemeko la nchi. Sasa hivyo vitu vitatu, radi, sauti na tetemeko la nchi..Tafsiri yake ndio ipo katika wale Malaika 7 waliopewa baragumu wazipige…, hawa malaika saba ndio walioleta hizo radi, sauti na matetemeko ya nchi, kila mmoja kwa sehemu yake mpaka saba wote walipokwisha kupiga/kupuliza hizo baragumu.

Ufunuo 8:7 inasema:..‘Malaika wa kwanza akapiga baragumu, kukawa mvua ya mawe na moto vilivyotangamana na damu, vikatupwa juu ya nchi; theluthi ya nchi ikateketea, na theluthi ya miti ikateketea, na majani mabichi yote yakateketea’.

Sasa kabla ya kuingia kwenye baragumu ni muhimu kujua kuwa Baragumu hizo zitaanza Kupigwa baada ya unyakuo kupita, yaani baada ya kanisa kunyakuliwa na kwenda mbinguni..wakati ambapo Mpinga-Kristo atanyanyuka duniani, na kwenda kuketi katika Hekalu la Mungu, katika nchi ya Israeli na kutaka kuabudiwa yeye kama Mungu (ukisoma 2Wathesalonike 2:1-10 utaona jambo hilo).

Kumbuka sasa wayahudi/waisraeli wengi leo hii hawamwamini Yesu kama ndiye Masihi, hivyo wengi hawajawa wakristo bado wanashika desturi za Torati ya Musa, huku wakimsubiria Masihi mwingine aje kuwaokoa, Kumbuka ni Mungu mwenyewe ndio kawafumba macho wasimtambue Bwana Yesu kuwa ndiye Masia wa kweli, hivyo mpaka unyakuo unapita watabakia katika hali hiyo hiyo ya upofu, hivyo wataikosa mbingu… 

Lakini Mungu atawahurumia wao tu na kuwafumbua macho baada ya unyakuo kupita Sasa Wakati huo ndio Israeli watagundua kuwa Yesu Kristo waliyemkataa Zaidi ya miaka 2000 iliyopita ndiye Masihi wao waliokuwa wanamtazamia, watatubu ndipo Bwana atawafungua macho..(saa hiyo watu wamataifa walioachwa kwenye unyakuo wataendelea kudanganyika na kupotea) kwasababu kutakuwa hakuna tena mlango wa Neema kwa watu wa mataifa, Zaidi ya kusubiria kuipokea ile chapa ya mnyama na kuingia katika siku ya ghadhabu ya Bwana..na watu wa mataifa kumbuka ni watu wote tofauti na Taifa la Israeli (yaani waafrika, wahindi, wazungu, wachina na wengine wote).

Hivyo baada ya unyakuo kupita Bwana atawatumia mashahidi wake wawili kwa Roho ya Musa na Eliya, kuwarejesha Israeli kwenye mstari na kuihukumu dunia kwa sehemu Fulani…Kwa uelewa Zaidi juu ya urejesho wa Israeli na huduma ya hawa mashahidi wawili…(fungua mfululizo huu katika sura ya 7 na ya 11 au bofya hapa⏩Ufunuo 7&11…soma yote vizuri kisha ndipo uendelee na hapa)…Kwasababu sehemu kubwa ya baragumu hizi saba zinahusu huduma ya hawa mashahidi wawili. Na baragumu hizi saba zitakuwa ni mwanzo wa UTUNGU, wa siku ile kuu ya BWANA..

Sasa tukirudi kwenye zile baragumu biblia inasema…

Ufunuo 8:7 ‘Malaika wa kwanza akapiga baragumu, kukawa mvua ya mawe na moto vilivyotangamana na damu, vikatupwa juu ya nchi; theluthi ya nchi ikateketea, na theluthi ya miti ikateketea, na majani mabichi yote yakateketea’.

Kipindi kifupi sana baada ya unyakuo kupita Bwana atawanyanyua Mashahidi wawili na atawapa amri ya kuipiga dunia kama watakavyo ukisoma katika Ufu.11,utaona hilo, mambo haya yatatekelezwa na mashahidi hawa wawili, kutatokea na mtikisiko katika anga, kutakuwa na matukio ya mvua za mawe, ingawa pia katika roho mvua ya mawe inaashiria kitu kingine..Lakini kutakuwa na vipindi vibaya sana vya mvua ya mawe, kama ile ilivyotokea wakati wa wana wa Israeli walipokuwa Misri, ambayo iliharibu mimea yote na mazao yote ya chakula katika nchi ya Misri, na tunasoma ni Musa ndiye aliyeleta pigo lile kwa amri ya Mungu, na kadhalika katika baragumu la kwanza litakapopigwa wale mashahidi wawili ndio watakaoleta mapigo hayo..

Ufunuo 8:8 ‘Malaika wa pili akapiga baragumu, na kitu, mfano wa mlima mkubwa uwakao moto,

kikatupwa katika bahari; theluthi ya bahari ikawa damu.

9 Wakafa theluthi ya viumbe vilivyomo baharini, vyenye uhai; theluthi ya merikebu zikaharibiwa’’.

Katika pigo hili bado litatekelezwa na hao hao mashahidi wawili, kama vile Musa alivyogeuza maji kuwa damu mbele ya Farao, ndivyo mashahidi hawa wawili watageuza maji kuwa damu mbele ya yule mnyama (Ufu.11:6)..na theluthi ya bahari itakuwa damu…theluthi inayozungumziwa hapo..ni sehemu ndogo ya bahari yaani eneo la mashariki ya kati pale! (Bahari ya Mediterenia na maziwa yaliyo kando kando) Eneo la mashariki ya kati Ndio litakaloathirika na mapigo hayo kwa sehemu kubwa…mahali ambapo yule mnyama atakuwepo, kama vile kipindi cha Farao sio maji yote ya dunia nzima yaligeuzwa kuwa damu hapana isipokuwa ni yale tu ya Misri, ndivyo itakavyokuwa siku hizo,watu wote waliopo mashariki ya kati, maji yatageuka kuwa damu.Na samaki watakufa na shughuli za usafirishaji zitasimama…Huo ni mwanzo wa utungu tu wa hukumu ya Mungu itakayoijilia dunia nzima,

Katika siku za mwisho mara baada ya baragumu kuisha vitakuja vitasa saba, ambavyo hivyo ndio vinabeba hukumu ya Mungu katika utimilifu wote, ndani ya hivyo vitasa sana, maji yote ya dunia nzima yatageuzwakuwa damu, na chemichemi haitakuwa theluthi tena kama tunavyoona hapa katika baragumu hizi.
Tuendelee..

Ufunuo 8:10 ‘Malaika wa tatu akapiga baragumu, nyota kubwa ikaanguka kutoka mbinguni, iliyokuwa ikiwaka kama taa, ikaanguka juu ya theluthi ya mito, na juu ya chemchemi za maji. 

11 Na jina lake ile nyota yaitwa Pakanga; theluthi ya maji ikawa pakanga, na wanadamu wengi wakafa kwa maji hayo, kwa kuwa yalitiwa uchungu’.

Nyota inayozungumziwa hapa sio kimondo..kwasababu haiwezekani kimondo kimoja kiangukie mito yote na chemchemi zote za maji…Nyota inayozungumziwa hapo ni ‘shetani’ yeye ndiye nyota iliyoanguka kutoka mbinguni..Na kwasababu yake yeye mito na bahari na nchi vimepigwa na vinapigwa kwa laana ya Mungu…Ndio maana ukisoma kwenye kitabu cha ufunuo 12:12, utaona inasema… ‘ Kwa hiyo shangilieni, enyi mbingu, nanyi mkaao humo. Ole wa nchi na

bahari! Kwa maana yule Ibilisi ameshuka kwenu mwenye ghadhabu nyingi, akijua ya kuwa ana

wakati mchache tu’.

Unaona hapo anasema ole wa nchi na bahari, ikimaanisha kuwa kuanguka kwa shetani duniani, bahari itaathirika pia, itageuka kuwa damu, na maji kuwa machungu na

katika pigo hili…la Baragumu ya tatu…Bwana ataipiga mito na chemichemi za maji..Maji yatatiwa uchungu..kama yale wana wa Israeli waliyokutana nayo mahali palipoitwa ‘mara’

Kutoka 15: 22 ‘’Musa akawaongoza Israeli waende mbele kutoka Bahari ya Shamu, nao wakatokea kwa jangwa la Shuri; wakaenda safari ya siku tatu jangwani wasione maji. 

23 Walipofika mahali palipoitwa Mara hawakupata kuyanywa yale maji ya Mara, kwa kuwa yalikuwa machungu; kwa ajili ya hayo jina lake likaitwa Mara.

 24 Ndipo watu wakamnung’unikia Musa,wakisema, Tunywe nini?’’

Watu wengi wanaokaa katika mashariki ya kati na baadhi ya maeneo duniani..watateseka, lakini pigo hili halitauwa la dunia nzima. 

Ufunuo 8: 12 ‘’Malaika wa nne akapiga baragumu, theluthi ya jua ikapigwa, na theluthi ya mwezi, na theluthi ya nyota, ili kwamba ile theluthi itiwe giza, mchana usiangaze theluthi yake, wala usiku vivyo hivyo’’.

Unazidi kuona, bado ni theluthi inayopigwa sio kitu kizima…Ikifunua kuwa ni mwanzo tu wa Utungu! Itafika wakati sio theluthi tena itakayopigwa bali yote…Malaika huyu wanne alipopuliza baragumu lake, Jua theluthi ya jua ikapigwa…na mwezi, na kama tunavyofahamu jua likipungua nguvu kitu gani kitatokea…ni wazi kuwa kutakuwa na baridi isiyokuwa ya kawaida na baadhi ya shughuli zitasimama…Ndicho kitakachotokea siku hiyo, watu wataona jua limepungua nguvu sasa hapa dunia nzima itaathirika na pigo hili…Na hiyo Itatangaza kuwa kipindi kifupi sana baadaye jua lote litazima..kama tutakavyojifunza tutakapofika kwenye vitasa saba katika Ufunuo mlango wa 16.

Ufunuo 8:13 “Kisha nikaona, nikasikia tai mmoja akiruka katikati ya mbingu, akisema kwa sauti kuu, Ole, ole, ole wao wakaao juu ya nchi! Kwa sababu ya sauti zisaliazo za baragumu za malaika watatu, walio tayari kupiga”.

Hapa Yohana anaoneshwa Tai akiruka katikati ya mbingu, sasa huyu Tai sio ndege tai, bali ni mmoja wa malaika anayebeba tabia kama za Tai katika roho, ukisoma kwenye tafsiri nyingine utaona ni ‘’angel’’ yaani malaika ndio maana utaona hata Katikati ya wale wenye uhai wanne kulikuwa na mmoja mwenye uso kama wa Tai.

Sasa Malaika huyu Yohana alimwona katika roho akisema…ole wao wakaao juu ya nchi! Kwasababu ya sauti za baragumu za malaika watatu waliobakia..Ikifunua kuwa madhara yatakayoletwa kwa baragumu za hao malaika watatu waliosalia yatakuwa mabaya zaidi ya hao wanne waliotangulia.

Na kama tunavyosoma hapo, inasema ole wakaao juu ya nchi!!…Ikifunua kuwa ni madhara yatakayosababishwa na kuanguka kwa shetani, yatakuwa juu ya hao wakaao juu ya nchi kulingana na ufunuo 12:12 “Ole wa nchi na bahari! Kwa maana yule Ibilisi ameshuka kwenu mwenye ghadhabu nyingi, akijua ya kuwa ana wakati mchache tu’’…Madhara juu ya bahari yameshapita…theluthi ya bahari, chemichemi na mito kuwa damu, na viumbe vya majini kufa…sasa yanayofuata ni kwa wale wakaao juu ya nchi..Tutayaona hayo zaidi katika sura inayofuata..

Swali ni je! Umempa Kristo maisha yako?..Una uhakika akija leo utakwenda naye mbinguni?, kama hauna uhakika basi ni wazi kuwa utaachwa akija, kwahiyo utii ushauri wake leo unaosema…

Ufunuo 3:18 “Nakupa shauri, ununue kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto, upate kuwa tajiri, na mavazi meupe upate kuvaa, aibu ya uchi wako isionekane, na dawa ya macho ya kujipaka macho yako, upate kuona.

19 Wote niwapendao mimi nawakemea, na kuwarudi; basi uwe na bidii, ukatubu.

20 Tazama, nasimama mlangoni, nabisha; mtu akiisikia sauti yangu, na kuufungua mlango, nitaingia kwake, nami nitakula pamoja naye, na yeye pamoja nami”.

Mfungulie mlango wa moyo wako leo kwa kutubu na kumaanisha kuziacha dhambi zako na yeye atakupokea…Toka kwenye kamba za madhehebu ambazo zinakufungia mlango wa maarifa na kukufanya usimjue Mungu kama anavyotakiwa kumjua.

Bwana akubariki sana..Kwa Mwendelezo >>>Ufunuo: Mlango wa 9

Ikiwa utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara,  kwa njia ya whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255789001312. Na kama utapenda kwa njia ya E-mail basi tuandikie email yako katika boksi la maoni chini. jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Zinazoendana:

KUFUKIZA UVUMBA NDIO KUFANYAJE?

NINI MAANA YA KUTOKA KATIKA MADHEHEBU?

UMEPATA UHAKIKA WA KUTOKUINGIA HUKUMUNI KATIKA SIKU ILE?

ALIPO NA ATAKAPOKUWEPO BIBI-ARUSI WA YESU KRISTO.


Rudi Nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments