INJILI KULINGANA NA TEKNOLOJIA

INJILI KULINGANA NA TEKNOLOJIA

Mungu amekuwa akizungumza na wanadamu kwa njia tofauti tofauti na kwa wakati tofauti tofauti, 

Katika historia ya kanisa ujumbe Mungu alioutoa kwa kanisa la kwanza sio sawa na ujumbe alioutoa kwa kanisa la pili..na wala sio sawa na ujumbe alioutoa kwa kanisa la mwisho. Mungu anaongea kulingana na wakati, ni muhimu sana kulitambua hilo. Kwa mfano wakati ulipotimia wa Mungu kumleta mwana wake katika agano jipya watu wengi ikiwemo waalimu wa torati na mafarisayo hawakuweza kuiamini injili yake kwasababu hawakuuelewa ujumbe wa saa yao. Walishikilia torati ya Musa lakini walisahau kuwa Musa alisema ”atakuja nabii mwingine kama mimi mwaminini yeye”. Lakini waliukataa ujumbe wa Yesu Kristo wakabaki kushikilia mapokeo yao.

Katika hichi kipindi cha siku za mwisho tunaona kuwa yote yaliyotabiriwa na BWANA YESU KRISTO yanaenda kutimia, Licha ya kwamba Bwana kumtuma mjumbe wake(William Branham) kutuamsha kujiweka tayari kwa ajili ya kumlaki Bwana mawinguni tunaona pia Mungu amekuwa akizungumza na sisi kwa kupitia maumbile ya ulimwengu (nature) kutufundisha na kututhibitishia kuwa nyakati hizi tunazoishi ni za mwisho.

Kwa mfano maendeleo makubwa ya teknolojia tunayoyaona sasa hivi yana hubiri dhahiri injili ya kuja kwa BWANA YESU KRISTO. Baadhi ya hayo ni:

TEKNOLOJIA YA SIMU YA MKONONI NA MITANDAO:

Leo hii sio jambo la kushangaza kuona mtu mmoja anawasiliana na mwingine aliye taifa la mbali maelfu ya maili. Kwa sekunde tu!, watu wanaweza wakaonana na kuzungumza kwa mfumo wa video (yaani video chat).Watu wanaweza kupelekeana taarifa na habari kwa mfumo wa televisheni ndani ya dakika chache tu na dunia nzima ikapata habari ya mambo yanayoendelea ulimwenguni, teknolojia imefanikiwa kuifanya dunia kuwa kama kijiji.

Mungu kayaruhusu haya yote kutokea kwa kasi kubwa katika karne hii ya 20 na ya 21 ili kutufundisha na sisi watoto wa Mungu ya kuwa katika kipindi chetu cha mwisho mawasiliano yetu na Mungu yanapaswa yawe makubwa kuliko vipindi vyote vya nyuma vilivyotutangulia, tunajua kwa dunia ya sasa kuwa na chombo cha mawasiliano (kama simu) ni muhimu kwa ajili ya kujuzana habari sana sana kwa matukio ya gafla, pasipo hicho hauwezi kuendana na jamii/maisha ya sasa vivyo hivyo na sisi kama wana wa Mungu tumefika wakati ambao kila mtu anapaswa awe na Roho Mtakatifu kama chombo chake cha mawasiliano katika hichi kipindi cha uovu na mafundisho ya uwongo kuenea kila mahali.

Leo hii mtu anaweza kutafuta ukweli wa jambo fulani kwa kutumia mtandao (internet) na sisi pia kama wana wa Mungu tunahitaji Roho Mtakatifu kutufundisha na kutuongoza katika kweli yote, na kama vile zamani ujumbe ni lazima upelekwe na mtu fulani(mjumbe) lakini sasahivi mjumbe haitajiki tena kwasababu kuna simu ambazo zimerahisisha mambo kupata habari kwa haraka vivyo hivyo katika wakati wetu tunaoishi sasa hivi Mungu alishawapeleka wajumbe wengi sasa tupo katika hatua ya sisi kuwasiliana na Mungu moja kwa moja mjumbe haitajiki tena kama kuna Roho Mtakatifu.

Biblia inasema..

Yeremia 31:33 ” Bali agano hili ndilo nitakalofanya na nyumba ya Israeli, baada ya siku zile, asema Bwana; Nitatia sheria yangu ndani yao, na katika mioyo yao nitaiandika; nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu. Wala hawatamfundisha kila mtu jirani yake, na kila mtu ndugu yake, wakisema, Mjue Bwana; kwa maana watanijua wote, tangu mtu aliye mdogo miongoni mwao hata aliye mkubwa miongoni mwao, asema Bwana; maana nitausamehe uovu wao, wala dhambi yao sitaikumbuka tena”.

Tumeona hapa katika hizi siku za mwisho ni muhimu kuwa na Roho Mtakatifu kukufundisha ndani yako binafsi na kukuongoza katika kweli yote, maana saa tunayoishi ni ya hatari manabii wa uwongo waliotabiriwa na mafundisho mengi ya uwongo yameenea kila mahali hichi ndicho kile kipindi Bwana alichosema.

Mathayo 24:23-26 “Wakati huo mtu akiwaambia, Tazama, Kristo yupo hapa, au yuko kule msisadiki. Kwa maana watatokea makristo wa uongo, na manabii wa uongo, nao watatoa ishara kubwa na maajabu; wapate kuwapoteza, kama yamkini, hata walio wateule.

Tazama, nimekwisha kuwaonya mbele. Basi wakiwaambia, Yuko jangwani, msitoke; yumo nyumbani, msisadiki”.

Ni wakati wa kutafuta uhusiano wako binafsi na Mungu, leo hii ukitaka kumwita mtu kwa haraka mahali fulani mbali ni lazima umpigie simu, kama hana simu basi hawezi kujua kama unamhitaji kwa wakati huo, vivyo hivyo usipokuwa na Roho wa Mungu hutaweza kufahamu wakati utakapoitwa haraka kwenda kumlaki Bwana mawinguni, watakaoenda ni wale tu wenye mahusiano na mawasiliano mazuri na Mungu.

TEKNOLOJIA YA NDEGE:

Kwa vizazi vya nyuma suala la mtu kupaa hewani lilikuwa ni jambo lisilowezekana lakini sasa mtu kusafiri kwenda kwenye magimba ya nje ya dunia limekuwa ni jambo la kawaida kwa kutumia roketi.

Hii inatufundisha kuwa kama sayansi imefanikiwa kufanya hivi, na sisi wakristo tunaomngojea Bwana wakati wetu wa kupaa mawinguni umekaribia, kama vile wanasayansi walivyokuwa wakitafiti kwa miaka na miaka huko nyuma ni jinsi gani wangeweza kuruka juu hewani na kufika kwenye magimba mengine nje ya dunia na kufanikiwa katika kizazi hichi baada ya kutaabika kwa muda mrefu, inatufundisha sisi wana wa Mungu kuwa ndege yetu ya kwenda mbinguni imeshaandaliwa na iko tayari katika hichi kizazi chetu baada ya kusubiria kwa muda mrefu, na kama vile mtu akitaka kusafiri kwa ndege ni lazima awe na tiketi naye amekata mapema(booking).

 Vivyo hivyo na sisi tunapaswa sasa hivi kuwa na Roho Mtakatifu kama tiketi yetu ya kuingia katika ndege hiyo ya mbinguni na tunapaswa tu-book mapema kabla ya ndege kuondoka ili tuwe na uhakika wa safari yetu kabla nafasi hazijajaa.

Jiulize ewe ndugu..simu yako ni ipi?? kama hapo ulipo hukosi kuwa na simu mfukoni na unajua kabisa katika dunia ya sasa usipokuwa na simu hauwezi kuendana na jamii inayokuzunguka lakini hutaki kuwa na simu ya roho ambayo ni Roho Mtakatifu unatazamia nini hapo??..

Jibu ni dhahiri kwamba unategemea siku ile ikujie gafla kama mtego unasavyo..wakati wengine wakiwa na Roho wa Mungu akizungumza nao katika hichi hichi kizazi unachoishi wewe wakijiweka tayari kuchukuliwa juu wewe utakuwa huna habari…habari itakufikia baadae wakati wakristo wa kweli wameshaondoka kwasababu huna simu yako mwenyewe (Roho Mtakatifu) ingekupasa upigiwe simu ya kuondoka lakini kwasababu huna Roho Mtakatifu utasubiria uletewe habari kwasababu hiyo basi itakupasa uingie katika ile dhiki kuu..mimi binafsi nisingependa kubaki kwenye dhiki kuu sijui wewe??

Na je! tiketi yako ni nini??..

Kumbuka ndege ipo tayari na ina nafasi chache tu (limited number of seats) na kumbuka ndege sio gari uende saa hiyo hiyo na kupanda uondoke, ina process. Hivyo inahitaji booking mapema, wanashauri walau ukate tiketi wiki moja au mbili kabla kwa uhakika wa safari yako, na katika siku ya safari unapaswa ufike airport masaa 3 kabla kwa ajili ya hatua ya makaguzi (check-in process) usipozingatia hivi vigezo huwezi kusafiri. Vivyo hivyo katika safari yetu ya kwenda mbinguni ndege yetu ipo tayari hatua tuliyopo sasa ni ya booking kwa ajili ya kupata nafasi katika sehemu ya ufalme.

Na hatua hii inakaribia kumalizika unatakiwa uwe na tiketi yako mkononi (Roho Mtakatifu) nafasi zinaenda kujaa, na zikishajaa hatua itakayofuatia ya makaguzi(check- in). Ni kwa wale tu walio na tiketi zao wengine wasio na tiketi haitawahusu, na hatua zote hizi zinafanyika tukiwa hapahapa duniani. kabla ya kwenda kupanda ndege yetu ya kwenda mbinguni.

Tukumbuke Mungu karuhusu haya mabadiliko makubwa ya teknolojia yatokee katika kizazi chetu. Ili sisi tujifunze, tusipojifunza yatakuja kutuhukumu katika siku ile ya Bwana..Je! hauoni ni wakati gani huu wa hatari tunaouishi??..Na bado unaendelea kuupenda ulimwengu kuliko kumpenda Mungu. unakuwa mwasherati wakati Mungu anasema “hamjui kuwa miili yenu ni hekalu la Roho Mtakatifu”.

Unatazamiaje Roho wa Mungu aje juu yako, una kuwa mlevi, vuguvugu haueleweki wewe ni mkristo au ni nani, una kuwa msengenyaji, unajichanganya na watu waovu wa ulimwengu huu hao ndio rafiki zako wakati biblia inasema ‘msifungwe nira pamoja na wasio amini”.

Una kaa na watu wenye mizaha, maneno machafu yanatoka midomoni mwako na bado unajiita mkristo, unavaa mavazi yasiyo na heshima na kufanana na wanawake wa ulimwengu huu.

Huna muda wa kusoma neno na kusali na kuomba lakini unapata muda mwingi wa kuchati kwenye mitandao katika vitu visivyokuwa na maana, shetani amekupofusha akikudanganya kwamba wewe ni bibi arusi wa Kristo na kwamba yote ni sawa.

Lakini jua jambo moja katika kizazi hichi hichi unachoishi wewe kuna wakristo kweli kweli ulimwenguni kote waliojazwa Roho Mtakatifu wanaushinda ulimwengu katika mazingira kama hayo hayo yakwako unayoishi wewe na watatuhukumu maana biblia inasema ‘watakatifu ndio watakaoouhukumu ulimwengu’.

Umehubiriwa injili kila siku unaisikia bado unaishi maisha unayoishi sasa. Kristo alisema ”itakufaidia nini uupate ulimwengu mzima na kupata hasara ya nafsi yako?” mambo ya ulimwengu huu yanakusonga mpaka unashindwa kuwa mkristo kama unavyopaswa uwe,

Tubu! badilika muda umeenda kuliko tunavyodhani mambo yote yameshakuwa tayari. Huu sio wakati tena wa sisi kumngojea Bwana bali Bwana ndiye anayetungojea sisi.

TAFUTA ROHO MTAKATIFU MAANA HUO NDIO MUHURI WA MUNGU!

Mungu akubariki.

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Nyinginezo:

INJILI YA MILELE.

JE UMEYABATILISHA MAMBO YA KITOTO

BWANA ALIPOSEMA KUWA YEYE NI “MUNGU WA MIUNGU” ALIKUWA NA MAANA GANI?..JE! YEYE NI MUNGU WA SANAMU?

JE! WATAKAOENDA MBINGUNI NI WENGI?


Rudi Nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments