KWANINI YESU NI ADAMU WA PILI?

KWANINI YESU NI ADAMU WA PILI?

Jina la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe.

Umewahi kujiuliza kwanini Yesu anajulikana kama Adamu wa Pili au Adamu wa mwisho?

Leo tutajifunza ni kwanini yeye anajulikana hivyo, na kwa kujua huko kutatupa msingi wa kumwelewa Mwana wa Mungu kwa viwango vingine..kama maandiko yanavyosema katika Waefeso 4:13

Waefeso 4:13 “hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na KUMFAHAMU SANA MWANA WA MUNGU, HATA KUWA MTU MKAMILIFU, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo”

Sasa siri ya Yesu kufananishwa na Adamu ya mwisho, mtu wa kwanza kufunuliwa alikuwa ni Mtume Paulo, hebu tusome kidogo…

1Wakorintho 15:45 “Ndivyo ilivyoandikwa, Mtu wa kwanza, Adamu, akawa nafsi iliyo hai; ADAMU WA MWISHO NI ROHO YENYE KUHUISHA.

46 Lakini hautangulii ule wa roho, bali ule wa asili; baadaye huja ule wa roho.

47 Mtu wa kwanza atoka katika nchi, ni wa udongo. Mtu wa pili atoka mbinguni”

Huyo ni Bwana Yesu, mtume Paulo anayemzungumzia hapo.

Sasa ili tumwelewe Adamu wa Mwisho, tabia zake zitakavyokuwa, hebu tumsome kwanza huyu Adamu wa kwanza, alivyokuwa.

Kama wengi wetu tujuavyo Adamu ndiye mtu wa kwanza kuumbwa, na akapewa mamlaka juu ya vitu vyote vya ulimwengu, kwamba akatawale na kuvitiisha chini yake. Na ahadi hiyo hakupewa Adamu peke yake, bali na uzao wake wote, kwasababu sisi wote tulikuwa tumeshaumbwa katika viuno vya Adamu. (tulikuwa kama mbegu tu ambazo bado hazijapandwa). Hivyo Adamu na uzao wake wote ndio walioahidiwa kumiliki na kutawala kila kitu kilichopo chini ya mbingu. (Mwanzo 1:26).

Lakini kama tunavyojua, Adamu alianguka na kupoteza mamlaka yale, akaiuza haki yake ya Umamlaka na kumpa shetani, (ndio maana shetani kuanzia huo wakati akaitwa mkuu wa ulimwengu), hapo kwanza hakuwa hivyo, Adamu ndiye aliyekuwa mkuu wa ulimwengu. Na anguko la Adamu lilisababisha na sisi wote kuanguka kwasababu tulikuwa tupo katika viuno vya Adamu. Hivyo na sisi wote tutakaozaliwa baadaye tutakuwa hatuna mamlaka yoyote, kwasababu Baba yetu Adamu, alishayapoteza.

Hivyo kama si rehema za Mungu na huruma zake, tungekuwa tumeshafutwa kitambo na pengine Mungu angeshaanza uumbaji mwingine. Lakini kwasababu alituhurumia..Ikambidi amlete Adamu mwingine wa pili, kwasababu Adamu wa kwanza kashaharibu….huyu Adamu mwingine hatakuja kwa lengo la kuzaliana. Maana kama angekuja kwa lengo la kuzaliana, ingempasa na yeye awe na Hawa wake na kuzaa vizazi vipya duniani, visivyo na dhambi ambavyo ndivyo vitapewa urithi. Lakini huyu Adamu wa pili hakuletwa duniani kwa kusudi hilo, bali kwa kusudi la kukomboa, Maana yake ni kwamba, hatazaa watu wengine bali vile vile vizazi vya Adamu anavikomboa na kuvifanya uzao wake!.

Sasa anavikomboaje?. Ndio hapo alisema maneno yafuatayo…

Yohana 3:3 “Yesu akajibu, akamwambia, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa mara ya pili, hawezi kuuona ufalme wa Mungu.

4 Nikodemo akamwambia, Awezaje mtu kuzaliwa, akiwa mzee? Aweza kuingia tumboni mwa mamaye mara ya pili akazaliwa?

5 Yesu akajibu, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa kwa maji na kwa Roho, hawezi kuuingia ufalme wa Mungu.

6 Kilichozaliwa kwa mwili ni mwili; na kilichozaliwa kwa Roho ni roho.

7 Usistaajabu kwa kuwa nilikuambia, Hamna budi kuzaliwa mara ya pili”.

Hapo katika mstari wa 6 anasema, kilichozaliwa kwa Mwili ni mwili, maana yake Adamu wa kwanza ndiye aliyetuzaa sisi kimwili, lakini kuzaliwa kwa roho hatuna budi kuzaliwa na huyu Adamu wa pili (Yesu Kristo), kwasababu yeye ndiye anayetuzaa katika roho na si katika mwili kama Adamu baba yetu wa kwanza.

1Wakorintho 15:45 “Ndivyo ilivyoandikwa, Mtu wa kwanza, Adamu, akawa nafsi iliyo hai; ADAMU WA MWISHO NI ROHO YENYE KUHUISHA”.

Kwahiyo kama yule Adamu wa kwanza alivyokabidhiwa mamlaka yote ya duniani na Mungu, kadhalika na huyu Adamu wa pili alikabidhiwa mamlaka yote ya duniani, na si tu ya duniani, bali hata mbinguni.

Mathayo 11:27 “Akasema, Nimekabidhiwa vyote na baba yangu;……..”

Mathayo 28:18 “Yesu akaja kwao, akasema nao, akawaambia, NIMEPEWA MAMLAKA YOTE MBINGUNI NA DUNIANI”

Umeona? Hapo…Nguvu alizonazo Yesu. Si kama watu wanavyomdhania!

Na kama vile Adamu wa kwanza alivyopewa mamlaka hayo pamoja na uzao wake wa kimwili, kadhalika Adamu wa pili Yesu Kristo, mamlaka hayo alikabidhiwa pamoja na uzao wake wote katika roho, maana yake wote watakaozaliwa mara ya pili katika roho, wanakuwa uzao wake na wanakuwa wanarithi Baraka zote alizokabidhiwa Bwana Yesu na Baba.

Warumi 8:16 “Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu

17 na kama tu watoto, BASI, TU WARITHI; WARITHI WA MUNGU, WARITHIO PAMOJA NA KRISTO; naam, tukiteswa pamoja naye ili tupate na kutukuzwa pamoja naye”

Haiishii hapo!!..Kama vile Adamu wa kwanza alivyowasababishia wazao wake wote kuingia kwenye matatizo baada ya kuasi kwake, na hata wale wasio na hatia wakajikuta wanazaliwa katika laana. Kadhalika Adamu wa pili (Yesu Kristo), atauingiza uzao wake wote aliouzaa katika roho, katika hali ya kubarikiwa daima, kwa maana hatatenda dhambi. Umeona umuhimu wa kuzaliwa mara ya pili katika roho???..

Warumi 5:17 “Kwa maana ikiwa kwa kukosa mtu mmoja mauti ilitawala kwa sababu ya yule mmoja, zaidi sana wao wapokeao wingi wa neema, na kile kipawa cha haki, watatawala katika uzima kwa yule mmoja, YESU KRISTO.

18 Basi tena, kama kwa kosa moja watu wote walihukumiwa adhabu, kadhalika kwa tendo moja la haki watu wote walihesabiwa haki yenye uzima.

19 Kwa sababu kama kwa kuasi kwake mtu mmoja watu wengi waliingizwa katika hali ya wenye dhambi, kadhalika kwa kutii kwake mmoja watu wengi wameingizwa katika hali ya wenye haki”

Umeona ni jinsi gani, Mkuu wa Uzima Yesu Kristo, biblia inavyomfunua kama Adamu wa pili?.

Kumbuka wote waliozaliwa mara ya pili katika roho hao ndio wa uzao wa Yesu Kristo, na ni lazima kila mtu azaliwe mara ya pili kwa mbegu isiyoharibika ya Yesu Kristo ili aweze kuuona ufalme wa mbinguni kama yeye mwenyewe alivyosema. Mbegu ya Adamu imeshaharibika, ndio maana tunaumwa, tunakufa, tunateseka, tunarithi mauti n.k.

Lakini tunapozaliwa katika mbegu isiyoharibika ya Yesu Kristo, mauti, shida, dhiki, magonjwa yote yanakuwa yamekwisha… Na yatakwisha kikabisa kabisa wakati wa ukombozi wa miili yetu, utakaokuja siku ile ya unyakuo, tutakapovikwa miili ya utukufu. (Waefeso 4:30).

1Petro 1:23 “Kwa kuwa mmezaliwa mara ya pili; si kwa mbegu iharibikayo, bali kwa ile isiyoharibika; kwa neno la Mungu lenye uzima, lidumulo hata milele”.

Je umezaliwa mara ya pili?..

Kama bado unasubiri nini?..Hakuna tumaini lolote katika Uzao wa Adamu wa kwanza… yeye kashaharibu mambo yote, hana mamlaka tena…Mamlaka yote kwasasa yapo kwa huyu Adamu wa Pili Yesu Kristo. Na unaingia katika uzao wake kwa kuzaliwa mara ya pili…maana yake kwa kutubu dhambi zako zote na kubatizwa katika ubatizo sahihi wa maji mengi na kwa jina la Yesu Kristo na kupokea Roho Mtakatifu (Matendo 2:38),. Hapo utakuwa umezaliwa kwa maji na kwa Roho,.

Na utakuwa umeingizwa katika uzao wa Yesu Kristo.

Bwana Mkuu, anayemiliki mbinguni na duniani, Adamu wa mwisho, aliyeshinda mauti na shida akubariki.

+255693036618/ +255789001312

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Jiunge na magroup yetu ya whatsapp kwa kubofya hapa > WHATSAPP-Group


Mada Nyinginezo:

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
4 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Anonymous
Anonymous
1 year ago

Utukufu kwa Mungu wetu aliye mbinguni

Emmanuel Kitengule
Emmanuel Kitengule
1 year ago

Asante kwa kutuondolea ujinga wa kiroho.

Anonymous
Anonymous
2 years ago

Amina