JINSI MWISHO ULIVYOKARIBIA.

JINSI MWISHO ULIVYOKARIBIA.

Ukiitafakari hii neema tuliyopewa sisi watu wa mataifa ambao hapo mwanzo tulikuwa ni watu wasio na Mungu duniani ni kubwa sana, kiasi kwamba Mungu tangu zamani aliwaficha watu wake wengi, hata manabii wake waliomcha yeye katika Israeli, hawakuweza kuielewa neema hiyo, Mungu aliiweka katika SIRI kubwa sana, ambayo aliitunza mpaka wakati ulipofika wa kufunuliwa kwake, na siri yenyewe Mtume Paulo aliisema katika

Waefeso 3:3 ikiwa mmesikia habari ya uwakili wa neema ya Mungu niliyopewa kwa ajili yenu;

3 ya kwamba KWA KUFUNULIWA NALIJULISHWA SIRI HIYO, kama nilivyotangulia kuandika kwa maneno machache.

4 Kwa hayo, myasomapo, mtaweza kuutambua ufahamu wangu KATIKA SIRI YAKE KRISTO.

5 SIRI HIYO HAWAKUJULISHWA WANADAMU KATIKA VIZAZI VINGINE; kama walivyofunuliwa mitume wake watakatifu na manabii zamani hizi katika Roho;

6 YA KWAMBA MATAIFA NI WARITHI PAMOJA NASI WA URITHI MMOJA, NA WA MWILI MMOJA, NA WASHIRIKI PAMOJA NASI WA AHADI YAKE ILIYO KATIKA KRISTO YESU KWA NJIA YA INJILI;.

Unaona hapo siri yenyewe ni kuwa kumbe hata sisi mataifa ni warithi wa ahadi za Ibrahimu kama wayahudi, katika Kristo. Watu ambao hapo mwanzo tulikuwa tunaonekana kama mbwa kwa wayahudi na ndivyo tulivyokuwa. Lakini Mungu alivyo wa upendo,alituingiza sisi kwa nguvu kupitia Yesu Kristo nasi tuwe warithi sawasawa na wao.

Hivyo ndugu kama wewe ni msomaji mzuri wa biblia utagundua kuwa tangu kipindi cha wana wa Israeli walipokuwa Babeli , Mungu alimfunulia mtumishi wake Danieli muda wa siku zilizobakia mpaka dunia kuisha, ukisoma Danieli 9 utaona kuwa Nabii Danieli aliambiwa muda wa MAJUMA 70 umewekwa kwa watu wake (yaani Waisraeli), mpaka kila kitu kitakapokamilika. Na kumbuka juma moja ni sawa na miaka 7 kibiblia, hivyo ukipiga hesabu utaona jumla yake ni miaka 490 [70×7=490] tu, tangu ule wakati walipotoka Babeli mpaka ulimwengu kuisha.

Lakini ukisoma pale utaona hayo majuma 70 yaligawanywa katika vipindi vitatu, yaani majuma 7 ya kwanza, halafu na majumba 62, kisha juma 1 la mwisho , kukamilisha majuma yote 70. Hatuna muda wa kueleza kwa urefu juu ya migawanyiko hiyo lakini biblia inasema lile juma la 69 litaishia na masihi (YESU KRISTO) kusulibiwa.

Danieli 9: 26 “Na baada ya yale majuma sitini na mawili, MASIHI ATAKATILIWA MBALI, naye atakuwa hana kitu; na watu wa mkuu atakayekuja watauangamiza mji, na patakatifu; na mwisho wake utakuwa pamoja na gharika, na hata mwisho ule vita vitakuwapo; ukiwa umekwisha kukusudiwa.”

Kisha linakuwa limebakia juma moja, ambalo ni sawa na miaka 7 tu ili kila kitu kiwe kimeisha.

Lakini juma hili la mwisho ukichunguza halikuendelea mara baada ya Kristo kusulibiwa, kwasababu kama lingeendelea basi mwisho ulipaswa uwe umeshafika miaka 7 tu mara baada ya kifo cha BWANA YESU, Lakini sasa tunaona imepitia takribani miaka 2000 na mwisho bado haujaja. Jambo ambalo halikuwahi kuonekana katika unabii wowote katika agano la kale. Jambo ambalo manabii wa Mungu hawakuliona wala kufunuliwa.

Na ndio maana hatupaswi kuacha kushukuru neema ya Kristo, kwasababu wokovu huu tunauona sasa ulipaswa uwe kwa WAYAHUDI tu peke yao watu wa Mungu. Jaribu kutengeneza picha kama mwisho ungefika ule wakati Kristo anaondoka duniani sisi wengine leo hii tungekuwa wapi?,Maana hata mitume wa Kristo walitazamia mwisho ungefika baada ya Bwana Yesu kufufuka..

Matendo 1:6 “ Basi walipokutanika, wakamwuliza, wakisema, JE! BWANA, WAKATI HUU NDIPO UNAPOWARUDISHIA ISRAELI UFALME?

7 Akawaambia, Si kazi yenu kujua nyakati wala majira, Baba aliyoyaweka katika mamlaka yake mwenyewe.

8 Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi.

9 Akiisha kusema hayo, walipokuwa wakitazama, AKAINULIWA, WINGU LIKAMPOKEA KUTOKA MACHONI PAO.”

Kama Bwana asingesema hayo,sisi watu wa mataifa tungekuwa waabudu mizimu, na masanamu, tungekufa na baada ya kufa moja kwa moja ni kuzimu, lakini ashukuruwe Mungu neema ile haikutupita ambayo ililetwa na BWANA WETU YESU KRISTO, ambaye katika ule wakati wa kusulibiwa kwake aliusitisha muda wa WAISRAELI kwanza, usiishe ili atukomboe sisi watu wa mataifa, kwa neema yake, Alituhurumia sisi kwa kulitenga lile juma moja kwanza lililosalia mpaka dunia kuisha, ili hapo katikati atukomboe sisi watu wa mataifa. Na ndio hii miaka 2000 sasahivi tuliyopo ya hii neema. Kwamba kwa kipindi cha miaka takribani 2000 tuingie ndani ya safina sisi watu wa mataifa.

Lakini ndugu fahamu pia hii neema haitadumu milele, tupo ukingoni sana na leo hii tutaona ni jinsi gani ilivyokaribu kuondoka kushinda hata sisi tunavyofikiri, na ikiondoka Mungu anamalizia lile juma 1 moja la mwisho lililobakia (yaani miaka 7) kwa wayahudi WATEULE wake tu!! kisha mwisho wa dunia unawasili. Ndugu ukilijua hilo hutafanya mchezo na wokovu wako sasa.

Mungu aliwapiga upofu makusudi wayahudi(Waisraeli) wasiupokee wokovu tangu wakati ule Kristo kusulibiwa ili sisi tuupate, kwasababu kama wangeupokea wokovu wa KRISTO wakati ule basi dunia ingekuwa imeshakwisha. Mungu aliwajeruhi wayahudi kwa ajili yetu, na ndio maana unaona sasa hivi wengi wao hawamwamini Yesu kama ndiye yule masiya waliokuwa wanamtazamia.. Ni kwasababu gani?, ni kwasababu Mungu alipiga mwenyewe upofu ili tu sisi tuokoke, Mungu aliwatia mwenyewe jeraha sio kwasababu wao walikuwa na dhambi nyingi kushinda sisi hapana, kinyume chake sisi ndio tuliokuwa na dhambi nyingi kuliko wao, lakini Mungu alifanya vile kutuhurumia sisi (yaani mimi na wewe) tufikilie wokovu. Soma kitabu cha Warumi sura ya 11 yote utaona jambo hilo.

Lakini pamoja na hayo tunasoma miaka mingi iliyopita Mungu aliwaahidi kuwarudia watu wake wateule wayahudi, baada ya kipindi fulani mbele, na kuwaimarisha tena. Na Ndio sasa tunasoma katika kitabu cha Hosea, yeye anasema:

HOSEA 6:1 Njoni, tumrudie Bwana; maana yeye amerarua, na yeye atatuponya; yeye amepiga, na yeye atatufunga jeraha zetu.

2 BAADA YA SIKU MBILI ATATUFUFUA; SIKU YA TATU ATATUINUA, NASI TUTAISHI MBELE ZAKE.

3 Nasi na tujue, naam, tukaendelee kumjua Bwana; kutokea kwake ni yakini kama asubuhi; naye atatujilia kama mvua, kama mvua ya vuli iinyweshayo nchi.

Umeyaelewa maneno hayo?, Huo unabii unawahusu wayahudi tu! {yaani waisraeli}, Hosea anasema njoni tumrudie Bwana, akiwaambia wayahudi wenzake katika Roho, baada ya SIKU MBILI atatufufua na siku ya tatu atatuinua, nasi tutaishi mbele zake.

Kama ukisoma biblia katika kitabu cha 2Petro 3:8 utafahamu kuwa kwa Mungu SIKU MOJA NI SAWA NA MIAKA 1000, Hivyo hapo utaona kuwa unabii unaweza ukatafsiriwa hivi “Njoni, tumrudie Bwana; maana yeye amerarua, na yeye atatuponya; yeye amepiga, na yeye atatufunga jeraha zetu. baada ya miaka 2000 atatufua na mwaka wa 3000 atatuinua”.

Ndugu tangu Kristo kuondoka hadi sasa, miaka 2000 inakaribia kuisha, na miaka ya hivi karibuni tutaanza wa 3000, na huo mwaka wa 3000 utakuwa ni milenia ya ule utawala wa miaka 1000 wa Yesu Kristo duniani (Ufunuo 20:4). Sasa kama hapo anavyosema atatufufa, atafunga jeraha zetu na kutuponya, hiyo inamaanisha kuwa huo ndio utakuwa ule wakati wa wayahudi kurudiwa na Mungu wao, kumaliza lile juma moja la mwisho lililokuwa limesalia (yaani miaka 7) ili dunia kuisha. Utakuwa ni wakati wa Israeli kurudishiwa ufalme kama walivyomuuliza Bwana siku ile kabla ya kupaa kwake.

Ndugu neema ikishalirudia Taifa la Israeli, unyakuo wa kanisa utakuwa umeshapita, kitakachokuwa kimebakia katika mataifa yote ulimwenguni ni MAJUTO NA MAOMBOLEZO, fikiri Bwana ametuhurumia kwa kipindi kirefu hichi chote ili mtu tu yeyote asiangamie lakini bado unaichekezea hii neema iliyopo kwa kitambo tu. Bwana aliposema kutakuwa na kilio na kusaga meno, alimaanisha kweli wala hakutudanganya. Miaka 2000 hii inaisha, Taifa la Israeli linazidi kunyanyuka siku baada ya siku, ule mwisho unakaribia, je! Umejiwekaje tayari sasa?. Kwanini bado unaichezea hii neema ya msalaba ambayo sisi hatukistahili kuipata?. Utajibu nini siku ile?. Au utajitetea vipi?.

Waebrania 2: 3 “SISI JE! TUTAPATAJE KUPONA, TUSIPOJALI WOKOVU MKUU NAMNA HII? AMBAO KWANZA ULINENWA NA BWANA, KISHA UKATHIBITIKA KWETU NA WALE WALIOSIKIA;”

Hizi ni saa za majeruhi kama hujakamilishwa katika wokovu fanya bidi sana, utubu, ubatizwe katika ubatizo sahihi wa maji tele na katika Jina la Yesu Kristo, upate ondoleo la dhambi zako, kisha udumu katika ushirika wa Kristo na mafundisho ya biblia angali siku ile inakaribia.

Kwasababu moja ya hizi siku dunia itakuwa imekwisha kabisa.

Ubarikiwe sana.

Tafadhali “share” kwa wengine ujumbe huu, na Mungu atakubariki.

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Nyinginezo:

NI KWA NAMNA GANI TUTASHINDA MAJARIBU?

JE! DAMU INA UMUHIMU WOWOTE KATIKA MAISHA??

ZIFAHAMU NYAKATI SABA ZA KANISA NA WAJUMBE WAKE SABA.

JE! MTU ANAPOFUNGA KWA MUDA WA SAA 24,ANAPASWA KUNYWA MAJI AU KITU CHOCHOTE?

JE! NI SAHIHI KUMUITA MARIA MAMA WA MUNGU?


Rudi Nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments