UHARIBIFU WA MTU.

UHARIBIFU WA MTU.

Mathayo 15.1 “Ndipo Mafarisayo na waandishi toka Yerusalemu walipomwendea Yesu wakisema,

2 Mbona wanafunzi wako huyahalifu MAPOKEO YA WAZEE, kwa maana hawanawi mikono walapo chakula.

3 Akajibu, akawaambia, Mbona ninyi nanyi huihalifu amri ya Mungu kwa ajili ya MAPOKEO YENU?

4 Kwa kuwa Mungu alisema, Mheshimu baba yako na mama yako, na Amtukanaye baba yake au mama yake kufa na afe.

5 Bali ninyi husema, Atakayemwambia babaye au mamaye, Cho chote kikupasacho kusaidiwa na mimi ni wakfu,

6 basi asimheshimu baba yake au mama yake. Mkalitangua neno la Mungu KWA AJILI YA MAPOKEO YENU.

7 Enyi wanafiki, ni vema alivyotabiri Isaya kwa habari zenu, akisema,

8 Watu hawa huniheshimu kwa midomo; Ila mioyo yao iko mbali nami.

9 Nao waniabudu bure, WAKIFUNDISHA MAFUNDISHO YALIYO MAAGIZOYA WANADAMU.

10 Akawaita makutano akawaambia

11 Sikilizeni, mfahamu; Sicho kiingiacho kinywani kimtiacho mtu unajisi; bali kitokacho kinywani ndicho kimtiacho mtu unajisi.

12 Ndipo wanafunzi wake walipomwendea, wakamwambia, Wajua ya kuwa Mafarisayo walipolisikia neno lile walichukizwa?

13 Akajibu, akasema, Kila pando asilolipanda Baba yangu wa mbinguni litang’olewa.

14 Waacheni; hao ni viongozi vipofu wa vipofu. Na kipofu akimwongoza kipofu mwenzake, watatumbukia shimoni wote wawili.

15 Basi Petro akajibu, akamwambia, Tueleze mfano huo.

16 Yesu akasema, Hata sasa ninyi nanyi mngali hamna akili?

17 Hamjafahamu bado ya kuwa kila kiingiacho kinywani hupita tumboni, kikatupwa chooni?

18 Bali vitokavyo kinywani vyatoka moyoni;

navyo ndivyo vimtiavyo mtu unajisi.

19 Kwa maana moyoni hutoka mawazo mabaya, uuaji, uzinzi, uasherati; wivi, ushuhuda wa

uongo, na matukano.

20 HAYO NDIYO YAMTIAYO MTU UNAJISI; LAKINI KULA KABLA HAJANAWA MIKONO HAKUMTII MTU UNAJISI”

Habari hiyo ni baada ya Mafarisayo kuwashutumu wanafunzi wa Bwana Yesu, Ni kwanini hawanawi mikono kabla ya kula chakula.

Sasa katika Torati hakuna mahali popote Bwana Mungu aliwaagiza wana wa Israeli wanawe mikono kabla ya kula chakula, hakuna mahali popote kwenye biblia (katika Agano la Kale) Mungu alitoa maagizo ya namna hiyo..Yalikuwa ni mapokeo yalitengenezwa na wazee wa kiyahudi, kwamba ni lazima watu wanawe kabla ya kula,ni mambo waliyojitungia wao wenyewe tu!, na si kutoka kwa Mungu…Na ndio maana utaona hapo mafarisayo wanawalaumu wanafunzi wa Yesu “kwanini wanayahalifu wapokeo ya wazee”..na sio mapokeo ya Mungu.

Kwa ufupi utaratibu wa kunawa mikono kabla ya kula “yalikuwa ni mafundisho ya wanadamu” na si mafundisho ya Mungu. Sasa kwa kawaida tendo lolote au pokeo lolote la kimwili sio baya, lakini linapochukua nafasi ya mapokeo ya ki-Mungu ndipo linapokuwa ni Baya na lenye madhara makubwa sana.

Kwa mfano pokeo hilo la desturi ya kunawa mikono kabla ya kula chakula sio baya, ni lizuri na linafaa sana,hata kwetu tunalo, kwanza kwa ajili ya usafi na kwaajili ya ustaarabu. Lakini shida inakuja ni pale linapotumika kama ndio sababu ya Mungu kumbarikia mtu au kumlaani mtu. Na kutafsiriwa isivyopasa kwamba ndio kitu cha Muhimu sana Mungu anachokiangalia kwa mtu, na kwamba akikihalifu hicho basi ni dhambi kubwa sana kwa huyo mtu, Jambo ambalo Mungu hajaliagiza mahali popote pale kwa watu wake.Ndio maana Bwana Yesu alizidi kuwaambia maneno yale.

“8 Watu hawa huniheshimu kwa midomo; Ila mioyo yao iko mbali nami.

9 Nao waniabudu bure, WAKIFUNDISHA MAFUNDISHO YALIYO MAAGIZOYA WANADAMU”.

Sasa tukirudi kwenye kiini cha Somo a kinachosema ni kitu gani kimtiacho Mtu unajisi??

Sasa ni vizuri tukafahamu maana ya neno “unajisi” kama lilivyotumika hapa lina maana gani…Kumbuka unajisi uliotumika kwa wanyama “najisi” sio sawa na lilivyotumika hapa “kwamba vimtokavyo mtu moyoni ndivyo vimtiavyo mtu unajisi”…unajisi uliotumika kwa wanyama una maanisha “wanyama wasio safi” kwa kiingereza “unclean animals”..kwahiyo unajisi hapo kwa wanyama umetumika kama “kitu kisicho-kisafi”

Lakini katika mstari huu wa Mathayo 15:19 Bwana aliozungumzia kitu kimtiacho Mtu unajisi..hakumaanisha kuwa ni “kitu kimfanyacho mtu kutokuwa safi” hapana bali unajisi kama ulivyotumika pale ni “kitu kinacho mharibu mtu”..kwa lugha ya kiingereza ni “Thing that defiles a man”..Kwahiyo neno unajisi hapo limetumika kama “Uharibifu”…na sio “kitu kisichosafi”

Kwahiyo hiyo sentensi kwa ufasaha zaidi tunaweza kuutafsiri hivi..

17 Hamjafahamu bado ya kuwa kila kiingiacho kinywani hupita tumboni, kikatupwa chooni?

18 Bali vitokavyo kinywani vyatoka moyoni;navyo ndivyo VIMHARIBUVYO MTU.

19 Kwa maana moyoni hutoka mawazo mabaya, uuaji, uzinzi, uasherati; wivi, ushuhuda wa uongo, na matukano.

20 hayo ndiyo YANAYOMHARIBU MTU; lakini kula kabla hajanawa mikono Hakumharibu mtu”

Kwa sentensi hiyo basi tunaweza tukaona ni mambo gani yanayomuharibu Mtu…Ni mambo gani yanayoweza kuiharibu nafsi ya mtu, ni mambo gani yanayoweza kumletea mtu dhiki, na mateso, na mauti, wakati mwingine hata magonjwa…Hayo sio mengine zaidi ya matendo yote ya giza, kama uasherati, utukanaji, wizi, uuaji, mawazo mabaya n.k

Vyakula au kwa ufupi riziki za ulimwengu huu, haziwezi kutufanya tupatikane au tusipatikane na madhara, vyakula havina ulinzi wowote katika maisha yetu..Mali hazina ulinzi wowote katika maisha yetu, Bali vitokavyo mioyoni mwetu ndivyo vyenye ulinzi..Kadhalika vile vitokavyo mioyoni mwetu ndivyo vyenye kuleta kuharibu pia.

Tunajijenga kwa vile vyema vitokavyo mioyoni mwetu, na tunajiharibu kwa vile vibaya vitokavyo mioyoni mwetu… Huoni mawazo mabaya ndiyo yanayompeleka mtu kuua, kuiba, kuafanya uasherati, kutukana, kupandikiza chuki na masengenyo haya yote ndiyo yanayomletea mtu uharibifu wake mwenyewe..

Ndugu yangu ni vizuri kushika mapokeo tuliyopokea kwa waalimu wetu wa dini, au wazazi wetu kwamba tuzingatie mlo kamili, tujitunze kwa kila namna, tuchemshe maji ya kunywa, tufanye check-up kila mara ili tuepukane na magonjwa hatarishi, na tuwe watanashati..hayo ni mazuri sana na yanatufaa lakini pamoja na hayo ongezea kufahamu kitu hichi kimoja tena… “kikuingiacho mwilini mwako hakikuharibu wewe, bali kikutokacho moyoni mwako ndicho kikuharibucho”..Moyo wako msafi ndio utakaokupa afya mifupani mwako na maisha marefu ya kuishi sio aina ya vyakula unavyobadilisha, wala checkup unazozifanya kila wiki.

Mithali 4: 20 “Mwanangu, sikiliza maneno yangu; Tega sikio lako, uzisikie kauli zangu.

21 Zisiondoke machoni pako; UZIHIFADHI NDANI YA MOYO WAKO.

22 MAANA NI UHAI KWA WALE WAZIPATAO, NA AFYA YA MWILI WAO WOTE.

23 LINDA MOYO WAKO KULIKO YOTE UYALINDAYO; Maana ndiko zitokako chemchemi za uzima.

24 Kinywa cha ukaidi ukitenge nawe, Na midomo ya upotovu uiweke mbali nawe.

25 Macho yako yatazame mbele, Na kope zako zitazame mbele yako sawasawa.

26 Ulisawazishe pito la mguu wako, Na njia zako zote zithibitike;

27 Usigeuke kwa kuume wala kwa kushoto; Ondoa mguu wako maovuni”

Neno la Mungu linatuambia tulinde mioyo yetu kuliko vyote tuwezavyo kulinda maana ndiko zitokazo chemchemi za Uzima.

Ni matumaini yangu kuwa Bwana amekujalia kuona na kujua kile alichotaka ukione siku ya Leo. Na kutafuta Ulinzi wa Moyo wako.

Kama hujampa Bwana Yesu maisha yako, hujachelewa ni kheri ufanye hivyo sasa hivi, maana nyakati tunazoishi ni nyakati za hatari, miaka imesogea sana na Kristo yupo mlangoni kurudi..Anza mwaka huu kwa kuanza kuishi maisha mapya katika Kristo, tubu kwa kumaanisha kuziacha dhambi zako, na kisha katafute mahali wanapobatiza ubatizo sahihi wa maji tele na kwa Jina la Yesu Kristo, ukabatizwe kwa ajili ya ondoleo la dhambi zako kulingana na Matendo 2:38, Na Bwana Yesu Mwenyewe atakupa kipawa cha Roho wake Mtakatifu atakayeweza kukusaidia kushinda dhambi na kukuongoza katika kuijua kweli yote ya Biblia..Na kwa kufanya hivyo utakuwa umeokoka! Na kuwa na tumaini la Uzima wa Milele, na kwenda mbinguni na Bwana atakapokuja kulichukua kanisa lake.

Bwana akubariki.

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Zinazoendana:

MADHARA YA DHAMBI YA UASHERATI.

MSHAHARA WA DHAMBI

DALILI ZIPI ZITAMTAMBULISHA MTU KUWA AMEFANYIKA KIUMBE KIPYA?


Rudi Nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments