SAUTI NYUMA YA ISHARA.

SAUTI NYUMA YA ISHARA.

 Mungu amekuwa akisema na watu mara nyingi kwa kutumia ishara, kwa kusudi la kuonya au kuhadharisha watu wake jambo ambalo litakuja kutokea endapo watu hawatatubu, wageuke na kuziacha dhambi zao. Kwahiyo Mungu amekuwa akiwatumia watu wake wafanyike ishara ili kizazi hicho kiamini na kutubu, na kwamba kisipoamini na kutubu kitaadhibiwa kwa sababu ya kutokusadiki sauti nyuma ya hiyo ishara ambayo Mungu amekipa kizazi hicho.

ISHARA YA YONA:

Yona 1-4,Tunaona katika biblia mfano hai ni Yona, Mungu alipompa maagizo ya kwenda kukionya kizazi cha watu wa Ninawi kiache uovu na kitubu, kimgeukie Mungu kwa kuwa maovu yake yamekuwa mengi, lakini tunafahamu kuwa Yona alikaidi na kukimbilia Tarshishi lakini tunaona ule ulikuwa ni mpango wa Mungu Yona kufanya vile ili amezwe na yule samaki kule baharini na akae tumboni mwa samaki siku tatu, mchana na usiku ili kusudi kwamba Mungu amfanye yeye kuwa ishara kwa faida ya watu wa Ninawi ili kwa kuona ile ishara watubu, maana pasipo ile ishara watu wa Ninawi wasingeamini na wangeishia kuangamizwa,

Lakini tunafahamu ile habari kuwa baada ya wale watu kuisikia ile ishara ya Yona ya kukaa tumboni mwa samaki siku tatu waliogopa na kutubu na kuacha njia zao mbaya. Ile ishara ilikuwa ni neema ya Mungu kwa watu wa Ninawi.Vivyo hivyo ishara kama hiyo wangeonyeshwa watu wa Sodoma na Gomora wasingeangamizwa kwani wangetubu wote, kama Bwana Yesu Kristo alivyosema mathayo 21:11.

ISHARA YA YESU KRISTO:

Baada ya maovu kuwa mengi Mungu alimtuma mwanawe Yesu Kristo ulimwenguni kufanyika ishara ili vizazi vyote vilivyobakia vitubu, watu waokoke na ghadhabu ya Mungu ambayo itakuja kuupata ulimwengu wote hivi karibuni, ilikuwa ni ngumu sana kwa wakati ule kumwamini Kristo kuwa ndiye mwokozi wa ulimwengu kama asingefanyika kuwa ishara kwa dunia nzima iamini, na ishara hiyo ilikuwa ni kufa na kukaa siku tatu kaburini na kufufuka, kama yeye mwenyewe alivyotabiri katika 

Mathayo 12:38-40″ Hapo baadhi ya waandishi na Mafarisayo wakamjibu, wakasema, Mwalimu, twataka kuona ishara kwako. Akajibu, akawaambia, Kizazi kibaya na cha zinaa chatafuta ishara, wala hakitapewa ishara, ila ishara ya nabii Yona. Kwani kama vile Yona alivyokuwa siku tatu mchana na usiku katika tumbo la nyangumi, hivyo ndivyo Mwana wa Adamu atakavyokuwa siku tatu mchana na usiku katika moyo wa nchi. “

 Kwahiyo Bwana Yesu Kristo alipomaliza kazi yake hapa duniani alipaswa apae aondoke lakini angeondoka bila kufanyika ishara ulimwengu tusingeamini, hivyo basi ilimpasa afe akae kaburini siku tatu kama Yona kisha afufuke ndipo apae, ili sisi kwa kuiona ile ishara tumuamini Yesu kuwa yeye ndiye masihi kweli na katumwa na Mungu, ili kwa maneno yake tutubu na kumgeukia Mungu tuiepuke ghadhabu inayokuja. kwahiyo kwa ishara ya Yesu Kristo mpaka sasa sisi tunaokolewa, na asiyemwamini atahukumiwa kama walivyohukumiwa watu wa kizazi cha Nuhu na watu wa Sodoma na Gomora, mpe Yesu Kristo maisha yako leo.

ISHARA KWA KIZAZI CHETU:

Katika kizazi chetu pia Bwana amekuwa akiwatumia watu wake mbali mbali kama ishara kwenye mataifa mbalimbali na jamii mbalimbali, kwa kusudi la  kukionya kizazi kimgeukie Mungu, kiache njia zake mbaya.Tunaona katika Taifa letu hili la Tanzania Bwana alitupa ishara, inawezekana haujawahi kuisikia habari hii, au kama ulishawahi kuisikia pengine haukuelewa sauti ya Mungu nyuma ya hiyo ishara.

Mnamo Tarehe 9/10/2015 . Wahanga  6 wakiwa katika harakati za kuwaokoa wenzao waliokuwa wamefunikwa na kifusi katika mgodi wa madini huko Nyangalata wilayani Kahama mkoani Shinyanga, kifusi kilishuka na kuwafunika hao watu sita ambao walienda kuwaokoa wenzao, na baada ya muda mrefu kupita  walidhaniwa wameshakufa, mule chini shimoni umbali wa zaidi ya mita 120, Walikaa siku 41 usiku na mchana, katikati ya giza nene, pasipo msaada wowote. Lakini katika hali yao humo shimoni walikuwa wakimlilia Bwana, wakifanya ibada, chakula chao kilikuwa ni mende na vyura, hawakujua hewa ilikuwa inatoka wapi ni dhahiri kuwa ulikuwa ni muujiza wa Mungu..

Kumbuka ndugu Mungu hakuwaacha hawa ndugu mule shimoni siku 41, kuwaburudisha watanzania, Mungu angeweza kuwatoa siku ile ile ya kwanza waliyomlilia lakini Mungu aliwaacha siku zile zote ili kwa kupitia wale tuisikie sauti ya Mungu nyuma ya ile ishara, ili tutubu na kumgeukia Mungu.

Lakini cha ajabu ishara hizi tunaziona kawaida. kama ishara ya Yona kukaa siku tatu tu! watu wa Ninawi waliamini na kutubu kwa kuvaa nguo za magunia je! si zaidi hawa ndugu waliokaa siku 41 usiku na mchana katika moyo wa nchi?? Je! masikio yetu yamezibwa? tunaliona hili jambo  kuwa la kawaida, hatuelewi sauti iliyo nyuma ya ishara kwamba Mungu anatuvuta sisi tutubu na tumgeukie yeye..kibaya zaidi kizazi chetu hichi cha siku za mwisho ndio kile kilichotabiriwa kufanana na sodoma na gomora Bwana Yesu alisema

 Mathayo 12:41-42″ Watu wa Ninawi watasimama siku ya hukumu pamoja na watu wa kizazi hiki, nao watawahukumu kuwa wamekosa; kwa sababu wao walitubu kwa mahubiri ya Yona; na hapa yupo aliye mkuu kuliko Yona.  Malkia wa kusini atasimama siku ya hukumu pamoja na watu wa kizazi hiki, naye atawahukumu kuwa wamekosa; kwa sababu yeye alikuja kutoka pande za mwisho za dunia ili asikie hekima ya Sulemani, na hapa yupo aliye mkuu kuliko Sulemani.”

 Mungu ametuma manabii wake na watumishi wake wengi, sauti yake imesambaa kila mahali kwa ishara nyingi na miujiza. Pia tunaona Kwa kizazi chetu Mungu alimtuma mjumbe wake ndugu William Branham na kumpa ishara mbili kama alizopewa Musa ili watu waamini, na Mungu aliruhusu kitendo cha kimiujiza kinaswe katika kamera na kihakikiwe na wanasayansi kuwa ni kweli ili watu watazame na waamini.Tazama video na picha hapa chini.

sikiliza video hii usikie ishara mbili alizopewawilliam branham kwa uthibitisho wa huduma yake, na ujumbe aliopewa.

SAUTI NYUMA YA ISHARA.       Malaika wa Mungu katika mwanga juu ya kichwa cha william branham, uliomtokea juu yake alipokuwa akihubiri. picha hii ilipopigwa ilihakikiwa na wanasayansi kuwa ni ya kimiujiza mwaka 1950, jambo hili la kimiujiza lilishuhudiwa na mamia ya watu waliokuwa mkutanoni siku hiyo

 Hakika Mungu hawezi kufanya jambo lolote bila kuwafunulia watumishi wake hao manabii amosi 3:7, Kwa ishara zote hizi Mungu amezungumza na kizazi chetu kwa njia tofautitofauti, hata hatuna udhuru wa kujitetea siku ya hukumu, Tutawezaje kupona tusipoujali wokovu mkuu namna hii

Lakini bado unaendelea kuwa mwasherati, mlevi,mwizi,mwongo,mchawi, mzinzi, msengenyaji, unaupenda ulimwengu kuliko kumpenda Mungu, uko kwenye tamaa na udanganyifu wa mali vinavyokusonga ukae mbali na Mungu, unaishi maisha ya uvuguvugu haujulikani kama wewe ni mkristo au la,Bwana Yesu alisema katika ufunuo: 3 kwamba watu kama hao atawatapika, na unajua matapishi hayarudiwagi, jichunguze biblia inasema yeye ajionaye kuwa amesimama, na aangalie asianguke. Kama hujazaliwa mara ya pili ni bora ufanye hivyo angali muda upo, Kristo yupo mlangoni kulichukua kanisa lake, ndugu tunaishi katika kizazi ambacho kinaweza kikashuhudia kuja kwa Bwana Yesu mara ya pili, kwamaana dalili zote zinaonyesha na maandiko yanatimia, pengine hatutakuwa na kizazi baada ya hiki, je! utakuwa wapi siku hiyo? jiulize!

Ubarikiwe!

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Nyinginezo:

IELEWE SAUTI YA MUNGU.

VITA BADO VINAENDELEA.

SHETANI KWA SASA NI MZURI WA UMBO KAMA MALAIKA WATAKATIFU AU NI MWENYE MAPEMBE NA MAKWATO NA MAKUCHA MAREFU?

KWANINI MUNGU AWACHOME WATU KWENYE ZIWA LA MOTO NA HALI YEYE NDIYE ALIYEWAUMBA?


Rudi Nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
2 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Samweli
Samweli
1 year ago

Kazi njema Mungu ni Mwema kwa kunipa kuona haya Yana nijenga Ahsante.