2Nyakati 29:34 Lakini makuhani walikuwa wachache, wasiweze kuchuna sadaka zote za kuteketezwa; basi ndugu zao Walawi wakawasaidia, hata ilipokwisha kazi, na hata makuhani walipojitakasa; kwa kuwa Walawi walikuwa wenye mioyo ya adili kwa kujitakasa kuliko makuhani.
Nakusalimu katika jina la Bwana Yesu.
Fundisho hili linawahusu sana sana viongozi wa kiroho / Watumishi wa Mungu wanaohudumia kundi la Mungu. Mfano wachungaji au maaskofu.
Kuna wakati wale walioteuliwa kuwa viongozi wa juu kabisa wanaweza wasiwajibike ipasavyo katika nafasi zao, je! Wewe kama mwangalizi wao ufanye nini?
Mfano tukirejea habari hiyo tunaona Mfalme Hezekia alipokusudia kulitakasa hekalu la Mungu, ambalo lilikuwa limefungwa na kusahauliwa, na baba yake.
Alitafuta makuhani wa kuhudumu upya katika nyumba ya Mungu. Ikumbukwe kuwa makuhani tu ndio walioruhusiwa kufanya shughuli zote za madhahabuni, ikiwemo kuvukiza uvumba na kuandaa zile sadaka zilizoletwa mbele ya nyumba ya Bwana.
Lakini hapo biblia inatuambia, Makuhani walikuwa wachache!. Utajiuliza ni kwanini? Sio kwamba hawakuwepo kabisa, walikuwepo, lakini biblia inatuambia waliokuwa na mioyo ya adili ya kuipenda kazi ya Mungu ndio walikuwa wachache.
Pengine, wengine walikuwa na udhuru zao, wakiona kuahirisha shughuli zao, na kwenda kuhudumu madhabahuni ni kuvurugiwa ratiba ni kazi ya kuchosha, haina faida, wengine hawakuwa tayari kujitakasa, kwa kuacha mambo mabovu yasiyowapasa makuhani, wengine wakawa wazito, wanavutwa vutwa sana, kazi ambayo inapaswa ifanyike haraka n.k..
Hivyo hiyo ikapelekea kundi la viongozi wa juu kabisa likawa chache sana. Na kimsingi ni lazima wawepo wahudumu wa kutosha katika kazi hiyo ya madhabahuni. Sasa wafanyaje. Ndipo hapo utaona Walawi ambao kazi zao ni za nje, ya hema kama vile usimamizi wa malango, kulinda hekalu, na kuimba. Ikabidi sasa waingizwe ndani kwa ajili ya kusaidia kazi za kikuhani.
Na sababu ya kufanya hivyo biblia inasema, wenyewe walikuwa ni “wenye mioyo ya adili kwa kujitakasa kuliko makuhani”.
Walikuwa na moyo wa kumtumikia Mungu zaidi hata ya wale wanaostahili. Hivyo wakapewa kazi za juu zisizowastahili na wakafanya vizuri na Mungu akawabariki, ijapokuwa ilikuwa ni kinyume na taratibu.
Hata sasa katika kanisa, ni rahisi kuona wenye ngazi za chini, ni wepesi na wenye mioyo ya uaminifu katika nyumba ya Bwana kuliko wale viongozi wa juu. Utaona ni kiongozi wa wakina mama, lakini kwenye maombi haudhurii, kuwafuatilia wanawake wenzake haangahiki. Lakini hapo hapo utaona kabinti kadogo, kanajibidiisha, haachi maombi yapite, anawapigia simu yeye kuwakumbusha kana kwamba ndio kiongozi mkuu, anatoa taarifa za maboresho na changamoto kwa kiongozi wake, mambo ambayo hata huyo kiongozi hajui.
Sasa katika mazingira kama haya? Unadhani kiongozi ni nani? …Uongozi sio cheo, uongozi ni MOYO, uaminifu na kujitoa. Ikiwa wewe ni mwangalizi, hakikisha huyu aliye na MOYO ndio unampa wajibu na majukumu yote ya uongozi katika nafasi hiyo. Hata kama hajawekewa mikono, au hana uzoefu wowote, au hajatambulika rasmi.
Huyo huyo ndiye Mungu aliyemchagua, hao wengine ni makapi.
Kwani Bwana Yesu alishatangulia kusema maneno haya.
Mathayo 19:30 “Lakini wengi walio wa kwanza watakuwa wa mwisho, na walio wa mwisho watakuwa wa kwanza”.
Sio kwamba Mungu anao upendeleo.. Lakini alisema.. “ walioalikwa hawakustahili”(Mathayo 22:8).
Halidhalika hata katika ngazi nyingine zote, ikiwa mchungaji msaidizi haipendi kazi yake, usione vibaya, kumpa kazi hiyo shemasi mwenye MOYO wa kuwahudumia watu. Mungu atamtengeneza mwenyewe. Lakini ikiwa wewe ni kiongozi-mlegevu, tubu geuka, ipende nafasi yako, hudumu hapo kwa uaminifu kwasababu umepewa dhamana ambayo utakuja kuitolea hesabu yake siku ile ya hukumu.
Bwana awe nawe.
Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini auPiga namba hizi: +255789001312 au +255693036618
Mafundisho mengine:
Uadilifu ni nini kibiblia?
Kwa namna gani tumefanyika Makuhani na Ufalme?.(Ufunuo 1:6)
Kwanini Yesu aliwaambia wale wakoma wakajionyeshe kwa makuhani?
VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 1
Sadaka ya unga na sadaka ya kinywaji zilikuwaje?
Rudi nyumbani
Print this post