Wengi wetu tunafahamu kitu gani kilitokea kabla ya Edeni, kwamba ibilisi/ shetani, alimwasi Mungu na kuondolewa katika nafasi yake aliyokuwapo, biblia inasema alikuwa ni Kerubi aliyetiwa mafuta, na alinyanyuliwa juu ya Mlima wa Mungu, yaani juu ya malaika wengine wote, alikuwa ni mzuri na mkamilifu katika njia zake zote na alikuwa na hekima nyingi sana, mpaka siku ile uovu ulipoonekana ndani yake, Sasa kulingana na wingi wa sifa alizokuwa nazo, na wingi wa heshima uliomzunguka tunafahamu moyo wake ulinyanyuka akatamani kuwa kama Mungu.(ukisoma Ezekieli 28:11-18, Isaya 14:12 utaona jambo hilo.)
Sasa ni nani aliyemdanganya shetani?
Jibu ni kwamba hakuna aliyemdanganya shetani, bali alijidanganya yeye mwenyewe, pale alipoona amenyanyuliwa na Mungu, hivyo alitamani awe Zaidi ya pale alipo, HILO TU! alionywa lakini alikataa, mpaka alipotolewa katika ile nafasi na kufukuzwa katika yale makao ya nuru ya utukufu aliyokuwepo, na baada ya kufukuzwa Bwana Mungu hakumuua mpaka majira yatakapofika, wala hakumnyanganya HEKIMA, na UZURI aliokuwa nao, wala hakumnyanganya NGUVU alizokuwa nazo, alichomuondolea ni ile nafasi aliyokuwa nayo mbinguni ya utukufu wa Mungu, hivyo baada ya hapo kwa kujua muda wake ni mfupi akaanza kuujenga ufalme wake na wale malaika walioasi pamoja naye, kwa hekima aliyokuwa nayo na kwa nguvu alizokuwa nazo,
Ni sawa tu na mkuu wa majeshi aliyeasi na kuondolewa katika nafasi yake ya ukuu wa majeshi, na kuamua kuondoka na wafuasi wake wengi kwenda msituni, kuanzisha kikundi cha uasi, sasa huyo mwanajeshi aliyeasi atakua amepoteza nafasi yake katika nchi lakini sio uzoefu wake, au ujuzi wake, au akili zake, ndivyo ilivyo kwa shetani baada ya kuasi hakuondolewa ujuzi wake, wala uwezo wake wa kufanya mambo,wala akili yake. Wengi wanafikiri kuwa siku shetani alipolaaniwa alibadilika na kuwa kitu cha ajabu sana na cha kutisha chenye mapembe na sura mbaya kisichoweza kufikiri, hapana, bali aliondolewa utukufu ule wa Mungu ndani yake. Na tunafahamu kitu chochote kikiondolewa utukufu wa Mungu, basi kinakuwa ni kama mfu tu katika roho.
Sasa baada ya Bwana Mungu kuanza uumbaji wa mwanadamu wa kwanza (Adamu), tayari shetani alikuwa ameshatengeneza ufalme wake ulioasi, unaojulikana kama ufalme wa giza. Na huu Ufalme wake una kazi moja tu, “kuenda kinyume na kila kitu ufalme wa Mungu unachokifanya”. Ukiamini kuwa upo wakati utasimama wenyewe na kutawala kila kitu.
Kwahiyo baada ya Adamu kuumbwa, Shetani kwa hekima yake alijua Mungu kamweka mwanadamu katika nafasi ya juu sana, kama alivyokuwa yeye, hivyo njia pekee aliyojua anaweza kuuimarisha ufalme wake ni kumwangusha mwanadamu kwa kumletea mawazo kama aliyokuwa nayo yeye hapo kwanza, “mawazo ya kujiinua kutaka kuwa kama Mungu”. Alijua kabisa njia pekee Bwana Mungu anayochukizwa nayo kwake ni KUJIINUA, Hivyo akamletea sasa mawazo kama yale yale kupitia nyoka, Tunasoma.
Mwanzo 3: 1 “Basi nyoka alikuwa mwerevu kuliko wanyama wote wa mwitu aliowafanya Bwana Mungu. Akamwambia mwanamke, Ati! Hivi ndivyo alivyosema Mungu, Msile matunda ya miti yote ya bustani? 2 Mwanamke akamwambia nyoka, Matunda ya miti ya bustanini twaweza kula; 3 lakini matunda ya mti ulio katikati ya bustani Mungu amesema, Msiyale wala msiyaguse, msije mkafa. 4 Nyoka akamwambia mwanamke, Hakika hamtakufa, 5 kwa maana Mungu anajua ya kwamba siku mtakayokula matunda ya mti huo, mtafumbuliwa macho, NANYI MTAKUWA KAMA MUNGU, mkijua mema na mabaya”.
Mwanzo 3: 1 “Basi nyoka alikuwa mwerevu kuliko wanyama wote wa mwitu aliowafanya Bwana Mungu. Akamwambia mwanamke, Ati! Hivi ndivyo alivyosema Mungu, Msile matunda ya miti yote ya bustani?
2 Mwanamke akamwambia nyoka, Matunda ya miti ya bustanini twaweza kula;
3 lakini matunda ya mti ulio katikati ya bustani Mungu amesema, Msiyale wala msiyaguse, msije mkafa.
4 Nyoka akamwambia mwanamke, Hakika hamtakufa,
5 kwa maana Mungu anajua ya kwamba siku mtakayokula matunda ya mti huo, mtafumbuliwa macho, NANYI MTAKUWA KAMA MUNGU, mkijua mema na mabaya”.
Unaweza ukaona hapo, shetani kitu alichoona kinaweza kikawavutia sana ili waasi ni hili neno WATAKUWA KAMA MUNGU. Jambo ambalo hata yeye mwenyewe hakuweza kulifikia kuwa kama Mungu, badala yake lilimshusha chini kutoka katika nafasi yake ya ukuu mpaka kuwa pepo. Na tunaona Adamu na Hawa nao baada ya kula tunda, badala ya kuwa kama Mungu kama walivyoahidiwa na shetani, wakapoteza ile nafasi yao kama shetani alivyopoteza ya kwake, wakafukuzwa nao vile vile kutoka katika Edeni bustani ya Mungu aliyokuwa amewaumbia wao. Unaona? Shetani aliwafundisha wasiridhike na nafasi waliyokuwa nayo pale Edeni, aliwafundisha wanaweza kuwa Zaidi ya pale.
Sasa shetani na yeye hajabadilika; mbinu aliyoitumia kuwaangusha malaika wenzake walioasi naye, na aliyotumia kuwaangusha wanadamu wa kwanza Adamu na Hawa, anaitumia hata leo kuwaangusha wanadamu, kuhakikisha anawatoa katika nafasi zao, na hatumii njia nyingine Zaidi ya kuwaletea watu “roho ya kujiinua (KIBURI)” Anajua kiburi ndicho kilichomshusha yeye chini, na ndio hicho hicho anawapachikia watu ili washushwe chini kutoka katika nafasi zao. Na kama ilivyo kawaida yake, shetani analilenga kanisa kwanza Zaidi ya watu wa ulimwengu huu, hivyo anafanya juu chini kuipachika hii roho ndani ya kanisa,
Inatokea wananyanyuka watu wachache [ambao shetani anawatumia pasipo wao kujua ] ndani ya kanisa wanaoanza kumsifia labda mchungaji, au mwalimu, au askofu, utasikia wataanza kumwambia “unajua wewe askofu huwa ukizungumza tu, mimi huwa nakuona unakuwa kama malaika”..unajua wewe mchungaji ni wakipekee sana, yaani una karama zote, yaani tumezunguka kote hakuna mfano wako, yaani wewe ni shujaa na wakipekee sana, wewe ni kiboko yao,n.k. sasa kwa sifa zote hizo ni rahisi yule mtu wa Mungu kujiona yeye kweli ni bora kuliko wengine, pasipo kujua kuwa ni roho ya shetani inataka kumpeleka mahali fulani, ananyanyuka moyo na yeye kuanza kuamini kwamba ni bora kuliko wengine, na mwisho wa siku anajikuta ameshajiinua kupita kawaida.
Na mbinu nyingine shetani anayopenda kuitumia pasipo watu wengi kujua, ni mapepo, anapenda kutumia mapepo kuwapandikizia watu wengi kiburi, kwamfano inatokea mtu kaenda kumuombea mtu mwingine na yule mtu akalipuka mapepo, na yale mapepo, yakaanza kumsifia, “wewe ni mtu hatari sana, tunakuogopa, yaaani unatuunguza na unatutesa sana tangu siku nyingi, yataendelea kumwambia sisi tumetoka jupita tumewajaribu, wachungaji wengi tumewashinda ni wewe peke yako ndio unayetutesa”..na yataendelea kumwambia hadithi nyingi za uongo ambazo zote maudhui yake ni kumnyanyua yule mtumishi, na yule mtumishi pasipo kujua kwamba zile roho ni kongwe tangu Edeni na zinajua namna ya kumwangusha mwanadamu, atadhani kuwa zinamwambia ukweli, atadhani kuwa yeye kweli ndiye wa kipekee kuliko watu wote duniani, pasipo kujua kwamba “shetani ni mwongo tangu zamani na yeye ni baba wa uongo” maandiko yanasema hivyo. Sasa yule mtumishi atatoka pale na kuamini kuwa hakuna kama yeye na pasipo kujua kuwa amepandikiziwa roho ya kiburi tayari, atakwenda huku na huko kujisifu kuwa hakuna kama yeye.
Biblia inasema “inasema ajishushaye atakwezwa naye ajikwezaye atashushwa”
Ndugu/dada: mali, uzuri, cheo, ukubwa, umaarufu, utakatifu, utumishi,uchungaji, karama, kipaji, kipawa au chochote kile kisikupe kiburi, na kujiona kuwa unastahili heshima ya kipekee Zaidi kuliko wengine, visikufanye ujione kuwa baada ya Mungu mbinguni unafuata wewe. Hiyo ni roho halisi ya shetani kabisa aliyoiachia kuwaangusha watu. Ilimwangusha shetani na ndiyo hiyo hiyo anayotumia kuziangusha nyota nyingi za mbinguni leo (yaani watakatifu).
Biblia inasema katika 1Wakoritho 10: 12 “Kwa hiyo anayejidhania kuwa amesimama na aangalie asianguke”. Unyenyekevu ndiyo silaha pekee ya kuishinda roho ya kiburi ya shetani. Kama biblia inavyosema katika..
1 Petro 5: 5“..Naam, ninyi nyote JIFUNGENI UNYENYEKEVU, mpate kuhudumiana; kwa sababu MUNGU HUWAPINGA WENYE KIBURI, lakini HUWAPA WANYENYEKEVU NEEMA. 6 Basi nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake; 7 huku mkimtwika yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana kwa mambo yenu. 8 Mwe na kiasi na kukesha; KWA KUWA MSHITAKI WENU IBILISI, KAMA SIMBA ANGURUMAYE, HUZUNGUKA-ZUNGUKA, AKITAFUTA MTU AMMEZE. ”
1 Petro 5: 5“..Naam, ninyi nyote JIFUNGENI UNYENYEKEVU, mpate kuhudumiana; kwa sababu MUNGU HUWAPINGA WENYE KIBURI, lakini HUWAPA WANYENYEKEVU NEEMA.
6 Basi nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake;
7 huku mkimtwika yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana kwa mambo yenu.
8 Mwe na kiasi na kukesha; KWA KUWA MSHITAKI WENU IBILISI, KAMA SIMBA ANGURUMAYE, HUZUNGUKA-ZUNGUKA, AKITAFUTA MTU AMMEZE. ”
Je! Ni kiburi cha uzima kimekutawala mpaka unaona kuwa hata wokovu si kitu cha maana sana kwako?, Hebu tubu leo uoshwe dhambi zako, na kubatizwa katika ubatizo uliosahihi wa maji tele katika Jina la YESU, ili Bwana akupe ondoleo la dhambi zako. Ukae mbali na hila za ibilisi na mitego yake yote katika kizazi hichi.
Bwana akubariki sana.
Tafadhali “share” ujumbe huu kwa wengine.
Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
ZIFAHAMU HUDUMA KUU (10) ZA SHETANI DUNIANI.
MAMBO (2) YATAKAYOKUTENGA NA IMANI SIKU HIZI ZA MWISHO.
SHETANI KWA SASA NI MZURI WA UMBO KAMA MALAIKA WATAKATIFU AU NI MWENYE MAPEMBE NA MAKWATO NA MAKUCHA MAREFU?
KWANINI MUNGU AWACHOME WATU KWENYE ZIWA LA MOTO NA HALI YEYE NDIYE ALIYEWAUMBA?
Rudi Nyumbani
Print this post
halo shalom!
shalom
MUNGU AWAZIDISHIE ILI MZIDI KUFUNDISHA ULIMWENGU
Asante.nimejifunza
Amina.. karibu sana..
Hamjambo,ninaomba mnipe mandiko yanayozungumzia mada zifuatazo; (1)tutaenda mbinguni (2)tutatawala na mwokozi mbinguni miaka 7 (3)mwokozi atakuja mara ya pili juu mawinguni na kuchukua wateule wake waende mbinguni (4)mwokozi atakuja mara ya tatu kutawala na wateule duniani nitashukuru mtakapokuwa mnashughulikia hizo mada asanteni
Sasa wewe unaomba au unataka uthibisho? Maana Kuna tofauti kati ya anayeomba kitu! Na anayetaka uthibisho wa kitu! Kwa kifupi tunashindwa kuelewa unataka kujifunza au ni vipi