MPENDEZE MUNGU ZAIDI.

MPENDEZE MUNGU ZAIDI.


Biblia inasema katikaWaefeso 5:9 “kwa kuwa tunda la nuru ni katika wema wote na haki na kweli; 10 MKIHAKIKI NI NINI IMPENDEZAYO BWANA”. Mstari wa 10 unatuambia, mkihakiki ni nini impendezayo Bwana…Kwahiyo ni wajibu wetu, kuchunguza na kuhakiki ni mambo gani yanayompendeza Bwana zaidi.. Na leo tutajifunza moja ya jambo linalompendeza Bwana zaidi.

Katika habari ifuatayo tunaweza kujifunza jambo hilo kwa undani…tusome:

Luka 8:22 “Ikawa siku zile mojawapo alipanda chomboni yeye na wanafunzi wake, akawaambia, Na tuvuke mpaka ng’ambo ya ziwa. Wakatweka matanga.

23 Nao walipokuwa wakienda, alilala usingizi. Ikashuka tufani juu ya ziwa, chombo kikaanza kujaa maji, wakawa katika hatari.

24 Wakamwendea, wakamwamsha, wakisema, Bwana mkubwa, Bwana mkubwa, tunaangamia. Akaamka, akaukemea upepo na msukosuko wa maji, vikakoma; kukawa shwari.

25 Akawaambia, Imani yenu iko wapi? Wakaogopa, wakamaka, wakisema wao kwa wao, Ni nani huyu basi hata anaamuru upepo na maji, navyo vyamtii?”

Hapa tunaona, Bwana Yesu alikuwa anavuka kwenda ng’ambo ya pili, akiwa na wanafunzi wake, lakini njiani, alilala na hali ikabadilika..shetani akawatikisa kidogo..

Katika haya Maisha pia, tupo safarini, na safari ni safari tu inaweza kuwa ya nchi kavu, majini au angani…ilimradi inakutoa sehemu moja hadi nyingine, na katikati ya safari ni kawaida kukutana na vikwazo mbali mbali na changamoto mbali mbali…Na Maisha tunayoishi ndio hivyo, Safari ya mtu aliyemkabidhi Kristo Maisha yake, ni tofauti na ya mtu ambaye hajampa Kristo maisha yake. Safari ya aliyeokoka anakuwa anasafiri na Bwana Yesu, na atatafutwa na Adui kila kona, lakini yule ambaye hajampa Kristo Maisha yake anakuwa anasafiri peke yake na roho za mashetani.

Lakini katika safari hii, tunaona Bwana Yesu pamoja na wanafunzi wake walikuwa wanasafiri kihuduma, kwenda kuvua roho za watu upande wa pili..jambo ambalo shetani haliwezi kumpendeza hata kidogo…kwani muda mfupi tu baadaye, mtu mwenye mapepo mengi kama jeshi atakwenda kufunguliwa na kwa kupitia kufunguliwa kwake maelfu ya watu watatubu na kumgeukia Mungu, hivyo jambo hilo lisingemfurahisha shetani hata kidogo, kwahiyo suluhisho la haraka ni kuwaletea kikwazo safarini, ni kikwazo pekee baharini ni kuleta tufani.

Lakini tunaona wanafunzi walipoona ile tufani jinsi ilivyo kubwa, waliogopa mpaka kufikia hatua ya kukata tamaa, mpaka chombo kikaanza kujaa maji..na Bwana Yesu akiwa ndani humo humo…Walipoona hali imezidi kuwa mbaya ndipo wakaenda kumwamsha Bwana kuomba msaada na Bwana akawasaidia, kwa kuukemea ule upepo, na muda ule ule ukatulia.

Lakini tunajifunza Bwana hakufurahishwa sana na kile kitendo cha wao kukosa Imani, kwa ufupi wangepaswa tu kuamini kuwa wasingezama kwa namna yoyote ile na hivyo dhoruma itaisha kwa namna yoyote ile…lakini mpaka kufikia hatua ya kusema tunaangamia! Hiyo ni hatua ya mwisho ya kukata tamaa na kuliruhusu lile jambo litokee…kulikuwa hakuna haja ya kumwamsha Bwana walipaswa tu waamini kuwa hata iweje hawawezi kufa, kwani BWANA MKUBWA yupo nao ndani hata kama wasingeukemea ule upepo kitendo cha wao kuamini tu kuwa hawawezi kufa hiyo ilikuwa ni Imani tosha! Ya kuikatisha ile dhoruba!

Na sisi katika safari yetu kuna wakati Kristo analala, sio kwamba hayupo na sisi au katuacha hapana! Bali anakuwa amelala…shetani anapoleta misuko suko ya huku na kule, sio wakati wakuogopa na kupaniki ni wakati wa kuamini kuwa mambo yote yatakuwa shwari kwakuwa tunaye YESU moyoni mwetu…hata kama hanijibu kwa sasa, lakini chombo changu hakiwezi kuzama…Chombo cha wakina Petro kingewezaje kuzama na Kristo akiwa ndani?…unaweza kutengeneza picha Bwana Yesu anakufa maji?…au anajiokoa yeye peke yake na kuacha wanafunzi wake wafe maji?..unaona jambo hilo haliwezekani…Ni kitendo cha kuamini tu kuwa maadamu Yesu yupo ndani, awe macho au amelalala mambo yote sawasawa….tunaye Yesu moyoni mwetu hivyo ni shwari kuu…hata kama nje tunaona dhoruba, ni inapita tu!…

Lakini kwasababu Bwana Yesu ni msaada kwetu kwa hali zote, hata katika udhaifu wetu anatusaidia mwisho wa siku, ndio maana unaona japokuwa wanafunzi walikuwa wamepoteza tumaini la Maisha lakini Yesu aliwasaidia pia, akaukemea upepo kwa niaba yao lakini sio kwamba alipendezwa nao sana kwa kitendo hicho.…Kadhalika watu wengi leo Kristo anawasaidia kwa njia hiyo hiyo, inatokea mtu anapitia tatizo kidogo tu! Utaanza kuona anavyolalamika? Nakufa! Nakufa Mungu wangu! Nimekwisha mimi… Mungu hunisikii?..Ni kweli kwa kelele hizo utapata msaada! Lakini utakuwa hujampendeza Mungu…utakufaje na yeye yupo na wewe chomboni? Mapenzi ya Mungu ni haya kwamba ukiwa naye hakuna lolote litakalokutokea kwa madhara maadamu unaye Mungu..Maadamu unauhakika upo naye sawa…

Na maana ya kuwa na Kristo chomboni ni “kuwa na Kristo moyoni mwako kwa kuzishika amri zake na kuishi Maisha ya utakatifu”..hapo tufani inapokuja hauhitaji kumwamsha itaisha yenyewe…na utakuwa umempendeza Zaidi. Hutakuwa tatizo kidogo tu likitokea unapaniki, au unakata tamaa, au unatoa hitimisho kuwa utakufa!..Bwana atakuuliza Imani yako iko wapi?.

Bwana Yupo na wewe, wewe uliyeamua kumfuata hivyo usiogope mabaya yatakapokuja!..Bwana yupo na wewe, wewe uliyeamua kuyakabidhi Maisha yako kwake, hawezi kukuacha uangamie, ingawa dhoruba zitakuja hata ukiwa naye…lakini usiogope! Hakuna lolote litakalokutokea..Unapokwenda kuhubiri kama Bwana alivyokwenda na wanafunzi wake dhoruba inapokuja usiogope Bwana yu pamoja nawe, usianze kufikia hitimisho kwamba umekufa! Au umekwisha! Usianze kabisa kufikiria hayo mambo, ukianza kufikiria hivyo shetani atakupepeta kweli kweli…yeye mwenyewe alisema kuwa atakuwa pamoja nasi mpaka Ukamilifu wa Dahari. Sasa hawezi kutudanganya, maneno yake siku zote ni ya ukweli.

Wana wa Israeli Bwana alipowatoa Misri na kuwapeleka kwenye lile jangwa, lisilo na maji wala chakula, walipopitia njaa kidogo tu! Siku mbili tatu wakaanza kunung’unika..kwamba wapo katikati ya jangwa watatolea wapi chakula na maji?..Sasa unaweza kuwaza Mungu atakutoaje mahali penye chakula na akupeleka jangwani halafu asijue namna ya kukulisha kule jangwani?..kwahiyo walipoona kumekuwa kimya kidogo Mungu hazungumzi, wakaanza kupiga kelele tunaangamia! Tunaangamia! Ni kweli kwa kelele zile walipata nyama muda mfupi sana baadaye, pamoja na mana, wakala wakashiba lakini Mungu hakupendezwa nao…Walipaswa kujua tu! Maadamu wanaye Mungu, mambo yote yatakuwa sawasawa, Mungu hawezi kuwaacha wafe na njaa au wafe kwa kukosa maji!..Ni kitendo cha kutulia tu, muda mchache mbele wangekwenda kula mana na nyama za kutosha, na wangesahau kuwa walipitia njaa.

Bwana atusaidie, tuzidi kumpendeza yeye Zaidi na zaidi..na tuzidi kuyahikiki mambo gani yanayompendeza siku zote.

Ubarikiwe sana.

Pia kwa Maombezi/Ushauri/Maswali/Ratiba za Ibada Wasiliana nasi kwa namba 

+225693036618/ +225789001312

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


 

Mada Zinazoendana:

JIPE MOYO.

BWANA YESU ALIKUWA ANAONYESHA KUWA MUNGU NI MUNGU MWENYE AKILI TIMAMU.

UPONYAJI WA YESU.


Rudi Nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments