VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 11 (Mithali, Wimbo ulio bora, Mhubiri)

VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 11 (Mithali, Wimbo ulio bora, Mhubiri)

Karibu tujifunze biblia, Neno la Mungu wetu, ambalo ndio taa iongozayo miguu yetu, na mwanga wa njia yetu. Tumekwisha kuvipitia vitabu 20 vya mwanzo, hivyo kama hujavipitia basi ni vyema ukavipitia kwanza, ili tuweze kwenda pamoja katika vitabu hivi vinavyofuata.

Leo tutavitazama vitabu vitatu vya mbele, ambavyo ni Mithali, Mhubiri na Wimbo ulio bora. Vitabu hivi vitatu vimeandikwa na mtu mmoja anayeitwa Sulemani, katika majira tofauti tofauti. Kitabu cha Mithali na Wimbo ulio bora viliandikwa na Sulemani katika kipindi cha ujana wake, lakini kitabu cha Mhubiri alikiandika karibia na mwisho wa maisha yake. Hivyo leo tutakitazama kimoja baada ya kingine. (Lakini pia kabla ya kwenda kuvitazama ni vyema ukaavipitia wewe mwenyewe binafsi, ndipo uufuatilie ufupisho huu)

  1. Kitabu cha Mithali:

Kitabu cha Mithali kama tulivyosema ni kitabu kilichoandikwa kwa sehemu kubwa na Mfalme Sulemani na alikiandika katika ujana wake.. Zipo sehemu chache za kitabu hicho zilizoandikwa na Mtu aliyeitwa Aguri, na mfalme Lemueli (Mithali 30 na Mithali 31), lakini Kwingine kote kuliandikwa na Mfalme Sulemani.

 Ikumbukwe kuwa Sulemani, alimwomba Mungu hekima badala ya mali, na hivyo Mungu akampa vyote viwili, hekima pamoja na Mali ambazo hakuziomba (1Wafalme 3:11). Na hekima ni neno la kiujumla lenye maana ya “akili, na uwezo wa kupambanua mambo”. Na kuna hekima ya kiMungu na hekima ya kiulimwengu!. Sulemani alipewa hekima zote mbili! (Za kiMungu na za kiulimwengu).

Hekima za Kiulimwengu, zinamwezesha mtu aweze kuishi maisha ya mafanikio katika huu ulimwengu! Jinsi ya kutumia malighafi za ulimwengu huu, kufanikisha mambo yake. Kwamfano  watu waliogundua gari, au ndege, au simu wametumia hekima ya kiulimwengu kugundua vitu hivyo, ili viwasaidie katika changamoto za usafiri, na mawasiliano, kadhalika walioweka Methali kama “Asiyefunza na mamaye hufunzwa na ulimwengu” au “asiyesikia la mkuu, huvunjika guu” au “mtoto akililia wembe,mpe umkate”.. wametumia hekima za kibinadamu kujiwekea tahadhari wao na watoto wao, kiasi kwamba mtu yeyote akiisikia hiyo hekima na kuitii basi hatafunzwa na ulimwengu!. Sasa hekima kama hiyo sio hekima ya kiMungu, bali ya kiulimwengu lakini ina ukweli ndani yake.

Kwahiyo Mfalme Sulemani alipewa hekima za aina zote mbili (za KiMungu na za kiulimwengu). Ni muhimu kuufahamu huu msingi kwasababu, utatusaidia huko mbele kuelewa kwanini Sulemani alisema hekima zilimpoteza…(kwamba hazikuwa za kiMungu zilizompoteza bali za kiulimwengu).

Hivyo kwa akili nyingi Sulemani alizopewa na Mungu aliweza kutazama watoto, akatunga mithali za kidunia na kiMungu kuwahusu wao, vile vile aliweza kutazama watu wazima na wazee akatunga mithali kuhusu wao, kadhalika aliweza kutazama wafanya biashara akaweza kutunga mithali na kutunga mashauri kuwahusu wao na vile vile aliweza kutazama maisha ya watu waovu na wema, wapumbavu na werevu, pamoja na viumbe kama wanyama na miti, akatunga mithali juu ya hivyo vyote na akawapa wana wa Israeli wazitumie katika kuendesha maisha yao..

1Wafalme 4:29 “Mungu akampa Sulemani hekima, na akili nyingi sana, na moyo mkuu, kama mchanga ulioko pwani.

 30 Hekima ya Sulemani ikapita hekima ya wana wote wa mashariki, na hekima zote za Misri.

 31 Kwa kuwa alikuwa na hekima kuliko watu wote; kuliko Ethani Mwezrahi, na Hemani, na Kalkoli, na Darda, wana wa Maholi; zikaenea sifa zake kati ya mataifa yote yaliyozunguka.

 32 Naye akanena mifano elfu tatu, na nyimbo zake zilikuwa elfu moja na tano.

 33 Akanena habari za miti tangu mwerezi ulioko Lebanoni hata hisopo umeao ukutani; pia akanena habari za wanyama, na za ndege, na vitambaavyo, na samaki.

34 Wakaja wa mataifa yote ili waisikie hekima ya Sulemani, toka wafalme wote wa ulimwengu, waliokuwa wamepata habari za hekima yake”

Sasa kwa uwezo huo Mungu aliompa Sulemani na akili hizo, alijikuta anaweza kufanya biashara na kufanikiwa sana kwasababu alipewa akili za jinsi ya kuendesha biashara na zikafanikiwa, (Hicho ndio kilikuwa chanzo cha utajiri wa Sulemani), biblia inasema Sulemani alifanya biashara sana… Alifahamu siri nyingi za jinsi ya kufanya biashara na kufanikiwa!, mpaka wafalme wa dunia wakawa wanamfuata kutaka kujua anafanyaje fanyaje mpaka anafanikiwa…(hakuwa amekaa tu! Na kujikuta mali zinamjia, hapana bali alikuwa ni mtu mwenye uwezo mkubwa wa akili wa jinsi ya kutafuta mali).

1Wafalme 10:22 “Kwa kuwa mfalme alikuwa na merikebu za Tarshishi baharini pamoja na merikebu za Hiramu; mara moja katika miaka mitatu huja merikebu za Tarshishi, zikileta dhahabu, na fedha, na pembe, na nyani, na tausi.

23 Basi mfalme Sulemani akawapita wafalme wote wa duniani kwa mali, na kwa hekima.

24 Ulimwengu wote ukamtafuta Sulemani uso wake, ili waisikie hekima yake, Mungu aliyomtia moyoni.  25 Wakaleta kila mtu zawadi yake, vyombo vya fedha, na vyombo vya dhahabu, na mavazi, na silaha, na manukato, na farasi, na nyumbu, hesabu yake ya mwaka kwa mwaka.

26 Sulemani akakusanya magari na wapandao farasi; naye alikuwa na magari elfu na mia nne, na wapandao farasi kumi na mbili elfu, aliowaweka katika miji ya magari, na pamoja na mfalme huko Yerusalemu.

 27 Mfalme akafanya fedha humo Yerusalemu kuwa kama mawe, na mierezi akaifinya kuwa kama mikuyu iliyomo Shefela, kwa kuwa mingi.

28 Nao farasi aliokuwa nao Sulemani wakaletwa toka Misri; wakapewa wafanya biashara wake mfalme kwa makundi, kila kundi na thamani yake.

29 Tena gari huja kutoka katika Misri kwa shekeli mia sita za fedha, na farasi mmoja kwa mia hamsini; vivyo watu wakawaletea wafalme wote wa Wahiti, na wafalme wa Shamu, mikononi mwao”.

Vile vile Sulemani alikuwa na akili nyingi za “Jinsi ya kushinda vita”. Tofauti na wafalme wengine ambao jambo kidogo tu likizuka suluhisho ni kwenda vitani!.. Sulemani hakuwa hivyo, aliweza kutatua mambo kwa hekima tu!..Hivyo ikamfanya kuwa Mfalme katika Israeli ambaye hakuwahi kwenda vitani kupigana pigana hovyo!, hivyo uchumi wake ukastawi na watu wake!. Baba yake Daudi hakuwa na hiyo hekima!, yeye lolote likitokea kwamba maadui zake wamepanga vita, basi na yeye alipanga vita!, pasipo kufikiri sana njia mbadala ya kuvimaliza hivyo vita. Lakini Sulemani Mungu alimpa hiyo hekima..hakupigana vita katika ufalme wake wote na aliishi kwa amani.

Vile vile hakupungukiwa chakula wala mifugo, kwasababu alikuwa na akili za jinsi ya kuiongeza hiyo mifugo. Na aliyatimiza malengo yake hayo kwa kuwalazimisha watu wake kufanya kazi kwa nguvu (Israeli hawakupumzika), walifanyishwa kazi sana. (1Wafalme 12:4),

Kwa muhtasari huo basi, tutakuwa tumeshaanza kujua ni nini kimeandikwa katika kitabu cha MITHALI. Kwamba ni kitabu kilichojaa hekima za kiMungu na hekima za kidunia.

Hivyo tunaweza kukigawanya kitabu cha Mithali katika makundi hayo mawili.

  1. Mifano ya hekima za kiMungu, zilizoandikwa na Sulemani ndani ya kitabu cha Mithali

Mithali 1:7“Kumcha Bwana ni chanzo cha maarifa, Bali wapumbavu hudharau hekima na adabu”.. Mithali kama hii haiwezi kukubaliwa na wenye hekima ya ulimwengu huu…

Mithali 18:10 “Jina la Bwana ni ngome imara; Mwenye haki huikimbilia, akawa salama”.

Soma pia Mithali 19:23, Mithali 16:5, Mithali 3:11 n.k

  1. Mifano ya hekima za kiulimwengu, Sulemani alizoziandika ingawa zina ukweli ndani yake ni kama ifuatavyo..

Mithali 5:6 “Ewe mvivu, mwendee chungu, Zitafakari njia zake ukapate hekima.

 7 Kwa maana yeye hana akida, Wala msimamizi, wala mkuu,

 8 Lakini hujiwekea akiba ya chakula wakati wa jua; Hukusanya chakula chake wakati wa mavuno.

 9 Ewe mvivu, utalala hata lini? Utaondoka lini katika usingizi wako?

Mithali12: 27 “Mtu mvivu hapiki mawindo yake; Bali mwenye bidii anazo mali za thamani”

Mithali 18:18 “Kura hukomesha mashindano; Hukata maneno ya wakuu”

Mithali 19: 7 “Ndugu zote wa maskini humchukia; Jinsi gani rafiki zake huzidi kujitenga naye! Huwafuata kwa maneno, lakini wametoweka”

Mithali 27: 7 “Nafsi iliyoshiba hukinai sega la asali; Bali nafsi yenye njaa huona kila kitu kichungu kuwa kitamu”.

Soma pia Mithali 26:13, Mithali 26:20 n.k

Ni jambo gani tunajifunza katika kitabu cha Mithali?

Jambo kuu na la kwanza tunalojifunza ni hekima za KiMungu, ambazo zinatupeleka moja kwa moja kumpenda Mungu, kumtafuta, na kumtumikia. Kadhalika pia tunajifunza hekima za kidunia, ambazo zitatusaidia katika maisha yetu ya hapa duniani, hayo ndiyo mambo mawili makuu, tunayoweza kujifunza katika kitabu hichi.

  1. KITABU CHA WIMBO ULIOBORA.

Kama jina lake lilivyo “wimbo ulio bora”.. maana yake kuna nyimbo nyingi..lakini upo ulio bora!.. Zamani na hata sasa, nyimbo zilitungwa kwa lengo pia la kufikisha ujumbe!.. Na mara nyingi nyimbo zinakuwa ni jambo fulani la kama igizo lakini limebeba ujumbe Fulani ndani yake.. Sasa Sulemani alitunga nyimbo nyingi, biblia inasema alitunga nyimbo elfu moja na tano (1005), zinazohusu miti, mimea, maisha ya watu (soma 1Wafalme 4:30) lakini katika hizo zote, alikuwa na wimbo mmoja ambao aliuona ni bora kuliko mwingine wote.. Na huo ndio tunaousoma katika kitabu hicho cha Wimbo ulio bora.. (Ni wimbo unaomhusu Mtu na Mpenzi wake).

Hata sasa nyimbo zinazoonekana ni bora na watu wa kidunia ni nyimbo zinazohusu mahusiano zinazidi sana nyimbo za kawaida za kuelimisha au za Taifa. Kwanini?…kwasababu shetani naye anajua “wimbo ulio bora”

Hivyo kitabu cha Wimbo ulio bora ni kitabu chenye mashairi na Mwanaume mmoja, anayemsifia mke wake (yaani bibi arusi wake), na vile vile bibiarusi anamsifia mume wake.. kwa ufupi ni kitabu chenye mpangilio wa mashairi na majibizano, baina watu wawili, mume na mke. Na kimegawanyika katika sehemu kuu tatu. (Uchumba, ndoa changa na Ndoa iliyokomaa).

Kuanzia Mlango wa 1-3, inazungumzia mazungumzo ya wapenzi hao wakiwa bado katika hatua ya uchumba, Kuanzia Mlango wa 3 hadi wa 5, ni mazungumzo ya wapenzi hao wawili wakiwa tayari ndani ya ndoa, na kuanzia Mlango wa 5-8 ni Mazungumzo ya wapenzi hao wakiwa katika kilele cha ndoa yao.

Kitabu hichi kwa namna ya kimwili kinahubiri sana sana upendo kwa wana-ndoa, Maana yake watu waliofunga ndoa, kitabu hichi kimejaa maonyo na mafundisho kuwahusu wao(Jinsi inavyowapasa kupendana na kutunzana). Vile vile kimejaa maonyo na mashauri kwa watu ambao bado hawajaingia kwenye ndoa..kwamba wasiyaamshe mapenzi wala kuyachochoe mpaka wakati wake utakapofika.

Wimbo 2:7 “Nawasihi, enyi binti za Yerusalemu, Kwa paa na kwa ayala wa porini, Msiyachochee mapenzi, wala kuyaamsha, Hata yatakapoona vema yenyewe”.

Mbali na mafunzo tunayoyapata kuhusu wana ndoa na wale ambao hawayaingia bado kwenye ndoa, Mungu aliruhusu pia kitabu hiki kiwepo miongoni mwa vitabu vya biblia, na kiitwe wimbo uliobora kwasababu katika roho pia Kuna wimbo ulio bora ambao Mungu analiimbia kanisa lake!!, na kanisa vile vile kanisa linamwimbia yeye.

Ikumbukwe kuwa katika roho kanisa la Yesu linafananishwa na bibiarusi, na Kristo ndiye Bwana arusi mwenyewe..(soma 2Wakorintho 11:2, Ufunuo 21:9, Yohana 3:29), Kwahiyo upo wimbo unaoimbwa katika roho sasa, wimbo wa Bwana arusi kumrejesha mkewe, Bwana anawaita watu wake sasa, kwa sauti ya upole, na ya upendo kwa mashairi mazuri, anawaita watu katika hatua zote tatu…(hatua kabla ya kumpokea yeye, hapo ndio pale Bwana anamtumia mtu wahubiri wa kumvuta kwake, na mtu Yule anapotii, basi Bwana anakwenda naye katika hatua ya pili ya ndoa, hapo ndio pale mtu anapoamua kumpokea Yesu kama Bwana na mwokozi wa maisha yake na kubatizwa na kupokea Roho Mtakatifu, na baada ya hatua hiyo, Mungu anamwongoza katika hatua nyingine ya mwisho ya kukua kiroho..

Ni nini tunajifunza katika kitabu cha Wimbo ulio bora?

Cha kwanza ni kwamba sisi (kanisa) tuliompokea tunafananishwa na bibi-arusi wa Yesu, na kama ni bibiarusi maana yake hatupaswi kuudharau wito wake, unapotuita…ambao umekuwa kama wimbo kwetu!..vile vile tunapaswa tuushikilie wokovu na kudumu katika huo, kwasababu uhusiano wetu na Mungu wetu hauishii tu katika kumwamini, bali pia katika kudumu katika imani(ndio kudumu katika ndoa)….na hatupaswi kufanya uasherati, ukifanya uasherati wa kiroho kwa kumwacha Mungu na kwenda kuabudu miungu mingine, tukifanya hivyo basi tunamtia Bwana wivu..na wivu wa kimahusiano ni mbaya kuliko mwingine wowote ule.. kama yeye mwenyewe alivyosema

Wimbo 8: 6 “…Kwa maana upendo una nguvu kama mauti, Na wivu ni mkali kama ahera. Mwako wake ni mwako wa moto, Na miali yake ni miali ya Yahu”.

Pia tunajifunza kuwa na upendo na kuwa waaminifu kwa wapenzi wetu, tuliofunga nao ndoa!..

Na mwisho kitabu hichi kinawafunza wale ambao bado hawajaingia kwenye ndoa!, kwamba wasiyachochee mapenzi, kuyachochea mapenzi ni pamoja na kutazama picha chafu (pornography), kutazama filamu za kidunia ambazo nyingi sehemu kubwa zina maudhui ya mapenzi, vile vile kuzungumza mazungumzo machafu na kuwa na kampani ya watu ambao muda wote mada zao ni uasherati, hivyo ndio baadhi ya vichocheo vya mapenzi, ambavyo mwisho wake ni kuanguka katika uasherati na uzinzi.

  1. KITABU CHA MHUBIRI

Hichi ndio kitabu cha mwisho kilichoandikwa na Sulemani. Sulemani alikiandika kitabu hichi katika uzee wake..na ni kitabu cha hitimisho na kutoa jumla ya mambo yote!.. baada ya yeye kujaribu mambo yote, kuzipima hekima zote za kidunia, kufanya biashara nyingi na kufanikiwa, kujiongezea mali nyingi kuliko watu wote waliotangulia…mwisho wa siku anakuja na hitimisho!..na hitimisho hilo analiandika kama mahubiri!.. Anawahubiri wana wa Israeli.. anasema..

Mhubiri 1:1 “Maneno ya Mhubiri mwana wa Daudi, mfalme katika Yerusalemu.

 2 Mhubiri asema, Ubatili mtupu, ubatili mtupu, mambo yote ni ubatili.

3 Mtu ana faida gani ya kazi yake yote aifanyayo chini ya jua”

Anaendelea kwa kusema..

Mhubiri 1:12 “Mimi, Mhubiri, nalikuwa Mfalme wa Israeli katika Yerusalemu.

13 Nikatia moyo wangu ili kuyatafuta yote yanayotendeka chini ya mbingu, na kuyavumbua kwa hekima; ni taabu kubwa ambayo Mungu amewapa wanadamu, ili kutaabika ndani yake.

14 Nimeziona kazi zote zifanywazo chini ya jua; na, tazama, MAMBO YOTE NI UBATILI NA KUJILISHA UPEPO.

15 Yaliyopotoka hayawezi kunyoshwa, Wala yasiyokuwapo hayahesabiki.

16 Nikatafakari nikisema, Nimejipatia hekima nyingi kupita wote walionitangulia katika Yerusalemu; naam, moyo wangu umeona kwa wingi hekima na maarifa.

17 Nikatia moyo wangu ili kuijua hekima, na kujua wazimu na upumbavu; nikatambua ya kwamba hayo yote nayo ni kujilisha upepo.

18 YAANI, KATIKA WINGI WA HEKIMA MNA WINGI WA HUZUNI, Naye aongezaye maarifa huongeza masikitiko”.

Ukikitafakari kwa makini maneno hayo, utaona ni maneno ya kama mtu ambaye alikuwa anatamani jambo Fulani sana, kisha akalipata hilo jambo, halafu mwisho wa siku akaja kuliona kuwa si la maana sana kama alivyolitazamia!..

Kama tulivyojifunza mwanzo Sulemani alipewa hekima ya kiMungu na pia ya kidunia, hivyo kwa akili zake nyingi aliweza kuvumbua njia nyingi za kufanya biashara, na kufanikiwa.. akawa mwanauchumi mkubwa mpaka watu wa mataifa mengine wakaja kutaka kujua siri ya mafanikio yake, hata akapendwa na wanawake wengi wa kiulimwengu, na yeye pia akawapenda, na mwisho wa siku wakaja kumgeuza moyo,.. hivyo hekima za kidunia zikampotosha Sulemani, hata akamsahau Mungu na kusahau kufanya mema.. akazitumainia hekima zake za kidunia.

 Lakini alipokuwa mzee akagundua kuwa siku moja atakufa!, na mwingine atakuja kuvirithi hivyo vyote!.. na kama akifa na huku moyoni mwake hana utajiri kwa Mungu!.. ni sawa na kazi bure!..ni kujilisha upepo tu!!..hakuna faida yoyote ya yeye kuwa na kila kitu halafu anakuwa hajajaa mema??

Mhubiri 2:1 “Nikauambia moyo wangu, Haya, nitakujaribu kwa njia ya furaha basi ujifurahishe kwa anasa. Na tazama, hayo nayo yakawa ubatili.

 2 Nikasema juu ya kicheko, Ni wazimu; na juu ya furaha, Yafaa nini?

3 Moyoni mwangu nikapeleleza jinsi ya kuuburudisha mwili kwa mvinyo, na (moyo wangu ukali ukiniongoza kwa hekima) jinsi ya kushikana na upumbavu, hata niyaone yaliyo mema ya kuwafaa wanadamu, ili wayafanye hayo chini ya mbingu siku zote za maisha yao.

 4 Nikajifanyizia kazi zilizo kubwa; nikajijengea nyumba; nikajipandia mashamba ya mizabibu;

 5 nikajifanyizia bustani na viunga, na kuipanda humo miti yenye matunda ya kila namna;

 6 nikajifanyizia birika za maji, ya kuunyweshea mwitu mlimopandwa miti michanga.

 7 Nami nikanunua watumwa na wajakazi, nikawa na wazalia nyumbani mwangu; tena nikawa na mali nyingi za ng’ombe na kondoo, kupita wote walionitangulia katika Yerusalemu;

 8 tena nikajikusanyia fedha na dhahabu, na tunu za kifalme na za kutoka katika majimbo. Nikajipatia waimbaji, waume kwa wake, nao wale ambao wanadamu wanawatunuka, masuria wengi sana.

9 Basi nikawa mkuu, nikaongezeka kupita wote walionitangulia katika Yerusalemu; pia hekima yangu nikakaa nayo.

 10 Wala sikuyanyima macho yangu cho chote yalichokitamani; wala sikuuzuia moyo wangu katika furaha yo yote; maana moyo wangu ulifurahi kwa sababu ya kazi yangu yote, na hii ilikuwa sehemu yangu katika kazi yangu yote.

 11 Kisha nikaziangalia kazi zote zilizofanywa kwa mikono yangu, na taabu yote niliyotaabika katika kuzitenda; na tazama, yote ni ubatili na kujilisha upepo, wala faida hakuna chini ya jua”.

Ukiendelea kusoma kitabu hicho utaona Sulemani, anauchukia mpaka uhai.. anaona hakuna faida yoyote kujitumainisha katika hekima ya kidunia, ambayo hapo kwanza alikuwa anaiona ya maana!.. Magari, na majumba aliyokuwa anayatafuta!, mwisho wa siku anakuja kusema ni upumbavu yote!.. wanawake wengi aliokuwa anawatafuta mwisho wa siku anakuja kujuta anasema ni upumbavu!..biashara anazozifanya anakuja kusema ni kujilisha upepo!… Maana yake ni kwamba laiti kama angerudishwa nyuma, angefanya marekebisho makubwa sana!.. lakini tayari kashakuwa mzee, hivyo anatoa mahubiri wa Israeli.. anawashauri jambo jema la kutafuta!.. kwamba si hekima ya kidunia bali wamtafute Bwana..

Mhubiri 12:8 “Mhubiri asema, Ubatili mtupu; mambo yote ni ubatili!

9 Walakini, kwa sababu huyo Mhubiri alikuwa na hekima, aliendelea kuwafundisha watu maarifa, naam, akatafakari, akatafuta-tafuta, akatunga mithali nyingi.

 10 Huyo Mhubiri akatafuta-tafuta ili apate kuona maneno yapendezayo, na yale yaliyoandikwa kwa unyofu, yaani, maneno ya kweli.

 11 Maneno yao wenye hekima huwa mfano wa michokoo; na kama misumari iliyogongomewa sana; ndivyo yalivyo maneno yao walio wakuu wa makusanyiko, ambayo yatoka kwa mchungaji mmoja.

12 Tena, zaidi ya hayo, mwanangu, kubali maonyo; hakuna mwisho wo wote wa kutunga vitabu vingi; na kusoma sana huuchosha mwili.

13 HII NDIYO JUMLA YA MANENO; YOTE YAMEKWISHA SIKIWA; MCHE MUNGU, NAWE UZISHIKE AMRI ZAKE, MAANA KWA JUMLA NDIYO IMPASAYO MTU.

 14 KWA MAANA MUNGU ATALETA HUKUMUNI KILA KAZI, PAMOJA NA KILA NENO LA SIRI, LIKIWA JEMA AU LIKIWA BAYA”.

Umeona hapo jumla ya mambo yote Sulemani anayoitoa??….Anasema Mche Bwana na uepukane na uovu!.. hasemi tafuta mali, hasemi tena wala hashauri watu kutafuta utajiri, wala hagusii hekima yoyote ya kiulimwengu, bali anahitimisha kwa kusema maneno hayo mawili tu!!!..” MCHE MUNGU, NAWE UZISHIKE AMRI ZAKE, MAANA KWA JUMLA NDIYO IMPASAYO MTU”

Je! Unamcha Mungu na kuzishika amri zake?.. Huyu ni Sulemani ambaye alikuwa ni tajiri kupita sisi, ambaye ameonja kila kitu, ndio anahitimisha hivi, kashatusaidia kufanya utafiti, hatuhitaji tena sisi kufanya utafiti, yeye kafanya utafiti wa kupata mali nyingi na mwisho wa siku kaona ni ubatili!, na kujilisha upepo!.. basi na sisi hatuna haja ya kurudia hayo hayo, kwamaana tukirudia hayo hayo mwisho wa siku tutafika kwenye jibu hilo hilo la Sulemani, na wakati huo tutakuwa tumeshapoteza muda wa kutosha.

Bwana Yesu ambaye alikuwa na hekima kuliko Sulemani alisema maneno haya..

Marko 10: 24  “Wanafunzi wakashangaa kwa maneno yake. Yesu akajibu tena, akawaambia, Watoto, jinsi ilivyo shida wenye kutegemea mali kuingia katika ufalme wa Mungu!

25  Ni rahisi ngamia kupenya katika tundu ya sindano kuliko tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu”

Na tena akasema..

Marko 8:36 “ Kwa kuwa itamfaidia mtu nini kuupata ulimwengu wote, akipata hasara ya nafsi yake?

37  Ama mtu atoe nini badala ya nafsi yake?

38  Maana kila mtu atakayenionea haya mimi, na maneno yangu, katika kizazi hiki cha uzinzi na dhambi, Mwana wa Adamu atamwonea haya mtu huyo, atakapokuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika watakatifu”.

Imemfaidia nini Sulemani kuwa na hekima za kufanya biashara kuliko watu wote duniani, halafu hekima hizo zimekuja kumfanya akengeuke na kuabudu miungu mingine mwishoni?.. Ndio maana mwisho anasema na kutushauri kuwa ni ubatili hayo yote..tusiyatafute hayo!..kwasababu tutakufa na kuyaacha..bali tuutafute kwanza kutenda mapenzi ya Mungu hapa duniani.

Ndugu kama hujampokea Yesu, huu ndio wakati wako sasa wa kufanya hivyo, Yesu yupo mlangoni, Utafutaji wa mali usikusonge hata ukajikuta unaikosa mbingu!, kiungo chako kimoja kikikukosesha kikate!.. Ni heri ukose mali nyingi lakini uingie mbinguni kuliko upate dunia nzima halafu ukose uzima wa milele.

Hivyo kama hujaokoka!, hapo ulipo tubu, na kisha tafuta ubatizo sahihi ambao ni wa maji mengi na kwa jina la Yesu, na baada ya hapo Roho Mtakatifu atakuongoza katika kweli yote.

Maran atha!

Usikose mwendelezo wa vitabu vinavyofuata!!!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 1

Nini maana ya “katika wingi wa hekima mna wingi wa huzuni”.

HEKIMA YA KIMUNGU, INAINGIAJE MIOYONI MWETU?

Nini maana ya “Mwenye hekima huvuta roho za watu”.

Pambaja ni nini katika Biblia kama tunavyosoma katika kitabu cha Wimbo ulio bora 1:2?

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments