KISASI NI JUU YA BWANA.

KISASI NI JUU YA BWANA.

Moja ya dhambi kuu inayopeleka wengi kuzimu ni kutokusamehe…Bwana alisema, msipowasamehe watu makosa yao, Baba yenu wa mbinguni naye hatawasamehe ninyi makosa yenu (Mathayo 6:15). Ikiwa na maana kuwa, unaweza ukaomba toba kuanzia asubuhi mpaka jioni, lakini ikawa ni bure mbele za Mungu endapo ukiwa ndani ya moyo wako hujamsamehe mtu Fulani aliyekukosea.

Maadamu tupo hapa duniani, hatutaachwa kukosewa, kila siku tutaudhiwa, tutakasirishwa, tutaumizwa n.k lakini hatuna budi kusamehe kutoka moyoni, huo ndio mtihani wetu.Kama hujamsamehe mtu aliyekutukana kipindi Fulani nyuma, fahamu kuwa Bwana hajakusamehe tusi ulilomtukana mtu Fulani huko nyuma, aidha kwa mdogo au kwa moyo. Kama hujamsamehe mtu aliyekuudhi huko nyuma fahamu kuwa Mungu hajakusamehe maudhi yako uliyomwudhi mtu mwingine huko nyuma…

Kama hujamsamehe mtu aliyekusengenya fahamu kuwa na wewe hujasamehewa dhambi uliyowahi kumsengenya mtu mwingine, na makosa mengine yote, kama hujamsamehe aliyekutendea tambua na ya kwako pia hayajasamehewa, hali kadhalika kama ulimsamehe mtu na baadaye ukarudia tena kuukumbuka uovu wake na kumwekea kinyongo, Mungu naye ataukumbuka uovu wako uliowahi kumfanyia mtu Fulani huko nyuma, na hivyo toba zako zote ulizowahi kuzifanya zikawa ni bure.…Maandiko yanasema hivyo (Mathayo 18:23-35).

Kadhalika biblia imetuonya juu ya kisasi. Kisasi ni kitendo cha kumrudishia uovu mtu aliye kutendea uovu. Mafundisho yoyote yanayohusiana na kumlipizia mtu kisasi ni mafundisho ya uongo, yanayopalilia roho ya kutokusamehe, na yanalenga kuwapeleka watu jehanamu. Hubiri lolote linalokufanya utoke na hasira dhidi ya adui yako, limetengenezwa na roho ya Adui, Hubiri lolote linalokuachia hamu kubwa ya mtu Fulani anayekuchukia, au aliyekuudhi, kufa, au kuteseka, au kupigwa ni hubiri la shetani…Hubiri lolote linalokuacha katika hali ya kumpania mtu Fulani aliyekudharau ni fundisho lililotengenezwa na yule adui shetani..Biblia inasema…


Mithali 20:22 “Usiseme, Mimi nitalipa mabaya; Mngojee Bwana, naye atakuokoa”.


Waebrania 10:30 “Maana twamjua yeye aliyesema, Kupatiliza kisasi ni juu yangu, mimi nitalipa. Na tena, Bwana atawahukumu watu wake. 31 Ni jambo la kutisha kuanguka katika mikono ya Mungu aliye hai”


Warumi 12:19 “Wapenzi, msijilipize kisasi, bali ipisheni ghadhabu ya Mungu; maana imeandikwa, Kisasi ni juu yangu mimi; mimi nitalipa, anena Bwana. 20 Lakini, Adui yako akiwa na njaa, mlishe; akiwa na kiu, mnyweshe; maana ufanyapo hivyo, utampalia makaa ya moto kichwani pake. 21 Usishindwe na ubaya, bali uushinde ubaya kwa wema”

Roho wa Kristo anatupigania kwa namna isiyoweza kuonekana kwa macho, ukiona kuna mtu anakuchukia jua ni sehemu ndogo sana ya roho ya shetani inayojidhihirisha juu yako…, laiti ungefunuliwa macho katika ulimwengu wa roho uone ni maroho gani yanakuwinda usiku na mchana, na jinsi gani Mungu amekuepusha nayo, usingeona kama ndugu yako kukuchukia au kukusengenye ni Adui…Laiti ungeona ni kwa jinsi gani hata usiku wa leo ulikuwa umepaniwa maangamizi, na Mungu kaepusha huo mpango wa mapepo..usingeona mtu aliyekutukana kama ni Adui.

Hivyo leo hii kama ulikuwa una mpango wa kumlipizia mtu Fulani mabaya, uzike huo mpango leo na utaona Mungu atakavyokupa mema, utapata amani ambayo hujawahi kuipata na utaona mzigo Fulani mzito umeondoka ndani yako, huo mzigo utakaoona umeondoka ndio mzigo wa dhambi zako na wewe Mungu kaziondoa, tenga muda kumbuka ni wangapi hujawasamehe kwa moyo, ukishawapata tamka kuanzia leo umewasamehe, utaona kuna mzigo Fulani umeutua ndani ya moyo wako, hiyo hali ni konesha kuwa na wewe Kristo katua mzigo wako chini.
Bwana atusaidie katika jambo hili, tuweze kuishi Maisha ya msamaha na ya kujiepusha na visasi.

Bwana akubariki.
Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada zinazoendana:

SAMEHE KUTOKA NDANI YA MOYO WAKO.

Katika Marko 2:2-12, Kwanini Bwana Yesu alichukua hatua ya KUSAMEHE dhambi kwanza kabla ya kumponya yule kiwete?


Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments