Kama ukichunguza watu wote walioathiriwa na ulevi wa kupindukia huwa wanaonyesha tabia zinazofanana, moja ya tabia hizo ni kutokujali jambo lolote linaloweza kuja mbele yake, mtu akishalewa hata hajali tena thamani ya utu wake, anaweza akavua nguo mbele za watu, utakuta kabla hajanywa alikuwa ni mtu mwenye heshima lakini akishalewa tu, matusi yaanza kumtiririka mdomoni mwake, anakuwa sio mtu wa kujali, sio mtu wa kujizuia, sio mtu wa kuchukua tahadhari kwa kitu chochote kile kitakachokuja mbele yake, anaweza akasimama katikati ya barabara kuu sehemu ambayo magari yanapita na kuanza kujiongelea mwenyewe bila kujali kuwa anaweza kugongwa na gari akafa. Na ndio maana hata ajali nyingi zitokeazo zinasababishwa na madereva kuwa walevi..Ni kwasababu gani? Ni kwasababu FAHAMU ZAO zinakuwa zimeshawatoka kwa wakati huo na kama ufahamu umeshawatoka basi hata ule uwezo wa kufikiri, wa kujitawala na wa kuchukua tahadhari unakuwa umeondoka ndani yao.
Lakini mtu huyo huyo uje umwangalie baadaye zile pombe zimeshaisha kichwani mwake, na hapo ufahamu wake umeshamrudia atajishangaa ni kwanini amelala mtaroni, ni kwanini alikuwa anawavunjia watu wengine heshima, na ni kwanini alikuwa hathamini uhai wake kusimama katikati ya barabara n.k..