WACHUNGAJI WA BWANA MAKONDENI.

WACHUNGAJI WA BWANA MAKONDENI.

Japo Wayahudi walikuwa wanamtazamia masihi wao kwa muda mrefu na kwa shauku nyingi, lakini tunasoma siku za kuzaliwa mwokozi duniani ni kikundi cha watu wachache sana ndicho kilichojua, tena kwa kufunuliwa. Wengine wote waliosalia hawakuelewa chochote, walizidi kuendelea katika mambo yao, hawakujua kuwa wakati mwingine umeshafunguliwa. Na pia ukichunguza wale waliofunuliwa kuzaliwa kwa Bwana duniani utagundua wote ni watu waliokuwa wanaenenda katika haki na kuzishika amri zote za Mungu bila lawama, mfano tunamwona Zekaria, pamoja na mke wake Elizabeti, Tunamwona Simeoni, Tunamwona Yusufu, tunamwona, Ana, wote hawa kama tukitazama habari zao ni watu waliokuwa wamemaanisha kweli kweli kuutafuta uso wa Mungu,ni watu ambao macho yao siku zote yalikuwa yanaelekea mbinguni wakiutazamia wokovu ambao Mungu aliokuwa amewaahidia kupitia Masiya wao, na ndio maaana mwisho wa siku walikuja kufunuliwa ule wakati ulipofika.

Lakini pia kama tunavyosoma yapo makundi mengine mawili, ambayo hayo yalifunuliwa lakini haikuwa kwa njia kama za hawa wa kwanza, kundi la kwanza ni wale mamajusi kutoka mashariki na kundi la pili lilikuwa ni wale wachungaji wa makondeni. Na kama ukichunguza hawa nao hawakufunuliwa wakiwa mmoja mmoja bali walifunuliwa kimakundi. Hawa hawakuwa wanaichunguza torati, wala kuijua sana dini, wengine walitoka mbali kabisa nje ya Israeli. lakini ni kwanini na wao pia Neema hii ya kipekee iliwafikia ?. Mungu alikuwa anayosababu kuwachagua na wale, Lakini Leo tutawaangalia wale wachungaji waliokuwa wakilinda makundi yao kule kondeni.

Kama tunavyosoma habari:

Luka 2:8 “Na katika nchi ile ile walikuwako wachungaji wakikaa makondeni na kulinda kundi lao kwa zamu usiku.

9 Malaika wa Bwana akawatokea ghafula, utukufu wa Bwana ukawang’aria pande zote, wakaingiwa na hofu kuu.

10 Malaika akawaambia, Msiogope; kwa kuwa mimi ninawaletea habari njema ya furaha kuu itakayokuwa kwa watu wote;

11 maana leo katika mji wa Daudi amezaliwa, kwa ajili yenu, Mwokozi, ndiye Kristo Bwana.

12 Na hii ndiyo ishara kwenu; mtamkuta mtoto mchanga amevikwa nguo za kitoto, amelala katika hori ya kulia ng’ombe.

13 Mara walikuwapo pamoja na huyo malaika, wingi wa jeshi la mbinguni, wakimsifu Mungu, na kusema,

14 Atukuzwe Mungu juu mbinguni, Na duniani iwe amani kwa watu aliowaridhia.

15 Ikawa, malaika hao walipoondoka kwenda zao mbinguni, wale wachungaji waliambiana, Haya, na twendeni mpaka Bethlehemu, tukalione hilo lililofanyika, alilotujulisha Bwana.

16 Wakaenda kwa haraka wakamkuta Mariamu na Yusufu, na yule mtoto mchanga amelala horini.

17 Walipomwona wakatoa habari waliyoambiwa juu ya huyo mtoto.

18 Wote waliosikia wakastaajabu kwa hayo waliyoambiwa na wachungaji.

19 Lakini Mariamu akayaweka maneno hayo yote, akiyafikiri moyoni mwake.

20 Wale wachungaji wakarudi, huku wanamtukuza Mungu na kumsifu kwa mambo yote waliyosikia na kuyaona, kama walivyoambiwa.”

Tukianzia juu kidogo tunafahamu baada ya Yesu kuzaliwa biblia inatuambia Mariamu na Yusufu walikosa sehemu ya kukaa kwani vyumba vya wageni vilikuwa vimejaa hivyo wakalazimika usiku ule ule kutafuta mahali pa kumlazia mtoto, wakaona kuliko kulala kando kando ya njia ni heri wajitulize chini ya zizi la kulizishia ng’ombe huko kwa muda. Mungu aliruhusu iwe hivyo kwa makusudi ili kutimiza kusudi Fulani. Kwani huyo mtoto atakuja kufananishwa na mwanakondoo, Hivyo mwanakondoo hawezi kuishi katikati ya majumba ya kifalme bali ni sharti katika mazizi ya mifugo.

Na ndio hapo tunakuja kuona muda huo huo wale malaika wakawaendea wale wachungaji waliokuwa wamekaa kule makondeni kuwapasha habari za kuzaliwa kwa mwokozi. Swali linakuja Ni kwanini basi wawe wale wachungaji na si watu wengine kama wakulima, au watoza ushuru, au wahasibu, au matabibu, au maaskari?. Embu jaribu kufikiria lingekuwa ni kundi la watoza ushuru ndio waliopelekewa taarifa zile, kwanza usiku ule wangekuwa wapo kitandani wamelala katika majumba yao ya kifahari, pili hawajui mambo ya zizini yalivyo, pengine wangefika tu pale wangetapika kwa harufu za vinyesi na mikojo ya ile mifugo, na pengine wangekutana na ile mbolea iliyoganda pale chini kwa vinyesi vya mifugo wasingeweza kukanyagisha miguu yao waingie ndani ya zizi lile, ule ungekuwa ni mtihani mkubwa sana.

Pia Jaribu kufikiria kama Herode angepelekewa yeye taarifa za kuzaliwa kwa mfalme, unadhani angeweza kuingia ndani ya zizi lile lililochakaa la kale?. Ni wazi kuwa asingeweza, utunzaji wa mifugo ni jambo ambalo linahitaji moyo wa kujitolea na wa kipekee sana na wa uvumilivu. Ukiwa mfugaji huna budi kuweka mbali kinyaa, na kukubali kuchafuliwa na mazingira ya mifugo yaliyopo.

Na ndio maana utaona hata wale wachungaji waliokuwa na mifugo, wakati mwingine walikuwa tayari hata kwenda kulala huko makondeni, kwenye hatari nyingi, wakikaa siku nyingi, usiku na mchana kulihudumia kundi, lisije likafa kwa kukosa malisho. Ni kazi ambayo inahitaji moyo sana.

Hivyo siku ile ya kuzaliwa jicho la Bwana lilipozunguza Israeli yote na kutazama ni watu gani watakaoweza kustahimili kukutana na mwokozi katika mazingira yale magumu ya zizini, ndipo walipoonekana wale wachungaji waliokuwa wamekaa makondeni.

Wakati ule Yusufu na Mariamu wakiwa katika hali ya upweke wakiwaza ni nani atakayekuja kuwatazama mahali hapa pachafu, ni nani atakayekuja kusaidia kuweka mazingira safi na kuwafariji mahali pale pasipostahili kukaa mtu. Ndipo ghafla wakaona kundi kubwa la wachungaji linaingia katika zizi lile kwa furaha na kwa shangwe. Haleluya! mahali pale paligeuka kuwa kama Ikulu. Pengine hata watu waliokuwa wanaishi kando kando ya zizi lile walishangaa umati huo wa wachungaji wametoka wapi usiku ule, wakishangilia kwa furaha kuu na vigelegele, Na kwa jinsi walivyokuja kulakiwa kwa shangwe hata Mariamu na Yusufu hawakujali tena kama wapo katika zizi la kulishia ng’ombe, mahali pale palichangamka ghafla, Kwasababu wenyeji wao wamewasili, haraka moja kwa moja wakaanza kuzoa mavi ya kondoo na ng’ombe yaliyokuwa yapo karibu na wao,kwani hilo ni jambo la kawaida kwao, mambo ambayo mhasibu yeyote asingeweza kufanya, mambo ambayo mtoza ushuru yeyote asingeweza kufanya, askari yeyote asingeweza kufanya. 

Basi haraka haraka wakawaandalia wakawasaidia kufanya yale mambo ambayo hawakauweza kuyafanya peke yao, pengine uchafu ambao hawakuweza kuutoa,walisaidiwa na wale wachungaji na zizi lile likageuka kuwa mahali pa kukaa mtu. Na ndipo wakatoa habari zake, na kurudi makwao kwa furaha kuu na kwa shangwe. Ilikuwa ni furaha iliyokuja kwa kujua kuwa miongoni mwa wale wachache sana kati ya mamilioni ya waliokuwa Israeli, wao na walipata neema ile.

Lakini Mambo hayo kwa sasa yanafunua nini?, kama ilivyokuwa kuja kwa Bwana mara ya kwanza, ndivyo itakavyowa kuja kwa Bwana mara ya pili kulichukua kanisa lake. Kama kipindi kile Wayahudi wengi walikuwa wanamtazamia masihi wao siku moja aje kuwakomboa, ndivyo ilivyo kwa kanisa la sasa, Watu wote wanaojiita wakristo wanamtazamia Kristo kuja kulichukua kanisa lake.

Na kuja kwa sasa hivi sio kwa kuishi tena duniani kama alivyokuja mara ya kwanza, hapana bali ni kwa lengo la KUNYAKUA. Na yeye mwenyewe alituambia atakuja kwa siri kama mwivi ajavyo usiku, mfano tu wa jinsi alivyokuja kwa mara ya kwanza halikuwa ni jambo lililotangazwa mabarabarani kwa kila mtu aliyepita, bali walifunuliwa watu wachache sana, wale tu ambao muda wao wote walikuwa wanaenenda katika haki yote, na kuutazamiwa wokovu huo, mfano wa Ana na Simoni. Vivyo hivyo na leo hii watakaofunuliwa siku ile ni wale tu watu ambao macho yao na mawazo yao yote yanaelekea mbinguni, usiku na mchana wanatamani Bwana aje alichukue kanisa lake waende zao kwa Baba. Watu wa dizaini hiyo siku ile ikifika haitawajia kama mwivi bali watajua kwani ni Mungu mwenyewe atawafunulia.Watavuna walichokuwa wamekipanda kwa muda mrefu.

Lakini pia lipo kundi lingine, ambalo leo tutaliangalia, linalofananishwa na wale wachungaji waliokuwa kule makondeni. Kama tunavyofahamu Bwana akija hatakuja kwa ajili ya ulimwengu mzima, bali atakuja kwa ajili ya Kanisa lake. Hivyo siku ile atapita katika kanisa lake kwa siri kuwachukua walio wake na kuondoka. Na ndio maana tunaona hata Bwana kuja kwake kwa kwanza kulianzia katika HORI LA KULIA NG’OMBE, KATIKA ZIZI LA MIFUGO, mahali ambapo kondoo wapo, mahali ambapo kondoo wake wanalishiwa, wanapotengewa chakula ndipo alipokuja. Na kama tunavyojua kondoo wa Kristo wapo katika kanisa lake. Na ndiko huko huko Bwana atakapotulia. Hatakuja katikati ya taasisi Fulani ya serikali au chama Fulani cha kisiasa au jumuia Fulani ya kikabila, au katikati ya taifa fulani. Hapana bali katika kanisa lake teule,walipo kondoo wake.

Na hivyo kama vile UTUKUFU wa Bwana ulivyowaangazia kwanza wale wachungaji waliokuwa makondeni, vivyo hivyo Utukufu wa kurudi kwa pili kwa Bwana utawaangazia kwanza wachungaji wake wote waaminifu walio duniani wanaojitaabisha kwa ajili ya kulilisha kondoo, Usiku na mchana wanaokaa huko makondeni, wanaozunguka huku na kule, wanaotafuta hiki na kile kwa ajili ya kulilisha kundi lake, Na hivyo siku wasiyodhani utukufu wa Mungu utawaangazia wote kwa pamoja, wao ndio watakuwa wa kwanza kufahamu ujio wa Kristo, hata kama watakuwa hawana maarifa ya kutosha juu ya mafunuo ya Mungu, lakini siku hiyo ikifika fahamu tu ndio watakaokuwa wa kwanza kuuona utukufu wa Mungu. Hatabakia mchungaji yeyote aliye mwaminifu ambaye hata uona utukufu huo, hata awe mbali kiasi gani, atauona tu.

Wengi wanaona kulichunga kundi la Mungu, ni kazi ya kujichosha, isiyo na malipo kujitaabisha kwa ajili ya watoto wa Mungu, wanaona kama hakuna faida yoyote, wanaona ni kheri wakafanye shughuli zao nyingine, kuliko kuhangaika na vinyesi vya mifugo, ni kazi isiyopewa heshima yoyote. Lakini kumbuka kuwa Kristo hatakuja kwa waasibu, wala kwa wafanyabiashara, wala kwa wanasiasa, wala kwa madaktari, bali kwa kanisa lake, na hivyo ni sharti awaone kwanza wale walichungao kundi hilo kisha wafuate wengine. Atawatafuta kwanza wale watoa posho wake, aliowaweka katika kanisa lake, wawape watu wake posho kwa wakati.

Hivyo nataka kukutia moyo wewe ambaye utatoa muda wako kulitazaa kundi la Mungu, usikate tamaa, kwasababu ipo siku UTUKUFU MKUU wa Bwana utakuangazia na siku hizo si mbali. Zidi kulihurumia kundi la Bwana kwa jinsi Mungu anavyokupa neema, ikiwa ni usiku ikiwa ni mchana, endelea kuitenda kazi, fundisha, onya , karipia, Na wakati wa Bwana ukifika utakuwa wa kwanza kulipokea lile fungu la utukufu wake.

Ubarikiwe sana.

Tafadhali “share” ujumbe huu kwa wengine, Na Bwana atakubariki.

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Zinazoendana:

SIRI YA MUNGU.

UPUMBAVU WA MUNGU.

KWANINI YESU ALIMUITA BABA YAKE “ABA”?


Rudi Nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments