“Mimi na ndugu yangu tumekuwa na desturi ya muda mrefu kukaa pamoja na kushirikishana NENO LA MUNGU mara nyingi ili kuepuka usumbufu wa watu tumekuwa tukiondoka na kwenda mbali na makazi ya watu, sehemu zenye utulivu na kutumia muda mwingi kulitafakari NENO LA MUNGU, pamoja na kutiana moyo katika safari yetu ya Ukristo. Siku moja wakati tunatembea muda wa mchana kama saa 7 huku tunazungumza habari za Mungu na kutafakari ghafla mbele yetu njiani umbali si mrefu sana, tulioana punda watatu wamefungwa NIRA wanafuata njia, wakikokota kigari cha mzigo wa majani na nyuma kulikuwa na mtu mmoja aliyekuwa akiwaendesha hao punda, lakini jambo moja lilitushangaza kidogo ni kuona punda 3 wamefungwa nira huku wakikivuta kile kigari wakati mara nyingi inakuwa ni punda wawili tu!.
Hivyo tulipokaribia kuwasogelea ili tuone vizuri, Yule punda aliyekuwa katikakati yao alitoweka wakabaki punda wawili kama kawaida. Wakati tunalishangaa hilo tukio lilitokea wale punda walifika mahali wakakuta na mtaro, uliokuwa mgumu kidogo kuvuka kutokana na ule mzigo waliokuwa wanauvuta, hivyo Yule Bwana wao aliokuwa anawaongoza alipoona wamesimama aliwachapa kwa fimbo yake aliyokuwa nayo, lakini japo ule mzigo ulikuwa ni mkubwa kwa wao kuuvukisha katika ule mtaro mwishoni walifanikiwa kupandisha na kuendelea na safari.