Lalama kwa uhai wa watoto wako wachanga wazimiao kwa njaa(Maombolezo 2:19)

by Admin | 15 May 2024 08:46 am05

Mafundisho maalumu kwa watumishi wa Mungu na Watenda kazi wote katika shamba la Bwana.

Maombolezo 2:19

[19]Inuka, ulalamike usiku, Mwanzo wa makesha yake; Mimina moyo wako kama maji usoni pa Bwana; Umwinulie mikono yako; KWA UHAI WA WATOTO WAKO WACHANGA WAZIMIAO KWA NJAA, Mwanzo wa kila njia kuu. 

Ikiwa wewe ni mzazi au mlezi unaelewa ni uchungu mwingi kiasi gani  unakupata  pale unapoona mtoto wako anaangamia kwa kukosa mahitaji yake muhimu, mfano  wa chakula. Ndicho kilichotokea kwa mama Hajiri siku alipofukuzwa kwa Ibrahimu, akiwa kule jangwani amepotea hali ilikuwa mbaya sana, kwani chakula na maji viliwaishia kabisa, huwenda zilipita siku kadhaa hawakuona dalili yoyote ya kupata msaada. Hivyo alichokifanya Hajiri, ni kwenda mbali kidogo na kumlilia sana Mungu wake, na Mungu akasikia, akaonyeshwa palipo na maji, akaenda kumpa mwanae, kuonyesha ni jinsi gani alivyouthamini uhai wa Ishmaeli.

Mwanzo 21:14 Ibrahimu akaamka asubuhi na mapema akatwaa mkate na kiriba cha maji, akampa Hajiri akimtwika begani pake, na kijana, akamruhusu; naye akatoka, akapotea katika jangwa la Beer-sheba. 

15 Yale maji yakaisha katika kiriba, akamlaza kijana chini ya kijiti kimoja. 

16 Akaenda akakaa akimkabili, mbali naye kadiri ya mtupo wa mshale; maana alisema, Nisimwone kijana akifa; naye akakaa akimkabili, AKAPAZA SAUTI YAKE, AKALIA. 

17 Mungu akasikia sauti ya kijana. Malaika wa Mungu akamwita Hajiri kutoka mbinguni, akamwambia, Una nini, Hajiri? Usiogope, maana Mungu amesikia sauti ya kijana huko aliko. 

18 Ondoka, ukamwinue kijana, ukamshike mkononi mwako, kwa kuwa nitamfanya kuwa taifa kubwa. 

19 Mungu akamfumbua macho, naye akaona kisima cha maji; akaenda akakijaza kiriba maji, akamnywesha kijana. 

Umeona kama Hajiri asingemtafuta Mungu katika hali ile, ni wazi kuwa Yule kijana ambaye alikuwa amekusudiwa awe taifa kubwa angefia jangwani na yale maono yasingetokea.

Ndicho tunachojifunza katika vifungu hivyo, kwenye kitabu cha Maombolezo, anasema kesha, ulie, kwa ajili ya watoto wako wachanga wazimiao kwa njaa. Leo hii tuna watu wengi ambao wameokoka kwa kuisikia injili yetu. Lakini je, watu hao wanasimama au wanakufa?, Unapomhubiria mtu, hatutakiwi kusema yaliyobaki namwachia Mungu, bali ni kuhakikisha hafi kiroho kwa kukosa chakula cha uzima. Na hiyo inakuja kwa kuendelea kumfuatilia kumfundisha, Lakini zaidi sana KUMWOMBEA kwa Mungu usiku na mchana akue kiroho.

Tukiiga mfano wa Epafra jinsi alivyokuwa akiwaombea sana watu wa kolosai walioamini kwa injili yao.

Wakolosai 4:12  Epafra, aliye mtu wa kwenu, mtumwa wa Yesu Kristo, awasalimu, akifanya bidii siku zote kwa ajili yenu katika maombi yake, ili kwamba msimame wakamilifu na kuthibitika sana katika mapenzi yote ya Mungu.

Umeona? Ukomavu wa watu walio wachanga wa kiroho hutegemea sana maombi ya kina kwa waliowazaa. Hivyo wewe kama mtenda kazi hakikisha unakuwa na maombi mengi kwa ajili ya wale uliowahubiria injili wakaokoka vinginevyo watakufa kiroho, katika ulimwengu huu wa njaa na kiu ya Neno la Mungu, tenga masaa kuwaombea. Na maombi hayo yawe ya rohoni kabisa, sio ya juu juu, bali ya kuzama, ili Mungu awakuze, na matokeo ya kazi yako utayaona tu baada ya kipindi fulani, jinsi watakavyozidi kubadilika na kukomaa kidogo kidogo, hatimaye kuwa watumishi imara katika shamba la Mungu.

Bwana akubariki.

Shalom.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

NJIA YA ‘UTAJIRI MKUU’ KWA KIJANA.

NJAA ILIYOPO SASA.

LISHA KONDOO WANGU, LISHA WANA-KONDOO WANGU.

Rudi Nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2024/05/15/kwa-uhai-wa-watoto-wako-wachanga-wazimiao-kwa-njaamaombolezo-219/