NITAJUAJE KAMA MAOMBI YANGU YAMEFIKA (YAMEJITOSHELEZA)?.

NITAJUAJE KAMA MAOMBI YANGU YAMEFIKA (YAMEJITOSHELEZA)?.

Biblia inatufundisha kuomba bila kukoma…

Wathesalonike 5:17  “ombeni bila kukoma”

Leo tutatazama ishara chache ambazo zitatutambulisha kuwa kiwango cha maombi yetu kimejitosheleza au kimemfikia Baba yetu.

1.MZIGO KUPUNGUA NDANI YAKO.

Hii ni ishara ya kwanza itakayokutambulisha kuwa maombi yako yamefika kwa Bwana.

Unapoomba na kuona mzigo wa kile unachokiombea umepungua ndani yako, basi hiyo ni ishara kuwa kiwango chako cha maombi kimefikia kilele kwa muda huo.

Sasa swali utauliza utajuaje kuwa mzigo umepungua ndani yako?. Tuchukue mfano rahisi, Ulikuwa una jambo la muhimu au la siri ambalo ulikuwa umepanga kumweleza mtu Fulani (labda rafiki yako), na hujapata nafasi, ila unaitafuta kwa bidii, kiasi kwamba huwezi kutulia mpaka umemweleza jambo hilo, au umpe taarifa hiyo, sasa kipindi utakapokutana naye na kumweleza yote ya moyoni mwako, kuna hali Fulani unajiona mwepesi baada ya hapo, (unajiona kama huna deni tena, umeutua mzigo), unaona amani inarudi, na unakuwa huru.. Sasa hiyo hali unayoisikia baada ya kufikisha ujumbe kwa uliyemtarajia ndio kwa lugha nyingine ya (Mzigo kupungua ndani yako).

Kwahiyo hata sisi tunapoomba, yaani tunapopeleka hoja zetu mbele za Mungu, kabla ya kuzipeleka tunakuwa na mzigo mzito ndani yetu, lakini tunapokaa katika hali ya utulivu na kusema na Mungu kwa unyenyekevu mambo yetu na hoja zetu, basi kuna hali/hisia fulani ambayo Bwana Yesu anaiachia ndani yetu, inayotupa wepesi katika roho zetu, na kupunguza ule mzigo, kiasi kwamba, kama ulikuwa unamwombea Mtu, kuna hali Fulani inakuja ndani yako kuwa maombi yako yamemfikia Mungu, na hivyo amani ya kipekee inashuka ndani yako, na unajikuta ile hamu ya kuendelea kuombea hilo jambo inaisha, badala yake inakuja hali nyingine ya kumshukuru Mungu na kumshangilia na kumfurahia.

2. ANDIKO KUKUJIA au KUMBUKUMBU YA JAMBO FULANI.

Hii ni ishara ya pili ya maombi yetu kumfikia Baba..

Unapokuwa katika maombi, halafu ghafla likaja andiko katika ufahamu wako, na andiko hilo linauhusiano mkubwa na kile ulichokuwa unakiombea.. basi fahamu kuwa maombi yako yamefika, na hivyo Bwana anakuthibitishia kwa kukupa hilo andiko. Au unaweza kuwa unaomba halafu ghafla ukaletewa kumbukumbu Fulani ya kisa Fulani katika biblia, ambapo kupitia kisa hiko imani yako ikanyanyuka na kujikuta unapata amani au furaha kubwa.. basi hiyo ni ishara kuwa maombi yako yamefika, na hivyo katika hiyo hatua na kuendelea ni wakati wa kumshukuru Mungu na kuutafakari ukuu wake, kwasababu Bwana kashajibu na kusikia.

Vile vile unapokuwa katika maombi na moyoni una mzigo mkubwa kwa kile unachokiombea, halafu ghafla ikaja kumbukumbu Fulani ya kipindi Fulani cha maisha ambacho Mungu alikupigania ukauona mkono wake, au ukaja ushuhuda Fulani kichwani mwako wa mtu mwingine, na ghafla ukajiona umepata nguvu nyingine basi hiyo ni ishara kuwa hoja zako zimefika mbele zake na hivyo Bwana amekuthibitishia kwa kukukumbusha uweza wake na mkono wake.

3. NGUVU MPYA.

Unaweza usisikie chochote unapokuwa katika maombi, (yaani usisikie mzigo kupungua ndani yako) au usiletewe andiko lolote, lakini ukajikuta  unapata nguvu ya kuendelea mbele zaidi….

Maana yake kabla ya maombi ulikuwa umekata tamaa, hata nguvu ya kuendelea mbele ulikuwa huna, lakini baada ya maombi..unaona kuna ujasiri umeongezeka ndani yako, kuna nguvu ya kuendelea mbele imekuja ndani yako, ingawa moyoni mzigo bado hujapungua..

Sasa hiyo hali ya kutiwa nguvu kabla ya kupokea majibu ya maombi yako ni ishara kuwa Maombi yako YAMEMFIKIA BWANA, ila wakati wa kupokea majibu yako bado!…Hivyo Bwana anakutia nguvu ili usije ukazimia kabisa, au ukaanguka kabisa…wakati huo zidi kujisogeza mbele zake kwa maombi ya shukrani…

Kwamfano unaweza kuwa unasumbuliwa na ugonjwa ambao ni mbaya sana, na umemwomba Mungu kwa muda mrefu, akuponye na hapo ulipo upo katika hali ya mauti uti, lakini ukajikuta unapata unafuu mkubwa sana, na hata kuendelea na shughuli zako kana kwamba huumwi kabisa.. lakini ule ugonjwa bado haujaondoka!.. sasa hiyo hali ya kupata unafuu baada ya maombi, ni ishara kuwa Bwana alishasikia maombi yako, ila siku kamili ya muujiza mkuu bado!, (na itafika tu)..lakini amekutia nguvu ili kukuonyesha kuwa yupo pamoja na wewe na ili usije ukazimia kabisa..

Vile vile unaweza kumwomba Bwana akupe kazi fulani nzuri ambayo kupitia hiyo utayafanya mapenzi yake, lakini badala ya kukupa hiyo shughuli unayoiomba muda ule uliomwomba, yeye anakupa riziki za kukutosha tu wakati huo.. (ulitegemea upewe kazi lakini yeye anakupa riziki tu)…Ukiona hivyo jua ni ishara ya kuwa maombi yako yameshamfikia yeye, Ndio maana anakutia nguvu…ni suala la muda tu!, mambo yote yatakaa sawa..

Isaya 40:27 “Mbona unasema, Ee Yakobo, mbona unanena, Ee Israeli, Njia yangu imefichwa, Bwana asiione, na hukumu yangu imempita Mungu wangu asiiangalie?

 28 Je! Wewe hukujua? Hukusikia? Yeye Mungu wa milele, Bwana, Muumba miisho ya dunia, hazimii, wala hachoki; akili zake hazichunguziki. 

29 Huwapa nguvu wazimiao, humwongezea nguvu yeye asiyekuwa na uwezo

30 Hata vijana watazimia na kuchoka, na wanaume vijana wataanguka; 

31 bali wao wamngojeao Bwana watapata nguvu mpya; watapanda juu kwa mbawa kama tai; watapiga mbio, wala hawatachoka; watakwenda kwa miguu, wala hawatazimia.”.

Zipo ishara za kutambulisha kuwa maombi yetu yamemfikia Baba yetu, lakini kwa hizi chache itoshe kusema kuwa Bwana Mungu wetu anatupenda na anatujali na anasikia maombi yetu. Lakini kumbuka kuwa kama bado hujampokea Yesu, (yaani hujaokoka), basi fahamu kuwa Mungu hasikilizi maombi yako wala hajibu. (Yohana 9:31)

Sasa ni kwanini hajibu, wala hasikilizi maombi ya watu ambao hawajampokea?.. Ni kwasababu mtu wa namna hiyo hawezi kuomba sawasawa na mapenzi yake, (kwasababu yeye mwenyewe alisema kuwa mafanikio ya mpumbavu yatamwangamiza, Mithali 1:32) na Mungu hapendi mtu yeyote aangamie wala apotee, bali wote wafikie toba na wafanikiwe..Hivyo atahakikisha kwanza unapata wokovu ndipo mengine yafuate..

Kwahiyo suala la kwanza ni wokovu kabla ya mambo mengine yote.. Kama hujampokea Yesu, kwa kutubu dhambi zako, na kubatizwa katika ubatizo sahihi, basi ni vizuri ukafanya hivyo mapema iwezekanavyo, ili uwe mshirika wa Baraka za Mungu.

Lakini kama tayari umeshampokea Yesu na umesimama vizuri katika imani, basi fahamu kuwa yote unayomwomba Mungu atakupatia sawasawa na ahadi zake, hivyo zidi kumwamini na wala usiishiwe nguvu.

Bwana akubariki

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

WALIPO WAWILI AU WATATU KWA JINA LANGU

KUNA AINA NGAPI  ZA MAOMBI?

YAFUATAYO NI MAWAZO YA ADUI HIVYO USIYASIKILIZE.

SAUTI NYUMA YA ISHARA.

MAOMBI KWA WENYE MAMLAKA.

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments