NJIA YA ‘UTAJIRI MKUU’ KWA KIJANA.

NJIA YA ‘UTAJIRI MKUU’ KWA KIJANA.

Kama tunavyofahamu kuna hatua tatu za maisha ya mwanadamu; Kuna Utoto, Ujana, na Uzee. Na hatua ambayo mtu analazimika kufanya maamuzi juu ya hatma ya maisha yake ni Ujana. Biblia inasema katika Yeremia 21:8b”….Tazama naweka mbele yenu njia ya uzima, na njia ya mauti.” Njia hizi zinatokea mbele ya mtu anapofikia UJANANI. Hivyo inahitajika busara nyingi na hekima ya Mungu katika kuchagua njia ya kuiendea.

Katika biblia tunaweza kujifunza mifano ya vijana wawili ambao walifanya maamuzi ya kuchagua njia za kuendea na hatma zao zilivyokuwa mwishoni.

KIJANA WA KWANZA:

Mathayo 19:16-22

“16 Na tazama, mtu mmoja akamwendea akamwambia, Mwalimu, nitende jambo gani jema, ili nipate uzima wa milele?

17 Akamwambia Kwani kuniuliza habari ya wema? Aliye mwema ni mmoja. Lakini ukitaka kuingia katika uzima, zishike amri.

18 Akamwambia, Zipi? Yesu akasema, Ni hizi, Usiue, Usizini, Usiibe, Usishuhudie uongo,

19 Waheshimu baba yako na mama yako, na, Mpende jirani yako kama nafsi yako.

20 Yule kijana akamwambia, Haya yote nimeyashika; nimepungukiwa na nini tena?

21 Yesu akamwambia, Ukitaka kuwa mkamilifu, enenda ukauze ulivyo navyo, uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni; kisha njoo unifuate.

22 Yule kijana alipolisikia neno lile, akaenda zake kwa huzuni; kwa sababu alikuwa na mali nyingi”.

Tunamwona kijana huyu alijaribu kumfuata Yesu lakini kuna vikwazo vilikuwa mbele yake vinamkwamisha, ni mtu wa kipekee ambaye Bwana Yesu alimpenda hata kufikia hatua ya kumpa nafasi ya kipekee ya kufanyika moja wanafunzi wake, pengine angefanikiwa mtihani ule angekuwa mwanafunzi wa 13, na pengine leo hii tungekuwa tunasoma nyaraka zake, au angekuwa miongoni mwa watakao keti pamoja na Kristo katika ufalme wake kuwahukumu kabila 12 za Israeli, Lakini kikwazo kimoja tu nacho ni cha MALI kilimfanya akunje uso wake na kuondoka kwa huzuni, na kuipoteza nafasi ile ya kipekee. Pengine alisema moyoni mwake, ;kwa taabu nilizojitesa kupata utajiri wote huu, halafu leo hii mtu huyu mmoja anataka kunigeuza kuwa maskini ndani ya siku moja, hilo haliwezekani?. Kwakweli jambo hilo lisingeweza kumuingia akilini kama lisivyoweza kuwaingia akilini watu wengi leo.

Kumbuka pia kijana huyu sio kana kwamba alikuwa ni mtenda dhambi la! Alikuwa anaenenda katika haki tangu utoto wake, lakini kuna kitu aliona bado kimepunguka ndani ya moyo wake, kwamba hana uzima wa milele. Na alipomwendea Yesu na kumuuliza! Akaambiwa maneno yale. Lakini hakufahamu kwamba Yesu kumwambia vile sio kana kwamba anataka kumwekea kitanzi cha kuwa maskini la! Bali ni kumtengeneza awe kama wanafunzi wake wengine..na ndio maana kama ukiendelea kusoma mbele kidogo utaona aliwaambia wale wanafunzi wake wale walioacha kila kitu na kumfuata kuwa watapata mara mia na kuurithi uzima wa milele, soma;

Mathayo 19:27-29 “27 Ndipo Petro akajibu, akamwambia, Tazama, sisi tumeacha vyote tukakufuata; tutapata nini basi?

28 Yesu akawaambia, Amin, nawaambia ya kwamba ninyi mlionifuata mimi, katika ulimwengu mpya, atakapoketi Mwana wa Adamu katika kiti cha utukufu wake, ninyi nanyi mtaketi katika viti kumi na viwili, mkiwahukumu kabila kumi na mbili za Israeli.

29 Na kila mtu aliyeacha nyumba, au ndugu wa kiume au wa kike, au baba, au mama, au watoto, au mashamba, kwa ajili ya jina langu, atapokea mara mia, na kuurithi uzima wa milele”.

Hivyo kama kijana yule angekuwa mvumilivu tu, baada ya muda mchache haya maneno ya faraja yangekuwa sehemu yake, na huo uzima wa milele alioukuwa anautafuta angeupata pamoja na mali zake mara mia. Lakini kwa kuwa alipenda kuweka MALI kwanza basi alimkosa Mungu. Alishindwa kufahamu yale maneno yanayosema 

“Mathayo 16:25 Kwa kuwa mtu atakaye kuiokoa nafsi yake, ataipoteza; na mtu atakayepoteza nafsi yake kwa ajili yangu, ataiona.

26 Kwani atafaidiwa nini mtu akiupata ulimwengu wote, na kupata hasara ya nafsi yake? Au mtu atatoa nini badala ya nafsi yake?”.

Tunaona habari ya YULE KIJANA ikaishia pale pale, mali alibakiwa nazo lakini Kristo alimkosa.

KIJANA WA PILI:

Lakini tumwangalie kijana mwingine aliyechukua maamuzi sahihi katika maisha yake kwa kuamua kumfuata KRISTO kwa moyo wake wote, na huyu si mwingine zaidi ya kijana MUSA. Kijana huyu alizaliwa katika jumba la kifalme la Farao, hakujua shida, wala njaa ni nini!! Biblia inasema ni mtu aliyekuwa na Elimu kubwa ya kidunia kwasasa tunaweza tukasema ni msomi mwenye PH.D, Alikuwa ni mwenye ujuzi wa maneno, alikuwa ni tajiri sana katika ngome ya Farao ambayo kwa wakati huo ilikuwa inatawala dunia nzima, ni kijana ambaye angetaka chochote angepata, angetaka wanawake wazuri kuliko wote angepata, kama ni viwanja, na mashamba alikuwa navyo, na zaidi ya yote umaarufu alikuwa nao tayari.

Lakini ilifika wakati akakutana na KRISTO moyoni mwake, pengine maneno kama yale yale yalimjia moyoni mwake, “nina kila kitu lakini nimepungukiwa na nini, ili niupate uzima wa milele??”. Tunasoma kwenye biblia Musa akaacha vyote kwa ajili ya Kristo akakimbilia nyikani, kwenye taabu kwa ajili ya Mungu wake.

Waebrania 11: 24-27

“Kwa imani Musa alipokuwa mtu mzima, akakataa kuitwa mwana wa binti Farao;

25 akaona ni afadhali kupata mateso pamoja na watu wa Mungu kuliko kujifurahisha katika dhambi kwa kitambo;

26 AKIHESABU YA KUWA KUSHUTUMIWA KWAKE KRISTO NI UTAJIRI MKUU KULIKO HAZINA ZA MISRI; kwa kuwa aliyatazamia hayo malipo.

27 Kwa imani akatoka Misri, asiogope ghadhabu ya mfalme; maana alistahimili kama amwonaye yeye asiyeonekana.”

Hivyo Baada ya miaka 40 tunamwona Musa tena, akirudi Misri akiwa kama mungu kwa Farao, biblia inasema hivyo, zaidi ya yote japo aliacha ndugu zake, mashamba n.k. alikuja kuvipata vyote na zaidi, Wana wa Israeli wote walikuwa kama watoto wa Musa, na zaidi ya yote hakukuwahi nyanyuka nabii kama Musa aliyezungumza na Mungu uso kwa uso, mpaka leo hii tunaisoma habari yake, Mungu alimpa kumbukumbuku lisilofutika milele, tunamwona miaka mingi baada ya kufa,akitokea na kuongea na Bwana YESU kule mlimani.(Mathayo 17). Kwasababu alihesabu kushutumiwa kwake Kristo ni UTAJIRI MKUU kuliko hazina zote za Misri.

Vivyo hivyo na sisi je! Tumehesabu hivyo??. Je! Umehesabu kushutumiwa kwa kuacha dhambi, anasa, ulevi, uasherati, biashara haramu, rushwa, fashion, ufisadi, ibada za sanamu n.k. kwa ajili ya Kristo kuwa ni utajiri mkuu kuliko mambo yote ya ulimwengu?.

Wewe ni kijana sasa ni wakati wa kuchukua uamuzi sahihi kwa kumfuata BWANA YESU KRISTO kwa gharama zozote utakazoambiwa ukijua ya kwamba Mungu hafanyi hivyo kwa kukutesa bali kukupa tumaini zuri katika siku zako za mwisho. Kama ni utafutaji mali ndio unaokusonga jaribu kuweka kwanza kando uutafute ufalme wake na haki yake. Kama ni cheo au ukubwa vinakusonga, viweke kwanza kando, umtafute Mungu, na hayo mengine yatafuata huko baadaye.

Hivyo chukua uamuzi kama wa kijana Musa, na sio Yule kijana mwingine. Wakati ndio huu biblia inasema

Mhubiri 12: 1 Mkumbuke Muumba wako SIKU ZA UJANA WAKO, Kabla hazijaja siku zilizo mbaya, Wala haijakaribia miaka utakaposema, Mimi sina furaha katika hiyo.”

Na Pia inasema.

 Maombolezo 3:26 “Ni vema mtu autarajie wokovu wa Bwana Na kumngojea kwa utulivu. Ni vema mwanadamu aichukue nira WAKATI WA UJANA WAKE.”

Ni maombi yangu kuwa ujana wako utaishia katika njia njema ya uzima.

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
6 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Sephania
Sephania
1 year ago

AMINA MBALIKIWE

M
M
2 years ago

Amina

Martin
Martin
4 years ago

Kwakuchukia maendeleo ya watu wengine

Martin
Martin
4 years ago

Naomba mnisaidie namba mnayo tumia whtssap