JINSI YA KUPIGANA MAOMBI YA VITA.

JINSI YA KUPIGANA MAOMBI YA VITA.

Zaburi 144:1 “Na ahimidiwe Bwana, mwamba wangu, Anifundishaye mikono yangu vita, Vidole vyangu kupigana

Nakusalimu katika jina kuu la Bwana wetu Yesu Kristo, karibu tujifunze maneno yake ya uzima. Leo tutaona namna ya kuomba maombi ya vita. Tukisema maombi ya vita tunamaanisha maombi ya kushindana na nguvu zote za Yule mwovu katika ulimwengu wa Roho, maombi ya kulegeza vifungo na nira, na minyororo, na kuangusha ngome pamoja na kuta za Yule mwovu zinazokinzana na sisi katika ulimwengu wa Roho, kupitia majeshi yake ya mapepo wabaya.

Ndugu ni lazima ufahamu, Kuna aina nyingi za maombi, kuna maombi ya shukrani, maombi ya mahitaji, maombi ya upatanisho n.k.. Yote haya yana wakati wake wa kuyatumia. Lakini pia yapo maombi ya Vita, ambayo ni lazima sana na ni muhimu kwa Mkristo kuyatumia.

Hivyo siku ya leo tutaona ni jinsi gani tunaweza kutumia maombi haya ili tuziangushe ngome za adui yetu ibilisi kiwepesi.

Baadhi ya watakatifu hawajui namna ya kuomba, wanafikiri pale unaposema shindwa shetani! Shindwa shetani! Kwa Saa tatu, au usiku kucha ndivyo wanavyomwangusha ibilisi. Uhalisia ni kwamba, hatumshindi ibilisi kwa maneno yetu kuwa mengi, Bali tunamshinda ibilisi kwa Neno la Mungu kukaa ndani yetu kwa wingi. Ambalo hilo litakusaidia kujua SILAHA unazopaswa uzitumie kumpiga nazo shetani. Bila kufahamu Silaha zako za kiroho, ni ngumu sana kumshinda shetani kimaombi. Kwasababu maombi yako yatakuwa ni ya juu juu, yasiyokuwa na nguvu za kiroho.

Bwana asipokufundisha kupigana vita, haijalishi maombi yako yatakuwa na maneno mengi kiasi gani, huwezi angusha ngome za adui. Hivyo penda sana kulisoma Neno la Mungu kwa kulitafakari kwasababu huko ndiko utakapojifunza kupigana vita vyako.

Kibiblia zipo silaha nyingi ambazo Mungu alizitumia kuwapigania watu wake, na Leo tutaziorodhesha chache, na tutaona jinsi tunavyoweza pia kuzitumia rohoni. Kwasababu kumbuka Neno la Mungu halijaandikwa kutupa stori  Fulani tu, tuifurahie halafu basi hapana, bali kila tendo, kila Neno linatafsiri kubwa sana rohoni.

Hivyo hizi ni baadhi ya silaha ambazo Mungu alizitumia kuwasaidia watu wake kupigana vita;

MVUA YA MAWE:

Mvua ya mawe

Mungu aliangusha mvua ya mawe kubwa sana, kwa wale watu wa Yerusalemu na wenzake walioungana kupigana na Yoshua kipindi kile wanaenda kuimiliki nchi yao, Utaona baadhi yao waliuliwa na Israeli, lakini wengi wa hao Mungu alimalizia kutoa hazina yake ya mvua kubwa ya mawe ikawaangamiza wengi sana kuliko hata wale waliouliwa na Yoshua.

Yoshua 10:11 “Kisha ikawa, hapo walipokuwa wakimbia mbele ya Israeli, hapo walipokuwa katika kutelemkia Bethhoroni, ndipo Bwana alipowatupia mawe makubwa kutoka mbinguni juu yao hata kufikilia Azeka, nao wakafa; hao waliokufa kwa kuuawa na hayo mawe ya barafu walikuwa ni wengi kuliko hao waliouawa na wana wa Israeli kwa upanga”

Jinsi ya kuomba: Bwana peleka, mawe yako ya barafu, katika madhabahu Zote za ibilisi, peleka mvua yako ya barafu katika vilinge vya kichawi, vinavyosimama kinyume na imani yangu. Haribu, bomoa, kila mbinu iliyoundwa dhidi yangu mimi (Taja maeneo yote ya maisha yako). Kama ulivyomshindia Yoshua nishindanie na mimi. [Hivyo Endelea kuita mvua hiyo na katika ulimwengu wa Roho, kwa jinsi unavyoiita kwa imani ndivyo inavyokuwa].

KIKOTO:

Yesu alipoingia hekaluni, alikutana na watu walioigeuza nyumba ya Mungu kuwa pango la wanyang’anyi. Ndipo akaunda kikoto kile, akapindua meza zote na kuwachapa wote waliofanya biashara pale, akawafukuza hekaluni kwa mamlaka yote, hekalu likawa safi kwa muda mfupi.

Yohana 2:15 “ Akafanya kikoto cha kambaa, akawatoa wote katika hekalu, na kondoo na ng’ombe; akamwaga fedha za wenye kuvunja fedha, akazipindua meza zao; 16  akawaambia wale waliokuwa wakiuza njiwa, Yaondoeni haya; msiifanye nyumba ya Baba yangu kuwa nyumba ya biashara”

Namna ya kuomba: Bwana naunda kikoto chako, napindua madhahabu zote za kipepo zilizoundwa moyoni mwangu na Yule adui, ninatawanyisha, ninasambaratisha, kila uovu, kila sanamu iliyopachikwa na Ibilisi (taja maeneo yote yanayohitaji maombi), kinyume na mapenzi ya Mungu. Ninavuruga kazi zote za ibilisi, kikoto cha Bwana kisafishe mwili wangu, kisafishe ibada yangu, kisafishe maisha yangu ya rohoni, kisafishe nyumba yangu, Naondosha uovu wa kila namna hata katika kazi yangu. [Sasa kwa jinsi unavyoomba kwa bidii na kurejea tukio hilo, ndivyo katika Roho Bwana anamnyuka shetani kwa namna ile ile. Ng’ang’ania hapo omba kwa imani kwa muda mrefu, kwasababu ndivyo ibilisi anavyodondoshwa].

KELELE ZA VITA:

kelele za vita

Bwana hutumia vitisho pia, kuwaondoa maadui, utakumbuka wakati Fulani wana wa Israeli, walizungukwa na maadui kwa muda mrefu. Hadi nchi ikaingiwa na njaa, watu wakaanza kulana ili waishi. Lakini jinsi Mungu alivyowaondoa maadui zao inashangaza. Kwasababu alifanya tu, kuwasikilizisha sauti za vita. Hivyo wale maadui waliposikia waliogopa sana wakawa wanakimbia kwa hofu kubwa sana huku wanaacha nyara zao nyuma. Baadaye Wayahudi kwenda wanashangaa hawawaoni maadui zao, wakijuliza ni nini kimetokea, mpaka waache na nyara, wakagundua kuwa ni Bwana ndiye aliyewatetea. Ndipo wakazichukua nyara kiwepesi na vita vikawa vimeisha kwa namna ile.

2Wafalme 7:6 “Kwa maana Bwana alikuwa amewasikizisha Washami kishindo cha miendo ya magari, na kishindo cha farasi, kama kishindo cha jeshi kubwa; wakaambiana, Tazama, mfalme wa Israeli amewaajiri wafalme wa Wahiti, na wafalme wa Wamisri, waje wapigane nasi.  7 Kwa hiyo wakaondoka, wakakimbia kungali giza bado, wakaziacha hema zao, na farasi zao, na punda zao, na kimo chao vile vile kama kilivyokuwa, wakakimbia wapate kujiponya nafsi zao”

Namna ya kuomba: Bwana peleka sauti zako za vita, katika ngome ya ibilisi, wafukuze waende mbali nami, hazina zote na vipawa vyote walivyoniibia katika roho na mwili ninavirejeza kwa Sauti yako ya vita. Watawanyike kwa njia saba. Vyote walivyoviiba navirejesha, fungua mipaka yangu, safisha hema yangu, adui atoweke kwa sauti za vita vya Bwana. [ Omba kwa kutaja maeneo yote ambayo unataka Bwana akutetee katika hayo].

UPOFU:

Wale malaika wa Bwana walioshuka Sodoma ili kuipeleleza, walikutana na wenyewe wa mji ule, ambao walitaka kulala nao. Hivyo malaika wale wakiwa nyumbani kwa Lutu. Maandiko yanaema waliwapiga upofu watu wale wasiweze kuiona nyumba mpaka asubuhi. Utakumbuka pia Paulo alipofika katika kile kisiwa kilichoitwa. Alishindana sana na Yule mchawi mpaka akamwomba Mungu ampige kwa upofu akawa kipofu kwa muda.

Mwanzo 19:10”Lakini wale watu wakanyosha mikono yao, wakamwingiza Lutu kwao nyumbani, wakaufunga mlango.  11 Kisha wakawapiga hao watu walioko mlangoni kwa upofu, wadogo kwa wakubwa, hata wakachoka kwa kuutafuta mlango”.

Namna ya kuomba: Bwana piga upofu majeshi ya mapepo yote mabaya yaliyokuja kufanya vita kinyume changu mimi, wasione roho yangu, uufiche uhai wangu ndani yako, shusha kiwi na giza mbele yao. Wapapase, wasione huduma yangu, (taja mambo yako yote ambayo unatamani ibilisi asiyaone), waangamie na kuishia shimoni, watafute lakini wasione. [Hivyo Kwa jinsi unavyosimamia vifungu hivyo ndivyo unavyoshinda vita rohoni kiwepesi kwasababu mambo hayo yanatendeka kwelikweli].

JIWE LA MUNGU:

maombi ya vita jiwe la Yesu

Jiwe la Mungu ni Yesu. Yeye mwenyewe alijifananisha na jiwe hilo lililo zito sana na gumu. Akasema. Likimwangukia mtu linamsaga tikitiki, na yoyote atakayeliangukia atavunjika vunjika Kuonyesha ni jinsi gani lilivyo bora, ndio lile lililopiga sanamu ya Nebukadreza, na kuisaga kama unga, na kupotea kabisa(Danieli 2:34).

Mathayo 21:44  “Naye aangukaye juu ya jiwe hilo atavunjika-vunjika; naye ye yote ambaye litamwangukia, litamsaga tikitiki”.

Namna ya Kuomba: Yesu simama mwenyewe unitetee, kama jiwe lililo hai lenye nguvu na imara. Piga kila aina ya kuta nzito za ibilisi zinazozuia upenyo wangu. Nazibomoa kwa jiwe hili, ninalirusha katika kila Nyanja, impige ibilisi katika kipaji cha uso wake, aanguke kama Goliathi mbele ya Daudi. Wewe uliye jiwe piga kila ngome, ya mwovu lisage na kuharibu na kusagasaga, kazi zote za mwovu mbele yangu ziwe kama makapi mbele ya Upepo.[Lielekeze jiwe hili, liangushe kwelikweli kwa imani ndivyo itakavyokuwa katika ulimwengu wa roho]

Natumai mpaka hapo umeshapata mwangaza wa namna ya kulitumia Neno kuomba maombi haya ya vita, Kwasababu ya muda, hatuwezi toa maelezo ya silaha zote zilizo katika biblia, Hivyo hizi ni silaha nyingine ambazo zitumie, zikusaidie.

6) UPEPO WA KUSULISULI NA RADI:  Andiko la kusimamia (Zaburi 77:18). Omba Bwana avuruge, na kuichosha mikakati yote ya adui dhidi yako mfano wa kisulisuli kizungushacho makapi.

7) GHARIKA YA BWANA: Andiko la kusimamia (Mwanzo 6:17). Kama Bwana alivyoangamiza waovu wakati ule wa Nuhu kwa gharika Omba Bwana akafungue madirisha yake ya mbinguni, agharikishe majeshi ya kipepo yanayokufuatilia yakuangamize, yaangamie kama majeshi ya Farao katika bahari ya Shamu.

8) UPANGA WA BWANA: Andiko la kusimamia (Ufunuo 19:15). Omba ule upanga wa Bwana ukatao kuwili, ukate, na kuua mambo yote maovu ya adui yanayosimama mbele yako

9) KUTAWANYWA USEMI: Andiko la kusimamia (Mwanzo 11:7-9). Kama alivyouvuruga usemi wa wajenzi wa Babeli wasielewane, vivyo hivyo akaruge hila za ibilisi na mapepo yake zisipatane juu yako.

10) MOTO WA BWANA: Andiko la kusimamia (2Wafalme 1:10). Moto ukaunguze mapando yote, ya ibilisi, aliyoyapanda moyoni mwako,

11) NZIGE, PARARE, MADUMADU, TUNUTU: Andiko la kusimamia (Yoeli 2:25). Bwana akatume jeshi lake la waharibuo, wakatafune kazi zote za mwovu, wakalete hasara, warudishe nyuma, na kudhoofisha ufalme wote wa giza.

12) MAJIPU YA BWANA: Andiko la kusimamia (Kutoka 9:9). Bwana alete hali mbaya ya mateso, kwa wakuu wote wa giza wafanyao vita kinyume na wewe.

13) TETEMEKO: Andiko la kusimamia (1Samweli 14:15) . Bwana alete utisho na mashaka, na tetemeko kwa wakuu wa giza na mapepo yasimamo kinyume cha kazi ya Mungu.

14) UKAME (kiu na njaa): Andiko la kusimamia (Amosi 8:11). Bwana alete ukame wa kiroho, kwa majoka yote yanayosimama kutaka kumeza watu wa Mungu, yafe na kuteketea kwa kukosa mawindo ya watu.

15) RUNGU LA BWANA: Andiko la kusimamia (Yeremia 51:20).  Lipige na kuleta majeraha katika ufalme wa giza, liziraishe mapepo yote na vikaragosi vyake vyote vifanyavyo vita na wewe.

Zipo na silaha nyingine nyingi katika maandiko Hatuwezi kuziorodhesha zote, Hivyo kwa jinsi Neno la Mungu linavyokaa ndani yako, ndivyo utakavyoweza kuzivumbua na kuzitumia. Na zote hizo ni sharti tuziombe katika jina la Yesu na uweza wa damu yake.Maombi ya namna hii yana nguvu sana, na yatakufanya udumu kwa muda mrefu katika kuomba. Na kufungua vifungo vingi sana katika ulimwengu wa Roho.

Kumbuka pia, vita hivi hatuvielekezi kwa wanadamu, bali kwa Shetani na majeshi yake ya mapepo na kazi zake zote. Kwasababu maandiko yanasema vita vyetu sio juu ya damu na nyama, maana yake ni kwamba sio juu ya wanadamu wenzetu. Bali ni juu ya falme za giza, zikawaachilie mateka, waje kwa Bwana, na sio tuwaue wao pamoja na mateka wao.

Waefeso 6:12  “Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho. 6.13  Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama”

Bwana akubariki.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Jiunge na kundi letu la mafundisho ya Biblia whatsapp kwa kubofya hapa >> WHATSAPP-GROUP

Mada Nyinginezo:

KUNA AINA NGAPI  ZA MAOMBI?

FAHAMU JINSI MUNGU NA SHETANI WANAVYOZUNGUMZA NA WATU.

VITA DHIDI YA MAADUI

NITAJUAJE KAMA MAOMBI YANGU YAMEFIKA (YAMEJITOSHELEZA)?

JINSI SHETANI ANAVYOZUIA MAJIBU YA MAOMBI YETU.

Kwanini kuna watu wanafanyiwa deliverance (Maombi ya kufunguliwa), lakini baada ya muda wanarudiwa tena na hali ile ile sababu ni nini?

Nini maana ya “Andiko huua, bali Roho huhuisha (2Wakorintho 3:6)

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
5 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Anonymous
Anonymous
1 year ago

Mungu awatunze

SAGARA
SAGARA
1 year ago

Mbarikiwe sana kwa ujumbe mzuri

Letcia Alphonce
Letcia Alphonce
1 year ago

Asante

NIYIKIZA
NIYIKIZA
1 year ago

Asanteni