Imekuwa ni ngumu kwa watu wengi kuisikia sauti ya Mungu ikizungumza maishani mwao, hii ni kutokana na kwamba hawamjui wanayemwomba au, pengine jinsi walivyofundishwa na viongozi wao wa Imani, wakielezwa kuwa Mungu wakati wote akitasema na mtu huwa inasikika sauti kama ya mtu mwingine wa pili ndani yake akimpa maelekezo Fulani ya kufanya, na hali hiyo mtu haifikii mpaka atakapofikia kiwango Fulani cha kiroho…
Na ndio hapo utamwona mtu anapambana na kutumia nguvu nyingi kufikia hilo lengo la kusikia hiyo sauti ya Roho Mtakatifu ikizungumza naye ndani kama mtu Fulani, lakini kwa bahati mbaya anaishia kutokusikia chochote na mwisho wa siku kukata tamaa, akidhani kuwa Mungu hazungumzi naye na kumwona Mungu kama ni mgumu sana kufikika kirahisi… Lakini kumbuka Bwana anasema katika Neno lake.
Isaya 65: 12 “…….. NILIPOITA HAMKUITIKA; NILIPONENA, HAMKUSIKIA; bali mlitenda yaliyo mabaya machoni pangu, mlichagua mambo nisiyoyafurahia”.
Unaona hapo? Bwana anazungumza na kila mtu, ananena lakini hatusikii, anaita lakini sisi ndio hatuitiki, tatizo linakuja ni hatujui jinsi ya kuielewa sauti yake, tunataka Mungu azungumze kwa njia zetu sisi kama vile mtu anaongea na rafiki yake, lakini hatutaki yeye azungumze katika njia zake na hapo ndipo tunapomkosa. Njia pekee ambayo Mungu anatumia sikuzote kuzungumza na watu ni kwa kupitia Neno lake tu!, hivyo usipokuwa na Neno la Mungu ndani yako, ni ngumu kuielewa sauti ya Mungu,kwani ni kweli atazungumza na wewe lakini hautamwelewa hata kidogo..
Na ndio maana jambo la kwanza analolifanya Bwana kwa mtu, ni kulijaza Neno lake ndani yake ili atakapozungumza naye aweze kuisikia kiwepesi na kuielewa, tunaweza kuchukua mifano kadhaa ya maisha ya kawaida tu:
Inatokea mtu labda ni mwajiriwa, na amefanya kazi muda mrefu katika cheo cha kawaida tu,na amekuwa pengine akidharauliwa, au akichukiwa, au akinyanyaswa kazini hivyo akadhamiria kumwomba Mungu kwa machozi ampandishe cheo, amutoe mahali alipo na kumpandisha hatua moja zaidi, lakini mara tu alivyoomba hivyo, ndio kwanza mambo kazini yakazidi kubadilika na kuwa magumu zaidi, dharau zikaongezeka, manyanyaso yakazidi, chuki zikazidi kuongezeka na bado kazi zinazidi kuwa nyingi na akiangalia mshahara ni ule ule.
Sasa kwa namna ya kawaida huyu mtu,(Tumpe jina la Rachel) ni rahisi kusema moyoni mwake Mungu hasikii maombi yake, na Mungu hajajibu maombi, licha ya kufunga na kuomba kwa muda mrefu hakuna matokeo yoyote. Lakini kwasababu Neno la Mungu halijakaa ndani yake anaamua kughahiri na kusema Mungu hanisikii..
Lakini tujifunze wazo la Mungu juu ya Rachel lilikuwa ni lipi?
Tukirudi katika maisha ya Rachel ya nyumbani ya kawaida, ni mwanamke aliyeolewa na mume mmoja mkristo, anaishi na watoto wake wawili anaishi pia na kijakazi wake aliyemwajiri amsaidie kazi za nyumbani. Anawapenda na kuwajali sana watoto wake na mume wake lakini tatizo la Rachel lilikuwa ni moja, hakumjali sana mfanyakazi wake wa ndani, alikuwa akimwamsha asubuhi na mapema sana kabla yao kuamka, na kumpa majukumu ya kazi za nyumbani, na aliporudi nyumbani kutoka kazini akimkuta Yule kijakazi akiwa na baadhi ya shughuli hakumwacha apumzike hata kidogo, alimwongezea nyingine, na wakati Rachel na wanawe wanalala saa 3 usiku, Yule kijakazi wake aliendelea na kazi mpaka saa 5 usiku, licha ya kufanya kazi kwa muda mrefu hivyo Rachel hakulithamini hilo, wakati mwingine alikuwa akimkemea, na kumuudhi na zaidi ya yote hakutilia maanani suala la kumwongezea mshahara kwa wingi wa kazi alizompa. Lakini Yule kijakazi aliona ni haki yake kufanyiwa vile, wala hakuona vibaya wala kulalamika wala kuona kama anaonewa.
Sasa tukirudi katika maisha ya Rachel ya kazini kwake ndio tunamkuta anapitia hali kama ya Yule kijakazi wake nyumbani na hajui tatizo ni nini?. Boss wake hampendi, wakati mwingine anajitahidi kuonyesha bidii lakini hapandishwi mshahara..Lakini Kwasababu alifanya uamuzi wa busara kwenda kumwomba Bwana juu ya suala hilo, Bwana naye hakukawia kumjibu…Na majibu Bwana aliyompa ndio hayo; visa kazini kuwa vingi zaidi ya vile alivyokuwa navyo mwanzo, dharau kuongezeka, kuchukiwa na boss, wengine kupandishwa cheo na Rachel kubaki katika hali ile ile, n.k..
Lakini Rachel angetaka kujinyenyekeza zaidi na kutaka kulitafakari Neno la Mungu, angeelewa kuwa Mungu ameshamjibu, Alichopaswa kufanya ni kuchunguza matukio yaliyotokea baada ya yeye kuomba vile na kwa msaada wa Roho Mtakatifu angejua kuwa Mungu alimwambia maneno haya..
Mathayo 7:12 Basi yo yote myatakayo mtendewe na watu, nanyi watendeeni vivyo hivyo;
Na pia…
Luka 6: 38 “Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa; kipimo cha kujaa na kushindiliwa, na kusukwa-sukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa”.
Hiyo ilikuwa ni sauti ya Mungu kwa Rachel, Mungu kwa kuwa alimpenda, hivyo akamjibu kulingana na Neno lake, kwahiyo Rachel angeligundua lile haraka moja kwa moja angetubu, na kuacha kumwendesha na kamripia kijakazi wake vibaya, angeacha kumkemea pasipo sababu, angeacha kumdharau, angeacha kumshindilia kazi nyingi, mpaka saa za usiku wa manane, angempa muda mwingi wa kupumzika, angemwongeza mshahara kulingana na wingi wa kazi anazozifanya
Sasa bila kutumia nguvu nyingi angeanza kuona mabadiliko makubwa kazini ndani ya muda mfupi na yeye angeanza kufanyiwa kama anavyomfanyia kijakazi wake, Mungu atamfanyia fadhili ghafla anapandishwa cheo, kupendwa na watu waliokuwa wanamchukia, mara kaongezewa mshahara, mara anaanza kupendwa na mkubwa wake, anapata amani na watu wote,..kwasababu lile neno Bwana alilosema.
“. Kwa kuwa kipimo kile kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa”. Linatimia juu yake, Hivyo Mungu ni lazima ahakikishe Neno lake linatimia katika kazi yake. Na majibu ya maombi yake anayaona wazi.
Mfano mwingine utakuta Dada mwingine umri wake umeenda, kila mwanamume atakayemwona anamkimbia, anaona wengine wanaolewa hata walio wadogo kuliko yeye, lakini yeye anapitwa tu, kwahiyo anaamua kufanya uamuzi wa busara kumwomba Mungu ampe mume mzuri, ambaye atakuwa anajitambua, mcha Mungu, na anayejiheshimu na mwenye upendo na malengo.
Hivyo baada ya maombi hayo ya kina muda mfupi tu baadaye anakutana na mahubiri yanayolenga mwenendo wa mwanamke, na ndani ya mahubiri hayo anasikia mada ihusuyo uvaaji wa mwanamke umependezao Mungu, anasikia ndani yake ni machukizo kwa Mungu mwanamke kuvaa suruali na vimini na kaptura, haipendezi mbele za Mungu mwanamke wa kikristo kuweka mawigi, na lipstick,na wanja, anasikia Neno linalosema..
1 Timotheo 2: 9 “Vivyo hivyo wanawake na wajipambe kwa MAVAZI YA KUJISITIRI, pamoja na adabu nzuri, na moyo wa kiasi; si kwa kusuka nywele, wala kwa dhahabu na lulu, wala kwa nguo za thamani; 10 bali kwa matendo mema, kama iwapasavyo wanawake wanaoukiri uchaji wa Mungu.”
1 Timotheo 2: 9 “Vivyo hivyo wanawake na wajipambe kwa MAVAZI YA KUJISITIRI, pamoja na adabu nzuri, na moyo wa kiasi; si kwa kusuka nywele, wala kwa dhahabu na lulu, wala kwa nguo za thamani;
10 bali kwa matendo mema, kama iwapasavyo wanawake wanaoukiri uchaji wa Mungu.”
Sasa kwasababu pengine mwanamke yule hajajifunza kusikia sauti ya Mungu jinsi inavyozungumza, moja kwa moja anapuuzia lile Neno na kuendelea na maisha yake ya uvaaji usiompendeza Mungu, wakati muda huo huo unakuta kuna mwanamume mahali Fulani Mungu kamweka mwenye vigezo vyote anavyovihitaji, lakini Yule mwanaume ni mkristo anasubiri Mungu amletee mwanamke mwenye vigezo vya usafi wa mwili na utakatifu, mwenye kujisitiri, asiyefanana na wanawake wa ulimwengu huu.
Sasa kwasababu Yule dada hana Neno la Mungu ndani yake kujua kwamba ile ni sauti ya Mungu, inayotaka kumtengeneza kumwandaa kumpata mume anayemuhitaji, anadharau anaona wanaohubiriwa yale ni wanawake waliokosa mwelekeo..Hivyo anajikuta anamkosa yule mwanamume na kuendelea katika hali hiyo hiyo ya kutokuolewa kwa muda mrefu na hata akiolewa ataoloewa na mtu ambaye hana vile vigezo anavyovitaka…Shida ni kwamba hajaielewa sauti ya Mungu ilipokuwa inasema naye.
Kadhalika unakuta mwingine ni mgonjwa pengine ana ugonjwa usiotibika labda HIV, Ikafikia wakati akahitaji Mungu amponye ugonjwa wake, aliomba kwa imani akijua kabisa Mungu kamsikia maombi yake, hivyo akaenda huku na kule kwa mtumishi huyu mpaka mtumishi Yule, kutoka taifa hili mpaka taifa lile, kutafuta uponyaji wake alifanya hivyo kwa muda mrefu lakini hakuona matokeo yoyote ya kupona ugonjwa wake. Mwisho wa siku akaamua kukata tamaa na kusema moyoni mwake Mungu hasikii wala hajibu maombi.
Lakini ukirudi nyuma ya maisha ya huyu mtu, siku ile ile alipoomba Mungu amponye, Mungu alimsikia, baada ya siku chache alifungua redio akasikia mahubiri yanayosema “chanzo cha mambo yote ni dhambi,” Chanzo cha magonjwa ni dhambi, chanzo cha kifo ni dhambi n.k… Hivyo akasikia mafundisho hayo na kweli yakamchoma moyo, na aliposikia kwamba atubu kwa kumaanisha kuacha dhambi kabisa, akabatizwe kwa jina lake Yesu Kristo apate ondoleo la dhambi zake, na kumwishia Mungu katika maisha ya utakatifu, hakutakuwa na jambo lolote au mlima wowote utakaosimama mbele yake, kwasababu waliomwamini yeye wamepewa amri zote za kukanyaga, nge, na nyoka na nguvu zote za Yule mwovu,..
Lakini yeye aliposikia habari za toba, za kuacha uasherati, kuacha rushwa, kuacha sigara, usengenyaji, n.k. akadhani kuwa yale ni mahubiri tu ya siku zote ya walokole pasipo kujua kuwa ile ni sauti ya Mungu inayotaka kumpeleka katika kupokea uponyaji wake.
Laiti angekuwa na Neno la Mungu ndani yake, angefahamu kuwa biblia inasema katika Mithali 3: 7 ”…..Mche Bwana, ukajiepushe na uovu. 8 Itakuwa afya mwilini pako, Na mafuta mifupani mwako”.
Yeremia 30: 17 “Maana nitakurudishia afya, nami nitakuponya jeraha zako, asema Bwana,…”
Wakati mwingine magonjwa yanakuwa ya kimaagano na hayawezi kuondoka kama mtu hajaamua kwanza kuvunja maagano hayo na kuingia katika agano jipya la damu ya YESU. Watu wengi wanamkimbilia Mungu awaponye, awainue, awafundishe, lakini hawajui kanuni za Mungu za kuzungumza na wanadamu, wao wanataka wajibiwe tu kama wanavyotaka wao. Hapana Mungu haendi hivyo, siku zote Mungu yupo katika Neno lake. Na huko ndipo utakapoweza kuisikia sauti ya Mungu. Mahali pengine popote kwako itakuwa kama ngurumo tu. Kama wewe sio mkristo (nikimaanisha Mkristo wa kweli aliyesimama na Bwana na Neno la Mungu limejaa ndani yako ) kamwe hutaweza kuisikia sauti ya Mungu ikisema na wewe, utaomba kila siku hutaona chochote, utafunga na kulia hutapata chochote, tatizo sio Mungu tatizo ni wewe..Sikiliza Mungu anavyosema..
Isaya 66: 4 “Mimi nami nitachagua mapigo yao, nitaleta hofu zao juu yao; kwa sababu nilipoita, hawakuitika; na niliponena, hawakusikia; bali walifanya yaliyo maovu machoni pangu, NA KUYACHAGUA NISIYOYAFURAHIA”.
Hivyo ndugu isikie sauti ya Mungu leo inayozungumza na wewe sasahivi, unataka kwenda katika unyakuo?? Tubu! dhambi zako ukaoshwe kwa damu ya Yesu, na kuishi maisha matakatifu. Unataka kuponywa?? Acha dhambi!.. unataka kufunguliwa?? Acha uasherati!!, acha kutazama Pornography, acha ulevi, acha sigara, acha usengenyaji, acha wizi, acha rushwa, acha uvaaji mbovu kama wanawake wa kidunia,..Acha kutazama vitu visivyokuwa na faida yoyote katika maisha yako ya kiroho badala yake anza sasa kujifunza Neno la Mungu ili atakapozungumza na wewe usikie, pale anapokujibu uelewe. Ndugu maombi hayajibiwi kwa mafuta ya upako, wala maji, wala chumvi, Mungu atakujibu na kukufungua kwa NENO LAKE TU!!! Na si kingine.
Mungu akubariki.
Kwa mawasiliano/ Maombezi/Ushauri/ Piga:+255693036618/ +255789001312
Tafadhali “share” kwa wengine ujumbe huu.
Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mada Zinazoendana:
IELEWE SAUTI YA MUNGU.
USIPOLITENDEA KAZI NENO LA MUNGU.
SAUTI AU NGURUMO?
UPENDO NI NINI NA JE! KUNA AINA NGAPI ZA UPENDO?
TOA HUDUMA ILIYO BORA.
Rudi Nyumbani
Print this post
Asante mtumishi ubarikiwe mno
ahsante ubarikiwe mtumishi
Asante kwa mafundisho…
Amen sana kwa somo zuri naona kupiga hatua katika kumjua Mungu na njia zake za kusema na mimi hasa kwa Neno lake, lakini kuna watumishi wanasema kuwa kuna sauti ya Mungu kama sauti ndani ya mtu na wengine wanasema ndoto, imekaaje hii hasa ndoto??
Amen Bwana azidi kutubariki sote
God bless you mtu wa Mungu
Amen. Ubarikiwe nawe pia.
MUNGU akubariki
ASANTE SANA KWA NENO ZURI’ MAFUNDISHO MAZURI’ YAMENIJENGA KIROHO.
Kwa mara ya kwanza natoa comment kwa post hizi za Google kiukweli nimejifunza kitu kikubwa sana Mungu akubariki sana. 🙏🙏
Amen nawe pia ubarikiwe
Asante Sana Kwa ujumbe huu. Nimepata kitu kikubwa Sana. Barikiwa.
Amen nawe pia ubarikiwe.
Asante kwa ujumbe mzuri
nimejifunza kitu kikubwa Mungu akubariki sana mtumishi kwa ujumbe huu mzuri.
Amen ubarikiwe na Bwana…
Ahsante kwa ujumbe mzuri sana.
Mungu akubariki mtumishi wa Mungu.
Amen nawe pia ubarikiwe ndugu yetu.