Kuja kwa Bwana duniani kulikuwa kwa kitofauti sana, wakati ambapo Israeli ilimtazamia aje kipindi ambacho uzao wa Daudi unaonekana wazi kwa wafalme waliokuwa wanatawala Yuda zamani za wafalme. Lakini yeye hakutokea hicho kipindi, walipotazamia labda pengine angetokea wakati ambapo wamerudishwa kutoka Babeli lakini hakuonekana hata katika hicho kipindi, wengine walizani utawala wa Umedi hautaisha hata ajapo lakini hakutokea pia ndani ya utawala ule mpaka ulipoisha, Wengine walitazamia labda ingekuwa ni katika utawala wa Uyunani, lakini hata huo nao hakutokea, mpaka ulipoanza utawala mwingine mpya uliojulikana kama Rumi ya kipagani, na ndipo akaja kuzaliwa mwokozi wa ulimwengu Bwana Yesu Kristo, Ni siku ambazo Israeli tayari imeshapoa sana, siku ambazo Israeli tayari imeathiriwa na tamaduni za kigeni za kipagani , siku ambazo Israeli imeshasahau hata kama kuna masihi mkombozi wao anayetakiwa kuja isipokuwa kwa wayahudi wachache tu ndio waliokuwa wanamtazamani, lakini taifa lote lilishalala na ndio maana hata siku ile Mamajusi kutoka mashariki walipoleta taarifa za kuzaliwa mfalme wa wayahudi, biblia inasema habari zile sio tu zilimfadhaisha Herode peke yake bali na Yerusalemu yote pia. Alishuka wakati viwango vya maovu katika Israeli na dunia nzima vipo juu, Bwana alikiita kizazi kile, kizazi cha zinaa na uzinzi , Lakini huo ndio wakati Mungu aliouchagua kumleta mwanae duniani.