Ipi tofauti kati ya KUHANI na MCHUNGAJI.

by Admin | 23 May 2024 08:46 am05

Jibu: Makuhani ni watu waliokuwa wanahudumu katika “Hema ya Mungu” wakati wana wa Israeli wakiwa jangwani na katika “Hekalu la Mungu” baada ya wana wa Israeli kuingia katika nchi ya ahadi na kumjengea Mungu nyumba.

Kazi ya Makuhani ilikuwa ni “kuwapatanisha watu na Mungu wao” kupitia damu za wanyama. Vile vile Makuhani walikuwa na kazi ya kuwafundisha wana wa Israeli torati, na wote walitoka katika kabila moja lililoitwa Lawi.

Kwa mapana na marefu kuhusu makuhani wa agano la kale, pamoja na kazi zao na tofauti yao na walawi wengine fungua hapa >>>Tofauti kati ya makuhani na walawi ni ipi?

Lakini tunapokuja kwa “Wachungaji” wenyewe ni watu maalumu walioteuliwa na kuchaguliwa na MUNGU kulichunga na kulilisha kundi lake kupitia Mafundisho ya Neno la Mungu, maonyo na Maombi!. (Soma Yohana 21:15-17).

Na hawa wanafanya kazi mfano wa zile za kikuhani katika nyumba ya Mungu. Isipokuwa wenyewe hawawapatanishi watu kwa damu za wanyama bali kwa damu ya BWANA YESU kupitia Neno lake. Hivyo Wachungaji nao ni MAKUHANI WA BWANA.

Lakini si tu wachungaji walio makuhani wa Bwana peke yao, bali hata watu wengine wote waliojazwa Roho Mtakatifu wana sehemu ya huduma ya kikuhani… Kwani ndivyo maandiko yasemavyo kwamba sote tumechaguliwa kuwa MAKUHANI KWA MUNGU WETU.

Ufunuo 1:5 “tena zitokazo kwa Yesu Kristo, shahidi aliye mwaminifu, mzaliwa wa kwanza wa waliokufa, na mkuu wa wafalme wa dunia. Yeye atupendaye na kutuosha dhambi zetu katika damu yake,

6  na kutufanya kuwa ufalme, NA MAKUHANI KWA MUNGU, naye ni Baba yake; utukufu na ukuu una Yeye hata milele na milele. Amina”

Hivyo kila mmoja aliyejazwa Roho Mtakatifu anayo huduma ya upatanisho (ambayo ndiyo ya kikuhani) ndani yake kupitia ile karama aliyopewa, ndio maana sote tuna uwezo wa kuhubiri injili na kuchungana sisi kwa sisi kupitia Neno la Mungu.

2Wakorintho 5:18 “Lakini vyote pia vyatokana na Mungu, aliyetupatanisha sisi na nafsi yake kwa Kristo, naye alitupa huduma ya upatanisho;

19  yaani, Mungu alikuwa ndani ya Kristo, akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake, asiwahesabie makosa yao; naye ametia ndani yetu neno la upatanisho.

20  Basi tu wajumbe kwa ajili ya Kristo, kana kwamba Mungu anasihi kwa vinywa vyetu; twawaomba ninyi kwa ajili ya Kristo mpatanishwe na Mungu”.

Kama wewe ni Mchungaji, unayesimamia kundi kama kiongozi,  basi simama katika nafasi yako ya kuchunga na kulisha kwani kuna hatari kubwa ya kutokufanya hivyo..

Ezekieli 34:1 “Neno la Bwana likanijia, kusema,

2 Mwanadamu, toa unabii juu ya wachungaji wa Israeli, toa unabii, uwaambie, naam, hao wachungaji, Bwana MUNGU asema hivi; Ole wao wachungaji wa Israeli, wanaojilisha wenyewe; je! Haiwapasi wachungaji kuwalisha kondoo?

3 Mnawala walionona, mnajivika manyoya, mnawachinja walionona; lakini hamwalishi kondoo.

4 Wagonjwa hamkuwatia nguvu, wala hamkuwaponya wenye maradhi, wala hamkuwafunga waliovunjika, wala hamkuwarudisha waliofukuzwa, wala hamkuwatafuta waliopotea; bali kwa nguvu na kwa ukali mmewatawala.

5 Nao wakatawanyika, kwa sababu hapakuwa na mchungaji; wakawa chakula cha wanyama- mwitu, wakatawanyika.

6 Kondoo zangu walitanga-tanga katika milima yote, na juu ya kila kilima kirefu; naam, kondoo zangu walitawanyika juu ya uso wote wa dunia; wala hapakuwa na mtu aliyewaulizia, wala kuwatafuta.

7 Basi, enyi wachungaji, lisikieni neno la Bwana;

8 Kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, kwa sababu kondoo zangu walikuwa mateka, kondoo zangu wakawa chakula cha wanyama-mwitu wote, kwa sababu hapakuwa na mchungaji, wala wachungaji wangu hawakutafuta kondoo zangu, bali wachungaji walijilisha wenyewe wala hawakuwalisha kondoo zangu;

9 kwa sababu hiyo, enyi wachungaji, lisikieni neno la Bwana;

10 Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, mimi ni juu ya wachungaji; nami nitawataka kondoo zangu mikononi mwao, nami nitawaachisha hiyo kazi ya kuwalisha kondoo; nao wachungaji hawatajilisha wenyewe tena; nami nitawaokoa kondoo zangu vinywani mwao, wasiwe tena chakula chao”.

Bwana YESU atusaidie sana.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

WACHUNGAJI WA BWANA MAKONDENI.

TOFAUTI YA MITUME, MANABII, WAINJILISTI, WACHUNGAJI NA WAALIMU NI IPI?

JE! UNAMPENDA BWANA?

Kwa namna gani tumefanyika Makuhani na Ufalme?.(Ufunuo 1:6)

JE! NINAWEZA KUPOTEZA FURAHA YA WOKOVU?

Rudi Nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2024/05/23/ipi-tofauti-kati-ya-kuhani-na-mchungaji/