NJIA YA MSALABA

NJIA YA MSALABA

Yohana 19: 16 “Basi ndipo alipomtia mikononi mwao ili asulibiwe; nao wakampokea Yesu.

17 Akatoka, hali akijichukulia msalaba wake, mpaka mahali paitwapo Fuvu la Kichwa, au kwa Kiebrania, Golgotha.

18 Wakamsulibisha huko, na wengine wawili pamoja naye, mmoja huku na mmoja huku, na Yesu katikati.

19 Naye Pilato akaandika anwani, akaiweka juu ya msalaba, imeandikwa, YESU MNAZARETI, MFALME WA WAYAHUDI”

Bwana Yesu alisema mimi ndimi NJIA, na KWELI na UZIMA..mtu haji kwa Baba ila kwa njia ya mimi (Yohana 14:6). Litafakari hilo neno “ILA KWA NJIA YA MIMI” Kumbuka aliposema ILA KWA NJIA YA MIMI hakumaanisha kuwa wafuasi wake au washabiki wake.Hapana alimaanisha kitu kingine kabisa tofauti na hicho.

Tuchukue mfano leo hii, mwanariadha maarufu duniani, ambaye amepokea tuzo bora kuliko wote duniani…atoe sentensi aseme “mtu hawezi kuifikia tuzo niliyo nayo mimi isipokuwa kwa njia yangu mimi” je! Kwa sentensi hiyo unadhani atakuwa anamaanisha  kuwa ili mtu awe kama yeye anapaswa awe mshabiki wake au mfuasi wake??…Ni wazi hamaanishi hivyo, utagundua kuwa anamaanisha kwamba mtu akitaka kuwa kama yeye, ni lazima kwanza awe mwanariadha kama yeye, na pili awe na bidii kama za kwake, ajue mbinu anazozitumia za yeye kufanikiwa..

Unaona kwahiyo NJIA ya mwanariadha sio kuwa mshabiki wake wala mfuasi wake bali ni kuwa na bidii kama ya kwake, kufanya mazoezi magumu kama aliyoyafanya yeye, kujitoa kama alivyojitoa yeye, kutokata tama kama yeye asivyokata, kukubali kupitia changamoto zote kama alizozipitia yeye pasipo kukata tamaa n.k…Kwahiyo utagundua kuwa kumbe Kupata tuzo kama aliyoipata yeye sio jambo jepesi ni zaidi na kuwa mshabiki wake au kuwa mfuasi wake.

Kadhalika na Bwana Yesu aliposema mtu haji kwa Baba ila kwa njia yake yeye…hakumaanisha tuwe wafuasi wake, au washabiki wake, kwamba tumshabikie kila mahali tueleze sifa zake na umahiri wake tu, halafu inatosha, hapana alimaanisha kuwa ili mtu afike kwa Baba kama yeye atakavyofika, hana budi kupitia njia kama alizopitia yeye, na si njia nyingine yeyote.. Ilikuwa ili aipate tuzo iliyo bora ilimpasa, kudharaulika, kutukanwa, kutemewa mate kwa ajili ya Imani, kutengwa, kuchukiwa pasipo sababu na zaidi ya yote ilimpasa siku moja ABEBE MSALABA WAKE aelekee Golgotha.

“17 AKATOKA, HALI AKIJICHUKULIA MSALABA WAKE, mpaka mahali paitwapo Fuvu la Kichwa, au kwa Kiebrania, Golgotha.”

Na yeye akasema mtu yeyote akitaka kumfuata na apitie njia hiyo hiyo, akubali kuchukiwa, akubali kutemewa mate, akubali kudharaulika kwa ajili ya Imani, akubali kukataliwa, akubali kuyaacha mambo ya ulimwengu hata ikiwezekana ndugu, wazazi na jamii na Mwisho wa yote na yeye pia akubali KUBEBA MSALABA WAKE kuelekea Golgotha yake kama yeye alivyofanya. Kwasababu hawezi kuwaambia watu wabebe misalaba yao na wakati yeye mwenyewe habebi.

 Ni njia ngumu lakini ndio Mungu aliyoichagua, tukitaka kufika kwa Baba mbinguni hatuna budi tupitie hiyo…hakuna njia nyingine ya Mkato, ni lazima tubebe Misalaba yetu. Ndio maana Bwana Yesu alisema mara nyingi kila mahali..

Mathayo 16: 24 “Wakati huo Yesu aliwaambia wanafunzi wake, MTU YE YOTE AKITAKA KUNIFUATA, NA AJIKANE MWENYEWE, AJITWIKE MSALABA WAKE, ANIFUATE. Kwa kuwa mtu atakaye kuiokoa nafsi yake, ataipoteza; na mtu atakayepoteza nafsi yake kwa ajili yangu, ataiona”.

Na kama Mungu, alivyompa Bwana wetu Yesu Kristo nguvu ya kushinda majaribu mazito kama yale, nguvu hiyo hiyo atatupa sisi endapo tutakubali kumfuata yeye kwa mioyo yetu yote na kwa roho zetu zote. Endapo tutaikubali hii njia ya msalaba iliyodharaulika..

Bwana baada ya kudharaulika kwa ajili ya Imani, mwisho wa siku aling’aa kama jua, Biblia inasema aliidharau aibu,na hivyo Mungu akamuadhimisha mno, akamkirimi jina lile lipitalo kila jina.

Wafilipi 2: 8 tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba.

9 Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina;

10 ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi;

11 na kila ulimi ukiri ya kuwa YESU KRISTO NI Bwana, kwa utukufu wa Mungu Baba”.

Bwana atusaidie tusiwe WASHABIKI WAKE au WAFUASI WAKE, bali tuwe watu tunayoiendea njia yake, tukiwa ni walevi na bado tunajiita wakristo sisi bado ni washabiki, tukiwa tunaenda kanisani na bado tunasengenya sisi bado tu ni washabiki, gharama za mbio hatuzijui, ikiwa bado tunavaa nusu uchi na mavazi yasiyostahili mbele za Mungu, bado sisi ni washabiki hatutaweza kufika kwa Baba wanaofika kwa Baba ni wale wanaoiendea NJIA YA BWANA YESU KRISTO, yeye hakuwa mlevi, hakuwa mtukanaji, hakuwa mwizi, hakuwa mwabudu sanamu, hakuwa mwasherati, hakuwa mfuasi wa mambo ya ulimwengu huu. Hiyo ndiyo njia tunayowekewa tuifuate, kama Mwana wa Mungu kapitishwa kwa hiyo, unadhani sisi wengine tutatengenezewa njia nyingine mbadala ya mkato?? Hapana njia ni moja tu, na imeshawekwa na kuthibitishwa na Mungu nayo ni njia ya YESU KRISTO.

Hivyo kama hujampa Bwana Yesu Maisha yako, usikawie kufanya hivyo, nyakati hizi tunazoishi ni za hatari, muda unakaribia kusimamishwa, na umilele kuanza, Bwana asirudi leo na kukukuta upo hivyo ulivyo, asikukuta katika hali hiyo ya uvuguvugu uliyo nayo, Mkabidhi leo maisha yako kikamilifu, kwa kudhamiria kabisa kutoka moyoni mwako, Kuanza maisha mapya na UKAIFUATE NJIA YA MSALABA, na yeye mwenyewe atakuwezesha kuiendea, Na kuumaliza mwendo salama. Ili siku ile uwe na ujasiri wa kusimama mbele zake.

Wafilipi 1: 6 “..yeye aliyeanza kazi njema mioyoni mwenu ataimaliza hata siku ya Kristo Yesu;

Bwana akuangazie Neema yake.

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments