NITASHINDAJE HALI YA KUUMIZWA NA MANENO YA WATU!

NITASHINDAJE HALI YA KUUMIZWA NA MANENO YA WATU!

Wakati mwingine, unaweza ukapitia hali ya kusemwa vibaya, kwa siri au hadharani, Tambua tu hiyo ni hali ya kawaida, wewe sio wa kwanza, hata walio watu wakuu na wakubwa na wanaoheshimika wanasemwa vibaya, hata kama wamefanya mazuri mangapi katika jamii, eneo la kuzungumziwa vibaya, haliepukiki katika Maisha yao.
 
Mtu aliyekuwa mkamilifu, na asiye na dhambi, na Zaidi ya yote ni Mungu, (Bwana wetu Yesu Kristo) alisemwa vibaya mara nyingi sana, sasa kama yeye alisemwa vibaya na alikuwa hana dhambi hata moja! Wewe ni nani usizungumziwe vibaya?..Kwahiyo hilo ni jambo ambalo halikwepeki maadamu bado tupo hapa duniani..Wakati mwingine unaweza ukaambiwa maneno makali hata na watu wako wa karibu sana, ambao usingeweza kutazamia kama wangekwambia maneno hayo…
 
Mfano katika Biblia tunamwona mtu mmoja aliyeitwa YEFTHA, Huyu alikuwa mzaliwa wa kwanza kwa Baba yake, lakini mama yake alikuwa ni kahaba, kwahiyo alizaliwa na mama kahaba, na baadaye Baba yake akaoa mke wa halali akazaa naye Watoto, lakini hao Watoto walipokuwa mkubwa wakamtamkia hadharani Yeftha kwamba hatakuwa mrithi pamoja nao kwasababu yeye ni mwana wa mwanamke mwingine kahaba, wakamfukuza..Na niwazi kuwa pia walitaka kumdhuru maana aliwakimbia na kuhamia kabisa nchi nyingine, na sio tu ndugu zake walimchukia, bali na Taifa zima lilimtenga. (Habari hizi utazipata katika kitabu cha Waamuzi Mlango wa 11 na kuendelea).
 
Kwahiyo Yeftha akaondoka katika nchi yake, akiwa peke yake, watu maskini wasio na maana (mabaradhuli) waliochoka kama yeye, wakaenda kuungana naye huko alikokwenda… Lakini Mungu alilitazama teso lake, wakati ulipofika alimnyanyua Yeftha kama alivyomnyanyua Yusufu, na akawa MWAMUZI katika Taifa Teule la Mungu (Israeli)..Shujaa wa Bwana,haleluya!!..Wale wote waliomfukuza walikuja kumwomba msaada kwa kumsihi sana, Taifa zima lilikuja kumwomba msaada katika vita. Kwasababu maandiko yanasema katika
 
1Samweli 2 :6 “Bwana huua, naye hufanya kuwa hai; Hushusha hata kuzimu, tena huleta juu.
7 Bwana hufukarisha mtu, naye hutajirisha; Hushusha chini, tena huinua juu.
8 Humwinua mnyonge kutoka mavumbini, Humpandisha mhitaji kutoka jaani, Ili awaketishe pamoja na wakuu, Wakakirithi kiti cha enzi cha utukufu; Kwa maana nguzo za dunia zina Bwana, Naye ameuweka ulimwengu juu yake”.
 
Sasa leo tutajifunza ni namna gani tutashinda hali ya kusemwa au kutamkiwa maneno mabaya. Unajua wanadamu wote tumeumbwa na moyo, moyo kwa lugha nyingine tunaweza kusema ni (utu wa ndani), sasa uwezo wa moyo kuhifadhi hisia au maumivu ni mkubwa kuliko mwili, kidonda cha mwili kikipona kimepona kikishabaki kovu kinakuwa sio kidonda tena, hata upaguseje pale hapawezi kusababisha maumivu tena, Zaidi ya yote pakipona ndio panaweka gamba gumu zaidi(sugu)…kwasababu kidonda kimeshapona…Lakini moyo haupo hivyo, vidonda vyake haviponi kirahisi hivyo na inaweza ikapita miaka hata 10, lakini pale palipoumizwa pakiguswa tena kidogo tu! Ni kama umeanza mwanzo tena.
 
Kwahiyo hapo ni kuwa makini sana..Vinginevyo tusipofahamu namna ya kushughulika na utu wetu wa ndani, tutakuwa tunaishi Maisha ya maumivu na kutokusamehe kila siku…
Sasa dawa ya kuzuia kuumizwa ni ipi?
Ni kujitahidi kutokuweka jambo moyoni, au kwa lugha nyingine unakuwa unajitahidi kuyapotezea kwenye kichwa chako baadhi ya mambo, unakuwa huyachukulii kwa uzito..Kwamfano mtu amekwambia labda neno la “kukudhalilisha au kukushushia heshima”..jambo lile kabla ya kuanza kuliweka moyoni na kuanza kulitafakari na kujiuliza uliza kwanini mtu yule kaniambia vile, kwani kanionaje?….Utumie muda huo kufikiri ingekuwa ni wewe umemwambia vile, ungekuwa na maana gani?.
 
Ukiona mtu kakutukana, hebu fikiria wewe uliowatukana moyoni mwako, je! ulikuwa una nia gani mbaya nao?..utagundua basi tu! Uliwatukana pengine kwa hasira za pale pale na iliishia hapo tu!…huwezi kufikiri kwamba mtu uliyemtukana kwamba afikiri unamchukia, au una kinyongo naye… au umemtafakari sana, au yupo kwenye akili yako muda wote, na umekusudia kumwumiza, kwa kiwango anachokifikiria moyoni mwake…..wewe ulimtukana tu kwasababu zako… basi imeishia hapo tu!.
 
Kadhalika na wewe unapotukanwa au unapodharauliwa, hupaswi kuliweka jambo moyoni, kwasababu yule aliyekudharau, pale alipokudharau pengine haikupita hata dakika tano kashasahau kwamba alikudharau…Hivyo wewe unabaki na majeraha, wakati mwenzako moyo wake umeshasafishika siku nyingi, na pengine anampango wa kuja kuendelea kuwa na wewe, na kushirikiana na wewe kwa mambo mengine.
 
Hiyo ndio namna ya kujiponya majeraha yako…Hekima hiyo tunaisoma pia katika maandiko matakatifu, Sulemani Mwana wa Daudi aliiandika…
 
Mhubiri 7:21 “Tena, usitie moyoni mwako maneno yote yaliyosemwa; usije ukamsikia mtumwa wako mwenyewe ali anakutukana.
22 Kwa kuwa mara nyingi moyo wako pia unajua ya kwamba wewe mwenyewe umewatukana watu wengine”.
 
Na mambo mengine yote! Yachukulie tu juu juu, jiweke kama ingekuwa ni wewe umemfanyia mwingine. Lakini endapo kila kitu kinachozungumzwa mbele yako wewe unakitafsiri tu na kukiweka moyoni mwako! Na kusema aaa anamaanisha nini kusema vile?…aa kwanini aseme vile?…aa kwani kaona nini kwangu?…au kwasababu niko hivi ndio maana kasema vile?…au kwasababu yeye ana kile na mimi sina?…Ukiishi kwa utaratibu huo, sura yako kila siku haitakosa huzuni, na uchungu, na macho hayataisha machozi, na kununa, na utakuwa mtu wa kunung’unika na kufurahia mabaya ya watu wengine, na hatimaye kutafuta namna ya kulipa kisasa na wengine wanaishia kwenda kwa waganga wa kienyeji na manabii wa uongo, kutafuta dawa ya kushughulika na maadui zako.
 
Lakini ukjifunza kuishi Maisha hayo Biblia inayotufundisha, kamwe hutapata majeraha ya moyo na utaishi Maisha ya msamaha na kuvumilia, na kupendana na watu, na ndivyo pia utakavyozidi kupendwa na watu, na hutaona kama kila mtu ni adui yako, Na hata kama utakuwa unajiona upo chini na wengine wapo juu kumbuka Bwana anaziona njia zako njema…na hivyo wakati ukifika Bwana atakunyanyua tu kama alivyomnyanyua Yusufu au Yeftha, haijalishi itachukua miaka mingapi, lakini atakuja kukulipa mema tu!. Yusufu alipokuwa Misri hakuwahi kunung’unika kwa wale ndugu zake kwa kumuuza, Zaidi baadaye aliwakaribisha wote na kula pamoja nao.
 
Bwana akubariki sana.Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
 

Mada zinazoendana:

SAMEHE KUTOKA NDANI YA MOYO WAKO.

TOBA IGUSAYO MOYO WA BWANA.

KWANINI PALE BWANA YESU ALICHUKUA HATUA YA KUMSAMEHE DHAMBI KWANZA KABLA YA KUMPONYA YULE MTU MWENYE KUPOOZA?(MARKO 2).

KISASI NI JUU YA BWANA.

EPUKA MUHURI WA SHETANI


Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
2 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Mary Athanas Njawala
Mary Athanas Njawala
3 years ago

Shujaa naomb unitumie haya masomo kwa njia ya email yng yananibariki sana