WALA HAKUSIMAMA MTU PAMOJA NAYE, YUSUFU ALIPOJITAMBULISHA KWA NDUGUZE

WALA HAKUSIMAMA MTU PAMOJA NAYE, YUSUFU ALIPOJITAMBULISHA KWA NDUGUZE

Mwanzo 45:1 “Hapo Yusufu hakuweza kujizuia mbele yao wote waliosimama karibu naye. Akapiga kelele, na kusema, Mwondoeni kila mtu mbele yangu. Wala hakusimama mtu pamoja naye, Yusufu alipojitambulisha kwa nduguze.  2 Akapaza sauti yake akalia, nao Wamisri wakasikia. Watu wa nyumba ya Farao nao wakasikia.  3 Yusufu akawaambia ndugu zake, Mimi ndimi Yusufu; baba yangu angali hai bado? Wala ndugu zake hawakuweza kumjibu, maana waliingiwa na hofu mbele yake”.

Nakusalimu katika jina kuu sana la mwokozi wetu Yesu Kristo.

Yusufu baada ya kuuzwa na ndugu zake kwa watu wa mataifa, akidhaniwa kuwa ndio habari yake imeishia pale, lakini kama tunavyoifahamu habari, mambo yalikuwa ni kinyume chake, badala ya kuwa mtumwa akawa msaada na nguzo kubwa sana sio kwa wa-Misri peke yao bali pia kwa dunia nzima.

Lakini nachotaka tuone leo, ni ile siku alipojitambulisha kwa ndugu zake, ambao hawakumtambua siku zote ijapokuwa alikuwa ni ndugu yao kabisa wa damu, utaona  siku hiyo Yusufu hakujidhihirisha mbele ya kila mtu tu ilimradi, hakujidhihirisha mbele ya watu wake Misri waliompokea, bali aliwaondoa kwanza wote, akabaki yeye kama yeye pamoja na wale ndugu zake 11 tu.

 Ulishawahi kujiuliza ni kwanini iwe vile? Kwani kuna ubaya gani yeye kujifunua mbele ya kila mtu?..Kulikuwa hakuna ubaya wowote, lakini upo ufunuo mkubwa sana nyuma yake, kuhusiana na mpango wa wokovu wa Mungu.

Kibiblia habari ya Yusufu ni picha halisi ya Bwana wetu Yesu Kristo. Yeye alipokuja  duniani  kama mfalme, biblia inasema watu wake (Wayahudi), hawakumkubali, bali kinyume chake ndio wakamuua, ili tu asiwe mfalme wao.

Yohana 1:11  “Alikuja kwake, wala walio wake hawakumpokea”

Lakini neema walioikataa ilipohubiriwa kwetu sisi (watu wa mataifa), tuliipokea kwa shangwe, na ndio maana tunaona mpaka sasa Bwana Yesu ndio msingi na ngome ya mataifa yote ulimwenguni. Lakini cha ajabu ni kwamba Yesu ambaye alitoka kwa wayahudi, mpaka sasa hawamtambui, ijapokuwa miaka 2000, inakaribia kuisha.. Bado hawaoni kuwa huyu Yesu ndiye tegemeo la dunia yote, wala hakutakuwa na masihi mwingine atakayekuja kuwaokoa zaidi ya huyo. Hilo hawalioni, ukienda kumuhubiria sasa Rabi wa kiyahudi habari za Yesu, anakuona kama wewe ni kafiri.

Lakini maandiko yanatabiri kuwa, wakati wao wa kurudiwa tena utafika, na Yesu atajitambulisha kwao kwa mara nyingine, macho ya mioyo yao yatatiwa Nuru, wakati huo, wayahudi wote, watalia na kuomboleza kwa maombolezo makuu pale Israeli, watalia sana ni kwanini walimsulibisha Bwana wao na mfalme wao, waliyekuwa wanamsubiria..

Zekaria 12:10 “Nami nitawamwagia watu wa nyumba ya Daudi, na wenyeji wa Yerusalemu, roho ya neema na kuomba; nao watamtazama yeye ambaye walimchoma; nao watamwombolezea, kama vile mtu amwombolezeavyo mwanawe wa pekee; nao wataona uchungu kwa ajili yake, kama vile mtu aonavyo uchungu kwa ajili ya mzaliwa wake wa kwanza. 

11 Siku hiyo kutakuwa na maombolezo makuu huko Yerusalemu, kama maombolezo ya Hadadrimoni katika bonde la Megido.  12 Nayo nchi itaomboleza, kila jamaa peke yake; jamaa ya nyumba ya Daudi peke yao, na wake zao peke yao; jamaa ya nyumba ya Nathani peke yao, na wake zao peke yao; 

13 jamaa ya nyumba ya Lawi peke yao, na wake zao peke yao; jamaa ya nyumba ya Shimei peke yao, na wake zao peke yao.  14 Jamaa zote zilizosalia, kila jamaa peke yake, na wake zao peke yao”.

Hapo ndipo neema itarudi Israeli, ambapo inafananishwa ni lile tendo la Yusufu kujifunua tena kwa ndugu zake na kumtambua..Wakalia pamoja.

Lakini kabla hayo yote hayajatokea,  ni sharti kwanza, watu wa nyumbani mwa Yusufu “WAONDOLEWE”.

Yusufu hawezi, kuwahudumia wote wawili kwa mpigo..Alikuwa na utaratibu wake. Na ndivyo hata Kristo atakavyofanya pindi neema inarudi Israeli, sisi watumishi wake, (tulio katika mataifa), atatuondoa kwanza, kwa tukio lijulikanalo kama unyakuo, ndio ajifunue kwa Israeli.

Ndugu yangu, kama hujui mpango huu wa Mungu ni kwamba  mpaka sasa Israeli imeshakuwa taifa tangu 1948, ni taifa huru linalojitegemea, na hivi karibuni neema hii ya injili itarejea kwao. Hivyo mimi na wewe hatuna muda mwingi, Unyakuo upo karibu, tunachokisubiria hapa ni parapanda tu, hakuna kingine, dalili zote Yesu alizozisema zimeshatimia,(hilo kila mtu anajua) Kama unadhani, dunia itaendelea kuwepo kwa miaka mingine elfu, hilo wazo lifute,

Ikiwa unyakuo utapita leo, maana yake ni kuwa hii dunia itakuwa imebakiwa na miaka saba(7) tu mpaka iishie, na ndani ya hicho kipindi, Israeli itampokea Kristo, kisha mpinga-Kristo atanyanyuka mahususi kupigana nao, na baada ya hapo, Mungu ataiadhibu hii dunia kwa wote watakaopokea chapa ya Mnyama.  Kisha Bwana atawaokoa watu wake Israeli, kwa kurudi kwake mara ya pili duniani, na dunia itakuwa imeisha.

Ndugu yangu, angalia maisha yako, angalia unapoelekea, angalia mpango wa Mungu ulivyojidhihirisha wazi mbele yetu, utaendelea mpaka lini kudumu katika dhambi? Au katika maisha ya uvuguvugu?. Ikiwa hujazaliwa mara ya pili ni heri ufanye hivyo sasa katika hichi kipindi kifupi tulichobakiwa nacho. Na mtu anazaliwa mara ya pili kwanza kwa kutubu dhambi zake kwa kumaanisha kuziacha, na pili kwa kubatizwa katika ubatizo sahihi wa maji mengi, na kwa jina la Yesu Kristo, na mwisho kupokea Roho Mtakatifu.

Hivyo ikiwa utahitaji msaada ya Toba, au ubatizo sahihi wa maji mengi, basi wasiliana nasi kwa namba zetu hizi nasi tutakusaidia.

Bwana akubariki.

Maran Atha.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

WATAMTAZAMA YEYE AMBAYE WALIMCHOMA; NAO WATAMWOMBOLEZEA.

SIKU YA TAABU YA YAKOBO.

MZEITUNI HALISI UTAKAPOPACHIKWA.

ALIPO NA ATAKAPOKUWEPO BIBI-ARUSI WA YESU KRISTO.

DHIKI KUU INAKUJA NA UNYAKUO UPO KARIBU.

MIHURI SABA

UNAWAZA NINI SASA, JUU YA UFALME WA MBINGUNI?

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments