MAMBO YA KUJIFUNZA KATIKA WARAKA WA TATU WA YOHANA.

MAMBO YA KUJIFUNZA KATIKA WARAKA WA TATU WA YOHANA.

Katika Kitabu hichi tunaona Mtume Yohana akiandika barua, kwa mtu, barua ya kumtakia mafanikio katika mambo yake yote, pamoja na afya njema, Hii ni barua ya kipekee sana mbali na barua nyingine zote tunazozijua za mtume Yohana ambazo aliziandika kwa makanisa, mfano ile ya ufunuo wa Yohana n.k.

Hii ilihusu kumtakia mtu mafanikio, katika Nyanja zote za maisha yake, ikiwemo kazi zake za mikono, biashara zake, miradi yake, elimu yake kama alikuwa nayo, mali zake, mipango yake, familia yake n.k…Na Zaidi ya yote katika upande wa afya, awe nayo tele..Ni wazi kabisa waraka huu ni wa faraja sana ambao hata sasa tunapenda kuutumia watu wengi, kumkumbusha Mungu kwamba alisema katika Neno lake “MPENZI NAOMBA UFANIKIWE KATIKA MAMBO YOTE NA KUWA NA AFYA YAKO, KAMA VILE ROHO YAKO IFANIKIWAVYO.”

Lakini ni muhimu tujifunze kitu, kabla Mtume Yohana hajazitoa hizo Baraka zote kwa uweza wa Roho wa Mungu je! ni kitu gani kilichomsukuma yeye kusema vile?.

Na ndio maana tunasoma mwanzoni tu wa nyaraka, kabla hajaeleza jambo lingine lolote alitoa kwanza mwongozo ule waraka unamuhusu nani, na ndio tunaona hapo anamtaja mtu mmoja anayeitwa GAYO. Kwamba waraka ule ulimuhusu yeye.

Tusome:

1Yohana 1“Mzee, KWA GAYO MPENZI, nimpendaye katika kweli.

2 Mpenzi naomba ufanikiwe katika mambo yote na kuwa na afya yako, kama vile roho yako ifanikiwavyo”.

Kama tunavyosoma waraka huu hakuandikiwa kila mtu, kama nyaraka nyingine zilivyokuwa, haukuandikwa kwa kila mkristo, kama nyaraka nyingine zilivyokuwa, Kumbuka zipo nyaraka zilikuwa zimeandikwa kwa watu wote, kama vile waraka wa Yuda,na wa Petro, na Waraka wa kwanza wa Yohana, kadhalika zipo zilizokuwa zimeandikwa kwa wakristo tu kwamfano Wakorintho, wagalatia, wakolosai, warumi,ufunuo n.k. na zipo pia zilizokuwa zimeandikwa kwa watu maalumu {yaani mtu mmoja mmoja} mfano wa nyaraka hizo ni waraka wa Timotheo, Filemoni,Tito, 2Yohana, na waraka wa tatu wa Yohana ambao ndio huu sasa unaomuhusu mtu mmoja anayeitwa GAYO.

Wengi tunaupenda huu waraka lakini tunashindwa kufahamu uliandikwa kwa nani, kumbuka haukuandikwa kwa watu wote, bali kwa mtu mmoja anayeitwa Gayo. Hivyo ili kwamba Baraka zile zilizoandikwa katika waraka ule zitufikie na sisi tunapaswa tufanane na huyu mtu anayeitwa GAYO vinginevyo hata tukidai vipi kwamba ni za kwetu, lakini ukweli ni kwamba haziwezi kuwa za kwetu, hazitatuhusu kabisa.

Sasa Ni vizuri tukimsoma huyu GAYO alikuwa ni mtu mwenye TABIA GANI tusome.

3 Yohana 1“ Mzee, kwa Gayo mpenzi, nimpendaye katika kweli.

2 Mpenzi naomba ufanikiwe katika mambo yote na kuwa na afya yako, kama vile roho yako ifanikiwavyo.

3 Maana nalifurahi mno walipokuja ndugu na kuishuhudia kweli yako, kama uendavyo katika kweli.

4 Sina furaha iliyo kuu kuliko hii, kusikia ya kwamba watoto wangu wanakwenda katika kweli.

5 MPENZI, KAZI ILE NI YA UAMINIFU UWATENDEAYO HAO NDUGU NA HAO WAGENI NAO,

6 WALIOKUSHUHUDIA UPENDO WAKO MBELE YA KANISA; UTAFANYA VIZURI UKIWASAFIRISHA KAMA IPASAVYO KWA MUNGU.

7 KWA MAANA, KWA AJILI YA JINA HILO, WALITOKA, WASIPOKEE KITU KWA MATAIFA.

8 Basi imetupasa sisi kuwakaribisha watu kama hao, ili tuwe watenda kazi pamoja na kweli.

9 Naliliandikia kanisa neno, LAKINI DIOTREFE, APENDAYE KUWA WA KWANZA KATI YAO, HATUKUBALI.

10 Kwa hiyo, nikija, nitayakumbuka matendo yake atendayo, atoavyo upuzi juu yetu kwa maneno maovu; wala hatoshwi na hayo, ILA YEYE MWENYEWE HAWAKARIBISHI HAO NDUGU, NA WALE WATAKAO KUWAKARIBISHA, HUWAZUIA, NA KUWATOA KATIKA KANISA.

11 Mpenzi, usiuige ubaya, bali uige wema. Yeye atendaye mema ni wa Mungu, bali yeye atendaye mabaya hakumwona Mungu.

12 DEMETRIO ameshuhudiwa na watu wote, tena na ile kweli yenyewe. Nasi pia twashuhudia, nawe wajua ya kwamba ushuhuda wetu ni kweli.

13 Nalikuwa na mambo mengi ya kukuandikia, lakini sipendi kukuandikia kwa wino na kalamu.

14 Lakini nataraji kukuona karibu, nasi tutasema uso kwa uso. [15] Amani kwako. Rafiki zetu wakusalimu. Wasalimu hao rafiki zetu, kila mtu kwa jina lake”.

Ukisoma kwa makini utagundua kwanini GAYO alistahili kutamkiwa maneno ya Baraka kama yale, kwanza utagundua kuwa alikuwa ni mtu mwenye huruma juu ya kazi ya Mungu, pale alipoona kuna uhitaji wa injili kupelekwa mbele, alijitoa kikamilifu kuichangia kazi ya Mungu, kwa kuwasafirisha wale watumishi wa Mungu kuipeleka injili kila mahali palipohitajika pasipo kujali kupungukiwa kwa namna yoyote,tofauti na wakristo wengi waliokuwepo katika makanisa yale na zaidi ya yote alikuwa anawakaribisha pia wageni (wakristo) waliokuwa wanatoka mbali kwa ajili ya kwenda kuifanya kazi ya Mungu.

Ilifikia mpaka hatua wale wote waliokuwa wanaifanya kazi ya Mungu ambao walikuwa katika maeneo yale aliwasaidia kiasi kwamba wakawa hawana uhitaji wowote kutoka kwa watu wasioamini, yeye aliwahudumia kwa vyote, unaweza kutengeneza picha hakukuwa na kikwazo chochote cha kifedha na kimazingira kilichokwamisha kazi ya Mungu maeneo yale, alifanya hivyo kwa bidii mpaka sifa zake zikavuma katika makanisa yote ya Kristo, na habari kumfikia Mtume Yohana.

Lakini wakati huo huo pia alikuwepo mtu mwingine aliyeitwa DIOTREFE, yeye hakuwa kama Gayo, alimwona Gayo kama anapoteza mali nyingi, kwa kazi isiyokuwa na maana au faida, ya kuwachangia wengine katika kuipeleka Injili. Aliona kuwa ni jambo lisilokuwa na maana kuwakaribisha wageni watu wasiowajua katika makanisa yao, na Zaidi ya yote alikuwa anawafukuza wageni wa kikristo waliotoka mbali kuja kujumuika nao, aliona wote waliofanya hivyo hawana mipango rasmi ya maisha yao, aliwaona kama wana fedha za kuchezea, Ni wazi kuwa Diotrefe alikuwa ni kikwazo cha Injili ya Kristo kwenda mbele. Huku akijifanya kuwa ndiye kiongozi..Lakini ni kiongozi ambaye hakupenda kujitoa kwa Mungu, mfano wa viongozi wengi waliopo leo.

Na ndio hapo tunaona waraka huu mtume Yohana anamwandikia GAYO peke yake aliyekuwa mwaminifu kwa kujitoa na kuokujali nafsi yake peke yake kwa ajili ya injili.. Tunasoma alianza tu na kumwambia.. “ Mpenzi naomba ufanikiwe katika mambo yote na kuwa na afya yako, kama vile roho yako ifanikiwavyo”. Maneno ya faraja kiasi gani!!

Unaona hapo baada ya wema wake kujulikana na taabu yake katika kujitoa katika kazi za Mungu, kudhihirika ndipo hapo Baraka nyingine zote zikafuata juu yake. Ni kwa vile biblia haiwezi kuandika kila kitu, lakini ni wazi kabisa Gayo kuanzia ule wakati alibarikiwa kwa namna isiyo ya kawaida, pengine alikuwa na shamba moja tu Mungu akampa 10, pengine alikuwa na nyumba 1 yenye vyumba vinne, alivyovifanya viwili vya kwake na vilivyosalia vya wageni, lakini Mungu alimwongezea nyumba nyingi nyingi, na mali na Zaidi ya yote, alipata afya njema na maisha marefu yenye heri yeye pamoja na familia yake yote. Alikuwa ni mfano wa Ayubu katikati ya jamii ya wakristo waliokuwepo wakati ule.

Lakini wengi wetu tunashindwa kufahamu kanuni za Mungu za kubarikiwa, Tunapenda kwenda kuombewa huku na kule, tunatoka kwa mtumishi huyu mpaka huyu, tunatamka haya maneno kila siku midomoni mwetu, Lakini bado tunaona hali ni ile ile, au matokeo ni machache.. Ni muhimu kujua kabla hatujamwomba Mungu atufanyie kitu Fulani tuangalia na vigezo vilivyowekwa nyuma yake ya kupata hicho kitu, vinginevyo tutaona kama Neno la Mungu ni uongo kwetu.

Leo hii unaona kazi ya Mungu katika kusanyiko lako inauhitaji Fulani, injili ya Kristo ili iende mbele kwa njia ya kupelekea wahubiri au vitabu, n.k. changia bila kujali itakugharimu kiasi gani,fadhili kwa chochote ulichonacho, wewe timiza tu wajibu wako kwasababu aliye juu anakuona. 

Unaona kazi ya Mungu mahali Fulani inakwama kwasababu imekosa ujuzi unaofanana na wa kwako ili iendelee, tumia huo ujuzi wako kurekebisha hilo eneo kwa bidii sana, na sifa zako zitavuma mbinguni..Siku moja hilo Neno “Mpenzi naomba ufanikiwe katika mambo yote” litatamkwa juu yako pasipo hata wewe kujua, na ndipo Mungu atakapokufanikisha katika mambo yako yote na kukupa afya yako..FANYIKA GAYO KUANZIA LEO. Kumbuka Baraka zile zinamhusu GAYO peke yake.

Kuna kipindi wana wa Israeli waliacha kuijenga nyumba ya Mungu na kila mmoja akaenda shambani mwake kufanya mambo yake mwenyewe, pasipokujali nyumba ya Mungu imekaa katika hali gani, Jambo hilo lilimuhuzunisha sana Bwana mpaka akaamua kuwapiga kwa taabu na shida na uhaba wa vitu pasipo hata wenyewe kujua…Ndipo Bwana akawatumia Nabii Hagai na kuwaambia maneno haya.

Hagai 2: 2 “Bwana wa majeshi asema hivi, ya kwamba, Watu hawa husema, Huu sio wakati utupasao kuja, huu sio wakati wa kujenga nyumba ya Bwana.

3 Ndipo neno la Bwana lilikuja kwa kinywa cha nabii Hagai, kusema,

4 Je! Huu ndio wakati wa ninyi kukaa katika nyumba zenye mapambo ya mbao, iwapo nyumba hii inakaa hali ya kuharibika?

5 Basi sasa, Bwana wa majeshi asema hivi, Zitafakarini njia zenu.

6 Mmepanda mbegu nyingi mkavuna kidogo; mnakula lakini hamshibi; mnakunywa lakini hamkujazwa na vinywaji; mnajivika nguo lakini hapana aonaye moto; na yeye apataye mshahara apata mshahara ili kuutia katika mfuko uliotoboka-toboka.

7 Bwana wa majeshi asema hivi, Zitafakarini njia zenu.

8 Pandeni milimani, mkalete miti, mkaijenge nyumba; nami nitaifurahia, nami nitatukuzwa, asema Bwana.

9 MLITAZAMIA VINGI, KUMBE VIKATOKEA VICHACHE; tena mlipovileta nyumbani nikavipeperusha. NI KWA SABABU GANI? Asema Bwana wa majeshi. NI KWA SABABU YA NYUMBA YANGU INAYOKAA HALI YA KUHARIBIKA, WAKATI AMBAPO NINYI MNAKIMBILIA KILA MTU NYUMBANI KWAKE.

10 Basi, kwa ajili yenu mbingu zimezuiliwa zisitoe umande, nayo nchi imezuiliwa isitoe matunda yake.

11 Nami nikaita wakati wa joto uje juu ya nchi, na juu ya milima, na juu ya nafaka, na juu ya divai mpya, na juu ya mafuta, na juu ya kila kitu itoacho nchi, na juu ya wanadamu, na juu ya wanyama, na juu ya kazi zote za mikono”.

Unaona hapo? Maombi yangu ni kwamba Bwana atufanye sote kuwa GAYO leo. Ili zile Baraka zote zilizoandikwa pale zisitupite.

Ubarikiwe.

Tafadhali “share” ujumbe huu kwa wengine.

Kwa maombezi/ Ushauri/ Ratiba za Ibada/Maswali/ Whatsapp/ Piga namba hizi: +255693036618/ +255789001312

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

 

Mada Nyinginezo:

KANUNI RAHISI YA KUFANIKIWA.

YESU MPONYAJI.

AMIN! NAWAAMBIA KIZAZI HIKI HAKITAPITA

YONA: MLANGO 1

NJONI, NUNUENI MLE NA MNYWE.

JIFANYIE RAFIKI KWA MALI YA UDHALIMU.


Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
7 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
JUZAN
JUZAN
1 year ago

Je mfalme Suleimani alikua na watoto wangapi?

CLEVEN GEORGE NASSARY
CLEVEN GEORGE NASSARY
2 years ago

Nina swali jingine mtumishi,Je ni kweli Mfalme Sulemani alizaa na Malkia wa Sheba?

Cleven Nassary
Cleven Nassary
2 years ago

Shalom Mtumishi wa Bwana,samahani naomba kuuliza hivi ni sahihi kwa msanii wa nyimbo za injili kumshirikisha msanii wa nyimbo za kidunia katika nyimbo au kushirikishwa na msanii wa nyimbo za kidunia katika nyimbo

lucas mhula
lucas mhula
2 years ago

Amen🙏🙏