VYA MUNGU MPENI MUNGU.

VYA MUNGU MPENI MUNGU.

Tunajua kuwa vya Kaisari tunavyopaswa tumpe ni “kodi” lakini je! Na Vya Mungu ambavyo tunapaswa tumpe ni vipi kulingana na Luka 20:25?

Tuanze kusoma mstari wa 21 ili tuelewe vizuri zaidi..

Luka 20:21 “Wakamwuliza, wakisema, Mwalimu, twajua ya kwamba wasema na kufundisha yaliyo ya haki, wala hujali cheo cha mtu, bali unafundisha njia ya Mungu kwa kweli

22  Je! Ni halali tumpe Kaisari kodi, au sivyo?

23  Lakini yeye alitambua hila yao, akawaambia,

24  Nionyesheni dinari. INA SURA NA ANWANI YA NANI? Wakamjibu, Ya Kaisari.

25  Akawaambia, Basi, vya Kaisari mpeni Kaisari, NA VYA MUNGU MPENI MUNGU.

26  Wala hawakuweza kumshitaki kwa maneno yake mbele ya watu; wakastaajabia majibu yake, wakanyamaa”.

Nataka tujifunze ni vigezo gani Bwana Yesu alitumia hapo kuhalalisha kuwa Kodi ni haki ya Kaisari, hiyo itatusaidia na sisi kujua vilivyo vya Mungu ni vipi?.. Na tunaona hakutumia kitu kingine chochote isipokuwa ile “Sura” inayoonekana kwenye ile sarafu pamoja na ‘Anwani” inayosomeka pale. Kwani Dinari ile ilikuwa na sura ya Kaisari na Anwani ya Kaisari, hivyo ni haki kuwa mali ya Kaisari.

Sasa kama vya Kaisari vilitambulika kwa sura iliyokuwa inaonekana juu ya Sarafu, ni wazi kuwa na vya Mungu vitatambulika kwa njia hiyo hiyo, Maana yake chochote chenye Sura ya Mungu hicho ni cha Mungu, na anapaswa apewe.. Sasa hebu tusome maandiko yafuatayo..

Mwanzo 1:27 “Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanamume na mwanamke aliwaumba”.

Umeona?..Kumbe! sisi tumeumbwa kwa Mfano wa Mungu, Nyuso zetu ni nyuso za Mungu, na kama tumeumbwa kwa mfano na Sura ya Mungu basi ni wazi kuwa sisi (yaani miili yetu na roho zetu) ni mali ya Mungu na si yetu! na hivyo ni LAZIMA TUMPE MUNGU VILIVYO VYAKE…Biblia inasema hivyo kuwa sisi si mali yetu wenyewe..

1Wakorintho 6:19  Au hamjui ya kuwa mwili wenu ni hekalu la Roho Mtakatifu aliye ndani yenu, mliyepewa na Mungu? WALA NINYI SI MALI YENU WENYEWE

Na tena inasema Miili yetu ni MALI INAPASWA ITOLEWE KWA BWANA..

1Wakorintho 6:13  “Vyakula ni kwa tumbo, na tumbo ni kwa vyakula; lakini Mungu atavitowesha vyote viwili, tumbo na vyakula. LAKINI MWILI SI KWA ZINAA, BALI NI KWA BWANA, naye Bwana ni kwa mwili”

Hiyo ikiwa na maana kuwa ni lazima tuitoe miili yetu kwa Bwana, ni lazima tumpe MUNGU vilivyo vyake, Tusipofanya hivyo tutakuwa tunafanya makosa makubwa sana..

Sasa tunampaje Mungu vilivyo vyake?

1.KWA KUOKOKA!

Kuokoka maana yake ni kumkabidhi Bwana roho zetu, kwa kutubu dhambi na kubatizwa kwa maji na kwa Roho.(Marko 16:16). Unapomwamini Bwana Yesu na kumkabidhi maisha yako, hapo umempa Mungu vilivyo vyake, na hivyo utakuwa umeyafanya mapenzi ya Mungu.. kwasababu Utu wako wa ndani umeumbwa kwa mfano wake.

2. KWA KUJITENGA NA DHAMBI.

1Wakorintho 6:13  “…LAKINI MWILI SI KWA ZINAA, BALI NI KWA BWANA, naye Bwana ni kwa mwili” Hapa maandiko yanaonesha dhahiri kuwa “mwili si kwa zinaa bali kwa Bwana ” maana yake mtu anayefanya zinaa inaiharibu mali ya Mungu, ambayo ni mwili wake.. Kwasababu mwili wake umeumbwa kwa mfano wa MUNGU, una anwani ya Mungu!!..

Hivyo si ruhusa kuuharibu kwa zinaa, au kwa pombe, au kwa sigara, au kwa kuuandika tattoo au kwa kuuvisha jinsi mtu atakavyo (nguo za kubana au zisizo za maadili) au kwa mambo mengine yote yanayofanana na hayo..

Hivyo kwa hitimisho ni kwamba.. Vya Mungu anavyopaswa apewe ni ROHO ZETU, na MIILI YETU. Kwasababu vitu hivyo vina sura na anwani ya Mungu mwenyewe, kama vile dinari iliyokuwa na sura na anwani ya Kaisari.

Bwana akubariki.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

Nini maana ya tumeumbwa kwa mfano na sura ya Mungu?

Tofauti kati ya mtu na mwanadamu ni ipi?

Naomba kufahamu maana ya “sura ya kijiti” katika Marko 12:26.

Makerubi wenye sura nne, ni kweli wapo? na je! wanyama wataenda mbinguni?

Nuru yetu inapaswa iangaze au isiangaze kulingana na Mathayo 5:16 na Mathayo 6:1?

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments