NIFANYE NINI ILI NIIKWEPE HUKUMU.

NIFANYE NINI ILI NIIKWEPE HUKUMU.

Watu wengi sana sio tu wasiomjua Mungu bali hata miongoni mwa wakristo, wakisikia jambo hili kuwa siku moja kuna kusimama hukumuni huwa linawatesa sana, na kuwahuzunisha sana na hilo linawafanya waishi Maisha ya wasiwasi mwingi. Lakini habari njema ni kwamba biblia inatumbia hukumu inakwepeka
.
 
Leo tutajifunza ni kwa jinsi gani tunaweza kuikwepa hukumu ya Mungu inayotisha, Na andiko pekee linalotuambia habari hiyo ni hili..
 
Yohana 5:24 “Amin, amin, nawaambia, Yeye alisikiaye neno langu na kumwamini yeye aliyenipeleka yuna uzima wa milele; wala haingii hukumuni, bali amepita kutoka mautini kuingia uzimani.”
 
Kama wengi tunavyofahamu huyu aliyesema maneno hayo ni Bwana wetu Yesu Kristo, lakini swali linakuja palepale je! Huko kumwamini Bwana kukoje, je! Ni kuamini tu kama yeye yupo?, au kumwamini tu kama yeye ni mwokozi mpaka kutufanya tusihukumiwe au vipi?. Mbona tumesikia wengi wamemwamini Kristo lakini wapo kuzimu?
 
Tusisahau kuwa biblia inatuambia hata mashetani wanaamini na kutetemeka, (Yakobo 2:19 ) wanaamini Yesu ni mwokozi, wanaamini maneno ya Mungu kuwa ni kweli,..hivyo hapo tunapaswa tujue biblia inapotuambia tumwamini Yesu na yeye aliyempeleka ni Zaidi ya kumfahamu tu wasifa wake.. Mfano ni sawa na umekutana na njia mbili mbele yako ukaona kibao kimoja kinasema kushoto ni shuleni, na kulia ni Sokoni, na wewe ukiangalia ulikuwa unatafuta mahali soko lilipo…Ni wazi njia ile ya kibao kinachokuelekeza sokoni utaiamini Zaidi kuliko ile ya kibao kinachokuelekeza shuleni..Sasa hiyo ni hatua ya kwanza, hatua ya pili ili ufike unapotaka kwenda ni sharti uifuate ile njia kwa gharama zozote hata kama itakuwa ina vumbi, na mikunjo kunjo haipendezi kama ile ya shule, utaifuata tu, lakini ikiwa hutaifuata na huku bado unataka ufike sokoni, ni wazi kuwa hutafika popote haijalishi umeifahamu njia sahihi kiasi gani.
 
Vivyo hivyo na kwa Bwana Yesu kumwamini tu pekee yake kuwa amekuokoa kwa kuongozwa sala ya toba, haikufanyi wewe usisimame hukumuni siku ile..Ni sharti uonyeshe kwa vitendo kuwa umemwamini yeye kwa kuifuata njia ya uzima, na vitendo hivyo ndivyo vinavyojulikana kama TOBA.
 
Toba ni kitendo cha kugeuka na kuanza safari kule ambako haukuwepo.. Sasa ikiwa mtu atakamilisha tu agizo hio basi Hukumuni hataingia.
 
Na hiyo inakujaje, mfano ikiwa leo hii umempa Kristo Maisha yako kwa mara ya kwanza, ukatubu dhambi zako zote ukaenda kubatizwa katika ubatizo sahihi, kumbuka muda huo bado mbingu haifanya chochote juu yako, bali inakuangalia kwanza, mwenendo wako, je! Ni kweli alichotubia na alichobatiziwa unakitelekeza kwa vitendo, je ni kweli huendi disco tena, je ni kweli huangalii picha chafu tena kwenye mitandao?, je ni kweli hauendi bar tena, je ni kweli hufanyi uasherati tena…sasa Mungu akishaona mtu huyu kageuka anazidi kupiga hatua kila siku katika kuielekea njia ya uzima…mtu wa namna hiyo hata kama hatakuwa mkamilifu wote, tayari mtu huyo anahesabiwa haki na mbingu kama mtakatifu..na hiyo ndio maana ya neema.
 
Hata ikitokea hajafikia ule utimilifu wote halafu akafia njiani mtu huyo moja kwa moja siku ile hataingia hukumuni. Kwasababu alikuwa anaonyesha nia ya kuelekea katika njia ya uzima..Mfano hai ni ule wa kipindi cha Sodoma na Gomora pale Lutu alipofuatwa na wale malaika, hawakumteketeza Lutu na wale watoto wake wawili sio kwamba walikuwa ni wenye haki sana mbele za Mungu hapana lakini pindi walipoonyeshwa tu njia ya uzima wao, wa kujiponya nafsi zao waliindea njia hiyo hiyo bila kugeuka nyuma, na mwisho wa siku wakajikuta wameokoka,Lakini mke wa Lutu aliyatamani ya nyuma japokuwa alitokewa na malaika japokuwa aliiamini ile njia kweli lakini moyo wake haukudhamiria kwa dhati kuifuata ile njia na ndio maana akawa jiwe la chumvi.
 
Ndugu ikiwa umemwamini Kristo halafu bado unatembea huku unageuka geuka nyuma, haijalishi ulitokewa na malaika wangapi siku ile ulipoamini,haijalishi ulitokewa na YESU mwenyewe, Kwenda hukumuni hakukwepeki, na unajua anayepandishwa hukumuni sikuzote ni mshtakiwa na hakuna mtu yeyote anayeweza kuyakwepa au kuyashinda mashtaka ya Mungu juu yake…bali wote watakaopanda hukumuni wataingia kwenye ziwa la moto..
 
Fahamu kuwa Mungu hatuhesabii haki kwa matendo yetu, vile vile usisahau hatuhesabii haki kwa matendo yetu maovu, lakini anaangalia ule moyo unaotamani kuhesabiwa haki ndio anaupa Haki, na moyo wowote wa namna hiyo siku zote utajitahidi kuishi Maisha ya haki kwa gharama zozote na ndipo Mungu anamalizia kuupa haki yote kwa neema yake.
 
Ikiwa hukulifahamu hilo basi huu ndio wakati wako sasa wa kuonyesha Imani yako kwa matendo, acha kwa moyo mmoja mambo yote mabaya na ya aibu uliyokuwa unayafanya huko nyuma, ulikuwa unaangalia picha za ngono, acha ulikuwa unafanya mustarbation acha, ulikuwa unafanya uzinzi acha, ulikuwa unavuta sigara acha, ulikuwa unatoa mimba acha, ulikuwa unauza madawa ya kulevya au unatumia acha, ulikuwa unatukana tukana ovyo acha, ili Mungu akuone nia yako amalizie kukupa HAKI YOTE bure,..hata ukifa leo uwe na ukakika wa kuingia uzimani bila kupita hukumuni.
 
Warumi 8:1 “Sasa, basi, hakuna hukumu ya adhabu juu yao walio katika Kristo Yesu”.
 
Ubarikiwe sana.
 
Tafadhali “Share” Ujumbe huu kwa wengine. Na Bwana atakubariki.

Mada zinazoendana:

KUNA HUKUMU ZA AINA NGAPI?

UFUFUO WA UZIMA NA WA HUKUMU.

UTALIPWA KATIKA UFUFUO WA WENYE HAKI.

KAMA MHUBIRI NI WOKOVU UPI UNAUPELEKA KWA WATU?

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments