Je ni kweli kila nafsi itaonja mauti kulingana na (Zaburi 89:48)?

Je ni kweli kila nafsi itaonja mauti kulingana na (Zaburi 89:48)?

Tusome,

Zaburi 89:48 “Ni mwanamume gani atakayeishi asione mauti, Atakayejiokoa nafsi yake na mkono wa kuzimu?”

Awali ya yote ni vizuri kufahamu kuwa Mwandishi aliyeandika maneno haya, alikuwa katika mazingira gani, Mwandishi alikuwa katika mazingira ya Sala (yaani kuomba) na si kuhubiri au kutoa mahusia kama Zaburi nyingine. Kuna maneno ya kuzungumza na Mungu na ya kuzungumza na Watu.

Tunapozungumza na Mungu katika sala, ni kawaida yetu kujishusha..huwezi kujiinua mbele za Mungu kwamba wewe unafaa, hata kama kweli unafaa, huwezi kusema wewe unastahili hata kama kweli unastahili, ni lazima uwe si kitu mbele za Mungu. (Soma Luka 18:11-14).

Vile vile Mwandishi alikuwa anamjua HENOKO mtu wa Saba, baada ya Adamu, ambaye hakuonja mauti, bali alitwaliwa na Mungu bila kufa!.

Hivyo kama angekuwa amemaanisha kuwa kila mtu ni lazima afe, basi atakuwa amesema uongo, maana anamjua Henoko kwamba hakufa. (Na biblia sio kitabu cha uongo!)

Kwahiyo maana yake ni kwamba, Mwandishi hakumaanisha kama watu leo wanavyoutafsiri huo mstari, kwamba kila mtu ni lazima afe, bali alisema vile akiwa na maana nyingine kabisa.

Zaburi hiyo ya 89, yote ni Zaburi ya sala ya unyenyekevu, ambapo mwandishi anasali huku akimwinua Mungu, na kujishusha yeye.. na si Zaburi ya mahubiri wala maonyo!, ndio maana ukianzia mstari wa juu kidogo utaona anasema..

“46 Ee Bwana, hata lini? Utajificha hata milele? Ghadhabu yako itawaka kama moto?

47 Ukumbuke jinsi mimi nisivyo wa kudumu; Kwa ubatili gani umeiumba jamii ya wanadamu!

48 Ni mwanamume gani atakayeishi asione mauti, Atakayejiokoa nafsi yake na mkono wa kuzimu?”

Sasa ili tuelewe vizuri, hebu chukua mfano umsikie mtu aliye mgonjwa sana anaomba hivi.. “Ebwani nisaidie mimi niliye mdhaifu, niliye karibia na kufa, ni mwanadamu gani leo hii anaweza kuishi bila kufa?”

Bila shaka kwa kuomba huko, atakuwa hajamaanisha kuwa hakuna mtu anaweza kuishi bila kufa!, bali amemaanisha kuwa yeye ni mdhaifu, na wanadamu wote ni wadhaifu na hakuna mtu anaweza kuishi bila kufa kwa nguvu zake na uwezo wake mwenyewe”.

Ndicho mwandishi alichokuwa anakimaanisha hapo?..

Alikuwa katika sala, kuzungumza na Mungu na hivyo kujionyesha kuwa yeye ni mavumbi tu, na wanadamu wote tu mavumbi tu, na ni dhaifu, ndio ikamfanya aombe sala ya namna hiyo ya unyenyekevu, lakini Hakuwa anatoa mahubiri au mafundisho, au mashauri kwa watu kuwa kila mtu ni lazima afe, bali alikuwa katika sala!, anamweleza Mungu na si mwanadamu!..kuonesha ishara ya kujishusha na unyenyekevu mbele za Mungu.

Kwahiyo kwa hitimisho Si kila mtu atakufa!, Henoko hakufa, Nabii Eliya hakufa, kadhalika kuna watu watanyakuliwa wakiwa hai wakati Bwana Yesu atakapokuja mara ya pili (kwenye tukio maarufu lijulikanalo kama unyakuo).

1Wakorintho 15:51 “Angalieni, nawaambia ninyi siri; HATUTALALA SOTE, lakini sote tutabadilika,

52 kwa dakika moja, kufumba na kufumbua, wakati wa parapanda ya mwisho; maana parapanda italia, na wafu watafufuliwa, wasiwe na uharibifu, nasi tutabadilika”.

Hapo anasema “hatutalala sote” maana yake “hatutakufa wote”..Unyakuo utawakuta wengine wakiwa hai, hivyo watakuwa hawajakionja kifo, na vile vile katika maandiko hakuna mahali popote panaposema kuwa kila nafsi itaonja mauti, msemo huo ni maarufu sana lakini kiuhalisia haupo katika biblia.

Lakini kufa si hoja, au kutokufa.. Hoja ni je! Tutakuwa wapi baada ya kifo, au siku ile ya unyakuo itatukutaje?, kama tukifa katika dhambi basi tutangamia milele katika lile ziwa la moto, lakini kama tukifa katika Kristo tutadumu milele Pamoja na Bwana. Vile vile kama tukiwa hai ndani ya Kristo mpaka unyakuo utakapofika basi tutanyakuliwa na kwenda naye mawinguni, lakini kama unyakuo ukitukuta huku tuko nje ya Kristo, basi tutabaki hapa katika dhiki kuu ya Mpinga Kristo.

Na Unyakuo wa kanisa ni siku yoyote! Na wakati wowote!.. Je umejiandaaje?, umempokea Kristo na kubatizwa na kumpokea Roho Mtakatifu ndani yako?

Bwana yu karibu!

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

Kwa kuwa ni shida mtu kufa kwa ajili ya mtu mwenye haki;

SALA YA ASUBUHI

Mtu wa kwanza kufa alikuwa nani?

SALA YA UPONYAJI/MAOMBI YA UPONYAJI.

Biblia inamaana gani inaposema “Wewe uchukiaye sanamu, wateka mahekalu?”

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments