JIPE NAFASI KATI YA TAARIFA UNAYOIPOKEA NA MAAMUZI UNAYOYATOA.

JIPE NAFASI KATI YA TAARIFA UNAYOIPOKEA NA MAAMUZI UNAYOYATOA.

Shalom, jina la Bwana libarikiwe.

Ni vema tukajifunza tabia kadha wa kadha za Mungu, ili na sisi tuziige hizo tuwe wakamilifu kama yeye. Leo tutajifunza tabia mojawapo ya Mungu, ambayo pengine unaweza ukastaajabu Mungu anawezaje kuonyesha angali yeye ni Mungu. Hivyo kwa kupitia hiyo tutajifunza na sisi mienendo yetu.

Kwamfano ukisoma kitabu cha Mwanzo, baada ya Mungu kumaliza uumbaji wake wote, baadaye utaona tena anasema “si vema”(Mwanzo 2:18). Sasa utajiuliza iweje aone tena si vema, kwani kazi yake hapo mwanzo ilikuwa haijakamilika? Inahitaji marekebisho.. Mpaka aanze tena uumbaji mwingine wa kumpa Adamu msaidizi?..

Jibu ni kwamba Sio kwamba hakulijua hilo? Hapana alishalijua na tayari alikuwa ameshamuumba Hawa katika akili yake tangu zamani (Soma Mwanzo 1:27). Lakini alijifanya kana kwamba amesahau, ili kutufundisha sisi pia, tuwe watu wa kupenda marekebisho. Marekebisho sio dhambi, ni karama ya Mungu..Kwani kwa kupitia hiyo tutafikia ukamilifu, ukiwa mtu wa kuridhika na maisha yaleyale, mienendo ile ile, huna maboresho yoyote, ujue tabia hii ya Ki-Mungu haipo ndani yako.

Vivyo hivyo kuna tabia nyingine, ya kushangaza aliionyesha Mungu, na leo tutajifunza. Utakumbuka wakati ule, anakwenda kuiteketeza Sodoma na Gomora, alikutana kwanza na Ibrahimu, na alipomaliza kuzungumza naye akabidi pia amweleze  Ibrahimu mpango wake, akamwambia maneno haya;

Mwanzo 18:20 “Bwana akasema, Kwa kuwa kilio cha Sodoma na Gomora kimezidi, na dhambi zao zimeongezeka sana, 

21 BASI, NITASHUKA SASA NIONE KAMA WANAYOTENDA NI KIASI CHA KILIO KILICHONIJIA; NA KAMA SIVYO, NITAJUA. 

22 Basi wale watu wakatoka huko wakaelekea Sodoma; lakini Ibrahimu alikuwa akali akisimama mbele za Bwana”

Tafakari kwa ukaribu hayo maneno..“nitashuka sasa nione kama wanayotenda ni kiasi cha kilio kilichonijia; na kama sivyo, nitajua”.. Ni nini unajifunza hapo, kwamba huyu ni mtu asiyechukua maamuzi ya haraka kwanza bila kwenda kuthibitisha kwa undani ukweli wa tukio lenyewe.

Sio kwamba Mungu alikuwa hana uhakika wa kilichokuwa kinaendelea..Lakini alijifanya kana kwamba hajui, akaacha shughuli zake mbinguni, akateremka chini, aingie sodoma, atembee kwenye miji yake, ili apate uhakika wa taarifa zilizomfikia. Alijipa nafasi kati ya kile anachokisikia na maamuzi anayoyatoa.

Na kweli alikuta vilevile kama vilio vyao vilivyomfikia, lakini faida yake ni kuwa ndani yake alimwona mwenye haki mmoja, naye ni Lutu na familia yake, ndipo akamwokoa na ghadhabu ile. Lakini kama Bwana angetoa hukumu yake moja kwa moja kutoka kule mbinguni, pindi tu alipopokea taarifa na kusema ‘haya nyie malaika kapigeni kiberiti miji ile’.. Lutu angeonekania wapi?.

Ni nini tunajifunza?

Tumeyabomoa maisha yetu sana, tumewaharibu wakina Lutu wetu, kwa kuchukua maamuzi ya haraka kwa kila tukio/Taarifa tunayoisikia, masikioni mwetu, au kwa kila jambo linalotokea ghafla mbele yetu.

Kwamfano Umesikia ndugu yako amekusengenya, usiwe na haraka wa kurudisha majibu ya chuki. Jifanye kama hilo ulilolisikia ni la uongo hata kama umelithibitisha.. Hiyo itakupa nafasi ya wewe, kutafakari kujua chanzo cha tatizo ni nini, na hatimaye utajikuta huwenda wewe ndio ulikuwa sababu ya yeye kuwa vile, na hapo utamsamehe, au kumwombea, au kujiombea wewe rehema. Lakini ukarudisha majibu ya kumchukia, au kumsema na wewe. Utajibomoa zaidi kuliko kujijenga.

Waweza sikia taarifa mbaya, au hujapendezwa na jambo Fulani au tukio fulani  kwenye kanisa, kabla hujazira na kuondoka, pata nafasi ya kuomba, na kumshirikisha Mungu, kupitia viongozi wako wa kiroho, kama vile Mungu alivyomshirikisha rafiki yake Ibrahimu. Hiyo itakusaidia kuchukua maamuzi yaliyo ya busara zaidi.

Hata katika mambo ya maisha, kwenye familia, ukoo, pengine hata kazini kwako, ofisini, n.k, zipo taarifa nyingi zinaweza kukufikia za wafanyakazi wenzako, hupaswi kuzimeza  moja kwa moja na kuzitolea maamuzi hata kama umezithibitisha kuwa ni za kweli.. Tuliza moyo wako, tafakari, omba, ndipo baadaye Mungu akuongoze cha kutenda. Utafanya vizuri zaidi.

Ni muhimu sana, kuweka “NAFASI” Katika mioyo yetu. Kile kinachoingia, kisirudishe majibu hapo hapo. Ni heri viingie mia, kikatoka kimoja chenye majibu ya busara, kuliko kuingia 100, vikatoka vyote 100, vyenye kisasi, na maumivu, na mapigo. Ilimgharimu Bwana asiziamini taarifa zake, iweje wewe uamini za kwako, au za wanadamu wengine?

Bwana atusaidie.

Shalom.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

NGUVU ILIYOPO KATIKA MAAMUZI.

DHAMBI ILIYOMKOSESHA SHETANI:

UUMBAJI BORA WA MUNGU, UPO NDANI YA MWANADAMU.

Na hekima imejulikana kuwa ina haki kwa watoto wake wote.

JINSI YA KUMSIKIA MUNGU, NA KUPOKEA MAFUNUO AU JUMBE KUTOKA KWAKE.

Je ni kweli ilikuwa desturi ya Bwana kuishika sabato?(Luka 4:16)

Ni miaka mingapi ya njaa Daudi aliyoambiwa achague? Ni miaka 7 au miaka 3?

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments