KWA MIOYO YAO WAKAREJEA MISRI.

KWA MIOYO YAO WAKAREJEA MISRI.

Jina la Mwokozi Yesu, libarikiwe.

Karibu tujifunze maandiko, Neno la Mungu wetu ambalo ndio taa iongozayo miguu yetu, na Mwanga wa njia yetu (Zab.119:105).

Safari ya wana wa Israeli ni funzo tosha, kwetu sisi tunaosafiri kutoka katika ulimwengu kwenda Kaanani yetu (yaani mbinguni). Hivyo tukijifunza kwa undani, jinsi safari ile ilivyokuwa tutaweza kujua tahadhari na sisi tunazopaswa kuzichukua katika safari yetu ya kwenda mbinguni.

Maandiko yanasema wana wa Israeli, walitolewa Misri kwa mkono hodari, lakini walipokuwa jangwani katika safari yao ya kwenda Kaanani, walikutana na changamoto chache, ambazo hizo ziliwafanya wamnung’unikie Mungu, na hata kufikia hatua ya kutamani tena kurudi Misri, walikotoka.

Hesabu 14:3 “Mbona Bwana anatuleta mpaka nchi hii ili tuanguke kwa upanga? Wake zetu na watoto wetu watakuwa mateka; JE! SI AFADHALI TURUDI MISRI?

4 Wakaambiana, NA TUMWEKE MTU MMOJA AWE AKIDA, TUKARUDI MISRI”.

Hesabu 11:4 “Kisha mkutano wa wafuasi waliokuwa kati yao, wakashikwa na tamaa; wana wa Israeli nao wakalia tena, wakasema, N’nani atakayetupa nyama tule?

5 Twakumbuka samaki tuliokula huko Misri bure; na yale matango, na matikiti, na mboga, na vitunguu, na vitunguu saumu;

6 lakini sasa roho zetu zimekauka; hapana kitu cho chote; hatuna kitu cha kutumaini isipokuwa hii mana tu. ”.

Na maandiko yanasema kwa kunung’unika huko, na kwa kutamani huko kurudi Misri, tayari walisharejea Misri katika mioyo yao, ijapokuwa katika mwili bado wapo jangwani.

Matendo 7:39 “Mtu huyo baba zetu hawakutaka kumtii, bali wakamsukumia mbali, NA KWA MIOYO YAO WAKAREJEA MISRI,

40 wakamwambia Haruni, Tufanyie miungu, watakaotutangulia; maana huyo Musa, ALIYETUTOA KATIKA NCHI YA MISRI, hatujui lililompata”.

Ndio maana katika wote walionung’unika na kutamani kurudi Misri, hakuna hata mmoja aliyeingia nchi ya Kaanani, wote walikufa jangwani. Kwanini?, kwasababu katika mwili walikuwa wametoka Misri lakini katika roho/moyo walikuwa  wapo Misri. Na kwasababu nia ya ndani inazungumza Zaidi kuliko mwonekano wa nje, wakaangamia wote jangwani bila kufika kule wanakokwenda.

Kadhalika mtu mwingine tunayeweza kujifunza kwake ni Mke wa Lutu, ambaye Bwana alisema “mkumbukeni huyo”(Luka 17:32).

Mke wa Lutu ni kweli alikuwa ameshaanza safari ya kutoka Sodoma, na Zaidi ya yote ameshaokoka kabisa(na inavyoelekea wakati anatoka alitoka kwa Amani na furaha kabisa kama wana wa Israeli walivyotoka Misri).. lakini biblia inasema alipofika mbele katika safari ile ALIGEUKA NYUMA!!..

Maana yake ni kwamba, mawazo yake, fikra zake, tamaa zake, zikatamani tena ya  Sodoma alikotoka… Labda alifika mahali akaanza kumlalamikia sana Lutu, na Mungu, kwanini katoka kule, sehemu nzuri na wanakwenda sehemu mbaya.. na kwa kosa hilo tu (la kurejea Sodoma kwa moyo wake).. mbele za Mungu alionekana tayari kastahili adhabu sawa na watu wa Sodoma na Gomora, haijalishi mwili wake haupo Sodoma. Na hivyo akageuka kuwa nguzo ya chumvi.

Ni kweli alikuwa ametoka, ameokoka, mwili wake haupo tena Sodoma, lakini Moyo wake upo Sodoma.. Na pasipo kujua kuwa moyo wa mwanadamu unanena zaidi kuliko kitu kingine chochote cha nje..akapumbazika na hivyo akajikuta anaangamia tu sawa na watu wa Sodoma.

Sasa mambo haya yaliyoandikwa katika biblia yanayowahusu wana wa Israeli na Mke wa Luthu, maandiko yanasema hayajaandikwa tu kutufurahisha! Au kutuhuzunisha, bali yaliandikwa kwaajili yetu ili sisi tusijifunze tusirudie makosa kama yao.

1Wakorintho 10:6 “Basi mambo hayo yalikuwa mifano kwetu, kusudi sisi tusiwe watu wa kutamani mabaya, kama wale nao walivyotamani.

7 Wala msiwe waabudu sanamu, kama wengine wao walivyokuwa; kama ilivyoandikwa, Watu waliketi kula na kunywa, kisha wakasimama wacheze.

8 Wala msifanye uasherati, kama wengine wao walivyofanya, wakaanguka siku moja watu ishirini na tatu elfu.

9 Wala tusimjaribu Bwana, kama wengine wao walivyomjaribu, wakaharibiwa na nyoka.

10 Wala msinung’unike, kama wengine wao walivyonung’unika, wakaharibiwa na mharabu.

11 Basi mambo hayo yaliwapata wao kwa jinsi ya mifano, yakaandikwa ili kutuonya sisi, tuliofikiliwa na miisho ya zamani.

12 Kwa hiyo anayejidhania kuwa amesimama na aangalie asianguke”.

Ndugu Dada/kaka.. kumbuka unapookoka, ni sawa na umeanza safari yako ya kutoka Misri, au Sodoma… Ulimwengu huu umefananishwa na Sodoma na Misri (Ufunuo 11:8). Hivyo hatuna budi kutoka Misri kweli kweli kwa miili yetu na mioyo yetu!.. sio tu kwa miili bali pia kwa mioyo yetu!.

Maana yake ni kwamba tunapomkiri Yesu, hatuna budi tuukatae ulimwengu kimwili na kiroho, tunapaswa tuache ulevi, mwilini na rohoni, tunapaswa tuache uasherati wa mwilini na wa rohoni, kama Bwana alivyosema katika…

Mathayo 5:27 “Mmesikia kwamba imenenwa, Usizini;

28 lakini mimi nawaambia, Kila mtu atazamaye mwanamke kwa kumtamani, amekwisha kuzini naye moyoni mwake”.

Hivyo tukisema hatuzini tu, na huku mioyoni tunaziwasha tamaa, hapo bado mioyo yetu ipo Misri, ijapokuwa kimwili tumetoka Misri, Tunapookoka na kusema si wauaji, si watoaji mimba, lakini mioyoni mwetu tunavinyongo na chuki kwa ndugu zetu na adui zetu, sisi bado ni wauaji tu (Mathayo 5:21-22) na bado tupo Misri kiroho, ingawa kimwili tunaelekea kaanani ambayo hatutaifikia..

Kadhalika ukiwa Misri na moyo wako upo kaanani, hapo bado upo Misri, haikusaidii chochote! Unapaswa utoke Misri, maana yake ni kwamba upo katika ulimwengu lakini una hamu ya kufika mbinguni, kila siku unasema siku moja nitaokoka, siku moja nitabadilika, siku moja nitaacha kuvaa vimini, siku moja nitaacha kujiuza, siku moja nitaacha ulevi.. Fahamu kuwa hiyo siku haitafika, na utakufa ukiwa bado Sodoma. Huu ni wakati wa kujiokoa roho zetu. Kwa kuamua kuokoka kweli kweli na si kuwa vuguvugu. Kwasbabu Bwana alisema watu wote walio vuguvugu atawatapika watoke katika kinywa chake.. (Ufunuo 3:15)

Bwana atusaidie tuokoke kweli kweli, tutoke Misri na Sodoma kiroho na kimwili..

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

Sodoma ipo nchi gani?

JE YESU AMEJIAMINISHA KWAKO?

NJIA YA MSALABA

NI WAPI MAHALI SAHIHI PA KULIPA ZAKA?

Ni kweli Paulo alipuuzia maonyo aliyopewa ya kwenda Yerusalemu?

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments