NJIA KUU YA KUINGIA KATIKA ULE MJI.

NJIA KUU YA KUINGIA KATIKA ULE MJI.

Isaya 35: 8 “Na hapo patakuwa na NJIA KUU, na njia, NAYO ITAITWA, NJIA YA UTAKATIFU; wasio safi hawatapita juu yake; bali itakuwa kwa ajili ya watu hao; WASAFIRIO, WAJAPOKUWA WAJINGA, HAWATAPOTEA KATIKA NJIA HIYO”.

Mtu yeyote anayejiita ni mkristo ni wazi kuwa yupo safarini, Na kama yupo safarini ni lazima afahamu malengo yake ni nini, kwamba anatoka wapi, na anakwenda wapi? Na Sababu ya yeye kumfanya utoke pale alipo aende huko anendako ni ipi?, Kadhalika ni lazima ajue ni njia gani atakayoipita, na chombo kipi atakachokitumia kusafiria pamoja na gharama zake..! Lakini ukiwa ni msafiri halafu hujui hayo yote, ni dhahiri kuwa utaitwa MTORO, kama vile Kaini alivyoambiwa na Bwana Mungu kwamba atakuwa“mtoro na mtu asiye na kikao duniani (Mwanzo 4:12)”. Na huo uzao wa Kaini unatenda kazi miongoni mwa kundi kubwa linalojiita la wakristo, hawana vikao, hawajulikana ni watu wa ulimwengu huu, au ni wasafiri wa kwenda mbinguni, Kumbuka Kaini na Habili wote walikuwa ni ndugu, isipokuwa mmoja hakuonekana kuwa mkamilifu mbele za Mungu.

Mtu aliye makini katika safari yake, siku zote anaona mwisho wa safari yake utakuwa ni upi hata kabla hajaianza hiyo safari, na atatambua ya kuwa wakati akiwa njiani atakutana na mambo mengi tofuati tofauti, na majira mengi tofauti tofauti, hivyo atakuwa makini akijua kuwa yupo safarini kwahiyo hatayatilia maanani mambo yanayopita ya njiani, hata akifika kituoni labda kwa muda mchache tu atashuka kuchuka chakula na kurudi kwenye chombo chake cha usafiri na kuendelea na safari yake, hatashikamana au kuambatana na shughuli zinazoendelea katika hicho kituo alichofika kwa muda tu, huwezi kuona anakwenda kuzunguka tena mijini, labda kwenye viwanja vya michezo, na majukwaa ya sinema, na kutangatanga huku na huko ni kwasababu gani? Kwasababu anajua akifanya hivyo muda wake hautamtosha hivyo ataachwa na kile chombo alichokuwa anasafiria, na hapo pia si sehemu yake aliyotarajia kufika, Kwahiyo yeye mahali popote anapopita atatafahamu ni mpitaji tu, 

kadhalika na katika ukristo wa kweli sisi ni wasifiriji tu, ulimwenguni sio kwetu,..Mkristo ni lazima afahamu yeye anatoka wapi, na anakwenda wapi, na kitu gani kinachompeleka huko aendako,,.Safari yetu sisi ni kutoka katika ulimwengu mmoja na kwenda katika ulimwengu mwingine, tunatoka katika ulimwengu huu uliopo sasa unaoharibika na kwenda katika ulimwengu mpya wa milele usioharibika, na ili kuufikia huo ulimwengu mpya ipo njia ya kuipitia, ndio hii Bwana anayoiita, “NJIA KUU”..Hii imeitwa Njia kuu kwasababu wanaopita juu yake ni wachache, na ni WATAKATIFU tu WALIOSAFARINI ndio watakaopita juu yake, Hakuna mtu mwingine yeyote atakayeweza kupita katika hiyo njia isipokuwa amekidhi hivyo vigezo.

Kumbuka katika huo ulimwengu ujao kutakuwa na MALANGO MAKUBWA ya kuuingilia, Na njia pekee itakayokuongoza kuuingia ni hiyo NJIA KUU inayojulikana kama Njia ya Utakatifu. Huko ndiko Yerusalemu mpya mji wa Mungu ulipo, (yaani bibi-arusi wa Kristo). Na ndio maana Bwana Yesu alisema,

Ufunuo 22: 14 “Heri wazifuao nguo zao, wawe na amri kuuendea huo mti wa uzima, NA KUINGIA MJINI KWA MILANGO YAKE.

15 Huko nje wako mbwa, na wachawi, na wazinzi, na wauaji, na hao waabuduo sanamu, na kila mtu apendaye uongo na kuufanya”.

Ndugu yangu, maneno ya Yesu Kristo ni kweli na uzima, hiyo njia ni NJIA KUU ni NJIA YA UTAKATIFU, haijasema ni njia ya dini, au ya dhehebu, au ya upako, au ya miujiza, au ya utajiri, au ya umaskini, hapana inasema ni NJIA YA UTAKATIFU, ikiwa na maana kuwa wale wasafiri ambao ni watakatifu ndio wanaoipita hiyo,na si mwingine yeyote unaweza ukadhani upo katika njia hiyo kwasababu tu wewe unayo dini, lakini ndugu kama huna UTAKATIFU haupo katika hiyo njia, hata kama utatoa zaka kiasi gani, kama wewe haujajiweka kama mtu anayesafiri, basi jua haupo katika njia hiyo. Biblia ipo wazi kabisa inasema.

Waebrania 12:14 “Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, NA HUO UTAKATIFU, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao”;

Unaona hapo?, wewe unayesema ni mkristo na unasema upo safarini, umefika katikati ya safari yako umekutana na anasa na burudani za ulimwengu huu, unasahau kuwa wewe ni mkristo unayesafiri unaanza na wewe kushikamana na hivyo vitu vya ulimwengu huu vinavyopita, unaanza na wewe kuhudhuria karama za ulafi, unaanza kujishughulisha na rushwa, unaanza kujichanganya na watu waovu wa ulimwengu huu, ulikuwa ni mwombaji mzuri hapo mwanzo lakini sasa biashara na udanganyifu wa mali vinakusonga, wewe kila wakati ni mali tu, unasahau maisha yako ya rohoni, hujui kuwa muda unazidi kwenda na kile chombo ulichokuwa unasafiria (Neema) hakiwezi kikakusubiria muda wote huo,

Ulikuwa unavaa vizuri na kujisitiri hapo mwanzo, lakini ukafika kituo ukakutana na fashion za ulimwengu huu, ukasahau kuwa upo safarini ukauacha utakatifu uliokuwa nao hapo mwanzo na wewe ukaanza kuvaa suruali na kaptura, ukaanza kuvaa nguo fupi, ukaanza kuvaa nguo zinazochora maumbile yako, ukaanza kupaka ma-lipstick, na wanja, na hereni na ma-wigi kama wanawake wa ulimwengu huu, hujui kuwa muda unazidi kwenda na kile chombo ulichokuwa unasafiria kimeshaanza kukuacha.

Mwanzoni mwa safari yako mawazo yako yalikuwa yameelekea mbinguni tu, ulikuwa unatamani ufikie kilele cha safari yako mapema, ulikuwa unafikiria kila siku habari za mbingu mpya na nchi mpya lakini umefika mahali umegota safarini, umeiacha NJIA KUU YA UTAKATIFU, umeanza kutazama pornography, umeanza kusengenya, umeanza kutukana, umeacha upole wako na ukarimu wako, ndugu ukiendelea hivyo hivyo hautauingia ule mji Yerusalemu ya Bwana, usijidanganye na Dini yako ukadhani inatosha kukufikisha mbinguni, kwasababu biblia ilishasema..”

Mithali 14: 12 Iko njia ionekanayo kuwa sawa machoni pa mtu, Lakini mwisho wake ni njia za mauti”..Kumbuka kama ilivyosema..Pasipo huo utakatifu hakuna mtu atakayemwona Mungu…

Isaya 35: 8 “Na hapo patakuwa na njia kuu, na njia, nayo itaitwa, NJIA YA UTAKATIFU; WASIO SAFI HAWATAPITA JUU YAKE; bali itakuwa kwa ajili ya watu hao; WASAFIRIO, WAJAPOKUWA WAJINGA, HAWATAPOTEA KATIKA NJIA HIYO.

9 Hapo hapatakuwa na simba, wala mnyama mkali hatapanda juu yake; hawataonekana hapo; bali waliokombolewa watakwenda katika njia hiyo.

10 Na hao waliokombolewa na Bwana watarudi, watafika Sayuni wakiimba; na furaha ya milele itakuwa juu ya vichwa vyao; nao watapata kicheko na furaha, huzuni na kuugua zitakimbia”.

Umeona biblia inasema watakaopita katika njia hiyo, ulimwengu utawaona ni wajinga, wataonekana kama watu wasiostahili kuwa katikati yao, wanawake waliokataa mitindo ya ulimwengu huu wataonekana washamba na wajinga, wanaume wasiokuwa walevi, wala waasherati, watu wanaoishi maisha matakatifu watadharauliwa, lakini hao ndio Mungu aliowachagua wapite katika njia ile KUU, Biblia inasema wajapokuwa ni wajinga machoni pa ulimwengu lakini hawatapotea katika njia hiyo.

Kumbuka ndugu, biblia imetuonya tufanane na wasafiri wenzetu wa Imani waliotutangulia, ambao walijikana kweli kweli, watu ambao mawazo yao yote yalikuwa ni mbinguni tu, kama tunavyowasoma katika

Waebrania 11: 36 “wengine walijaribiwa kwa dhihaka na mapigo, naam, kwa mafungo, na kwa kutiwa gerezani;

37 walipigwa kwa mawe, walikatwa kwa misumeno, walijaribiwa, waliuawa kwa upanga; walizunguka-zunguka wakivaa ngozi za kondoo na ngozi za mbuzi; walikuwa wahitaji, wakiteswa, wakitendwa mabaya;

38 (WATU AMBAO ULIMWENGU HAUKUSTAHILI KUWA NAO), walikuwa wakizunguka-zunguka katika nyika na katika milima na katika mapango na katika mashimo ya nchi.

39 Na watu hao wote wakiisha kushuhudiwa kwa sababu ya imani yao, hawakuipokea ahadi;

40 kwa kuwa Mungu alikuwa ametangulia kutuwekea sisi kitu kilicho bora, ili wao wasikamilishwe pasipo sisi…”

Waebrania 11: 13 Hawa wote wakafa katika imani, wasijazipokea zile ahadi, bali wakaziona tokea mbali na kuzishangilia, NA KUKIRI KWAMBA WALIKUWA WAGENI, NA WASAFIRI JUU YA NCHI.14 MAANA HAO WASEMAO MANENO KAMA HAYO WAONYESHA WAZI KWAMBA WANATAFUTA NCHI YAO WENYEWE.

15 Na kama wangaliikumbuka nchi ile waliyotoka, wangalipata nafasi ya kurejea.

16 Lakini sasa waitamani nchi iliyo bora, yaani, ya mbinguni. Kwa hiyo Mungu haoni haya kuitwa Mungu wao; maana amewatengenezea mji”.

Ndugu hawa watu walijikana nafsi zao kwasababu waliuona uzuri uliopo mbele yao, waliona furaha isiyokuwa na kifani kuingia katika ule mji, waliona ni heri maisha yao ya miaka 80 yasiwe ni kitu kulinganisha na miaka ya umilele inayokuja huko mbeleni. Ndugu kosa kila kitu lakini usikose mbingu, Biblia inasema wenye haki watang’aa kama jua, Mambo ambayo Mungu amewaandalia wampendao ni mambo ambayo jicho halijawahi kuona wala sikio kusikia, hakutakuwa na uchungu tena, wala kudharauliwa, watapewa miili ya utukufu wa ajabu, watatawala na Kristo Yesu kama wafalme na makuhani, milele na milele, tujitahidi tusikose huko.

Utajisikiaje unyakuo umepita na wewe umeachwa? Wenzako wamekwenda katika karamu ya mwanakondoo mbinguni na wewe umebaki?hapa duniani ukisubiria ziwa la moto? 

Utajisikiaje??..Ifuate hiyo NJIA KUU LEO, kwa kumpa Yesu Kristo maisha yako kama hujafanya hivyo angali muda upo, ukabatizwe katika ubatizo sahihi wa kuzamishwa kwenye maji tele na kwa Jina la YESU KRISTO, upate ondoleo la dhambi zako (Matendo 2:38) na kisha utapokea kipawa cha Roho Mtakatifu kitakachokuwezesha kuwa mtakatifu ili uweze kuiendea hiyo NJIA KUU YA UTAKATIFU ili siku ile Uingie katika ile Yerusalemu mpya ya Bwana aliyowaandalia watakatifu wake

Ufunuo 21: 1 “Kisha nikaona mbingu mpya na nchi mpya; kwa maana mbingu za kwanza na nchi ya kwanza zimekwisha kupita, wala hapana bahari tena.

2 Nami nikauona mji ule mtakatifu, Yerusalemu mpya, ukishuka kutoka mbinguni kwa Mungu, umewekwa tayari, kama bibi-arusi aliyekwisha kupambwa kwa mumewe.

3 Nikasikia sauti kubwa kutoka katika kile kiti cha enzi ikisema, Tazama, maskani ya Mungu ni pamoja na wanadamu, naye atafanya maskani yake pamoja nao, nao watakuwa watu wake. Naye Mungu mwenyewe atakuwa pamoja nao.

4 Naye atafuta kila chozi katika macho yao, wala mauti haitakuwapo tena; wala maombolezo, wala kilio, wala maumivu hayatakuwapo tena; kwa kuwa mambo ya kwanza yamekwisha kupita.

5 Na yeye aketiye juu ya kile kiti cha enzi akasema, Tazama, nayafanya yote kuwa mapya. Akaniambia, Andika ya kwamba maneno hayo ni amini na kweli.

6 Akaniambia, Imekwisha kuwa. Mimi ni Alfa na Omega, Mwanzo na Mwisho. Mimi nitampa yeye mwenye kiu, ya chemchemi ya maji ya uzima, bure.

7 Yeye ashindaye atayarithi haya, nami nitakuwa Mungu wake, naye atakuwa mwanangu.

8 Bali waoga, na wasioamini, na wachukizao, na wauaji, na wazinzi, na wachawi, na hao waabuduo sanamu, na waongo wote, sehemu yao ni katika lile ziwa liwakalo moto na kiberiti. Hii ndiyo mauti ya pili..”

Ubarikiwe.

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments