MUNGU NDIYE ANAYEISHAWISHI MIOYO.

MUNGU NDIYE ANAYEISHAWISHI MIOYO.

Shalom, mtu wa Mungu karibu tujifunze maneno ya Mungu, ambayo ndio kweli pekee inayoweza kumfungua mtu moja kwa moja bila kubakisha chembe zozote za vifungo nyuma..

Leo kwa neema za Bwana tutamtazama mtu anayeitwa Nehemia, Jina lake limekuwa kubwa kutokana na kuwa tunakiona kitabu chake kikiwa miongoni mwa vitabu vitakatifu (BIBLIA), Lakini Nehemia kama tunavyomsoma hakuwa mtu wa maana sana tukizungumza kwa ngazi za kibiblia, hakuwa nabii, wala hakuzaliwa katika familia za kikuhani, Nehemia alikuwa ni mnyweshaji wa mfalme, mhudumu aliyekuwa anayepanga vinywaji mezani pa mfalme.

Lakini leo hii tunaisoma bidii yake, na sio tu kuisoma bali pia tunaiona sehemu ya kazi yake kwa macho yetu, Ukienda pale Yerusalemu utakutana na watu wengi ikiwemo wayahudi na watu wa mataifa mbalimbali wakisimama mbele ya kipande cha ukuta, na kuomba dua zao mbele za Mungu usiku na mchana..Sasa ukuta ule ulijengwa na Nehemia miaka karibia 2500 iliyopita, na mpaka sasa upo.

Nehemia hakuwa mtu wa kuona maono, lakini ni mtu aliyejitoa kwa ajili ya kazi ya Mungu zaidi hata ya manabii na watu wengine..Wakati mwingine aliifanya kazi ya Mungu akidhani kama Mungu vile hayupo karibu naye mpaka akawa anafikia hatua ya kusema Unikumbuke Ee Mungu wangu kwa mema yote niliyowafanyia watu hawa (Nehemia 5:19, 13:14, 13:22)..
Leo hii sisi ndio tunaojua ni jinsi gani Mungu amemkumbuka..Kumbukumbu lake linasomwa vizazi baada ya vizazi,

Hivyo hatutaenda sana kwa undani kuutazama ujenzi aliofanya lakini tutajifunza kitu kimoja kwake ambacho kitatufaa sisi hata katika mambo yetu ya kawaida tunayoyapitia kila siku..Ukisoma pale utaona mwanzoni kabisa Nehemia alipokuwa anafanya kazi yake ya kuhudumu mezani pa mfalme, baadhi ya ndugu zake walimletea taarifa kuwa Yerusalemu umebomolewa, na kuta zake zimetoketezwa na moto, hivyo hilo lilimuhuzunisha sana na kumfanya alie na kuomboleza kwa muda mrefu, mbele za Mungu na kufunga..


Ukichunguza pale utagundua Nehemia alikuwa katika hali ya uzuni na maombolezo kwa muda wa miezi minne, akimwomba Mungu ampe kibali kutoka kwa mfalme kwenda kuikarabati nyumba ya Mungu iliyokuwa Yerusalemu na mji, lakini cha ajabu ambacho ninataka ukione hapa, ni kuwa wakati wote huo Nehemia akiwa katika maombolezo, mfalme hakugundua kitu chochote kinachoendelea ndani ya Nehemia..Mpaka wakati ambapo Nehemia ameacha sasa kuhuzunika, anacheka, anamuhudumia mfalme, ndipo mfalme akaona kitu cha tofauti katika uso wa Nehemia..

Nehemia 2:1 “Ikawa katika mwezi wa Nisani, mwaka wa ishirini wa mfalme Artashasta, na divai imewekwa mbele yake, nikaishika ile divai, nikampa mfalme. NAMI MPAKA SASA SIKUWA NA HUZUNI MBELE YA MFALME WAKATI WO WOTE.

2 Basi mfalme akaniambia, Mbona umesikitika uso wako, nawe huna ugonjwa? Nini hii, isipokuwa ni huzuni ya moyo? Ndipo nikaogopa sana.

3 Nikamwambia mfalme, Mfalme na aishi milele; kwani uso wangu usiwe na huzuni, iwapo mji, ulio mahali pa makaburi ya baba zangu, unakaa ukiwa, na malango yake yameteketezwa kwa moto?

4 Ndipo mfalme akaniambia, Una haja gani unayotaka kuniomba? Basi nikamwomba Mungu wa mbinguni.

5 Nikamwambia mfalme, Mfalme akiona vema, na ikiwa mimi, mtumishi wako, nimepata kibali machoni pako, tafadhali unipeleke mpaka Yuda, niuendee mji wa makaburi ya baba zangu, nipate kuujenga.”

Unaona? Ukiangalia utaona kile kitendo cha yeye kutokuonyesha dalili yoyote ya nje kuwa yupo katika maombolezo halafu mtu anamwambia yupo katika maombolezo ndicho kilichomwogopesha Nehemia, pengine alijiuliza kwanini wakati wote wa nyuma nikiwa katika huzuni inayoonekana mfalme hakugundua chochote iweje iwe leo?.Mungu tangu zamani huwa hategemei hisia za mtu kumsaidia kuleta majibu ya maombi yake..

Mungu hataki wakati mmoja tumlilie yeye, na wakati huo huo tumlilie mwanadamu, au wakati mmoja tumwonyeshe yeye hisia Fulani na wakati huo huo tumwonyeshe mwanadamu hisia hizo hizo, kwamfano unaweza ukawa unapitia shida Fulani, au unataka upandishe ngazi fulani kazini, au unamdai mtu na unafahamu kabisa mtu Fulani anaweza kukusaidia, na wewe ukafanya uamuzi wa busara kwenda kumwomba Mungu kwa kufunga, sasa ukianza kujionyesha tena kwa Yule mtu unashida Fulani, kwa vitendo Fulani Fulani ili akuone, nataka nikuambie Mungu atasubiri kwanza uache vitimbwi hivyo ndipo akusaidie,..Lakini ukitulia na kuishi kwa njia ya kuonyesha kama haupitii shida yoyote au huna haja ya chochote lakini ndani unapitia,..bali huku nyuma ni Mungu tu ndio unayemlilia kila siku, nataka nikuambie utauvuta muujiza wako haraka kuliko unavyodhani.

Na ndio maana Bwana Yesu alisema,

Mathayo 6.16 “Tena mfungapo, msiwe kama wanafiki wenye uso wa kukunjamana; maana hujiumbua nyuso zao, ili waonekane na watu kuwa wanafunga. Amin, nawaambia, wamekwisha kupata thawabu yao.

17 Bali wewe ufungapo, jipake mafuta kichwani, unawe uso;

18 ili usionekane na watu kuwa unafunga, ila na Baba yako aliye sirini; na Baba yako aonaye sirini atakujazi”.

Unaona? Mungu hapendi mambo yetu ya siri mtu mwingine ayajue, Embu jaribu kufikiria kama Nehemia angeonwa na mfalme wakati wa kuonesha huzuni zake mbele ya watu, ni wazi kuwa angedhani ni kwasababu ya kulia kwake ndio maana kaonewa huruma na mfalme, lakini siku alipobadilisha uso wake, ndipo alipomshangaa Mungu.
Na sisi tutumie kanuni hii ya Mungu ili tufanikiwe..Bwana akubariki sana.
Ikiwa bado maisha yako bado yapo mbali na wokovu, mlango wa neema bado upo wazi kwa ajili yako, nakushauri uingie sasa nawe uanze kuufurahia uzuri wa Mungu..Wewe mwenyewe unaona dunia inavyochosha, hakuna haya ya kueleza ulitazamia ingekupa amani moyoni mwako, lakini hiyo amani mpaka sasa huioni, Nataka nikuambie ni mmoja tu ndiye aliyeahidi kutoa AMANI ya kweli ambayo ulimwengu hautoi naye ni Yesu mwenyewe huipati kwa mwingine yeyote..

Yohana 14:27 “Amani nawaachieni; amani yangu nawapa; niwapavyo mimi sivyo kama ulimwengu utoavyo. Msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiwe na woga.”

Maran atha!


Mada zinazoendana:

UWEZA WA MUNGU UNAONEKANA WAPI?

JE! UNA MASIKIO YANAYOSIKIA?

NGUVU YA UPOTEVU.


Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments