VITA DHIDI YA MAADUI

VITA DHIDI YA MAADUI

Shalom karibu tujifunze Neno la Mungu, Maandiko yanatuambia “kumcha Bwana ni chanzo cha Maarifa”… Maneno ya Yesu Kristo yanafaida kubwa katika maisha zaidi hata tunavyofikiri.  Kwa jinsi tunavyozidi kumcha Bwana maarifa yetu ndivyo yanavyozidi kuongezeka siku baada ya siku, mpaka tunapofikia kiwango kile cha Maarifa cha kumfahamu yeye anachotaka tukifikie sisi kama tunavyosoma katika Waefeso 4:13. 

Nilipita sehemu Fulani, nikapisha na dada mmoja aliyekuwa anaongea na mwenzake, walikuwa wanatembea kwa kasi kidogo lakini nilifanikiwa kusikia moja ya kauli zake  akisema “tumepewa mamlaka ya kukanyaga nge na nyoka…akaendelea kumwambia mwenzake “adui yako akija mbele yako usimsubirishe we mkanyage..kwa maana tumepewa mamlaka hayo ”…Akiwa na maana kuwa mtu akija mbele yako ambaye yupo kinyume chako mdhuru kabla yeye hajakudhuru biblia imeturuhusu kufanya hivyo, tena hakikisha unammaliza kweli kweli.

Niliposikia hivyo nilisikitika sana, nikasema Bwana atusaidie kweli kweli,

Ndugu yangu nataka nikwambie..katika Agano jipya hatuna adui yoyote ambaye ni Mwanadamu…Adui yetu ni Shetani na majeshi yake, kwa maana kupigana kwetu sisi si juu ya damu na nyama, maandiko yanatuambia hivyo… Vita juu ya damu na nyama vilikuwa katika Agano la kale, ndio maana tunawaona watu kama wakina Daudi, Sulemani, Sauli na wengine wote ndio waliokuwa na maadui ambao ni wanadamu kwasababu, bado walikuwa hawalijui agano lililo bora zaidi. Kwa neema Mungu aliyowapa aliwaruhusu wawaone maadui zao kwa njia ya kibinadamu, lakini haikuwa hivyo tangu mwanzo. Tangu Edeni adui wa kwanza wa mwanadamu alikuwa ni shetani.

Kwahiyo baada ya dhambi Mungu aliruhusu tuishi katika vipengele pengele Fulani vya maisha ambavyo vingi havikuwa ni njia kamili au mpango kamili wa Mungu japo aliviruhusu, kwamfano aliruhusu talaka, aliruhusu ndoa za wake wengi. N.k

 Lakini ulipokuja utimilifu wote ulioletwa wa lile Neno lililofanyika mwili ambaye ni Bwana wetu Yesu Kristo, kwa Neema aliweka mambo yote kama yanavyopaswa yawe katika utimilifu wote..ndio maana Bwana aliwaambia “watu haikuwa hivyo tangu mwanzo”,..wao walikazana kumwambia Bwana mbona Musa alifanya hivi, alisema vile…lakini Kristo alizidi kuwaambia haikuwa hivyo tangu mwanzo..

Na leo jambo ni lile lile watu tunaweza kujiuliza mbona Daudi alikuwa na maadui na aliwaua na aliwalaani… na sisi tufanye hivyo hivyo, lakini Kristo anatuambia haikuwa hivyo tangu mwanzo…haikuwa hivyo tangu mwanzo kujilipiza kisasi, haikuwa hivyo tangu mwanzo kumlaani mwanadamu mwenzako (ambaye tunaona roho ya uadui ipo ndani yake)…Utauliza hayo maneno yanatoka wapi kwenye biblia?..soma

Luka 6:28 “wabarikieni wale ambao wawalaani ninyi, waombeeni wale ambao wawaonea ninyi.”

Mathayo 5:43 “Mmesikia kwamba imenenwa, Umpende jirani yako, na, Umchukie adui yako; lakini mimi nawaambia, Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi”..

38 Mmesikia kwamba imenenwa, Jicho kwa jicho,na jino kwa jino; Lakini mimi nawaambia, Msishindane na mtu mwovu; lakini mtu akupigaye shavu la kuume,mgeuzie na la pili” 

Hayo ni maneno ya Bwana Yesu mwenyewe..anasema “mmesikia imenenwa….”

Sasa swali wamesikia kutoka kwa nani? Jibu ni wamesikia kutoka Kwa mababa waliowatangulia ambao ndio hao wakina Musa, Daudi, Eliya na wengine wote…

Ndugu yangu unaposoma kitabu cha Zaburi, pasipo uongozo wa Roho Mtakatifu wa kujua nyakati Mungu alizokuwa anatembea kwa kila nyakati itakupoteza kwasababu ndani ya Zaburi hiyo hiyo kuna sehemu imehalalisha mvinyo, Ndani ya zaburi hiyo hiyo usipokuwa na msaada wa roho kuielewa unaweza ukajifunza chuki na visasi, ndani ya sheria za Musa na torati pasipo msaada wa roho unaweza kujifunza mauaji na kiburi…Na ndani ya hiyo hiyo biblia unaweza kujifunza uasherati kama wengi sasahivi wanavyoitumia kuhalalisha ndoa za mitara.

Sasa tukirudi kwenye suala la “Maadui zetu”…swali ni je! Maadui wetu ni wakina nani sasa?

Kumbuka Tangu mwanzo adui ni Ibilisi biblia inasema hivyo, yeye ndiye atushitakiaye mbele za Mungu mchana na usiku, na ni mfano wa simba angurumaye atafutaye mtu wa kummeza (1 Petro 5:8). Huyo ndio adui yetu wa kwanza na wa mwisho, hivyo kwa kutumia majeshi yake ya mapepo wabaya..ndio anafanya vita na sisi.

Anayatuma mapepo yake yanawaingia watu, kwahiyo Yule mtu anageuka kuwa ofisi ya shetani kwa kujua au pasipo kujua..ndio hapo unakuta mtu anakuchukia ghafla pasipo sababu, au anakutafutia hila, anaanza kukupiga vita, au kukutafutia madhara, au wivu au anafurahia kuanguka kwako!…au anatafuta namna ya wewe kuiacha imani, sasa chanzo sio Yule mtu, bali ni roho iliyoko ndani yake…roho iliyoko ndani yake ndio roho ya uadui.

Sasa sio jukumu letu sisi kupambana na Yule mtu, kama watu wa agano la kale walivyokuwa wanafanya bali ni jukumu letu kupambana na ile roho inayotenda kazi ndani yake,  Yule mtu yeye ni  kama ofisi tu!! Awe anajua au asiwe anajua.. Watu wa agano la kale kama wakina Daudi walikuwa wanapambana na watu kwasababu bado walikuwa hawajapewa neema ya kujua chanzo cha mambo yote ni wapi lakini sisi tumepewa….

Ndio hapo biblia inatuambia katika

Wafilipi 6:11 “ Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani.

12 Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; BALI NI JUU YA FALME NA MAMLAKA, JUU YA WAKUU WA GIZA HILI, JUU YA MAJESHI YA PEPO WABAYA KATIKA ULIMWENGU WA ROHO”

Hapo Neno linatuambia “tuweze kuzipinga hila za shetani na sio mwanadamu”.

Sasa namna ya kuipiga na kuikanyaga hii roho ya adui iliyopo ndani ya ndugu zetu!! Namna ya kuitowesha kabisha, na kuiharibu tumepewa silaha madhubuti za kuiangusha, pasipo kuidhuru ile ofisi shetani anayoitumia, maana nia na madhumuni ni kuipiga ile roho na kuiacha ile ofisi huru iokoke ili itumiwe na Mungu kama ofisi ya Nuru. Haleluya!!, sasa silaha za kuipiga ile roho ndio hizi zifuatazo.

Waefeso 6:13 “Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama..

1)   Basi simameni, hali mmejifunga KWELI VIUNONI– Hakikisha unaifahamu kweli yote ya biblia, unamfahamu Yesu Kristo katika ukweli wote,Maneno ya Mungu kama haya.

2)   Dirii ya Haki kifuani– Hakikisha unauelewa vizuri ufunuo wa kuhesabiwa haki kwa Imani, kwamba sio kwa matendo tunaokolewa bali kwa neema, sio kwa matendo tunaponywa bali kwa neema, si kwa matendo tunapata ulinzi kutoka kwa Mungu bali kwa neema, sio kwa matendo tunampendeza Mungu bali kwa Neema kupitia Yesu Kristo. Hiyo itakusaidia shetani anapoleta mashtaka yake ya kukuhukumu ndani ya moyo wako, au nje unakuwa na mafuta ya kutosha kumshinda hoja zake, na kutokupepeswa na maneno ya mwovu yanapokuja juu yako.

3)    kufungiwa miguu utayari tupatao kwa Injili ya amani– Hii ni silaha ya tatu madhubuti kabisa ya kuiharibu ile roho ya uadui ndani ya mtu, hatua hii ni ile mtu anapochukua hatua ya kwenda kumhubiria INJILI Yule mtu ambaye roho ya uadui ipo ndani yake, na kumhubiria sio tu kwa maneno bali kwa kielelezo cha matendo, unakwenda kumhubiria habari njema za wokovu, una mwombea, unaonyesha upendo, akikuomba chakula unampa,akikuomba nguo mvike, na hiyo inapelekea  Ile roho iliyoko ndani yake inapungua nguvu kwa kasi sana, na kutengeneza njia ya ushindi wa vita.

4)   Ngao ya Imani –Imani ni kuwa na uhakika wa mambo yatarajiwayo, kwa lolote lile shetani atakalolileta, una imani kuwa halitafanikiwa, na zaidi ya yote una Imani kuwa wewe ni mwana wa Mungu mrithi wa ahadi zake, na hakuna chochote kitakachokudhuru, hata jeshi la mapepo kiasi gani,hata waganga wote duniani wakiungana kupambana wewe hakuna jambo lolote litakalofanikiwa kwasababu upo chini ya damu. Na unaimani kuwa  lolote umwombalo Baba atakutendea

5)   Tena ipokeeni chapeo ya wokovu– Chepeo ni HELMET kwa kiingereza, kazi yake ni kulinda sehemu ya kichwa..Na sisi tunaposimama mbele ya Adui yetu shetani, silaha yetu nyingine ni tumaini la Wokovu tulionao, kwamba tumemwamini Yesu Kristo aliyetukomboa kwa damu yake, na kutuahidia ukombozi wa miili yetu, kwahiyo hakuna chochote kitakachoweza kututoa kwake kwa kupitia Roho wake Mtakatifu tumetiwa Muhuri mpaka siku ya ukombozi wetu (Waefeso 4:30). Na huko huko ndio unajifunza kusamehe. Kwasababu unajua na wewe ulisamehewa deni kubwa kushinda hilo la ndugu yako.

6)   Upanga wa Roho ambao ni neno la Mungu– Hii ndio silaha ya mwisho na ya umuhimu kuliko zote.. ukilifahamu Neno la Mungu, hakuna elimu yoyote ya shetani itakayokupiga chenga, kwasababu shetani naye anayo injili yake ambayo inafanana sana na injili ya Kweli, ambayo kwake nayo ni kama UPANGA anayokatakata nayo watu, ndio ile aliyokuwa anataka kumkata nayo Bwana kule jangwani injili ya “imeandikwa”..

lakini Bwana alimshinda kwasababu Neno la Mungu lilikuwa limekaa ndani yake kuliko shetani. Upanga wa Kristo ulikuwa mkali kuliko wa shetani aliweza kumkata shetani kwa kumjua hila zake na njama zake na mawazo yake… Waebrania 4:12 “ Tena Neno la Mungu li hai tena lina nguvu tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake, tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo”.alimshinda kwa Neno.

Hizo ndizo silaha 6 Muhimu na pekee za kushindana na Adui yetu shetani. Sasa kumbuka katika vita adui yako na yeye kavaa kama wewe, na yeye ana kweli yake kiunoni, ana dirii yake kifuani, ana chepeo yake kichwani ana injili yake miguuni, na ana upanga wake mkononi amepewa na shetani. Hivyo Ndivyo alivyo shetani ana injiili yake ya uongo ana imani yake ya uongo, ana wokovu wake wa uongo, ana haki yake ya uongo…yote hayo ni kwaajili naye kujilinda,lakini kwasababu sisi tunavyo vya ukweli na vyenye nguvu kuliko vyake tunamshinda. Lakini kama hatuna hata kimoja cha ukweli atatukatakata na upanga wake na kutuweka chini.

Sasa tutajuaje kwamba tumeshinda vita? Tutajua tumeshinda vita vizuri kama tutakuwa tumefanikiwa kumleta Yule mtu kwa Kristo, au tumempandia mbegu ya Kristo ndani yake, Kwasababu Yule ni mtu wa Mungu, anayestahili wokovu kama wengine tu! Kama sisi,  naye pia Mungu hapendi kumwona anakwenda kwenye ziwa la moto, naye anasikia maumivu kama sisi, na anahisia zote kama sisi tulizonazo.

Lakini endapo tukikosa shabaha! Na kuanza kupambana na Yule mtu badala ya kupambana na roho iliyopo ndani yake, na kuanza kumrudishia ubaya, kuanza kumlaani, kuanza kumwombea afe…na kusema Bwana katupa mamlaka ya kukanyaga nge na nyoka kwahiyo tumkanyage yeye kweli kweli, hapo tutakuwa hatujashinda vita bali tumeshindwa vita!! Na kugeuka kuwa vyombo vya shetani.

Na unajua ni sisi tu wakristo ndio hatuna hekima katika ukristo wetu, lakini watu wa ulimwengu huu kama biblia inavyosema wana hekima katika mambo yao…Kwamfano serikali inapotangaza vita dhidi ya UMASKINI, MARADHI na UJINGA..Huwezi kuona inakwenda kupambana na wagonjwa hospitalini, huwezi kuona inaenda kuua wagonjwa na kusema tunapapambana vita dhidi ya maradhi, au huwezi kuona inakwenda kuwaua maskini wa nchi na kusema tunapambana vita dhidi ya umaskini, au huwezi kuona serikali inakwenda kuwaua au kuwafukuza watu wasio na elimu kwa kisingizio cha kupambana vita dhidi ya Ujinga, badala yake utaona itaenda kutafuta suluhisho na tiba kwa watu wake waondokane na umaskini, maradhi na kukosa elimu..Lakini sisi wakristo ndio namba moja kuuwa watu wenye magonjwa ya kiroho, umaskini wa kiroho na ujinga wa kiroho na kusema ni maadui zetu! Yaani Inaonyesha ni jinsi gani hatujielewi!!!

Wakati Fulani Bwana alipokuwa anakwenda Samaria kuhubiri, wenyeji wa mji ule walimkataa, ndipo wanafunzi wake wakamwambia tushushe moto kama Eliya uwaangamize..lakini Bwana hakufanya vile kwasababu alijua tatizo sio hao watu bali ni roho iliyo ndani yao..akawaambia wanafunzi wake Mwana wa Adamu hakuja kuangamiza roho bali kuokoa.

Luka 9: 52 “akatuma wajumbe kutangulia mbele ya uso wake; wakaenda wakaingia katika kijiji cha Wasamaria, ili kumtengenezea mahali.

53 Lakini wenyeji hawakumkaribisha kwa vile alivyouelekeza uso wake kwenda Yerusalemu.

54 Wanafunzi wake Yakobo na Yohana walipoona hayo, walisema, Bwana, wataka tuagize moto ushuke kutoka mbinguni, uwaangamize; [kama Eliya naye alivyofanya]?

55 Akawageukia, akawakanya. [AKASEMA, HAMJUI NI ROHO YA NAMNA GANI MLIYO NAYO.]

56 Kwa maana Mwana wa Adamu hakuja kuziangamiza roho za watu, bali kuziokoa. Wakaondoka wakaenda mpaka kijiji kingine”

Sasa kama Bwana hakufanya hivyo kwanini sisi tufanye hivyo?? Tutakuwa na roho gani ndani yetu??..bila shaka itakuwa ni roho ya Ibilisi!! Roho ya kuangamiza badala ya kuokoa…

Nataka nikuambie tu ndugu, nge wetu ni shetani na nyoka wetu ni shetani, hao ndio tuliopewa mamlaka ya kuwakanyaga..na hatuwakanyagi kwa maneno bali kwa hizo silaha 6 hapo juu!!..Maombi ya kuwatakia shari ndugu zako acha kuanzia leo, maombi ya kuwalaani wale wanaokuudhi acha kuanzia leo, muhubiri au mwalimu anayekufundisha hivyo anakufundisha uongo na anakuhubiria uongo!!

Tena wengine wanaaambiwa watu kabisa waandike majina ya maadui zao wayaweke kwenye maboksi wayaombee wafe!! HAYO NI MAFUNDISHO YA MASHETANI!!..Kwanini usiweke jina la adui yako kwenye boksi umwombee ampe Kristo maisha yake? Kuliko kumwombea afe!!.Fikiria ni mama yako anaombewa afe na mtu mwingine wewe utafurahia kitendo hicho?. Mambo yale tunayotaka tutendewe sisi ndio tutendee wengine Bwana alitufundisha hivyo.

Warumi 12:14 “Wabarikini wanaowaudhi; barikini, wala msilaani.”

Ni maombi yangu kuwa Bwana atakujalia kuyaona hayo na zaidi ya hayo.

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Zinazoendana:

KISASI NI JUU YA BWANA.

KWA KUWA WASEMA MIMI NI TAJIRI.

OKOA BADALA YA KUANGAMIZA!

NA JINA LAKE AITWA, NENO LA MUNGU.

SAMEHE KUTOKA NDANI YA MOYO WAKO.

MAUTI NA KUZIMU ZIKAWATOA WAFU WALIOKUWAMO NDANI YAKE.

NITASHINDAJE HALI YA KUUMIZWA NA MANENO YA WATU!


Rudi Nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
6 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Emmanuel Kitengule
Emmanuel Kitengule
1 year ago

Kwa kweli Mungu atusaidie sana,UJINGA unatumaliza sana wakristo wa leo.Umenitoa kwenye kifungo cha UJINGA kwenye hili eneo.BARIKIWA SANA MWALIMU.

Hamisi Nkuluzi
Hamisi Nkuluzi
3 years ago

Safi sana mtumishi nimebarikiwa pia nakubaliana na mtazamo na msimamo wangu tusichanganya utekelezaji kwa kuchukua sehemu ya ule wa Sheria ya Torati ya Musa , tutashindwa kwa kutokuzingatia maelekezo ya Bwana Yesu.

Seth
Seth
3 years ago

Nimebarikiwa?