MAMBO NANE (8), AMBAYO WEWE KAMA KIONGOZI UTAIGWA.

MAMBO NANE (8), AMBAYO WEWE KAMA KIONGOZI UTAIGWA.

Uwapo katika nafasi yoyote ya uongozi, katika kanisa au kwenye huduma, labda mchungaji, mwalimu, mtume, nabii, shemasi, askofu, mzee wa kanisa. Na una watu walio chini yako, fahamu mambo ambayo utaigwa, Na hivyo kuwa makini sana katika maeneo hayo uyajenge.

Mtume Paulo aliyaona kwa mwanawe Timotheo, akayaandika;

2 Timotheo 3:10-11

[10]BALI WEWE UMEYAFUATA mafundisho yangu, na mwenendo wangu, na makusudi yangu, na imani, na uvumilivu, 

[11]na upendo, na saburi; tena na adha zangu na mateso, mambo yaliyonipata katika Antiokia, katika Ikonio, na katika Listra, kila namna ya adha niliyoistahimili, naye Bwana aliniokoa katika hayo yote. 

Paulo ametaja mambo saba ambayo Timotheo aliyaona kwake akayaiga, ni kama yafuatayo;.

la kwanza ni 

1) Mafundisho yake:

Wewe kama kiongozi kumbuka unachofundisha ndicho watakachofundisha wafuasi wako, ikiwa injili yako ni ya mafanikio, hicho hicho watakifuata na kukifundisha, ikiwa ni mafundisho ya wokovu watakifundisha hicho hicho, ikiwa ni shuhuda za wachawi nao pia watakuwa nazo hizo hizo kama kiini cha injili yao. Hivyo kuwa makini na fundisho lako vinginevyo utajikuta  unapotosha jamii yako ya waaminio, na utatoa hesabu juu ya hilo, mbele za Bwana siku ile.

2) Mwenendo wake:

Ukiwa ni mtu wa kidunia, usitazamie utazaa watu wa rohoni, uvaaji wako, unawafundisha wafuasi wako, kauli zako zitazungumzwa hizo hizo na washirika wako, ukiwa na tabia ya maombi, wanaokufuata nao pia wataiga mwenendo huo wa maombi, ukiwa ni mtakatifu nao pia watakuwa hivyo hivyo. Jichunge mwenendo wako, wewe ni kioo unaigwa mpaka hatua zako. Hivyo usifanye mambo kiwepesi wepesi, ukidhani wote wamekomaa wanaweza kujiamulia tu mienendo bila kukuangalia wewe. Liondoe hilo kichwani.

3) Makusudio yake:

Makusudi ya mtume Paulo, yalikuwa ni kuhubiri injili kwa mataifa kotekote wamjue Mungu (2Wakorintho 1:15-20). Hakuwa na kusudio la umaarufu, fedha, kuheshimiwa na wanadamu, hapana, bali kuhubiri injili tu peke yake, bila kujali dhiki, au kupungukiwa, ilimradi watu waokoke. Hivyo Timotheo naye alipoliona kusudi hilo akaiga, naye pia akawa mhubiri tu wa injili, asiyetafuta vya kwake ndani ya kazi ya Mungu. Halidhalika na wewe pia, nia yako hutakumbulikana mahali ulipo, Je! Unachokifanya ni injili ya Mungu kweli au una lengo lingine. Ikiwa ni Yesu wa mikate, basi ujue watu wako pia watakuwa hapo kumtafuta Mungu huyo huyo wa kwako. Kuwa na kusudi la Kristo ambalo aliliweka pia ndani ya mitume wake, yaani kulitumikia na kulichunga kundi, kama mtendakazi asiyekuwa na faida. Ukijua kuwa thawabu yako ipo mbinguni, usiwe na makusudio mengine, kwasababu wewe ni kioo.

4) Imani yake:

Imani, katika mambo yote, wewe kama kiongozi ukiwa ni mtu wa mashaka juu ya mambo ya rohoni.  Ikiwa huamini uponyaji wa ki-ungu, na wale pia watakuwa hivyo hivyo, huamini miujiza, na karama za Roho, vivyo hivyo na washirika wako watakuiga, ikiwa huamini katika mifungo, ikiwa huamini kuwa duniani kuna watakatifu, au mtu hawezi kuwa mtakatifu, vivyo hivyo watu wako nao watakuwa hivyo, Ikiwa unaamini katika ibada za sanamu, watakuwa kama wewe.  Jenga imani yako kwenye neno la Mungu tu, kuwa mtu wa imani usiwe Sadukayo. Fahamu kuwa mtumishi wa Mungu tafsiri yake ni kuwa mtu wa Imani.

5) Uvumilivu wake:

Kama kiongozi ni ukweli usiopingika utapitia vipindi mbalimbali vya kushinda na kushindwa, vipindi vya kukatishwa tamaa, kusemwa vibaya,  vipindi vya kuachwa peke yako n.k. Mtume Paulo alipitia vipindi vyote, na wanafunzi wake wakawa wanamwangalia, wakaiga mwenendo ule walipoona mafanikio yake yalipotanguliwa na vipindi vingi vya kuvunjwa moyo lakini akastahimili. Hivyo na wewe pia kama kiongozi wa wengine, simama imara, uvumilivu wako ni funzo kubwa kwa wengine. Wakati mwingine Mungu anaruhusu uyapitie hayo ili kuwaimarisha wengine katika dhiki zao, wakuonapo wewe unasimama katika changamoto, na wao pia hupokea nguvu ya kushindana na changamoto zao.

6) Upendo wake:

Kama kiongozi, upendo ni sehemu, kubwa sana, ambalo mtume Paulo alifanya bidii kulionyesha kwa wanafunzi wake na kanisa.  Unapolipenda kundi lako, vivyo hivyo na wale wataiga tabia hiyo na kuidhihirisha kwa wengine. Unapoonyesha chuki, nao pia watakuwa watu wa chuki, unapowajali nao pia watawajali wengine. Unapowasikiliza, tafsiri yake ni kuwa unawafundisha kuwasikiliza na wengine. Hivyo ni kuangalia sana na kuongeza bidii katika eneo hilo, uwe kielelezo.

7) Saburi yake:

Saburi ni kitendo cha kungojea ahadi za Mungu hata katika mambo magumu yanayokinzana na wewe, bado unasubiria tu. Kama kiongozi watu watatazamia jinsi unavyoyashikilia maono yako, bila kuyumbishwa, waige, na wenyewe kushikilia ya kwao. Kamwe usiwe mtu wa kusita-sita, utawavunja moyo wengi, na hatimaye watashindwa kusimama aidha pamoja na wewe, au wao wenyewe. Ijenge saburi yako, wala usiidharau, ni nguvu kwa mwingine aliye chini yako. Leo unaona jinsi gani saburi ya Ayubu ilivyo na fundisho kubwa kwetu. Vivyo hivyo na yako ujue ni darasa kwa wengine.

8) Adha na mateso yake:

Ukweli ni kwamba watu watatamani kusikia ushuhuda wa mapito yako au kuyaona mapito yako hususani yale magumu sana. Lakini waweza kudhani, haliwafahi sana kiroho, lakini wengine pia wakaiiga njia hiyo ya mateso kama yako, kwasababu wameona mwisho wake ulivyo mzuri. Hivyo usiogope kupitia mateso kwa ajili ya Bwana wala usione haya wakati mwingine kueleza shida ulizopitia kwa wengine, hilo nalo huigwa, Leo hii tunaposoma mapito ya mtume Paulo ni wazi kuwa yanatutia nguvu na sisi, kuwa tusonge mbele.

Hivyo, zingatia mambo hayo saba, kwa faida yako na wale walio chini yako. Kwasababu ndicho Paulo alichokiona kwa watoto wake.

Shalom.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

ROHO YA MPINGA KRISTO IKITENDA KAZI SIKU HIZI ZA MWISHO

Fahamu maana ya Mithali 29:4 “Mfalme huithibitisha nchi kwa hukumu; Bali yeye apokeaye rushwa huipindua.

IMANI “MAMA” NI IPI?

Bwana alimaanisha nini kusema “Mwanafunzi hawi mkuu kuliko mwalimu wake”?

Rudi Nyumbani

Print this post

About the author

Devis Julius administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments