KUWAHUDUMIA MALAIKA PASIPO KUJUA.

 KUWAHUDUMIA MALAIKA PASIPO KUJUA.

Biblia inatuambia moja ya kazi ya malaika ni kuwahudumia watakatifu, (Waebrania 1:14) na tunajua siku zote kama mtu ni muhudumu ni lazima akae eneo husika la wale anawahudumia, kwamfano Daktari anafanya kazi ya kuwahudumia wagonjwa, japokuwa anao kwake mwenyewe lakini huwezi kumkuta masaa yote yupo nyumbani bali muda wake mwingi utakumkuta anakesha mahospitalini, kwasababu huko ndipo wagonjwa walipo. Vivyo hivyo na malaika wa Bwana, wamepewa jukumu la kuwahudumia watakatifu, sasa japo makazi yao ni mbinguni lakini muda wao mwingi wapo duniani wanazunguka huko na huko kuhakikisha yale yote yaliyokusudiwa na Mungu juu ya watakatifu yanatimia.

Hivyo tusichokujua tu ni kuwa hata sasa tunapozungumza kuna mamilioni ya malaika wanaozunguza duniani kila siku, na kazi yao ni moja kuhakikisha kusudi la Mungu linatimia kwa namna zote. Na malaika kama biblia inavyotuambia ni viumbe wa rohoni hivyo Mungu amewapa uwezo wa kuchukua maumbile tofauti tofauti, wanaweza wakatembea kama nguzo ya moto, au wingu, au taswira za mnyama, au taswira ya mwanadamu. Kwahiyo katika sikuzote za maisha yako, kwa namna moja au nyingine ulishawahi kukutana au kupishana na malaika wa Mungu wengi pasipo hata wewe kujijua, Na ndio maana Mtume Paulo anasema:

Waebrania 13:1 “Upendano wa ndugu na udumu.

2 Msisahau kuwafadhili wageni; maana kwa njia hii wengine wamewakaribisha malaika pasipo kujua.”

Tukimwangalia Ibrahimu siku moja wakati amekaa nyumbani kwake ghafla aliona watu watatu wamesimama nyumbani kwake, Lakini Ibrahimu hakuwafukuza au kuwaita wapepelezi badala yake yeye ndiye aliyewashurutisha waangie nyumbani mwake wale na wanywe, na kumbe walikuwa ni malaika wa Bwana pamoja na Bwana mwenyewe wakiwa katika safari yao ya kwenda kuupeleleza mji..

Vivyo hivyo hao hao waliposhuka Sodoma, Lutu alipowaona kuwa ni wageni sio wenyeji wa pale hakusubiri wafike nyumbani kwake bali yeye ndiye aliyewakimbilia na kuwaambia waingie kwake! Wale na wanywe na walale, lakini wale watu walikataa kata kata, lakini Lutu hakuacha kuwashurutisha sana, na walipokubali baadaye ndipo Lutu alipojua kuwa wale hawakuwa watu wa kawaida.. Na Kuwafadhili wageni

 Sio lazima tu iwe wale wanaotaka kuja kulala nyumbani kwetu, lakini pia kuwatendea ukarimu wale ambao wanaonekana wanahitaji msaada kwa wakati huo, hususani wale tusiowajua….na ukarimu huo unaweza ukawa chakula, fedha, ushauri, n.k.

Biblia inatukumbusha tuwe wakarimu, ni wazi kuwa dunia ya sasa upendo umepoa kila mtu anajipenda nafsi yake, zamani ilikuwa mwenyeji ndio anamshurutisha mgeni aje kwake, lakini sikuhizi mwenye hitaji ndio anamshurutisha mwenye nacho amsaidie, na bado anaweza asiambulie chochote, utakuta muda mwingine unapishana na mtu barabarani anakuambia ninasikia njaa sijala, na hakuombi hata pesa anakuomba tu ukamnunulie muhogo mmoja pale apooze njaa! Utasikia huyo mtu anasema, mimi sina kitu na ukiangalia mfukoni ana kiasi tu kikubwa cha fedha ambayo haina matumizi imekaa tu kwenye pochi.. mwingine atakuambia naomba unilipie nauli, utaona mtu anasema sina pesa, lakini ukweli ni kuwa anayo lakini hataki kumpa, Ndugu kama unacho chochote wewe mpe tu! Sio lazima kiwe kingi, hata kama kakudanganya usijali chochote, kwa maana hujui huyo aliyekuomba ni nani?.

Mwingine hataonyesha dalili ya kukuomba chochote, lakini wewe ukimtazama utaona anao uhitaji Fulani, na huku ukiangalia una vichenchi chenchi vimebaki mfukoni wewe mpe tu, kwasababu hujui huyo unayempa ni nani…Lakini simaanishi  kwamba uumpe tu kila mtu, hata kama mtu anahitaji pesa ya sigara au pombe au madawa ya kulevya uumpe hapana!..Mtu wa namna hiyo hapaswi kupewa chochote kwasababu mtu mwenye shida kweli ya msingi hawezi kuomba vitu kama hivyo, vilevile hata malaika wa Bwana hawawezi kufanya hivyo. Ukimkuta Mtu kalewa halafu anakuomba kitu usimpe chochote, ukimkuta mtu kashika sigara halafu anakuomba usimpe! Mpe kwanza injili n.k

Lakini mbali na hao asilimia kubwa ya wengi wanaotuomba wanao matatizo..pengine hata wewe ilishakukuta ulifika wakati ulitamani mtu akusaidie kitu Fulani, pengine hata sio chakula, bali kitu Fulani kingine cha muhimu sana ambacho unahitaji tu kwa muda huo na hauna….sasa watu wa namna hiyo wapo mamia kwa mamia… tuwasaidie kwa vidogo tulivyo navyo. Utajisikiaje siku ile umefika mbinguni halafu malaika kama 100 wanatokea kila mmoja anakuambia ulishawahi kunisaidia mara 2 nilipokuwa duniani. Ni furaha kiasi gani unadhani Bwana Yesu ataona fahari juu yako kiasi, lakini siku ile mfano unafika na unaona malaika hawana habari na wewe, wakati unashangaa hilo  wanakuambia ulishawahi kutufukuza, au ulishawahi kutunyima kitu Fulani tulichowahi kukuomba tukiwa  duniani. Na wakati haukutani na malaika bali na MKUU mwenyewe Bwana Yesu, sasa tukiwa wabinafsi kila wakati kuna hatari kubwa sana ya kukosa mema Mungu aliyotuandalia..

Mathayo 25:31 “Hapo atakapokuja Mwana wa Adamu katika utukufu wake, na malaika watakatifu wote pamoja naye, ndipo atakapoketi katika kiti cha utukufu wake;

32 na mataifa yote watakusanyika mbele zake; naye atawabagua kama vile mchungaji abaguavyo kondoo na mbuzi;

33 atawaweka kondoo mkono wake wa kuume, na mbuzi mkono wake wa kushoto.

34 Kisha Mfalme atawaambia wale walioko mkono wake wa kuume, Njoni, mliobarikiwa na Baba yangu, urithini ufalme mliowekewa tayari tangu kuumbwa ulimwengu;

35 kwa maana nalikuwa na njaa, mkanipa chakula; nalikuwa na kiu, mkaninywesha; nalikuwa mgeni, mkanikaribisha;

36 nalikuwa uchi, mkanivika nalikuwa mgonjwa, mkaja kunitazama; nalikuwa kifungoni, mkanijia.

37 Ndipo wenye haki watakapomjibu, wakisema, Bwana, ni lini tulipokuona una njaa, tukakulisha, au una kiu tukakunywesha?

38 Tena ni lini tulipokuona u mgeni, tukakukaribisha, au u uchi, tukakuvika?

39 Ni lini tena tulipokuona u mgonjwa, au kifungoni, tukakujia?

40 Na Mfalme atajibu, akiwaambia, Amin, nawaambia, kadiri mlivyomtendea mmojawapo wa hao ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi.

41 Kisha atawaambia na wale walioko mkono wake wa kushoto, Ondokeni kwangu, mliolaaniwa, mwende katika moto wa milele, aliowekewa tayari Ibilisi na malaika zake;

42 kwa maana nalikuwa na njaa, msinipe chakula; nalikuwa na kiu, msininyweshe;

43 nalikuwa mgeni, msinikaribishe; nalikuwa uchi, msinivike; nalikuwa mgonjwa, na kifungoni, msije kunitazama.

44 Ndipo hao pia watajibu, wakisema, Bwana, ni lini tulipokuona wewe una njaa, au una kiu, au u mgeni, au u uchi, au u mgonjwa, au u kifungoni, tusikuhudumie?

45 Naye atawajibu, akisema, Amin, nawaambia, Kadiri msivyomtendea mmojawapo wa hao walio wadogo, hamkunitendea mimi.

46 Na hao watakwenda zao kuingia katika adhabu ya milele; bali wenye haki watakwenda katika uzima wa milele.”

Bwana akubariki. Tafadhali “Share” Ujumbe huu kwa wengine.


Mada zinazoendana:

HUDUMU YA MALAIKA WATAKATIFU.

JE! BAADA YA ULIMWENGU HUU KUISHA MALAIKA WATAKUWA NA KAZI GANI TENA?

JE! MBINGUNI KUNA MALAIKA WA KIKE?. NA JE! TUKIFIKA MBINGUNI TUTAFANANA WOTE?

KUNDI LA MALAIKA WALETAO MABAYA.

MALAIKA WA MAJI NI NANI? (UFUNUO 16:5)


Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments