UNAWAZA NINI SASA, JUU YA UFALME WA MBINGUNI?

UNAWAZA NINI SASA, JUU YA UFALME WA MBINGUNI?

Wingu la Mashahidi
Wingu la Mashahidi
UNAWAZA NINI SASA, JUU YA UFALME WA MBINGUNI?
/

Unawaza nini juu ya kuipeleka injili mbele?..Je unafikiri nini juu ya hali ya kiroho ya  wanao miaka kadhaa mbele?, endapo parapanda itakuwa haijalia miaka 20 ijayo, je hali ya kiroho ya wanao itakuwaje, ukilinganisha na kasi ya maadili kuporomoka?.. Je umewahi kufikiri kufanya chochote leo hii, ili miaka ya mbeleni watoto wako au Watoto wa wengine, wasikose chakula cha uzima?…

Kizazi tulichopo ni kizazi kinachoharibika kila siku, umewahi kufikiri hali itakuwaje miaka 10 mbeleni?..kama umewahi kufikiri kwamba hali utakuwa mbaya Zaidi kuliko sasa, basi pia jiulize leo hii unafanya nini ili wakati huo utakapofika, shetani asipate nafasi inayoiona mbeleni.

Kumbuka wewe usipotumia muda wako leo, au akili zako leo, au nguvu zako leo, kufikiri na kufanya jambo lolote juu ya ufalme wa Mbinguni, Bwana atafanya kupitia wengine, (kwasababu kazi yake ni lazima iende mbele) lakini wewe wewe utakuwa umejipunguzia thawabu zako mbele zake.

Hebu Leo tujifunze juu ya watu wawili katika biblia, ambao kupitia hao, tutapata hamasa na hekima katika kufikiri kuujenga ufalme wa mbinguni.

Mtu wa kwanza ni DANIELI, na wa pili ni YUSUFU. Watu hawa wawili wote walijaliwa uwezo wa kutafsiri ndoto, lakini kila mmoja kwa namna yake.

DANIELI:

Kuna wakati Mfalme Nebkadneza, (Mfalme wa Babeli) aliota Ndoto, lakini akawa ameisahau ile ndoto, na Danieli alipomwomba Bwana, aliweza kufunuliwa ndoto ile Pamoja na Tafsiri yake..na akaenda kumwambia mfalme, na ndoto ile na tafsiri yake vikathibitika..Na Mfalme akamtukuza sana Danieli, lakini si kama Yusufu.

YUSUFU:

Farao Mfalme wa Misri, naye aliota ndoto kama Nebukadneza…na ndoto ile alipoamka aliikumbuka…lakini cha ajabu ni kwamba hakuwaficha watafsiri wake ndoto ile, bali aliwahadithia alichokiota..yeye alichokuwa anahitaji tu ni maana ya ile ndoto..

Na alikuwa anajua kuwa watatokea waongo wengi, ambao watamwambia uongo..na kweli walitokea wengi wakampa tafsiri ya ndoto yake..lakini tafsiri zote hizo alizikataa..

Sasa ni Siri gani iliyofanya Tafsiri ya Yusufu ikubalike Zaidi ya zile nyingine zote??

Siri yenyewe ni mikakati baada ya kuielezea ile tafsiri..

Yusufu baada ya kusema kuna miaka 7 ya neema inakuja na 7 ya Njaa.. hakuishia hapo tu!.. lakini alitoa mikakati ni NINI CHA KUFANYA KATIKA HIYO MIAKA 7 YA NEEMA NA MIAKA 7 YA NJAA. Ndio utaona akamshauri Farao atafute mtu mwenye akili amweke juu ya kazi zake zote akusanye chakula cha kutosha katika miaka ya neema, ili itakapokuja miaka ya njaa basi hazina iwepo kubwa. (Hilo ndio wazo lililompandisha hadhi Yusufu, na wala si tu tafsiri)!..

Farao aliona hata kama tafsiri itakuwa ni ya UONGO, lakini wazo alilotoa YUSUFU NI LA HEKIMA NA AKILI…, hata kama Njaa haitakuja kama alivyotafsiri, lakini wazo tu la kuweka chakula akiba ni wazo kubwa sana na la akili sana, ambalo pengine katika utawala wake wote Farao hajawahi kushauriwa hivyo…

Tusome..

Mwanzo 41:28 “ Ndivyo nilivyomwambia Farao, ya kwamba Mungu amemwonyesha Farao atakayoyafanya hivi karibu.

29 Tazama, miaka saba ya shibe inakuja, katika nchi yote ya Misri.

30 Kisha kutakuja miaka saba ya njaa baada yake; na shibe ile yote itasahauliwa katika nchi ya Misri, na njaa itaiharibu nchi.

31 Wala shibe ile haitajulikana katika nchi kwa sababu ya njaa inayokuja baadaye, maana itakuwa nzito sana.

32 Na ndoto ya Farao kwa vile ilivyokuja mara mbili, ni kwa sababu neno hilo Mungu amelithibitisha, na Mungu atalitimiza upesi.

33 BASI, FARAO NA AJITAFUTIE MTU WA AKILI NA HEKIMA AMWEKE JUU YA NCHI YA MISRI.

34 FARAO NA AFANYE HIVI, TENA AKAWEKE WASIMAMIZI JUU YA NCHI, NA KUTWAA SEHEMU YA TANO KATIKA NCHI YA MISRI, KATIKA MIAKA HII SABA YA KUSHIBA.

35 NA WAKUSANYE CHAKULA CHOTE CHA MIAKA HII MYEMA IJAYO, WAKAWEKE AKIBA YA NAFAKA MKONONI MWA FARAO WAKAKILINDE KUWA CHAKULA KATIKA MIJI.

36 NA HICHO CHAKULA KITAKUWA AKIBA YA NCHI KWA AJILI YA MIAKA HIYO SABA YA NJAA, ITAKAYOKUWA KATIKA NCHI YA MISRI, NCHI ISIHARIBIKE KWA NJAA.

37 NENO HILO LIKAWA JEMA MACHONI PA FARAO, NA MACHONI PA WATUMWA WAKE WOTE.

38 Farao akawaambia watumwa wake, Tupate wapi mtu kama huyu, mwenye roho ya Mungu ndani yake?

39 Farao akamwambia Yusufu, Kwa kuwa Mungu amekufahamisha hayo yote, hapana mwenye akili na hekima kama wewe.

40 Basi wewe utakuwa juu ya nyumba yangu, na kwa neno lako watu wangu watatawaliwa. Katika kiti cha enzi tu nitakuwa mkuu kuliko wewe”.

Umeona?.. watafsiri wengine walikuwa wanakuja na tafsiri zao lakini mwisho wa siku wanamshauri Farao mambo yasiyo na hekima, wala yasiyojenga, wala yasiyo na manufaa..ndio maana hata tafsiri zao Mfalme alizikataa.. Lakini  Yusufu alipotoa tafsiri na mikakati bora baada ya ile tafsiri ndipo hata tafsiri yake ikathibitika.

Na utaona Yusufu alipokea kibali sana mbele ya Farao, Zaidi hata ya Danieli alivyotukuzwa na Nebukadreza.

Je na wewe unataka kibali leo mbele za Mungu? Kama Yusufu alivyopata mbele ya Farao??..kama ndio! basi anza kufikiri kuhusu Injili ya Kristo, katika siku za mbeleni, na anza kufanya kitu kuanzia sasa. Kama ni mhubiri basi weka hazina kwa vizazi vinavyokuja… Kama ni mtu wa kukirimu, basi changia injili kwa mali zako kwa kadiri uwezavyo, ili kusudi Watoto wanaochipukia wasikue na kukuta idadi ya disco na bar zimezidi makanisa, wasije wakakuta idada ya vikundi vya wahuni vimezidi vya watu wema, wasije  wakakutana na ugumu wa kuitafuta injili ya kweli, Zaidi ya huu tulionao sisi katika kizazi chetu..

 shetani anayo mikakati sasahivi ya kuharibu kizazi hata cha tano kijacho..na hata sasa kashaanza kufanya juhudi hizo, inatupasaje sisi, tunaosema tumeokoka sasa? Kama wewe umeipata injili ya kweli, kiurahisi, basi rahisisha pia kwa wanaokuja, ambao kwa ambao hawajasikia..ndivyo Mungu atakavyokupa kibali.

Mithali 13:22 “Mtu mwema huwaachia wana wa wanawe urithi”

Tujifunze kwa Yusufu, ili na sisi tupate kibali mbele za Mungu.

Maran atha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

FAHAMU TAFSIRI ZA NDOTO MBALIMBALI.

ALIPO NA ATAKAPOKUWEPO BIBI-ARUSI WA YESU KRISTO.

UKIOKOKA, JIANDAE KUPITISHWA USIPOPATAZAMIA.

Je! Shetani anao uwezo wa kuumba, kama Mungu?

Kwanini  vizazi vya ukoo wa Yesu vinajipinga katika Mathayo na Luka.

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments