Ipi tofauti kati ya maasi na maovu?

by Admin | 22 May 2024 08:46 pm05

Swali: Kuna tofauti gani ya kufanya maasi na kufanya maovu?


Jibu: Maovu ni mambo yote mabaya mtu anayoyafanya yaliyo kinyume na Mungu, na haya yanatokana na shetani (ndio maana anajulikana kama Mwovu, Mathayo 5:37)…mfano wa maovu ni mauaji, uasherati, dhuluma, wizi, ulawiti, ufiraji, ibada za sanamu na mambo mengine yanayofanana na hayo..

Lakini “Maasi” ni mabaya yote yanayofanywa na watu waliokuwa ndani ya Imani kisha wakatoka!!!. (kwa ufupi ni maovu ya watu waliokwisha kumjua Mungu).

Maana yake kama mtu alikuwa ndani ya Imani, na baadaye akakengeuka na kuisaliti ile Imani au kurudi nyuma kwa kuanza kufanya mambo mabaya… basi mambo hayo maovu ayafanyayo ndiyo yanayoitwa MAASI.

Mtu wa kidunia ambaye hajamjua Mungu bado, huyo hawezi kufanya MAASI!.. Kwasababu hakuna ALICHOKIASI!... Mpaka mtu afanye Maasi ni lazima awe AMEASI!..Sasa mtu ambaye hajamjua Mungu anakuwa anafanya MAOVU tu na si MAASI.. lakini akishamjua Mungu na akamwacha Mungu na kurudia maovu aliyokuwa anayafanya,.. basi yale maovu ayafanyayo ndiyo yanayoitwa MAASI.

Na watu wanaofanya Maasi wana hukumu kubwa kuliko wanaofanya Maovu, kwasababu tayari walishamjua Mungu na kisha wakamwacha kwa kurejea nyuma. Mfano wa watu waliokuwa wanatenda MAOVU na si MAASI katika biblia ni watu wa Sodoma na Gomora.

Mwanzo 19:15 “Hata alfajiri ndipo malaika wakamhimiza Lutu, wakisema, Ondoka, mtwae mkeo na binti zako wawili waliopo hapa, usipotee katika MAOVU YA MJI HUU.”

Na mfano wa watu waliokuwa wanafanya MAASI ni wana wa Israeli (kwasababu walikuwa walianza na Mungu lakini wakakengeuka baadaye)

Yeremia 3:22 “21 Sauti inasikiwa juu ya vilele vya milima, ni kulia kwao na maombi yao wana wa Israeli; kwa kuwa wameipotosha njia yao, wamemsahau Bwana, Mungu wao.

22 RUDINI, ENYI WATOTO WAASI, mimi nitaponya maasi yenu. Tazama, tumekuja kwako; maana wewe u Bwana, Mungu wetu.”

Na katika siku za mwisho biblia inatabiri KUONGEZEKA KWA MAASI!.. Maana yake watakaokuwa wanarudi nyuma na kuisaliti imani na kufanya vitu kwa makusudi watakuwa ni wengi kuliko wale walio wa kudunia wafanyao maovu pasipo kuijua njia ya kweli.

Mathayo 24:12 “Na kwa sababu ya KUONGEZEKA MAASI, upendo wa wengi utapoa”.

Kwahiyo kwa hitimisho ni kwamba “Maasi” ni “Maovu” yanayofanywa na watu waliorudi nyuma au waliomwacha Mungu!… Na watendao MAASI wana hukumu kubwa Zaidi ya watendao Maovu tu.. kwasababu wameyajua mapenzi ya Bwana wao halafu wakaasi.

Luka 12:47 “Na mtumwa yule aliyejua mapenzi ya bwana wake, asijiweke tayari, wala kuyatenda mapenzi yake, atapigwa sana.

48  Na yule asiyejua, naye amefanya yastahiliyo mapigo, atapigwa kidogo. Na kila aliyepewa vingi, kwake huyo vitatakwa vingi; naye waliyemwekea amana vitu vingi, kwake huyo watataka na Zaidi”.

Ukitoa mimba na huku unamjua KRISTO na unasema umeokoka ni UASI, ukiiba na huku unajua kabisa wizi ni dhambi na tena unajiita Mkristo huo ni UASI, ukifanya uzinzi na unasema umeokoka wewe ni Muasi, ukiabudu sanamu na huku unajua kabisa si sawa kufanya hivyo ni Uasi!..Na roho ya kuasi ni ROHO YA MPINGA KRISTO! (2Thesalonike 2:7).

Bwana atusaidie tusiwe WAASI wala tusifanye MAASI baada ya kumjua yeye, bali tudumu katika ukamilifu na utakatifu katika Roho wake Mtakatifu.

Lakini ikiwa wewe bado haujaokoka fahamu kuwa pia MAOVU yako uyafanyayo hayatakufikisha popote, mwisho wake ni katika ziwa la Moto..

Ni heri ukayasalimisha maisha yako kwa BWANA YESU ili akusafishe na kukupa uzima wa milele.

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

MUNGU HAJARIBIWI NA MAOVU BALI MEMA.

IMANI “MAMA” NI IPI?

SI MAPEPO YOTE NI YA KULIPUKA.

Je Adamu na Hawa, walikuwa hawafanyi mema kabla ya kula tunda?

MAMBO (2) YATAKAYOKUTENGA NA IMANI SIKU HIZI ZA MWISHO.

Rudi Nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2024/05/22/ipi-tofauti-ya-maasi-na-maovu/