Jina la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe, karibu tujifunze biblia neno la Mungu wetu, ambalo ni taa iongozayo miguu yetu na Mwanga wa njia yetu.
Leo tutajifunza juu ya mtu mmoja aliyeitwa Theofilo, ambaye biblia haijaeleza habari zake kwa urefu lakini amehusika pakubwa sana katika kuieneza injili.
Lakini kabla ya kwenda kumtazama huyu Theofilo hebu tuweke msingi kidogo kwa kuelewa juu ya baadhi ya nyaraka za kwenye biblia.
Katika maandiko hususani agano jipya tunaona nyaraka kadhaa, zikiandikwa kwa watu fulani, ambazo hizo zimekuwa msaada hata kwetu sisi wa nyakati hizi.
Kwamfano tunaona waraka ambao Paulo alimuandikia Timotheo, au Tito au Filemoni…Nyaraka hizo zilikuwa zinawasaidia hao watu kuwajenga na kuwaimarisha katika utumishi wao, lakini tunaona Mungu aliziruhusu zienee na kusomwa na watu wengi hata mpaka wakati wetu huu.
Hawa wakina Tito, Filemoni, na Timotheo hawakujua kuwa barua hizo walizotumiwa na Paulo zitakuja kusomwa na maelfu ya vizazi mbeleni..wao pamoja na Paulo hawakulijua hilo.
Ni sawa na wewe leo umwandikie Barua ndugu yako aliyeko mbali, lakini ipite miaka mingi sana huko mbele uje usikie hiyo barua uliyomuandikia inasomwa duniani kote..bila shaka utashangaa…Ndivyo ilivyokuwa kwa Paulo na hawa wakina Timotheo, Tito na Filemoni..waliandikiana barua wao kwa wao kwa lengo la kuimarisha utumishi wao.. lakini kumbe Mungu alikuwa ana malengo makubwa sana na hizo barua..
Hapa tumechukua mifano ya hawa watatu Timotheo, Tito na Filemoni kwasababu ndio wanaojulikana sana..
Lakini pia katika maandiko pia kulikuwa na mtu mwingine wa kipekee sana, ambaye hajulikani sana lakini alichangia pakubwa sana katika uandishi wa vitabu vya biblia.. mtu huyu si maarufu sana ukilinganisha na hawa wakina Timotheo..
Na mtu huyo si mwingine zaidi ya THEOFILO MTUKUFU.
Kama vile kulivyokuwa na waraka wa kwanza na wa pili Paulo aliomwandikia Timotheo, kulikuwepo pia na waraka wa kwanza na wa pili kwa Luka aliomwandikia huyu mtu anayeitwa Theofilo.
Wengi wetu hatujui kuwa kitabu cha Luka na cha Matendo ya Mitume, ni nyaraka maalumu kwa mtu Fulani, hazikulengwa kwa watu wote, au kwa kanisa kwa ujumla…bali zilikuwa ni barua maalumu kwa mtu Fulani ambaye ndiye huyu Theofilo, yaani maana yake ni kwamba kitabu cha Luka na Matendo ya Mitume.. kwa lugha nyingine kingeweza kuitwa Waraka wa Kwanza kwa Theofilo, na waraka wa pili kwa Theofilo..Kwasababu vitabu hivyo viwili vilikuwa ni waraka kwa Theofilo kama kitabu cha Timotheo wa kwanza na wa pili.
Sasa huyu Theofilo alikuwa ni nani?
Kwa ufupi ni kwamba huyu Theofilo, alikuwa ni mkuu fulani, ambaye inasemekana alikuwa Mrumi, na wala hakuwa myahudi. Alikuwa ni mtu mwenye cheo, lakini alikuwa ni mtu wa kipekee sana.
Kwani ulifika wakati akasikia habari zinazomhusu Yesu, na Mitume wake pamoja na Paulo. Lakini hakuwa na uhakika nazo, huku anasikia hichi kule anasiki kile n.k Kipindi anasikia hizo habari, tayari Bwana Yesu ameshaondoka na Mtume Paulo alikuwa ameshakuwa mzee sana, na Mitume walikuwa wameshatawanyika duniani kote..
Hivyo alichikifanya kwasababu alikuwa ni mtu mkubwa, na mwenye cheo, kwa hekima alikwenda kumtafuta mtu mmoja anayeitwa Luka ambaye alikuwa anatembea sana na Mtume Paulo katika safari zake.
Na lengo la kumtafuta huyu Luka ni ili apate taarifa za kutosha na uhakika wa mambo aliyokuwa anayasikia na kuambiwa na watu yamhusuyo Yesu na Mitume wake. Hivyo akamsihi na kumwomba amuandikie kwa waraka mambo yote, tukio moja baada ya lingine tangu kuzaliwa kwa Yesu, kupaa kwake na Matendo yake yote, pamoja na matendo yote ya Mitume.
Hatujui alimsapoti Luka kwa kiwango gani, kwaajili ya kuifanikisha hiyo kazi, lakini aliifanya kwa moyo.
Na Luka kwasababu alikuwa ni mmoja wa watu waliokuwa wanapenda Mungu na mwenye elimu kubwa ya ufalme wa Mungu, na hata ya kidunia,(kwani alikuwa ni Tabibu) alimuandikia huyu Mtukufu Theofilo, tukio moja baada ya lingine, tangu kuzaliwa kwa Yesu, mpaka kupaa kwake mbinguni, na hakuishia hapo tu..bali akaendelea kumwandikia habari za mitume wake aliowaacha baada ya kupaa kwake..
Akamwandikia matendo yao, jinsi walivyohubiri injili kwa nguvu za Roho na kufanikiwa kuanzia Yerusalemu mpaka mwisho wa dunia.. Na huko huko akamwelezea pia habari za Paulo jinsi alivyoipeleka injili kwa mataifa yote, safari zake na mafanikio yake yote.
Na Luka baada ya kukusanya taarifa hizo na kuziandika, ndipo akamtumia huyu Theofilo nyaraka hizo…Na nyaraka hizo ndizo tunazozisoma leo ambazo ni kitabu cha LUKA NA MATENDO YA MITUME.
Na bila shaka Theofilo baada ya kuzipokea nyaraka hizo mbili, aliridhika pakubwa sana, utata ukaondoka kichwani mwake na akamtukuza Mungu..na kuelewa na kupata uhakika wa mambo yote..
Hebu kwa ufupi tusome muhtasari wa nyaraka hizo Luka alizomwandikia Theofilo, na kisha tuende kutazama ni nini tunachoweza kujifunza kutoka kwa huyu mtu.
Luka 1:1 “Kwa kuwa watu wengi wametia mikono kutunga kwa taratibu habari za mambo yale yaliyotimizwa katikati yetu, 2 kama walivyotuhadithia wale waliokuwa mashahidi wenye kuyaona, na watumishi wa lile neno tokea mwanzo, 3 NIMEONA VEMA MIMI NAMI, KWA KUWA NIMEJITAFUTIA USAHIHI WA MAMBO HAYO YOTE TANGU MWANZO, KUKUANDIKIA KWA TARATIBU, THEOFILO MTUKUFU, 4 UPATE KUJUA HAKIKA YA MAMBO YALE ULIYOFUNDISHWA”.
Luka 1:1 “Kwa kuwa watu wengi wametia mikono kutunga kwa taratibu habari za mambo yale yaliyotimizwa katikati yetu,
2 kama walivyotuhadithia wale waliokuwa mashahidi wenye kuyaona, na watumishi wa lile neno tokea mwanzo,
3 NIMEONA VEMA MIMI NAMI, KWA KUWA NIMEJITAFUTIA USAHIHI WA MAMBO HAYO YOTE TANGU MWANZO, KUKUANDIKIA KWA TARATIBU, THEOFILO MTUKUFU,
4 UPATE KUJUA HAKIKA YA MAMBO YALE ULIYOFUNDISHWA”.
Huo ni waraka wa kwanza wa Luka aliomwandikia Theofilo Mtukufu..waraka mwingine wa pili ni kama ufuatao..
Matendo 1:1 “ Kitabu kile cha kwanza nalikiandika, THEOFILO, katika habari ya mambo yote aliyoanza Yesu kufanya na kufundisha, 2 hata siku ile alipochukuliwa juu, alipokuwa amekwisha kuwaagiza kwa Roho Mtakatifu wale mitume aliowachagua; 3 wale aliowadhihirishia nafsi yake, kwa dalili nyingi, baada ya kuteswa kwake, ya kwamba yu hai, akiwatokea muda wa siku arobaini, na kuyanena mambo yaliyouhusu ufalme wa Mungu”.
Matendo 1:1 “ Kitabu kile cha kwanza nalikiandika, THEOFILO, katika habari ya mambo yote aliyoanza Yesu kufanya na kufundisha,
2 hata siku ile alipochukuliwa juu, alipokuwa amekwisha kuwaagiza kwa Roho Mtakatifu wale mitume aliowachagua;
3 wale aliowadhihirishia nafsi yake, kwa dalili nyingi, baada ya kuteswa kwake, ya kwamba yu hai, akiwatokea muda wa siku arobaini, na kuyanena mambo yaliyouhusu ufalme wa Mungu”.
Huo ni waraka wa pili wa Luka aliomwandikia huyu Theofilo.
SASA NI NINI TUNAJIFUNZA KWA THEOFILO?.
Kabla ya kujua ni nini tunajifunza hebu tafakari ni mambo mangapi mazuri na ya kujenga tunayoyapata ndani ya hivyo vitabu viwili vya LUKA na MATENDO YA MITUME?.
Kama wewe ni msomaji wa biblia utajua ni jinsi gani, vitabu hivyo viwili vilivyokuwa vya muhimu na vyenye mafunzo mengi ya kiimani.
Theofilo aliona si vyema kusikia habari za Yesu juu juu tu, alitaka kujua alizaliwaje, katika mazingira gani, ndugu zake ni wakina nani, alihubiri nini, kwa muda gani, na alikufaje, alifufukaje na yupo wapi sasa hivi..Pengine alitaka hivyo kwa ajili ya faida yake na ya watoto wake na ndugu zake..
Lengo ni ili asipelekwe pelekwe na kila upepo wa elimu uliozagaa huko na huko, ili asichukuliwe na upotoshaji unaomhusu Yesu na wanafunzi wake..Hivyo akamtafuta Luka ambaye alikuwa ni mwenye elimu nyingi, na mwanafunzi wa Imani ya kikristo, amwandikie kwasababu aliamini ndiye chanzo salama na sahihi cha taarifa kwa wakati huo.
Na Luka akatimiza kiu yake kwa kumtafutia habari hizo kwa urefu na kumwandikia zote.
Ndio maana hapo Luka unaona anamwambia “NIMEONA VEMA MIMI NAMI, KWA KUWA NIMEJITAFUTIA USAHIHI WA MAMBO HAYO YOTE TANGU MWANZO, KUKUANDIKIA KWA TARATIBU, THEOFILO MTUKUFU”
Na kama tulivyojifunza, huyu Theofilo hakuridhika kusikia habari za Yesu tu! Na matendo yake..bali alizidi kutamani kujua Matendo ya Mitume wa Yesu kwa urefu.. kwani alikuwa anasikia tu habari za Mitume wake juu juu, alikuwa anamsikia tu Paulo, lakini yeye akataka kujua huyu Paulo ni nani, ni jinsi gani alimpokea Yesu, safari zake zilikuwaje, ni nini aliyopitia akiwa safarini, hatua kwa hatua..na Luka akamwandikia habari zote hakuacha kitu!
Hebu jiulize kwa kupitia safari na maisha ya Paulo tunayoyasoma katika kitabu cha Matendo ya Mitume tumejifunza mangapi leo?, Bila shaka ni mengi sana.. tumejifunza kumbe katika safari ya imani kuna kupanda na kushuka, wakati mwingine kuna kupitia dhiki na vifungo n.k.
Hivyo Theofilo kwa kutamani kuyajua hayo, na kutafuta kwa bidii taarifa hizo za Bwana Yesu, imekuwa msaada na kwetu sisi pia.
Kadhalika na sisi tunajunza hayo hayo…
Kwamba hatuna budi kuwa kama Theofilo..kuhusiana na masuala ya ufalme wa Mbinguni..
tunapotia bidii kutafuta kulijua Neno la kweli la Mungu, taarifa zile haziji kutusaidia sisi peke yetu, bali pia wengine, na hata vizazi vijavyo.. kwasababu kwa kutafuta huko..kutakuja kuwafaa wengine na kuwabariki wengine huko mbeleni, na kuwa kumbukumbu bora kwetu.
Unapoona Neno katika maandiko hulielewi kwanini usitafute kwa bidii kulijua na kisha kuliandika au kuwafundisha wengine au watoto wako kwa msaada wa wao?..Leo utaona halina maana lakini hujui Mungu kalikusudia nini mbeleni.
Pengine Theofilo aliutaka ule waraka kwa faida yake tu na watoto wake, kumbe Mungu alikuwa na mpango na huo waraka kwa mamilioni ya watu huko mbeleni. Hata sisi kuna mambo ambayo tunaweza kuyafanya sasa, tukidhani yanaishia hapa tu kumbe Mungu ana malengo nayo kuwa msaada kwa maelfu ya watu mbeleni..
Hebu jiulize ni taji kubwa kiasi gani alilonalo huyu Theofilo?.. ambaye hata hakuwa Myahudi?..
Siku ile atasimama na kumwambia Bwana kwa utafiti wake na bidii yake ya kutaka kujua habari za Kwake na Mitume wake, imekuwa Baraka watoto wake na ndugu zake, lakini Bwana atamwonyesha mabilioni ya watu katika vizazi vya mbeleni waliobarikiwa kwa jitihada yake hiyo..
Kwasasa huyu Theofilo hajui chochote kwasababu kalala, lakini siku ya ufufuo, ndipo atakapojua jinsi thawabu yake ilivyo kubwa..Na naamini kama angejua angetafuta pia habari nyingine nyingi ili apate taji bora zaidi.
Kwa bidii yake kitabu cha Luka na Matendo ya Mitume kimeweza kuwepo!.
Mathayo 8:11 “Nami nawaambieni, ya kwamba wengi watakuja kutoka mashariki na magharibi, nao wataketi pamoja na Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo katika ufalme wa mbinguni”
Na sisi Bwana atujalie tufanye jambo ambalo litatusaidia sisi na vizazi vijavyo..
Marana atha!
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali. Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
Mada Nyinginezo:
WEKA KUMBUKUMBU YA MAMBO BWANA ANAYOKUFANYIA KWASABABU YATAKUFAA MBELENI.
JE UNA MATUMAINI YA KUPATA TENA KILE ULICHOPOTEZA?
Uchaji ni nini kama tunavyosoma katika 1Timotheo 2:10?
USIPUNGUZE MAOMBI.
Rudi nyumbani
Print this post
Daah! Hakika mungu yupo.
Amen
Amina mtumishi wa MUNGU,,, hakika tunawajibika kutia bidii kutafuta habari za kweli kumuhusu BWANA wetu YESU KRISTO bila kujali kuna wimbi kubwa kiasi gani linalotoa mafundisho hayo… THEOFILO si kwamba hakuwahi kusikia kuhusu YESU na MITUME aliwahi lkini akatafuta mtu mmoja anayejua ukweli ili amuandikie kwa utaratibu mzuri kila alichotaka kujua kuhusu BWANA YESU NA MITUME… Haijarishi ni Mara ngapi umesikia habari kuhusu BWANA YESU KRISTO,, Unchopaswa kufanya ni kazana kumtafuta LUKA wako wa leo ili akuandikie kwa usahihi kile ambacho MUNGU amemfunulia ili kiwafae mamilion ya watu hasa kwa huduma hii ya INJILI MTANDAONI… MUNGU awabariki sana team hii ya Wingu la mashahidi, daima mmekuwa waalimu kwangu Kama LUKA mbele ya THEOFILO MTUKUFU…. barikiwa sana mtumishi wa MUNGU.