Kwa namna gani tumefanyika Makuhani na Ufalme?.(Ufunuo 1:6)

Kwa namna gani tumefanyika Makuhani na Ufalme?.(Ufunuo 1:6)

Swali: Biblia inasema katika Ufunuo 1:6 kuwa kupitia Bwana Yesu tumefanyika kuwa ufalme na makuhani, je tumefanyikaje kuwa hivyo?

Jibu: Awali ya yote tusome maandiko yafuatayo,

1 Yohana 4:17 “Katika hili pendo limekamilishwa kwetu, ili tuwe na ujasiri katika siku ya hukumu; kwa kuwa, KAMA YEYE ALIVYO, NDIVYO TULIVYO NA SISI ULIMWENGUNI HUMU”.

Hapo anasema “kama yeye alivyo ndivyo na sisi tulivyo”. Ikiwa na maana kuwa katika roho sisi tunafanana na Kristo kwa kila kitu.

Maana yake kama Kristo ni mwana wa Mungu basi na sisi ni wana wa Mungu sawasawa na Warumi 8:16.

Warumi 8:16 “Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu”.

Vile vile kama Kristo alikufa na kufufuka na kuketi katika kiti cha enzi, vile vile na sisi katika roho tulikufa pamoja naye kwa njia ya ubatizo (sawasawa na Warumi 6:4 na Warumi 6:8) kwa njia ya ubatizo

Warumi 6:4 “Basi tulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti yake, kusudi kama Kristo alivyofufuka katika wafu kwa njia ya utukufu wa Baba, vivyo hivyo na sisi tuenende katika upya wa uzima”.

Na vile vile kama Kristo alifufuka na sisi pia tulifufuka  pamoja naye na sasa tumeketi pamoja naye katika ulimwengu wa roho.

Waefeso 2:6 “Akatufufua pamoja naye, akatuketisha pamoja naye katika ulimwengu wa roho, katika Kristo Yesu”.

Kwahiyo kwa ufupi ni kwamba watu waliookoka kikamilifu wanafanana na Kristo kwa kila kitu, na hii ndio sababu kwanini shetani pamoja na mapepo yake yanawaogopa watu wa YESU KRISTO, ni kwasababu yanamwona Yesu Kristo ndani yao.

Sasa nafasi nyingine ya YESU iliyo kuu ni nafasi ya “ukuhani” na tena si kuhani tu, bali “KUHANI MKUU”.

Waebrania 8:1 “Basi, katika hayo tunayosema, neno lililo kuu ndilo hili: Tunaye kuhani mkuu wa namna hii, aliyeketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Ukuu mbinguni”.

Na kama Kristo alivyokuwa Kuhani, vile vile na sisi ni makuhani.

Na kumbuka kazi ya Makuhani ilikuwa ni kuwapatanisha watu na Mungu wao kwa njia ya SADAKA NA MAOMBI NA MAFUNDISHO.

Mfano Samweli, alifanya kazi ya kuwapatanisha Israeli kupitia sadaka zao , vilevile na kuwaombea na kuwafundisha njia iliyo sahihi..

1 Samweli 12:23 “Walakini mimi, hasha! Nisimtende BWANA dhambi kwa kuacha kuwaombea ninyi; lakini nitawaelimisha katika njia iliyo njema, na kunyoka”

Na Kristo ni hivyo kama Kuhani amesimama kutupatanisha na baba kwa njia ya kutuombea..

1 Yohana 2:1 “Watoto wangu wadogo, nawaandikia haya ili kwamba msitende dhambi. Na kama mtu akitenda dhambi tunaye Mwombezi kwa Baba, Yesu Kristo mwenye haki”.

Soma pia Warumi 8:34, utaona jambo hilo hilo.

Na pia Yesu anatupatanisha kwa Baba kwa njia ya sadaka ya mwili  wake alioutoa kwaajili yetu.

Na sisi pia kwakuwa tunafanana na yeye katika roho sawasawa na hiyo 1 Yohana 4:1, basi na sisi ni makuhani kama yeye na tunaweza kuzifanya kazi zile zile anazozifanya yeye sasa za kikuhani.

Na kazi hizo ni kuwapatanisha watu na Baba kwa njia ya MAOMBI, MAFUNDISHO NA SADAKA. Hivyo tumepewa na sisi huduma ya upatanisho kama aliyonayo Bwana wetu YESU KRISTO.

Utauliza tunalithibitisha vipi hilo kibiblia?…Tusome maandiko yafuatayo..

2 Wakorintho 5:18 “Lakini vyote pia vyatokana na Mungu, aliyetupatanisha sisi na nafsi yake kwa Kristo, naye ALITUPA HUDUMA YA UPATANISHO;

19 yaani, Mungu alikuwa ndani ya Kristo, akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake, asiwahesabie makosa yao; NAYE AMETIA NDANI YETU NENO LA UPATANISHO”

Ndio maana tunaweza kuombeana na Mungu akasikia (Yakobo 5:16) kwasababu na sisi ni makuhani kama yeye, Vile vile kwa kujitoa miili yetu na vitu vyetu kama sadaka tunaweza kujipatanisha na kuwapatanisha wengine na Mungu.

Na hiyo yote ni kwasababu Kristo ametufanya na sisi kuwa makuhani kama yeye sawasawa na Ufunuo 1:6.

Tofauti ya Kristo na sisi ni kwamba Kristo yeye ni KUHANI MKUU, na sisi tunabaki kuwa makuhani, (yeye ni mkuu wa makuhani, utukufu na heshima zinabaki kwake, Bwana wa mabwana, mwamba imara!!!).

Na ni kwa namna gani sisi ni UFALME?.

Ni kwa namna ile jinsi Kristo alivyo…Yeye ni Mfalme, na tena si mfalme tu, bali Mfalme wa wafalme.

Ufunuo 19:16 “Naye ana jina limeandikwa katika vazi lake na paja lake, MFALME WA WAFALME, NA BWANA WA MABWANA”

Na kama yeye ni Mfalme wa wafalme, maana yake anao wafalme anaowatawala ambao nao pia ni wafalme na hao si wengine zaidi ya wale wanaomwamini..  (Kwamaana hawezi kuitwa mfalme wa wafalme kama hana wafalme chini yake anaowatawala).

Na utukufu wa ufalme tulionao sasa utakuja kudhuhirika zaidi katika ule utawala wa amani wa miaka 1000 wa YESU KRISTO.

Ufunuo 20:6 “Huo ndio ufufuo wa kwanza. Heri, na mtakatifu, ni yeye aliye na sehemu katika ufufuo wa kwanza; juu ya hao mauti ya pili haina nguvu; BALI WATAKUWA MAKUHANI WA MUNGU NA WA KRISTO, NAO WATATAWALA PAMOJA NAYE HIYO MIAKA ELFU”

Je umeziona faida za kuwa ndani ya Kristo?.. Tunakuwa makuhani na tena wafalme…

Je! Tayari Umemwamini yeye?.

Kama bado unasubiri nini?..kumbuka tunaishi majira ya kurudi kwa Yesu mara ya pili.

Bwana akubariki.

Shalom..

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618

Mafundisho mengine:

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments