VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 6

VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 6

Shalom, Karibu tujifunze Biblia,

Huu ni mwendelezo wa uchambuzi wa vitabu vya Biblia leo tutasogea mbele kitabu kimoja kinachofuata cha Ezra.Katika vitabu vilivyotangulia vya Wafalme na Mambo ya Nyakati, tuliona ni kwa jinsi gani, Mungu alishughulika na Taifa la Israeli kupitia Wafalme wake, na Tumeona ni jinsi gani wafalme hao ambao walitaka wawatawale jinsi walivyokuwa mwiba kwao, mpaka kuwasababishia waingie katika matatizo mazito..

Tunamwona kwamfano Mfalme Sulemani japokuwa alikuwa ni mpakwa Mafuta wa Bwana lakini aliwatumikisha Israeli vikali sana, (1 Wafalme 12:4 ) jambo ambalo halikuwa mpango wa Mungu tangu mwanzo, tunalisoma hilo katika 1Samweli 8:11-18 na Pia ndiye aliyesababisha Taifa la Israeli kugawanyika sehemu mbili (Upande wa kaskazini na upande wa kusini), jambo ambalo pia halikuwa mpango kamili wa Mungu watu wake wagawanyike.


Na wafalme wengine wote waliofuata wa Israeli na Yuda kama Mfalme Yeroboamu, Mfalme Ahabu na Mfalme Manase waliwakosesha waisraeli sana, na kuwafanya watu waabudu sanamu na miungu migeni…Kwamfano Mfalme Manase hakuishia tu kuabudu sanamu bali pia aliitengeneza madhabahu ya mungu mgeni ndani ya lile Hekalu la Sulemani na kuiabudu huko,(2 Wafalme 21) na pia alimtoa sadaka ya kuteketezwa mwanawe, na alikuwa anafanya uchawi na uganga pamoja na kutazama bao na kujihusisha na wachawi na wapunga pepo. Huyo ni Mfalme anafanya mambo hayo yote, akafanya dhambi kuliko hata mataifa wasio mjua Mungu wa kweli.

Kwasababu hiyo basi Mungu akaghadhibika sana kuahidi kuwa watakwenda utumwani. Na wakati ulipofika walichukuliwa utumwani, ambapo mataifa 10 yalichukuliwa utumwani Ashuru na Yuda wakachukuliwa Babeli, na huko wakakaa miaka 70 sawasawa na unabii Mungu aliompa Nabii Yeremia. Na baada ya miaka hiyo sabini kuisha Mungu alitabiri kuwa watatoka. Sasa kama hujapitia uchambuzi wa vitabu hivi kwa ufupi ni vyema ukapitia ili tuende pamoja.

Sasa Ni mambo gani yalikuwa yanaendelea walipokuwa huko Babeli?..Tutakuja kuona tutakapofika katika kitabu cha Danieli na Ezekieli…Lakini kitabu hichi cha EZRA kinaruka mpaka wakati wana wa Israeli wanatoka Babeli…Kwa mpangilio mzuri kingepaswa kianze kwanza kitabu cha Danieli ndipo kifuate cha Ezra lakini biblia haijaviweka vitabu katika mfululizo huo.Kitabu cha Ezra kimeandikwa na Ezra mwenyewe.

EZRA NI NANI?

Biblia inasema Ezra alikuwa ni mwandishi mwepesi katika sheria ya Musa.

Ezra 7: 6 “.. huyo Ezra akakwea kutoka Babeli; naye alikuwa MWANDISHI MWEPESI KATIKA SHERIA YA MUSA, aliyokuwa ameitoa Bwana, Mungu wa Israeli; naye mfalme akamjalia matakwa yake yote, kama mkono wa Bwana, Mungu wake, ulivyokuwa pamoja naye”

Maana ya mwandishi mwepesi ni mtu ambaye YUPO TAYARI kufanya jambo, yaani mwepesi katika kufanya jambo fulani, sio mzito..Ndio maana hapo biblia imemtaja Ezra kama Mwandishi mwepesi.

Kadhalika Mwandishi katika desturi za wayahudi alikuwa ni mtu anayefanya kazi kama za sasahivi za uwakili, alikuwa ni mtu anayeijua sheria ya Musa vizuri na hivyo ni rahisi kufahamu kipengele fulani cha sheria kinasema hivi au vile…Katika Agano jipya utaona Bwana Yesu amewataja waandishi sehemu kadha wa kadha..soma (Mathayo 17:10, Mathayo 20:18, Mathayo 21:15, Mathayo 23:2 n.k).

Pamoja na kwamba walikuwa na kazi ya kuhukumu kwa kupitia vipande vya sheria na kufundisha watu, lakini pia walikuwa na kazi nyingine wanayoifanya ya kunakili torati…Kumbuka zamani hizo hakukuwa na mashine za photocopy kama tulizonazo leo…Hivyo Nakala zote zilikuwa zinatengenezwa kwa kunakiliwa tena mahali pengine…

Kwahiyo kazi ilikuwepo kubwa ya kutengeneza nakala nyingi kila siku, waandishi hawa walikuwa wanaandika usiku na mchana, Katika kunakili walikuwa na vigezo vyao vya kufuata, kwanza mwandishi lazima ayatamke maneno Dhahiri ndipo ayaandike, na pia wakati wa kuandika anapokutana na jina la Mungu takatifu YEHOVA alikuwa anasimama kwanza ananawa mwili wote na kuisafisha kalamu yake ndipo aliandike. Na nakala ikishakamilika, itahakikiwa kwa siku 30 kabla ya kuruhusiwa itumike, na endapo zitaonekana kurasa mbili au tatu zitahitaji marekebisho basi nakala nzima inaachwa, kazi inaanza upya. Na kila aya na kila Neno lilikuwa linahesabiwa kuhakikisha na kitabu halisi. Kulikuwa na sheria nyingine nyingi tu katika uandishi…

Hivyo kazi ya uandishi ilikuwa inaheshimiwa sana katika Israeli, na huyu Ezra alikuwa mmoja wao wa hao waandishi, lakini biblia inamtaja alikuwa ni mwandishi mwepesi, yaani alikuwa anaifanya kazi yake kwa kupenda pasipo kusukumwa, na katika ufasaha, tofauti na wengine, Ndiye aliyekiandika kitabu cha Mambo ya nyakati tulichotangulia kukipitia…
Na katika kitabu hichi Roho ya Bwana ilimjia na kuanza kuandika hatua kwa hatua jinsi wana wa Israeli walivyotoka Babeli na kurudi Israeli, kuanzia Kundi la kwanza lililotoka Babeli na kurudi Nchi ya Ahadi mara baada tu ya Mfalme Koreshi kutoa amri ya uhuru wao. Na Kundi hilo ndio tunalolisoma katika Ezra Mlango wa 2.

Naye pia Ezra alikuwa ni miongoni mwa waliotoka Babeli na kurudi nchi ya Ahadi lakini yeye alikuwa katika lile kundi la pili ambalo tunalisoma katika mlango wa 7. Wakati Ezra anarudi kulikuwa tayari kuna lile kundi la kwanza lililotangulia miaka kadhaa nyuma, hivyo kuna mambo ambayo walikuwa wameyasahau yahusuyo sheria za Mungu, na kadhalika hata nyumba ya Mungu ambayo walikuwa wanaijenga upya ilisimama… hivyo Ezra alikusudia moyoni mwake atakaporudi awafundishe na kuwakumbusha wana wa Israeli sheria zote za Mungu wa Israeli na nini torati ya Musa inasema, na Bwana alimsaidia kupata kibali mbele ya Mfalme wa Uajemi, na kusapitiwa kwa kila kitu alichokihitaji ili tu akawafundishe sheria za Mungu.

Ezra 7: 6 “huyo Ezra akakwea kutoka Babeli; naye alikuwa mwandishi mwepesi katika sheria ya Musa, aliyokuwa ameitoa Bwana, Mungu wa Israeli; naye mfalme akamjalia matakwa yake yote, kama mkono wa Bwana, Mungu wake, ulivyokuwa pamoja naye.

7 Nao wakakwea baadhi ya wana wa Israeli, na wa makuhani, na wa Walawi, na waimbaji, na mabawabu, na Wanethini, ili kwenda Yerusalemu, katika mwaka wa saba wa mfalme Artashasta.

8 Naye Ezra akafika Yerusalemu mwezi wa tano katika mwaka wa saba wa huyo mfalme.

9 Maana alianza kukwea kutoka Babeli siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza, naye akafika Yerusalemu siku ya kwanza ya mwezi wa tano, kama mkono mwema wa Mungu wake ulivyokuwa pamoja naye.

10 Kwa maana huyo Ezra alikuwa ameuelekeza moyo wake kuitafuta sheria ya Bwana, na kuitenda, na kufundisha maagizo na hukumu katika Israeli”.

Utaona mbeleni baada ya Ezra kuingia nchi ya Ahadi, alikuta kasoro nyingi watu tayari walikuwa wameshaanza kufanya machukizo ya kuoa wanawake wageni, kama alivyofanya Sulemani jambo lililosababisha Israeli kugawanyika, na Ezra kama Mwandishi aliijua vizuri Torati hivyo akawaonya na kuwasaidia Wana wa Israeli na kuwarejesha tena kwa Mungu wao.

Na kwa ushujaa wote huo Mungu alimuheshimu, hakuwa Nabii, hakuwa anaona maono, hakuwa mtu mkubwa sana, lakini kwa Moyo wake wa kuwasaidia ndugu zake na kuwarejesha kwenye Torati Mungu alimheshimu, mpaka leo hii tunazisoma habari zake. Hiyo yote ni kwasababu alikuwa msaada kwa wengine kama jina lake lilivyo EZRA Maana yake MSAADA. Hivyo ni vizuri ukakipita kitabu hichi mwenyewe utapata vitu vingi vipya usivyokuwa unavijua hapo kwanza.

Bwana akubariki. Usikose mwendelezo wa vitabu vinavyofuata.

Kwa maombezi/ Ushauri/ Ratiba za Ibada/Maswali/ Whatsapp/ Piga namba hizi: +255693036618/ +255789001312


Mada Nyinginezo:

NINI MAANA YA ELOHIMU?

MATOWASHI NI WAKINA NANI?

KITABU CHA UZIMA.

MUNGU NDIYE ANAYEISHAWISHI MIOYO.

MIHURI SABA.

NYAKATI SABA ZA KANISA NA WAJUMBE WAKE.

UNYAKUO.


Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments