YONA: Mlango 1

YONA: Mlango 1

Yona alikuwa mmoja wa manabii wa Israeli wakati wa utawala wa Yeroboamu Mfalme wa Israeli, ambaye Mungu alimtumia sana kutoa unabii kadha wa kadha katika Israeli, kama tunavyomsoma katika (2Wafalme 14:21-25). Lakini ilifika wakati BWANA akataka kumtuma kwa watu wa Mataifa, Mji wa NINAWI uliokuwa mji mkuu wa Taifa la ASHURU ambalo kwa wakati ule lilikuwa ni moja ya ngome yenye nguvu duniani ndilo lililokuja baadaye kuhusika kuwachukua wana wa Israeli utumwani (2Wafalme 18:11), Mataifa mengine yakiwemo BABELI pamoja na MISRI. Kumbuka taifa la Ashuru liliyachukua yale makabila 10 na kuyapeleka Ashuru, na makabila mawili ya Israeli yaliyosalia (Yaani YUDA na BENYAMINI) Mfalme Nebukadneza, alikuja kuyachukua utumwani Babeli.

Hivyo mji wa NINAWI uliokuwa mji mkuu katika Ashuru ulijaa maovu mengi sana, mfano wa Sodoma na Gomora, mpaka kufikia wakati Bwana kutaka kuuangamiza mji wote na watu wote waliokuwepo kule, lakini Mungu alivyo wa rehema hawezi kufanya jambo lolote kabla hajawaonya kwanza watu wake, ili pengine waghahiri uovu wao wasiangamizwe, na ndivyo alivyofanya kwa kumtuma YONA nabii katika mji ule Mkubwa uliokuwa mbali sana na taifa la Israeli.

Lakini tunasoma habari haikuwa hivyo kwa nabii YONA, badala ya kwenda NINAWI mji wa ASHURU alioagizwa na Bwana, yeye akaamua kuubuni mji wake yeye alioupenda ili akakae huko, ndipo akakimbilia TARSHISHI mji uliokuwa nchi ya Lebanoni ili tu AJIEPUSHE NA MAPENZI YA MUNGU.

Lakini alisahau kuwa ili afikie malengo yake hana budi kupitia “NJIA YA BAHARI”.. Hivyo akaamua kupanda Merikebu zinazoelekea Tarshishi, Na kama tunavyosoma habari alipokuwa katikati ya safari yake bahari ilichafuka na mambo yakaanza kuharibika..

 
Yona 1: 4 “Lakini Bwana alituma upepo mkuu baharini, ikawa tufani kubwa baharini, hata merikebu ikawa karibu na kuvunjika.

5 Basi wale mabaharia wakaogopa, kila mtu akamwomba mungu wake; nao wakatupa baharini shehena iliyokuwa merikebuni, ili kuupunguza uzito wake. Lakini Yona alikuwa ameshuka hata pande za ndani za merikebu; akajilaza, akapata usingizi.

6 Basi nahodha akamwendea, akamwambia, Una nini, Ewe ulalaye usingizi? Amka, ukamwombe Mungu wako; labda Mungu huyo atatukumbuka, tusipotee.

7 Wakasemezana kila mtu na mwenzake, Haya, na mpige kura, mpate kujua mabaya haya yametupata kwa sababu ya nani. Basi wakapiga kura, nayo kura ikamwangukia Yona.

8 Ndipo wakamwambia, Tafadhali utuambie, wewe ambaye mabaya haya yametupata kwa sababu yako; kazi yako ni kazi gani? Nawe umetoka wapi? Nchi yako ni nchi ipi? Nawe u mtu wa kabila gani?

9 Akawaambia, Mimi ni Mwebrania; nami namcha Bwana, Mungu wa mbingu, aliyeziumba bahari na nchi kavu.

10 Ndipo watu wale wakaogopa mno, wakamwambia, Ni jambo gani hili ulilolitenda! Kwa maana watu wale walijua ya kuwa amekimbia, ajiepushe na uso wa Bwana, kwa sababu alikuwa amewajulisha.

11 Basi wakamwambia, Tukutende nini, ili bahari itulie? Kwa maana bahari ilikuwa inazidi kuchafuka.

12 Naye akawaambia, Nikamateni, mnitupe baharini; basi bahari itatulia; kwa maana najua ya kuwa ni kwa ajili yangu tufani hii imewapata.

13 Lakini wale watu wakavuta makasia kwa nguvu, ili wapate kurudi pwani, wasiweze; kwa maana bahari ilizidi kuwachafukia sana.

14 Basi wakamlilia Bwana, wakasema, Twakuomba, Ee Bwana, twakuomba, tusiangamie kwa ajili ya uhai wa mtu huyu, wala usitupatilize kwa ajili ya damu isiyo na hatia; kwa maana wewe, Bwana, umefanya kama ulivyopenda.

15 Basi wakamkamata Yona, wakamtupa baharini, nayo bahari ikaacha kuchafuka.

16 Ndipo wale watu wakamwogopa Bwana mno, wakamtolea Bwana sadaka, na kuweka nadhiri.

17 Bwana akaweka tayari samaki mkubwa ili ammeze Yona, naye Yona akawa ndani ya tumbo la samaki yule muda wa siku tatu, mchana na usiku”.

Basi wakamkamata  nabii Yona, wakamtupa baharini, nayo bahari ikaacha kuchafuka.

Bwana aliyaruhusu yote haya yampate YONA ili kutuonya sisi kwamba tusipotaka kuenda katika njia ambayo Mungu kaikusudia tuiendee,yatatukuta kama hayo hayo. Kama biblia inavyosema
 
1Wakoritho 10: 11 “Basi mambo hayo yaliwapata wao kwa jinsi ya mifano, yakaandikwa ILI KUTUONYA SISI, tuliofikiliwa na miisho ya zamani. Kwa hiyo anayejidhania kuwa amesimama na aangalie asianguke.”
 

SWALI NI JE! NJIA YA BAHARI NI SALAMA?

Kibiblia BAHARI inawakilisha nini?…Ili kufahamu jambo hili ni vizuri tujue ni kitu gani kimo humo ndani yake .tukisoma. 

Ufunuo 13: 1 “KISHA NIKAONA MNYAMA AKITOKA KATIKA BAHARI, mwenye pembe kumi, na vichwa saba, na juu ya pembe zake ana vilemba kumi, na juu ya vichwa vyake majina ya makufuru.

2 Na yule mnyama niliyemwona alikuwa mfano wa chui, na miguu yake ilikuwa kama miguu ya dubu, na kinywa chake kama kinywa cha simba, yule joka akampa nguvu zake na kiti chake cha enzi na uwezo mwingi.”

Unaona hapo?.

Kumbuka YONA anawakilisha kundi la wakristo wasiotaka kudumu katika mapenzi ya Mungu (yaani VUGUVUGU).leo wanaenda na Mungu, kesho wanaenda katika akili zao, leo anafanya ibada kesho anakula rushwa. N.k. Sasa Kama vile  nabii YONA alivyokimbia uso wa Mungu na kuelekea njia ya BAHARINI na hatimaye kumezwa na yule SAMAKI MKUBWA, vivyo hivyo na kundi hili la wakristo wasiotaka kutengeneza mambo yao sasa vizuri na Mungu, hawajui kama wanakimbilia baharini pasipo wao kujua, ambapo kule kuna Yule mnyama mwenye vichwa saba na pembe kumbi ameandaliwa kuwameza.

Na bahari inawakilisha nini?

Tukirudi kusoma Ufunuo 17: 15 Kisha akaniambia, YALE MAJI ULIYOYAONA, hapo aketipo yule kahaba, ni jamaa na makutano na mataifa na lugha.” Kumbuka huyu kahaba anayezungumziwa hapa ameketi juu ya Yule mnyama aliyetoka baharini ambaye tumemsoma katika Ufunuo 13.

Kwahiyo bahari au maji mengi inawakilisha mahali penye mkusanyiko wa watu wengi, hivyo Yule mnyama anatoka mahali penye mkusanyiko wa watu wengi, mahali ambapo amekubaliwa na wengi, tukizungumza katika roho leo hii mfumo wa mpinga-kristo unatenda kazi katikati ya mataifa, na dini nyingi za uongo.

Kama vile Yona alivyoiacha njia ya Mungu na kuchagua Njia ya BAHARI akidhani kuwa ni salama, vivyo hivyo na wakristo wa leo walio vuguvugu, wanamsahau Mungu na kushikimana na mambo maovu ya ulimwengu huu, nabii Yona alisinzia pale alipoona kuna utulivu mwanzoni mwa safari yake, kadhalika kundi hili la wakristo vuguvugu wanasinzia kwasababu wanajiona wapo salama, wanaona hata wakifanya hivyo hakuna dhara lolote wanatakalolipata lakini hawajui kuwa kuna mnyama ameshaandaliwa kwa ajili yao chini ya Merikebu yao. Pale PEPO zitakapovuma ndipo watakapotambua kwamba hawapo salama, wakati huo unyakuo umeshapita, ndugu unajiona upo salama katika ulimwengu, hata ukitenda dhambi unaona hakuna dhara lolote linalokupata, angali unafahamu kabisa moyoni mwako umeukimbia uso wa Mungu na unayoyafanya sio sahihi na bado unajiita Mkristo, hujui kwamba ni NEEMA ya Mungu tu, imekushikilia dhidi ya Yule Mnyama utubu, ugeuze njia uepuke madhara yaliyopo mbeleni ambayo yapo karibuni kuupata ulimwengu mzima. Ipo siku NEEMA inayokushikilia itakwisha na moja ya siku hizi PEPO ZITAANZA KUVUMA BAHARINI. Kama biblia inavyosema katika..

Danieli 7: 1 “Katika mwaka wa kwanza wa Belshaza, mfalme wa Babeli, Danieli aliona ndoto, na maono ya kichwa chake, kitandani mwake; basi akaiandika ndoto, akatoa habari ya jumla ya mambo hayo.

2 Danieli akanena, akisema, Naliona katika maono yangu wakati wa usiku; na tazama, HIZO PEPO NNE ZA MBINGUNI ZILIVUMA KWA NGUVU JUU YA BAHARI KUBWA.

3 Ndipo wanyama wakubwa wanne wakatoka baharini, wote wa namna mbalimbali”………

Wanyama hao Nabii Danieli alionyeshwa, watatu wa kwanza walishapitia na Yule wa mwisho wanne, ndiye aliyeko sasa chini ya MERIKEBU(NEEMA), na moja ya hizi siku pepo zitamwamsha kutenda kazi tukiendelea kumsoma:

“7 Baadaye nikaona katika njozi ya usiku, na tazama,MNYAMA WA NNE, mwenye kutisha, mwenye nguvu, mwenye uwezo mwingi, naye alikuwa na meno ya chuma, makubwa sana; alikula na kuvunja vipande vipande, na kuyakanyaga mabaki kwa miguu yake; na umbo lake lilikuwa mbali kabisa na wale wa kwanza, naye alikuwa na pembe kumi.

8 Nikaziangalia sana pembe zake, na tazama, pembe nyingine ikazukia kati yao, nayo ilikuwa ndogo, ambayo mbele yake pembe tatu katika zile za kwanza zikang’olewa kabisa; na tazama, katika pembe hiyo mlikuwa na macho kama macho ya mwanadamu, na kinywa kilichokuwa kikinena maneno makuu”.

Kama vile Nabii Yona alikaa ndani ya tumbo la samaki siku tatu usiku na mchana, kadhalika Huyu mnyama atokaye baharini atalimeza hili kundi la watu, kwa kipindi cha miaka mitatu na nusu ndio kile kipindi cha dhiki kuu, mpinga-kristo atakaponyanyuka na kuanza kuleta dhiki isiyoelezeka kwa wale waliouvuguvugu kwa kuupenda ulimwengu huu, na kuiacha njia Mungu aliyowawekea wao waiendee.

Hichi kipindi kipo karibuni kutokea, Yule mnyama sasa anatenda kazi katika siri na watu wa Mungu wanasinzia hawaoni kuwa wapo katika hatari, wanadanganyika na utulivu uliopo sasa hivi kama vile nabii Yona alivyodhani lakini biblia inasema 

1Wathesalonike 5: 2 “Maana ninyi wenyewe mnajua yakini ya kuwa siku ya Bwana yaja kama vile MWIVI ajavyo usiku. Wakati wasemapo, Kuna amani na salama, ndipo uharibifu uwajiapo kwa ghafula, kama vile utungu umjiavyo mwenye mimba, wala hakika hawataokolewa”.

Ndugu usileweshwe na ulevi wa hii dunia hata kulala usingizi, Bwana yupo karibu kulichukua kanisa lake BIBI-ARUSI WA KWELI anayedumu katika Neno lake na UTAKATIFU, Na hatua za unyakuo zimeshaanza Bwana anawakusanya watu wake toka kila mahali, watu ambao macho yao yapo mbinguni, duniani wao ni kama wapitaji tu, hao ndio watakaofunuliwa siri za unyakuo lakini wengine wote ikiwemo wakristo vuguvugu, hawatajua lolote isipokuwa kumtazamia Yule mpinga-kristo mnyama atokaye baharini. Utajisikiaje siku ile wenzako wapo mbinguni kwenye KARAMU YA MWANA-KONDOO na wewe upo katika dhiki kuu na zaidi ya yote watakuja kutawala na Kristo milele na milele kama wafalme na makuhani wa Mungu na wewe upo kwenye ziwa la moto??. Ni vizuri utengeneze mambo yako sasa hivi kabla siku ile haijafika. Tubu ukabatizwe kwa Jina la BWANA YESU upate ondoleo la dhambi zako na uanze kuishia wokovu..

Mungu akubariki..

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Kwa maombezi/ Ushauri/ Ratiba za Ibada/Maswali/ Whatsapp/ Piga namba hizi: +255693036618/ +255789001312

Kwa mwendelezo >>> YONA: Mlango wa 2

Mada Nyinginezo:

UFUNUO: MLANGO WA 13

UFUNUO: MLANGO WA 17

DANIELI: MLANGO WA 7

NYAKATI SABA ZA KANISA NA WAJUMBE WAKE.

INJILI KULINGANA NA TEKNOLOJIA


Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
5 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
trackback

[…] UCHAMBUZI WA KITABU CHA YONA […]

Damy
Damy
2 years ago

Kazi yenu njema sana kwa hakika

Anonymous
Anonymous
2 years ago

Ameni

enock amilio
enock amilio
2 years ago

Asante