Fahamu maana ya Mithali 29:4 “Mfalme huithibitisha nchi kwa hukumu; Bali yeye apokeaye rushwa huipindua.

Fahamu maana ya Mithali 29:4 “Mfalme huithibitisha nchi kwa hukumu; Bali yeye apokeaye rushwa huipindua.

Mafundisho maalumu kwa watumishi wa Mungu (Wachungaji, Mitume, manabii, wainjilisti n.k.)

Mithali 29:4 “Mfalme huithibitisha nchi kwa hukumu; Bali yeye apokeaye rushwa huipindua”

Uongozi wa kidunia mara nyingi hutoa picha ya uongozi wa rohoni.

Kama andiko hilo linavyosema, “Mfalme huithibitisha nchi kwa hukumu; Bali yeye apokeaye rushwa huipindua” maana yake ni kuwa kiongozi anayetawala nchi na huku moyo wake ni wa rushwa, kamwe hilo taifa halitakaa liendelee vile ipasavyo.

Kwamfano, mtu anataka kupitisha bidhaa zisizo na ubora bandarini ili ziuzwe ndani ya nchi. Lakini taarifa zinamfikia kiongozi, badala Yule kiongozi azipige marufuku, anapokea pesa kutoka kwa wale wanaotaka kuingiza, hivyo athari inakwenda kwenye jamii kwa tamaa zake za mali.

Au anaingia mikataba ambayo haina manufaa kwa watu wake, kisa tu kaahidiwa atalipwa pesa nyingi kutoka kwao. Hivyo rushwa zipo nyingi sio tu za kipesa, lakini pia za kiuongozi, kisa Yule ni rafiki, au ndugu, anampa nafasi ya utawala, lakini Yule mwenye ujuzi na ueledi ananyimwa. Sasa taifa lake kiongozi huyu, haliwezi kusimama kwa namna yoyote.

Lakini akiwa ni wa haki (Mtoa hukumu za haki), ni lazima tu nchi hiyo itastawi, Kwasababu maandiko yanasema haki huinua taifa.

Mithali 14:34 ‘Haki huinua taifa; Bali dhambi ni aibu ya watu wo wote’.

Uongozi wa Rohoni.

Vivyo hivyo pia na viongozi wanaongoza kanisa la Kristo ambao kuna watu chini yao wanaowaangalia, katika ngazi yoyote iwe ni Maaskofu, Wachungaji, waalimu, wainjilisti, mitume na manabii. Wakiwa na mioyo ya rushwa ndani yao, kamwe kundi hilo halitathibitika.

Kwamfano, mchungaji anapendelea watu Fulani, anawapa nafasi ya uongozi au anawapa viti vya mbele, kisa tu wanachangia huduma kwa sehemu kubwa, hata kama haiwakidhi wanapewa kisa tu wana fedha nyingi, wanaachwa wale wenye uwezo wa Roho nyuma. Sasa Hiyo rohoni ni rushwa na ni mbaya sana kwa maendeleo ya kanisa.

Yakobo 2:1  Ndugu zangu, imani ya Bwana wetu Yesu Kristo, Bwana wa utukufu, msiwe nayo kwa kupendelea watu.2  Maana akiingia katika sinagogi lenu mtu mwenye pete ya dhahabu na mavazi mazuri; kisha akiingia na maskini, mwenye mavazi mabovu; 3  nanyi mkimstahi yule aliyevaa mavazi mazuri, na kumwambia, Keti wewe hapa mahali pazuri; na kumwambia yule maskini, Simama wewe pale, au keti miguuni pangu, 4  je! Hamkufanya hitilafu mioyoni mwenu, mkawa waamuzi wenye mawazo mabovu?

Mwingine atauza mafuta, au maji, au chumvi, kisha atasema ni lazima uvinunue ili upokee Baraka zako. Mwingine atasema ili unione mimi nikufanyie maombezi, toa kiwango Fulani, au nikutane na wewe kimwili. Hizo zote ni rushwa za kiroho na zinakuja kwa maumbile mengi sana.

Kunaweza kubuniwa michango ya aina mbalimbali katika kanisa, afadhali lengo lingekuwa ni kwa ajili ya maendeleo ya kazi ya Mungu, lakini unakuta lengo ni ili kiongozi apate fedha ajinufaishe maisha yake.

Mwingine anawachagua viongozi wa kanisani, kindugu, kisa Yule ni mjomba wake, au shemeji yake na kuacha wale walioteuliwa na Mungu.

Yote haya yakiwa ndani ya kiongozi yoyote, ambaye anasimama sio kwa ajili ya kundi bali kwa ajili ya nafsi yake. Kamwe mkusanyiko huo hauwezi kuendelea kiroho. Utazidi kudhoofika, kwasababu umekosa uongozi bora.

Ni vema kujihakiki wewe ambaye umeitwa kulichunga kundi, Maono yako ni nini kwa watu wa Mungu? Je! Ni Uwe tajiri na maarufu kupitia wao? Au ulijenge kanisa la Bwana? Kumbuka utatoa hesabu kwa utumishi wako siku ile ya mwisho, Na kama ukionekana uliwatesa na kuwanyanyasa utakatwa vipande viwili, kisha kutupwa katika ziwa la moto (Mathayo 24:48-51). Na adhabu yako inakuwa kubwa kushinda ya wengine kwasababu ulijua mapenzi ya Bwana wako lakini kwa makusudi hukuyafanya, Hivyo utaadhibiwa sana. Ogopa hukumu ya Mungu. Acha kuiga-iga mifumo ya makristo wa uongo. Tembea katika Neno, kielelezo chako akiwa Kristo ambaye hakuwa na upendeleo wala tamaa ya vitu.

Siku hizi ni siku za mwisho, tubu dhambi zako mgeukie Bwana kwa kumaanisha badili namna ya uongozi wako, simamia haki ya Mungu, uthibitike katika utumishi huo.

Bwana akubariki.

Shalom.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

Vifungu vya biblia kuhusu Uongozi.

Nini maana ya Mhubiri 10:16, inaposema Ole wako, nchi, akiwa mfalme wako ni kijana?

Rushwa inapofushaje macho?

Fanya bidii kuijua hali ya makundi yako (Mithali 27:23)

ROHO YA MPINGA KRISTO IKITENDA KAZI SIKU HIZI ZA MWISHO

Bwana alimaanisha nini kusema “Mwanafunzi hawi mkuu kuliko mwalimu wake”?

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments