FAHAMU JINSI MUNGU NA SHETANI WANAVYOZUNGUMZA NA WATU.

FAHAMU JINSI MUNGU NA SHETANI WANAVYOZUNGUMZA NA WATU.

Ulishawahi kuyatafakari kwa makini haya maneno ya Bwana Yesu?

Yohana 8:38 “Niliyoyaona kwa Baba ndiyo niyanenayo; nanyi vivyo hivyo mliyoyasikia kwa baba yenu ndiyo myatendayo”.

Maneno hayo aliwaambia wayahudi (Mafarisayo na waandishi) kipindi kile walipotaka kumuua?. Lakini unaweza kujiuliza ni lini walishakaa chini na kumsikiliza shetani, akizungumza nao kisha akawapa maagizo ya kumwangamiza Bwana Yesu? Ni lini?

Hatuwezi kudhani kuwa shetani alishawahi kukaa chini, na kuanza kunong’ona kwenye masikio yao, na kuwaambia “sasa wanangu wakati wa kumuua Yesu umefika haya nendeni”, Hilo halipo, lakini Bwana Yesu hawezi kusema uongo, ni lazima aliwaona wakimsikiliza shetani, kisha wakaitii sauti yake, na wakafanikiwa kuyafanya yale yote waliyoagizwa na shetani kutenda.. Na ndio maana ukiendelea kusoma pale, utaona anasema..

Yohana 8:44 “Ninyi ni wa baba yenu, Ibilisi, na TAMAA ZA BABA YENU NDIZO MPENDAZO KUZITENDA. Yeye alikuwa mwuaji tangu mwanzo; wala hakusimama katika kweli, kwa kuwa hamna hiyo kweli ndani yake. Asemapo uongo, husema yaliyo yake mwenyewe; kwa sababu yeye ni mwongo, na baba wa huo”.

Ndugu, sauti ya shetani, kamwe usitazamie utaisikia katika maono au ndoto, au kwa mapepo, hali kadhalika sauti ya Mungu vivyo hivyo, Utaisikia sauti ya Mungu kwa kutazama tu yale Mungu anatenda.. Vilevile utaisikia na kuielewa sauti ya shetani pale unapotazama ni nini anatenda..

Kwamfano, tukianzana na hawa wayahudi, ilifikia wakati walimwonea Yesu wivu kisa Mungu anamtumia kwa ukamilifu wote kuwavuta watu wote kwenye nuru, hapo ndipo wakaingiwa na wazo la kutaka kumuua, wazo ambalo walishawahi kuona watu fulani huko nyuma wakilifanya likawaletea matunda, na wao pia wakalichukua. Kumbe hawajui hilo wazo ndio sauti ya shetani yenyewe ikiwapa maelekezo.

Hata leo, wazo la wewe kutaka kurudi nyuma kuzini, tayari hiyo ni sauti ya shetani, na ndio hapo unaitii kwa kuanza kutazama picha za ngono mitandaoni,  unafanya punyeto, unakwenda disco, unatazama muvi zenye maudhui ya mapenzi mapenzi wakati wote, hujui kuwa ni tamaa za ibilisi unazozifanya.. yaani katika ulimwengu wa roho, Yesu anakuona umeketi na shetani kwenye meza moja, ukimsikiliza sauti yake kwa makini sana.

Lakini vivyo hivyo kwa watoto wa Mungu pia kanuni ni ile ile, nao wanamsikiliza Mungu kwa kumtazama vile atendavyo, Kama vile Bwana Yesu alivyosema “Niliyoyaona kwa Baba ndiyo niyanenayo”. Sio maono, hapana, Bwana aliona kazi nyingi za Mungu ulimwenguni hivyo akaziiga akazitenda..

Kwamfano moja ya kazi ambazo Yesu aliziona Baba yake anazifanya akaiga ni pamoja na kuwa na HURUMA,  KUSAMEHE, KUWAPENDA MAADUI na KUFADHILI hata kwa wasio na shukrani.

Luka 6:35 “Bali wapendeni adui zenu, tendeni mema, na kukopesha msitumaini kupata malipo, na thawabu yenu itakuwa nyingi; nanyi mtakuwa wana wa Aliye juu, kwa kuwa yeye ni mwema kwa wasiomshukuru, na waovu.

36 Basi, iweni na huruma, kama Baba yenu alivyo na huruma.

Unaona, hivyo na wewe ukionyesha tabia hizo, kuonyesha fadhili kwa watu wasio na malipo kwako, basi rohoni unaonekana umeketi na Mungu kwenye meza moja ukimsikiliza kwa makini akikupa maagizo ya kufanya, hiyo ni zaidi ya sauti, au ndoto, au maono elfu kumi, unayoweza kuyasikia.

Mathayo 5:46 “Maana mkiwapenda wanaowapenda ninyi mwapata thawabu gani? Hata watoza ushuru, je! Nao hawafanyi yayo hayo?

47 Tena mkiwaamkia ndugu zenu tu, mnatenda tendo gani la ziada? Hata watu wa mataifa, je! Nao hawafanyi kama hayo?

48 Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu”.

Kwahiyo, tujifunze kuitambua sauti ya Mungu wetu kwa kuzitazama kazi zake, vilevile tujifunze kuielewa sauti ya adui yetu ibilisi, ili tuweze kumkwepa na yeye, kwasababu kamwe tusitazamie, sikumoja atakuja kutunong’oneza kwenye masikio yetu “nenda ukazini”, hilo halipo.

Je! Umeokoka? Je! Unafahamu kuwa tupo katika muda wa nyongeza tu, siku yoyote Kristo anarudi. Unasubiri nini huko nje? Utajisikiaje usikie unyakuo umepita halafu wewe umebaki, utamweleza nini Bwana Yesu. Tubu dhambi zako leo kwa kumaanisha kabisa kumrudia Mungu wako, injili tuliyobakiwa nayo sio ya kubembelezewa wokovu tena, ni wewe mwenyewe kuona na kuchukua hatua. Muda umeisha.

Bwana akubariki sana.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

Je ni kweli imani ya mtu ndiyo itakayomuokoa, na si kitu kingine?

UNYAKUO.

TUMEFANYIKA KUWA WANA WA MUNGU!

Makerubi wenye sura nne, ni kweli wapo? na je! wanyama wataenda mbinguni?

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments