Bwana alimaanisha nini kusema “Mwanafunzi hawi mkuu kuliko mwalimu wake”?

Bwana alimaanisha nini kusema “Mwanafunzi hawi mkuu kuliko mwalimu wake”?

SWALI: Bwana Yesu alimaanisha nini kusema “Mwanafunzi hawi mkuu kuliko mwalimu wake”?


JIBU: Ukisoma kuanzia mstari wa juu yake kidogo anasema;

Luka 6:39 “Akawaambia mithali, Je! Aliye kipofu aweza kuongoza kipofu? Hawatatumbukia shimoni wote wawili?

40 Mwanafunzi hawi mkuu kuliko mwalimu wake, lakini kila mtu ambaye amehitimu hulingana na mwalimu wake”.

Akiwa na maana kuwa, Yule anayeongozwa hawezi kumzidi maarifa kiongozi wake, kama akiwa ni kipofu hata Yule anayeongozwa atakuwa ni kipofu pia, na mwisho wao wote utakuwa ni shimoni tu,  Kama alikuwa na maarifa fulani kidogo, hata Yule anayeongozwa atakuwa na maarifa hayo hayo madogo, kama alikuwa na mengi, vivyo hivyo na mwanafunzi wake atakuwa nayo. Lakini hawezi kumzidi kimo.

Halikadhalika katika kanisa la Kristo, ikiwa Kiongozi anayelichunga kanisa, atakuwa anafundisha mafundisho potofu, hakuna namna washirika wake wataacha kuyaishi na kufundisha mafundisho hayo hayo kwa wengine, haiwezekani wakafundishe mafundisho ya haki. Kwasababu Mwanafunzi hampiti mwalimu wake,

Hiyo ni kututahadharisha, tuwe makini na viongozi tunaowachagua watuongoze.  Ikiwa viongozi wetu hawatuhimizi kuishi katika utakatifu, na  maisha ya haki, na ya ufalme wa mbinguni. Tujue kuwa tutafanana na wao, tutakuwa mfano wa watu wa ulimwengu huu, na mwisho wetu utakuwa ni jehanamu tu pamoja na wao.

Lakini Bwana Yesu aliendelea kusema.. “lakini kila mtu ambaye amehitimu hulingana na mwalimu wake”. Ikiwa na maana mwanafunzi mzuri anayezingatia, huwa anafikia kiwango cha kulingana na mwalimu wake, Na hapo ndipo Bwana alipokuwa anapataka, lakini si zaidi yake.

Swali la kujiuliza Je! Ni kiongozi yupi uliyemchagua akuongoze?

Bwana Yesu mahali pengine alisema maneno hayo hayo kwa namna nyingine.. Alisema,

Mathayo 10:24 “Mwanafunzi hampiti mwalimu wake, wala mtumwa hampiti bwana wake.

25 Yamtosha mwanafunzi kuwa kama mwalimu wake, na mtumwa kuwa kama bwana wake. Ikiwa wamemwita mwenye nyumba Beelzebuli, je! Si zaidi wale walio wa nyumbani mwake”?

Ikiwa kama sote ni wanafunzi wa Bwana Yesu, tufahamu pia, Kristo alichukiwa na kudhihakiwa, na kutukanwa na kuitwa Beelzebuli, lakini ikiwa sisi wakati wote ni wakupendwa na dunia na kusifiwa, ni lazima tujiulize, kwanini hatujawa kama mwalimu wetu.

Sehemu nyingine, mwalimu wetu Yesu Kristo, aliwatawadha wanafunzi wake miguu, kama ishara ya unyenyekevu, japokuwa yeye alikuwa ni mkuu kuliko wao, akasema.

Yohana 13:14 “Basi ikiwa mimi, niliye Bwana na Mwalimu, nimewatawadha miguu, imewapasa vivyo kutawadhana miguu ninyi kwa ninyi.

15 Kwa kuwa nimewapa kielelezo; ili kama mimi nilivyowatendea, nanyi mtende vivyo.

16 Amin, amin, nawaambia ninyi, Mtumwa si mkuu kuliko bwana wake; wala mtume si mkuu kuliko yeye aliyempeleka.

17 Mkiyajua hayo, heri ninyi mkiyatenda”

Kwahiyo, tukiishi kama Kristo alivyoishi duniani, tutapita njia ile ile aliyoipitia yeye. pale alipostahili kupendwa na sisi tutapendwa, pale alipostahili kuchukiwa na sisi tutachukiwa, Pale aliponyenyekea na sisi tutanyenyekea.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

NINI MAANA YA KUWA MKRISTO?

Je ni sahihi kumwita mtu “Mkuu”?

Tofauti kati ya mtume na mwanafunzi ni ipi kibiblia?

Tofauti kati ya mtume na mwanafunzi ni ipi kibiblia?

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments