WEKA KUMBUKUMBU YA MAMBO BWANA ANAYOKUFANYIA KWASABABU YATAKUFAA MBELENI.

WEKA KUMBUKUMBU YA MAMBO BWANA ANAYOKUFANYIA KWASABABU YATAKUFAA MBELENI.

Jina la Bwana wetu Yesu, libarikiwe.

Kuna umuhimu mkubwa sana wa kuweka kumbukumbu za mambo Bwana anayoyafanya katika maisha yako, kwasababu aidha zitakusaidia wewe mbeleni au zitawasaidia wengine. Kila tendo la kimiujiza Bwana analokufanyia liandike chini. Kwasababu zitakuja nyakati ambazo utaishiwa nguvu, na kama utakuwa huna kumbukumbu yoyote kichwani kwako itakuwa ni ngumu kushinda majaribu hayo..

Nguvu ya Daudi kumshinda Goliathi, si upako aliokuwa nao, wala si maono aliyoona wala ndoto aliyoota, bali ni uwezo wa kukumbuka mambo Mungu aliyomtendea wakati alipokutana na simba na dubu, walipokuwa wanavizia kondoo, Bwana alivyomsaidia akawaua, na alipoliweka hilo moyoni, ulipokuja wakati wa jaribu kubwa kama hilo la Goliathi, aliweza kukumbuka jinsi Bwana alivyomsaidia kuwaua wale hayawani wakali, na akamchukulia Goliathi kuwa naye pia atamwua kama alivyowaua wale wanyama.

1 Samweli 17:32 “Daudi akamwambia Sauli, Asizimie moyo mtu ye yote kwa ajili ya huyu; mimi mtumishi wako nitakwenda kupigana na Mfilisti huyu.

 33 Sauli akamwambia Daudi, Huwezi wewe kumwendea Mfilisti huyu upigane naye; maana wewe u kijana tu; na huyu ni mtu wa vita tangu ujana wake.

34 Daudi akamwambia Sauli, Mtumishi wako alikuwa akichunga kondoo za baba yake, na alipokuwa akija simba, au dubu, akamkamata mwana-kondoo wa lile kundi,

35 mimi hutoka nikamfuata, nikampiga, nikampokonya kinywani mwake; na akinirukia, humshika ndevu zake, nikampiga, nikamwua.

36 Mtumishi wako alimwua simba na dubu pia; na huyu Mfilisti asiyetahiriwa atakuwa kama mmoja wao, kwa sababu amewatukana majeshi ya Mungu aliye hai.

37 Daudi akasema, Bwana aliyeniokoa na makucha ya simba, na makucha ya dubu, ataniokoa na mkono wa Mfilisti huyu. Sauli akamwambia Daudi, Enenda, na Bwana atakuwa pamoja nawe”

Umeona hapo?..Daudi alitumia tu USHUHUDA wa Dubu na Simba, kumwangusha Goliathi. Lakini hebu fikiri angekuwa ni mtu wa kusahau, matendo makuu ya Mungu, angepata wapi ujasiri wa kumsogelea Goliathi?.

Kwahiyo tunachoweza kujifunza ni kuwa Ushuhuda wa Daudi kuwaua Dubu na Simba, ulikuwa ni wa muhimu sana kwa nyakati zijazo.

Kadhalika yapo mambo mengi ya kimiujiza ujiza yanayoendelea kila siku katika maisha yetu, ambayo Bwana anayafanya, hatuna budi kuyahifadhi hayo, aidha kwa maandishi, au kama tunakumbukumbu nzuri basi tuyahifadhi mioyoni mwetu yasiweze kupotea.

Hebu tuangalie mfano mwingine wa mtu aliyetunza mambo makuu Mungu aliyoyafanya mbele ya macho yake, ambapo yakaja kuwa ya maana sana siku za mbeleni.

Na mtu huyo si mwingine zaidi ya Mariamu, mama yake YESU.

Asilimia kubwa ya habari tunazozisoma za kuzaliwa kwa Bwana Yesu, na matukio yaliyokuwa yanaendelea wakati wa kuzaliwa kwake, ni kutokana na Mariamu kuwasimulia watu, hakuna mwingine aliyekuwa na taarifa za kutosha kuhusu kuzaliwa kwa Yesu zaidi ya mama yake Mariamu.

Kwamfano habari za wale wachungaji makondeni tunazozisoma, Waandishi kama wakina Luka, Mathayo na Yohana hawakufunuliwa, bali walizipata kutoka kwa Mariamu, mama yake, kwani walikwenda kumuuliza ni nini kilikuwa kinaendelea wakati wa kuzaliwa kwake..Na Mariamu akawaeleza na ndio wakaandika habari hizo.. Hawakufunuliwa habari hizo na Roho Mtakatifu, wala hawakuona maono, hapana!, bali walihadithiwa na wakina Mariamu..

Luka mwenyewe anashuhudia hayo…

Luka 1:1 “Kwa kuwa watu wengi wametia mikono kutunga kwa taratibu habari za mambo yale yaliyotimizwa katikati yetu,

2  KAMA WALIVYOTUHADITHIA WALE WALIOKUWA MASHAHIDI WENYE KUYAONA, na watumishi wa lile neno tokea mwanzo,

3  nimeona vema mimi nami, kwa kuwa nimejitafutia usahihi wa mambo hayo yote tangu mwanzo, kukuandikia kwa taratibu, Theofilo mtukufu,”.

Umeona hapo?. Luka anasema “kama walivyotuhadithia”.. Maana yake ulipofika wakati wa kwenda kuandika habari za Bwana kiusahihi, waliwatafuta wakina Mariamu, na wengine wachache waliokuwepo wakati wa kuzaliwa kwake, wawasimulie yaliyokuwa yanajiri..

Sasa hebu tuchunguze zile habari za wachungaji makondeni Mwandishi Luka alizitolea wapi!..

Luka 2:8  “Na katika nchi ile ile walikuwako wachungaji wakikaa makondeni na kulinda kundi lao kwa zamu usiku.

9  Malaika wa Bwana akawatokea ghafula, utukufu wa Bwana ukawang’aria pande zote, wakaingiwa na hofu kuu.

10  Malaika akawaambia, Msiogope; kwa kuwa mimi ninawaletea habari njema ya furaha kuu itakayokuwa kwa watu wote;

11  maana leo katika mji wa Daudi amezaliwa, kwa ajili yenu, Mwokozi, ndiye Kristo Bwana.

12  Na hii ndiyo ishara kwenu; mtamkuta mtoto mchanga amevikwa nguo za kitoto, amelala katika hori ya kulia ng’ombe.

13  Mara walikuwapo pamoja na huyo malaika, wingi wa jeshi la mbinguni, wakimsifu Mungu, na kusema,

14  Atukuzwe Mungu juu mbinguni, Na duniani iwe amani kwa watu aliowaridhia.

15  Ikawa, malaika hao walipoondoka kwenda zao mbinguni, wale wachungaji waliambiana, Haya, na twendeni mpaka Bethlehemu, tukalione hilo lililofanyika, alilotujulisha Bwana.

16  Wakaenda kwa haraka wakamkuta Mariamu na Yusufu, na yule mtoto mchanga amelala horini.

17  Walipomwona wakatoa habari waliyoambiwa juu ya huyo mtoto.

18  wote waliosikia wakastaajabu kwa hayo waliyoambiwa na wachungaji.

19  LAKINI MARIAMU AKAYAWEKA MANENO HAYO YOTE, AKIYAFIKIRI MOYONI MWAKE.

20  Wale wachungaji wakarudi, huku wanamtukuza Mungu na kumsifu kwa mambo yote waliyosikia na kuyaona, kama walivyoambiwa”

Umeona hapo?, Mariamu aliyaweka hayo yote moyoni!, hakuyapuuzia tu na kuyaacha yapite!, bali aliyatunza, kwasababu alijua siku moja yatakuja kuwafaa wengine huko mbeleni, ambao ndio wakina Luka pamoja sisi.

Kadhalika tuchunguze sehemu nyingine tena Mariamu, aliyoweka kumbukumbu ya maisha ya Mwokozi Yesu..

Luka 2:48 Na walipomwona walishangaa, na mama yake akamwambia, Mwanangu, mbona umetutenda hivi? Tazama, baba yako na mimi tulikuwa tukikutafuta kwa huzuni.

49  Akawaambia, Kwani kunitafuta? Hamkujua ya kuwa imenipasa kuwamo katika nyumba ya Baba yangu?

50  Nao hawakuelewa na neno hilo alilowaambia.

51  Akashuka pamoja nao mpaka Nazareti, naye alikuwa akiwatii; NA MAMAYE ALIYAWEKA HAYO YOTE MOYONI MWAKE.

52  Naye Yesu akazidi kuendelea katika hekima na kimo, akimpendeza Mungu na wanadamu”

Umeona na hapo?..Kama Mariamu asingeyaweka moyoni leo hii tusingejua kama Bwana alikuwa ni mtii kwa Mungu na kwa wanadamu. Na sio tu hayo bali na mengine yote tunayoyasoma yanayomhusu Bwana, ni kutokana na mtu, au watu Fulani kutunza kumbukumbu hizo.

Jambo ambalo limekuja kuwa Baraka kwetu sisi, watu wa vizazi vya baadaye..

Kadhalika na sisi hatuna budi kujifunza katika hayo, tutunze kumbukumbu za yote Bwana anayoyafanya kwetu, au kwa watoto wetu, au kwa jamii yetu, ili kumbukumbu hizo ziweze kuja kutusaidia katika nyakati za baadaye za majaribu, na ziweze pia kusaidia vizazi vingine vijavyo kama vitakuwepo.

Mithali 13:22 “Mtu mwema huwaachia wana wa wanawe urithi; Na mali ya mkosaji huwa akiba kwa mwenye haki”.

Bwana atubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Pia kama utapenda uwe unafikiwa na masomo ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP basi bofya hapa ujiunge moja kwa moja  >>>> WHATSAPP


Mada Nyinginezo:

MAMA, TAZAMA, MWANAO.

Na ulimi laini huvunja mfupa.(Mithali 25:15)

SIKU YA HOFU YANGU NITAKUTUMAINI WEWE.

Hanithi ni nini katika biblia? (kumbukumbu 23:17)

Hapana hata mmoja aliyethubutu kuambatana nao;

HUYU MELKIZEDEKI NI NANI?

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments