MAMA, TAZAMA, MWANAO.

MAMA, TAZAMA, MWANAO.

Nakusalimu katika jina lipitalo majina yote la Bwana wetu Yesu Kristo, karibu  tuyatafakari maneno ya uzima maadamu bado tupo hai. Maandiko yanatuambia ;

Yohana 19:25 “Na penye msalaba wake Yesu walikuwa wamesimama mamaye, na umbu la mamaye, Mariamu wa Klopa, na Mariamu Magdalene.

26 Basi Yesu alipomwona mama yake, na yule mwanafunzi aliyempenda amesimama karibu, alimwambia mama yake, Mama, tazama, mwanao.

27 Kisha akamwambia yule mwanafunzi, Tazama, mama yako. Na tangu saa ile mwanafunzi yule akamchukua nyumbani kwake.”.

Unaweza ukajiuliza ni kwanini Bwana Yesu atengeneze mahusiano ya namna ile pale msalabani na sehemu nyingine yoyote. Bila shaka kulikuwa na watu wengi pale msalabani wakimtazama, walikuwepo wanawake wengi, vilevile walikuwepo wanafunzi wake wengine hata kama hawajaorodheshwa lakini utaona macho ya Bwana yaliwaelekea hao watu wawili tu. Mmoja ni mama yake, na mwingine ni yule mwanafunzi aliyempenda, ambaye ni mtume Yohana.

Jaribu kufikiria Bwana Yesu alikuwa na wadogo zake  wengine wengi lakini hakuna hata mmoja aliyemkabidhisha mama yake, halikadhalika alikuwa na mitume wengi lakini hakuna hata mmojawao aliyemkabidhi mama yake. Vilevile Yohana alikuwa na mama yake mzazi, lakini Yesu hakumwambia amtazame mama yake, kinyume chake alimwambia amtazame Mariamu mama wa Bwana wake. Na wakati huo huo biblia inatuambia Yohana  aliposikia maagizo hayo akamchukua na kumpeleka kwake kuishi naye.

Mahusiano ya namna hiyo, ya mtu kumtunza mama asiye mama yake, na  mwingine kumwita mwanangu, asiye mwana wake, hayaji hivi hivi bali yanatoka kwa Kristo tu, kwa kumwangalia yeye peke yake. Sisi kama kanisa la Kristo hatuwezi kupendana, wala kuchukuliana kama ndugu, kama macho yetu hayatamwelekea Kristo aliyesulibiwa.

Tukiwa ni watu wa kumtazama yule Kristo wa mikate tu, kamwe mahusiano kama haya tusahau kuyaona katikati yetu, kama tutakuwa tunakwenda kumtafuta Kristo kanisani kwasababu ya biashara zetu tu, ili mambo yaende vizuri na wala si kingine, basi tutakuwa tunakusanyika bure, na baada ya hapo kila mmoja ataendelea na mambo yake mwenyewe, kama walivyofanya wale makutano waliokuwa yanamfuata Yesu kila mahali, kwa ajili ya uponyaji tu na vitu vya mwilini utagundua  hakuna hata mmoja aliyemjua mwenzake, anakarama gani, japokuwa walikuwa maelfu kwa maelfu wamekutanika pamoja.

Vilevile leo tunaweza tukawa na idadi kama hiyo makanisani, lakini kama tutakosa umoja na upendo, na mshikamano, kamwe hatutaweza kuwa na nguvu ya kumwona Mungu. Kama tusipomwangalia Kristo katika ule msalaba wake, kamwe hatutakaa tupendane.

Bwana Yesu alisema..

Yohana 13:34 “Amri mpya nawapa, Mpendane. Kama vile nilivyowapenda ninyi, nanyi mpendane vivyo hivyo.

35 Hivyo watu wote watatambua ya kuwa ninyi mmekuwa wanafunzi wangu, mkiwa na upendo ninyi kwa ninyi”.

Bwana Yesu hafurahii, kuona tunasema sisi ni wakristo na huku, hatupendani sisi kwa sisi, kila mmoja anavita na mwenzake, anakinyongo na mwenzake, anajijali yeye tu, na huku wote mpo katika kanisa moja.  Hiyo ni ishara kuwa hatujafika Goligotha na kumsikia Kristo anasema nini kwa ndugu zake.

Na mahusiano yale, ambayo Kristo aliyatengeneza kwa Mariamu na Yohana, hayakuwa ya bure bure tu, yalikuwa na faida nyingi sana kwa wote wawili. Kwanza Mariamu hakujiona tena mpweke , baada ya kuondokewa na mtoto wake, kwani alimpata mtu aliyemjali kama Yesu mwenyewe, pili, Yohana, alifahamu mambo mengine yamuhusuyo Yesu kupitia Mariamu ambayo pengine alikuwa hayajui kabla, ikumbukwe kuwa mitume walimjua Yesu kwa miaka mitatu na nusu tu, lakini nyuma ya hapo miaka yote 30 walikuwa hawajui chochote, siri ya  Maisha yake zilikuwa kwa Mariamu mama yake.

Mariamu ni mwanamke ambaye aliyaweka mambo mengi sana ya Yesu moyoni, alikuwa si mtu wa kuchukulia mambo kawaida kawaida, au juu juu tu soma Luka 2:19

Hivyo ni wazi kuwa Yohana kwa kupitia Mariamu alipata kujua na mambo mengine ya ndani kumuhusu Kristo sikuzote alizokuwa anamtunza, tofauti na mitume wengine, na ndio maana utamwona Yohana, akitokewa tena na  Kristo akionyeshwa maono yale makubwa sana na siri nyingine kati ya hizo aliambiwa asiziandike, alipokuwa kule Patmo, akiandika kitabu cha Ufunuo.

Vivyo hivyo na sisi, tunaweza vunjika mioyo kwa mambo mengi humu ulimwenguni, tunaweza kosa tumaini, lakini Kristo akatupa ndugu ambao watakuwa faraja yetu,  Zaidi hata ya ndugu wengi tulionao, tunaweza tukawa hatujamjua Kristo vizuri, lakini yeye mwenyewe akatupa watu watakaotusaidia kumwelewa yeye kwa vizuri zaidi, kuliko hata waliotutangulia . Lakini hiyo yote haiji hivi hivi, bali inakuja  kwa kumtazama Kristo aliyemsalabani.

Maana yake ni kuwa kwa kuyatafakari yale mateso pale msalabani, kwa  jinsi alivyokufa kwa ajili yetu sisi tusiostahili, itatufanya na sisi kila siku, tujitoe kwa ndugu zetu wengine.

Hivyo na wewe pia fahamu kuwa katika kanisa lako, Kristo anavutiwa na Umoja wako, na Upendo wako kwa wakristo wenzako.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

MAMA UNALILIA NINI?

MAMBO YA KUJIFUNZA KATIKA WARAKA WA PILI WA YOHANA.

UFUNUO: Mlango wa 1

Nini maana ya kumwabudu Mungu katika Roho na kweli?

Bwana Yesu alimaanisha nini kusema “Saa yangu haijawadia?”

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments